Subcribe to our RSS feeds Join Us on Facebook Follow us on Twitter Add to Circles

Jumanne, 9 Septemba 2014

KIDAHIZO KATIKA KAMUSI.

Swali:-    Kidahizo ndiyo msingi wa kamusi. Fafanua kauli hii ukizingatia maumbo ya maneno yanayoweza kukaa katika nafasi ya kidahizo.


    Swali litajibiwa kwa kuligawa katika sehemu tofauti ili liweze kueleweka vizuri. Ambapo  tutaangalia maana ya kidahizo, maana ya kamusi, maelezo ya kina kuhusu kidahizo na kisha tutaangalia jinsi maumbo ya maneno yanavyoweza kukaa katika nafasi ya kidahizo.
Istlahi kidahizo imefafanuliwa na wataalamu wengi miongoni mwao ni pamoja na hawa wafuatao;
TUKI (1981) wanaafasili kidahizo kama neno linaloingizwa katika kamusi kwa chapa ilyokolezwa.
BAKIZA (2010) nao wanaeleza kuwa; kidahizo; ni neno linalochapishwa kwa hati zilizokozwa na pengine kutiwa rangi kwenye kamusi ambalo taarifa zake zinafanuliwa. Tunaweza kuwaunga mkono wataalamu hawa fasili yao kwani kidahizo huwa katika wino uliokolezwa na huingizwa katika kamusi ili kutolewa maana. Lakini kwa fsili ya jumla tunaweza kusema kuwa,
Kidahihizo ni neno linaloingizwa katika kamusi ili liweze kufafanuliwa kwa kupatiwa maelezo yanayohusu taarifa za kisarufi, maana, matumizi, etimolojia semi mbalimbali za lugha na nyingine.
Oxford (2010) wanaeleza kuwa; kamusi ni kitabu ambacho huwa kinaorodha ya maneno ya lugha fulani katika mpangilio wa alfabeti na huelezwa maana ya maneno hayo. Au kamusi ni orodha ya maneno yaliyopo katika mfumo wa eletroki kwa mfano yanaweza kuhifadhiwa katika kompyuta. Faslili hii ionekena kuwa na mashiko kwani kutokana na maendeleo ya sayansi na teknolojia si sahihi tene kufasiri kamusi kama kitabu bila kuihusisha na elektroniki katika uhidhi wake.
Kamusi hutungwa ikiwa na malengo mbalimbali kulingana na mahitaji na matumizi ya taaluma au mtumiajia fulani. Mfano zipo kamusi za uwanja husika kama sheria, isimu, falsafa na nyingine. hivyo uteuzi wa msamiati hulingana na uwanja unaotungiwa ambapo kama ni uwanja wa jumla lazima tutakuta msamiati wenye lugha sahili au lahisi. Hivyo msamiati unaokusanywa na kuwekwa katika kamusi ili kufasiliwa ndiyo huitwa kidahizo. Vidahizo hufafanuliwa kwa kupatiwa taarifa za kina ili anayetaka taarifa hizo azipate bila utata wowote.
Katika kamusi za Kiswahili vidahizo huwa na maneno ya kawaida yanayotumika katika Nyanja mbalimbali za mawasiliano miongoni mwa wazungumzaji wa Kiswahili. Msamiati unaoingizwa katika kamusi kama vidahizo hukusanywa katika sehemu tofauti  mfano machapisho mbalimbali, kama matini magazeti na vitabu mbalimbali.
Kidahizo kimegawanyika katika sehemu mbili yaani kidahizo huru na kidahizo mfuto. Hii ni kwa mujibu wa TUKI (2000). Kidahizo kikuu katika kamusi huwa ni umbo la msingi la neno. Mfano “lim.a” “li.a” wakati kidahizo mfuto, ni kinyambuo  kisichotumika sana au neno ambatani ambalo limeingizwa ndani ya maelezo ya kidahizo kikuu. Na kusoma maelezo ya maana ya kisarufi. Iwapo halitumiki sana au halijapata kutumika lakini likatumika tu kwa siku moja hupatiwa maana ya kisarufi tu. Kinyambuo cha kitenzi ambacho kina kategoria tofauti huingizwa kama kidahizo mfuto ndani ya umbo la msingi bila maelezo ya maana na kisha huingizwa tena kama kidahizo kikuu katika herufi ya alfabeti inayohusika.
Kidahizo kama msingi wa kamusi, hupangwa kwa kufuata utaratibu wa alfabeti. Kwa kila ukurasa neno la kwanza na la mwisho katika ukurasa limechapwa sehemu ya juu ya ukurasa ili kumwongoza msomaji atambue nafasi ya neno analohitaji au analotafuta, iwapo lipo katika ukurasa anaousoma au lipo nyuma au mbele ya ukurasa unaohusika maneno ya kumuongoza msomaji humwezesha kupitia kamusi na kugundua neno unalotaka kuliko kusoma ukurasa na kila kidahizo ili kupata neno unalotafuta.
Kidahizo ni msingi wa kamusi kwa kutokana nacho ndipo tunapata maana ya maana ya neno, etimolojia yake, matumizi na matamshi yake. Kwa hiyo bila kidahizo hatuwezi kuwa na kamusi. Msamiati wote unaokusanywa huwa ni kwa ajiri ya kutolewa maana katika kamusi ili kusaidia watumiajia wa lugha Fulani au wenye kuhitaji kujua msamiati wowote kutumia kamusi. Kwa hiyo naweza kusema hakuna kidahizo hakuna kamusi. Huo ndiyo umuhimu wa kidahizo katika kamusi.
Baada ya maelezo hayo mengi sasa tuone maumbo yanayoweza kutokea katika kamusi kama kidahizo.  Maumbo hayo ni kama haya yafuatayo.
Maumbo sahili; haya ni maumbo yanayoumbwa kwa neno huru yaani lisilo na utegemezi au lisiloweza kuambishwa.
                    Kwa mfano; maneno kama
                “barua”, “nyumba”, “bakuli” na “baba”.
Maneno haya ni huru. Hivyo maumbo haya huingizwa  katika kamusi kama kidahizo.
Maumbo ambatani; haya ni maumbo ya maneno ambayo huumbwa kwa kuunganisha maneno mawili tofauti, mfano nomino na kitenzi, nomino na nomino na mengine. Katka kamusi maneno haya huchukuliwa kama neno moja lenye kuwakilisha dhana fulani. Kwa mfano maumbo haya yametoka katika kamusi ya tuki (2001).
Kipeleleza-nyanbizi nm vi- [ki-vi-] asdic.
Kipazasauti nm vi- [ki-vi-] loud speaker.
Kipashamoto nm vi- [ki-vi-] chafing-dish.
Kipimahewa nm vi- [ki-vi-] barometer
Kitanguakimbanga nm vi- [ki-vi-] anticyclone
Maneno yote haya ni mwambatano lakini katika kamusi husimama kama neno moja na siyo kuwa tunaangalia maana ya neno moja moja. Hapa nisawasawa na maneno ya nahau, misemo nayo katika kamusi huchukuliwa kama neno moja lenye kuwakilisha dhana fulani. Mfano; TUKI (2001)
Kifungua kinywa,
 kick the bucket,
tia  nanga.
Maumbo changamani, ni maumbo ya maneno yanyokuwa na uchangamani. Ni maneno ambayo hayawezi   kusimama pekee katika kamusi. Maneno haya huwa na viambishi vinavyotenga mzizi wa  neno pia maneno haya hutengwa ili kuonesha uwezo wa kunyumbuliwa au kuchukua viamshi tofauti tofauti. Mfano;

M.toto 
M.tu
Nufaik.a
Nui.a
Maneno haya huweza kunyumbuliwa na kuleta maana nyingine tofauti na maneno sahili ambayo hayawezi kunyumbuliwa. Kwa mfano neno “nui.a” linaweza kunyumbuliwa na kupata maneno mengine kama, nuilia,nuilika, nuiana nuiza.
Maumbo hulutishi, haya ni maumbo ambayo kutokea kama kidahizo katika kamusi. Maneno haya huundwa kwa kuunganisha sehemu mbili za maneno tofauti na siyo kuunganisha maneno mazima. Kwa mfano;
Telephone
Mobitel
Telefax
Maumbo ya akronimia, haya ni maumbo yanayoingizwa katika kamusi kama kidahizo. Maumbo haya huwa katika ufupisho na huwakilishwa kwa herufi kubwa ambazo kila herufi hubaeba dhba Fulani. Mfano; kutoka Oxford (2006).
ISBN International Standard Book Number
ISA Industry Standard Architecture
ISDN Integrated Services Digital Network
SAD Seasonal Affective Disorders
Akronimia hizi hutokea upande wa kidahizo kuwakilisha maana  ama dhana iliyondefu kuwa katika maneno machache.
Maumbo rejerezi, katika kidahizo kuna maumbo ya maneno ya kumfanya msomajia arejelee neno jingine ili kupata ufafanuzi zaidi, maneno yanayorejelewa katika kamusi huoneshwa kwa mshale. Mshale huu ulenga kumuonesha msomaji kulitafuta neno analooneshwa. Kwa mfano;
Pally   → PAL
Pas.try  →see also CHOUX PASTRY
Pipe  → see also PIN PIPES
Mshale huu huwekwa baada ya kuwa taarifa zote kuhusu kidahizo hicho zimetolewa, na huenda kunahitajika maaelezo ya ziada kuhusu neno hilo kwa hiyo msomaji huoneshwa neno jingine kwa mshale ili aone tena maelezo hayo.
Maumbo dondoshi, haya ni maumbo ambayo huingizwa katika kamusi kama kidahizo baada ya sehemu ya neno hili kudondoshwa. Mfano wa maumbo hayo ni kama vile; kutoka katika Oxford (2006).
Phone kutokana na neno telephone
Gram kutokana na neno telegram.
Bike  kutoka na neno bicycle
Maumbo haya fupishi tunayakuta katika kidahizo cha kamusi na hubeba maana ambayo inapatikana katika neno zima ambalo halijafupishwa.
Maumbo radidi, haya ni maumbo ya neno linalojirudia rudia katika kamusi. Neno hili hubeba dhana  moja katika kamusi. Kwa mfano maneno kama,
Uramberambe nm [u-] coconut kernel
Mzengazenga nm mi-n[u-i] carrying two things by using a pole across the soulder
Mzikoziko nm mi [u-li- ] ipecacuanha.
Mnyunginyungi.
Maneno haya hubeba dhana moja inayowakilishwa na uradidi huo.
Maumbo mengine yanayoweza kuingizwa katika kamusi kama kidahizo ni maumbo ya homonimia. Maneno haya huwa na maumbo sawa na matamshi sawa lakini maana huwa tofauti. Katika kamusi huingizwa kama vidahizo vyenye maana tofauti na maana hizo hutofautishwa kwa kupewa namba.
Mfano
Kaa1.
Kaa2,
Kaa3
Panda1,
Panada2
Panda3
Vidahizo hivyo huonekana katika kamusi kama ilivyo mifano hapo juu.

Kwa kuhitimisha, tunaweza kusema kuwa uorodheshaji wa vidahizo katika kamusi hutegemea lengo la kamusi. Mfano kama kamusi ni ya kisheria huorodhesha vidahizo vyake katika  misingi ya kiseria. Maana za msingi ndizo huorodheshwa kwanza na kufuatiwa na maana zilizozuka baadaye au maana zinazohusishwa na neno hilo. Kidahizo ni cha msingi katika kamusi kwani huonesha herufi rasimi zinazopaswa kuunda neno.

Marejeo
BAKIZA (2010) Kamusi ya Kiswahili Fasaha. Kenya: Oxford University Press.
Mdee, J. S. (2010) Nadharia na Historia ya Leksokografia. Dar es Salaam: TUKI.
Oxford (2010) Oxford Advanced Learner’s Dictionary. New York: Oxford University Press.
TUKI (2001) Kamusi ya Kiswahili-Kiingereza. Dar es Salaam: TUKI.
TUKI (2004) Kamusi ya Kiswahili Sanifu. Dar es Salaam: TUKI.
TUKI (2006) English-Kiswahili Dictionary. Dar es Salaam: TUKI

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni