Subcribe to our RSS feeds Join Us on Facebook Follow us on Twitter Add to Circles

Alhamisi, 12 Juni 2014

MAANA YA HADITHI.



HADITHI

Masimulizi ni fasihi yenye kusimulia habari fulani (narrate). Ni masimulizi ambayo yanatumia lugha ya mjazo au nathari na mtiririko wake huwa mwepesi au sahili. Urefu wa hadithi hutofautiana kutoka kitanzu/kipera kimoja hadi kingine. Kwa jumla zipo hadithi ambazo ni za kubuni na zingine za kihistoria. Baadhi ya vipera vya utanzu huu ni;

i. Ngano

Hizi ni hadithi za kimapokeo zitumiazo wahusika kama wanyama, miti na watu katika kuelezea au kuonya kuhusu maisha. Utanzu huu unajumuisha fani kadhaa kwa mfano:

Istiara – hadithi ambayo maana yake ya wazi inawakilisha maana nyingine iliyofichika. Yaani hadithi nzima ni kama sitiari.

Mbazi- hadithi fupi yenye mafunzo itolewayo kama kielelezo wakati wa maongezi au wa kumkanya mtu

Kisa- hadithi fupi ya kufurahisha kuhusu tukio la kweli.

ii. Visakale

Masimulizi ya mapokeo juu ya wahenga au mashujaa wa kabila au taifa yenye kuchanganya chuku na historia. Kwa mfano hadithi za Liyongo

iii. Mapisi

Maelezo ya historia bila kutia mambo ya kubuni.

iv. Soga


Ni hadithi ndogo ndogo zinazohusisha utani na ucheshi kwa kiasi fulani. Hizi ni hadithi ambazo hutambwa katika mtiririko wa matukio ambao huzua kicheko. Soga hudhamiria kuchekesha kwa kukejeli pia. (wamitila: 2010)

v. Tarihi


Hizi ni hadithi ambazo husimulia au zimejengwa kwenye matukio ya kihistoria. Inawezekana matukio yanayosimuliwa yakawa ya kweli, yaani yalipata kutokea kihistoria. Hadithi hizi hutokea zaidi katika maandishi, mfano ni tarihi ya Kilwa, tarihi ya Pate n.k.

vi. Visasili


Ni utanzu unaofungamana na imani za dini na mizungu (rituals) ya jamii. Hizi ni hadithi za kale zenye kuwakilisha imani na mtazamo wa jamii inayohusika kuhusu asili ya ulimwengu na mwenendo wake, kuhusu asili yao wenyewe, na maana na shabaha ya maisha yao. Mara nyingi hadithi hizi huaminiwa kuwa ni kweli tupu, na hutumika kuelezea au kuhalalisha baadhi ya mila na madhehebu ya jamii inayohusika.

2. SEMI


Semi ni tungo au kauli fupifupi za kisanaa zenye kubeba maana au mafunzo muhimu ya kijamii. Baadhi ya tanzu katika kundi hili ni;

I. Methali


Methali ni semi fupi fupi zenye kueleza kwa muhtasari fikra au mafunzo mazito yaliyotokana na uzoefu wa kijamii. Mara nyingi mawazo hayo huelezwa kwa kutumia tamathali hasa sitiari na mafumbo. Methali nyingi huwa na muundo wenye sehemu mbili. Sehemu ya kwanza huanzisha wazo Fulani, na sehemu ya pili hulikanusha au kulikaamilsha wazo hilo. Kwa mfano; haraka haraka haina Baraka, tama mbele mauti nyuma.

II. Vitendawili


Ni usemi uliofumbwa ambao hutolewa kwa hadhira ili iufumbue. Fumbo hilo kwa kawaida huwa linafahamika katika jamii hiyo, na mara nyingi lina mafunzo muhimu kwa washiriki, mbali na kuwachemsha bongo zao. Vitendawili ni sanaa inayotegemea uwezo wa mtu kutambua, kuhusisha na kulinganisha vitu vya aina mbalimbali vilivyomo katika maumbile.

III. Misimu


Ni semi za muda na mahali maalum ambazo huzuka na kutoweka kutegemea mazingira maalum. Msimu ukipataa mashiko ya kutosha katika jamii huweza hatimaye kuingia katika kundi la methali za jamii hiyo.

IV. Mafumbo


Ni semi za maonyo au mawaidha ambazo maana zake za ndani zimefichika. Fumbo hubuniwa na msemaji kwa shabaha na hadhira maalum, hivyo ni tofauti na methali au vitendawili ambavyo ni semi za kimapokeo.

V. Lakabu


Haya ni majina ya kupanga ambayo baadhi ya watu hupewa au hujipatia kutokana na sifa zao za kimwili, kinasaba, kitabia au kimatendo. Majina haya huwa ni maneno au mafungu yaa maneno yenye maana iliyofumbwa. Mara nyingi majna haya huwa ni sitiari. Baadhi ya majina haya humsifia mhusika, lakini mengine humkosoa au hata kumdhalilisha. Mifano ya lakabu;

Mukwavinyika – mtekaji wa nyika
Baba wa taifa – mwl Nyerere
Simba wa Yuda – Hile Selassie

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni