Subcribe to our RSS feeds Join Us on Facebook Follow us on Twitter Add to Circles

Alhamisi, 12 Juni 2014

UHAKIKI WA DIWANI ZA KISWAHILI.


UHAKIKI WA DIWANI YA WASAKATONGE


UTANGULIZI

Diwani ya Wasakatonge ni miongoni mwa diwani za hivi karibuni zinazotanabaisha matatizo mbalimbali yanayoikumba jamii katika maisha yake ya kila siku. Matatizo hayo yanaonekana kuwa kama saratani isiyo na tiba. Hata hivyo, msanii ana matumaini kwamba, iwapo wananchi wa kawaida wataungana na kuamua kupambana, ni dhahiri kwamba matatizo hayo yatatoweka kabisa. Miongoni mwa matatizo hayo yataoneshwa kwenye kipengele cha maudhui huku yakishadidiwa na fani.

MAUDHUI: ni jumla ya mambo muhimu yanayoelezwa katika kazi ya kifasihi. Maudhui yanajengwa na vipengele vidogovidogo vifuatavyo; dhamira, ujumbe, mgogoro, mtazamo na falsafa.

DHAMIRA: ni jumla ya maana anayovumbua mwandishi aandikapo kazi yake na jumla ya maana anayoipata msomaji pindi anapoisoma kazi fulani ya kifasihi. Kifasihi kuna aina mbili za dhamira yaani dhamira kuu na dhamira ndogondogo. Dhamira kuu ni lile wazo kuu la mwandishi katika kazi, wakati dhamira ndogondogo ni zile dhamira zinazojitokeza ili kuipa nguvu dhamira kuu. Dhamira zilizojitokeza katika diwani hii ni kama ifuatavyo:

UONGOZI MBAYA: ni aina ya uongozi ambao haujali maslahi ya wananchi na taifa kwa ujumla. Ni uongozi unaotumia mabavu na unaojali maslahi binafsi, yaani haufuati misingi ya utawala wa sharia. Katika diwani hii msanii anaonesha kuwa nchi nyingi duniani hasa zile za kiafrika zinakabiliwa na tatizo la uongozi mbaya. Viongozi walio wengi ni madikteta ambao hawataki kuachia madaraka wala kuwapa watawaliwa uhuru wa kuzungumza.

Hali hii tunaopata katika shairi la “MADIKTETA” (uk.21) ambapo msanii anasema kuwa harakati za kusaka uhuru au demokrasia kwa njia ya mtu haijawahi kuzaa matunda yanayotarajiwa. Harakati hizi zimekuwa zikizalisha viongozi “Miungu watu” au marais walio madikteta, kama ilivyokuwa kwa Mabutu Seseko-huko Zaire (kwa sasa DRC), Bokosa-huko Afrika ya Kati na Idd Amini-huko Uganda. Madikteta hawa wamekuwa na kila aina ya uovu ikiwa ni pamoja na kukumbatia ukabila, udini na uvamizi kwa nchi nyingine. Haya tunayapata katika shairi la “SADDAM HUSSEIN” (uk.26:4) anasema;

4. “Nakuafiki, Saddam, si kwa uvamizi wako,Na ujue kwamba,
Huo si uasi
Kwa wakubwa mila,
Saddam, yamesha tendeka sana!”

Viongozi wa aina hii huwanyima wananchi wao uhuru wa kusema ikiwa ni pamoja na ule wa kujiamulia mambo yao wenyewe kama katika shairi la “MARUFUKU” namba 45 (uk.36)
“Sitakiki uone,
Ingawa una macho,
Sitaki useme,
Ingawa una mdomo,
Sitaki usikie,
Ingawa una masikio,
Sitaki ufikiri,
Ingawa una akili,
Sababu utazinduka,
Utakomboka,
Uwe mtu,
Hilo sitaki,
Marufuku.”

Viongzozi wabovu (madikteta) ni wapenda dhuluma na manyanyaso. Huwadhulumu na kuwanyanyasa raia wao na raia wa nchi nyingine kama inavyojidhihirisha katika mashairi ya “KOSA” (uk.3), na “FAHARI LA DUNIA” (uk.45). Katika shairi la “KOSA”, tunaona kuwa unyanyasaji wa wananchi wa kawaida hutokea pale ambapo wanapokuwa wanadai haki zao. Mshairi anasema:
3. “Kosa letu kubwa,
Kudai haki?
Yetu miliki?
Mna hamaki,
Na huku mnatukashifu!”

Katika shairi la “FAHARI LA DUNIA” (uk.45) tunaambiwa kuwa kuna kiongozi mwenye nguvu (Marekani) ambaye mchana kutwa usiku kuchwa linanyanyasa nchi nyingi bila sababu za msingi. Msanii anasema:
5. “Fahari la Dunia,
Kwa kiburi, linatesa,
Lajigamba,
Linatamba,
Kuwa mwamba,
Linaoneya.”

Viongozi wabovu siku zote ni wanyonyaji na hushirikiana na watu wengi wenye nguvu kubeba mirija ya unyonyaji na kuanza kuwanyonya raia wa kawaida. Hali hii hujitokeza sana katika nchi za Dunia ya tatu. Haya yote tunayapata katika mashairi ya “MVUJA JASHO” (uk.12-13), “MIAMBA” (uk.29-30), “MUMIANI” (uk.34) Katika shairi la “MVUJA JASHO” msanii anaonesha kuwa raia wa kawaida wanafanya kazi kubwa na ngumu sana lakini malipo yao hayalingani na jasho wanalolitoa. Katika shairi la “MIAMBA” tunaambiwa kuwa wanyonge hawana chao, jasho lao na wao wenyewe ni chakula cha wakubwa na watawala wao. Ubeti wa 4 wa shairi hili msanii anahoji juu ya suala hili kwa kutumia taswira ya wanyama:
4. “Wanyonge,
Wamo shidani,
Digidigi na nyani,
Wamo makimbizoni,
Fisi wafurahia,
Ni sharia za mbuga?”

Katika shairi la “MUMIANI” linaonesha waziwazi unyonyaji unaofanywa na viongozi au watu wa tabaka la juu dhidi ya tabaka la chini ambao wanaishi vijijini na mijini, waendao hospitalini na wapelekwao mahakamani. Katika ubeti wa 1 tunaambiwa kuwa:-
1. “Mumiani,
Mijini,
Watembea kwa mato,
Kuzifanya kazi zao,
Kuzinyonya damu zetu,
Hawangoji,
Tulale.”

Diwani hii inaendelea kuonesha kuwa viongozi wabovu ni wasaliti na wanafiki. Viongozi hawa wanakuwa wepesi kuwaomba wananchi ili kufanikisha jambo fulani. Lakini pindi jambo hilo linapofanikishwa tu viongozi hao huwaweka wananchi pembeni (huwasaliti wananchi). Miongoni mwa mashairi yanayoonesha usaliti na unafiki wa viongozi wa dini na wa kisiasa ni “SIKULIWA SIKUZAMA” (uk.22-23), “WASO DHAMBI” (uk.1), “UASI” (uk.8), “PEPO BILA KIFO” (uk.14), vilevile shairi la “NAHODHA” (uk.41) linaonesha kuwa kuna viongozi wengi wanaoshindwa kazi lakini hawataki kuachilia madaraka. Hata hivyo msanii anaonesha kuwa viongozi wa aina hii wanaweza kuondolewa madarakani iwapo tu wananchi wote wataungana na kuwapiga vita.

KUPIGA VITA UKOLONI: Ukoloni ni hali ya kuvuka mipaka ya nchi na kwenda kuitawala nchi nyingine kisiasa, kiuchumi na kiutamaduni. Kutokana na madhara yanayosababishwa na ukoloni, msanii ameona kuwa tusiukumbatie bali tuupige vita ili tuweze kuishi maisha mazuri ambayo huja baada ya kujitawala. Katika shairi la “NURU YA MATUMAINI” (uk.9-10) tunaambiwa kwamba wananchi wa kusini mwa Afrika walipiga vita ukoloni ili kuondokana na ubaguzi, dharau, ubwana na utwana na hatimaye kuishi katika mazingira ya haki na usawa.

Kwa vile ukoloni unamadhara, kama inavyooneshwa katika shairi hilo, wananchi hawanabudi kuacha tabia ya kuukaribisha tena. Katika shairi la “HATUKUBALI” (uk.30) linatuambia kuwa;
4. “Hatukubali tena,
Kutuletea usultani,
Kutuletea na ukoloni,
Kutuletea na uzayuni,
Hatukubali katu,
Ndani ya nchi yetu,
Iliyo huru.”

Mbali na kupiga vita ukoloni mkongwe bali tunajukumu la kuutokomeza ukoloni mamboleo ambao kwa kiasi kikubwa unachangia kutufanya masikini. Ukoloni mamboleo hutufanya tusiwe na kauli juu ya bidhaa tunazozalisha na hatimaye Taifa letu kuishia kwenye lindi la umasikini. Inaonesha kuwa ukoloni mamboleo hutufanya tutekeleze matakwa ya mataifa makubwa kwa lengo la kuwa nufaisha wao huku sisi tukibaki taabani. Haya tunayapata katika shairi la “HATUNA KAULI” (uk.8-9)
6. “Tumepewa yake mitaji,
Tuwe wasimamiaji,
Pia watekelezaji.”

Hali hii pia inajitokeza hata katika shairi la “WAFADHILI” (uk.38-39) ambapo tunaambiwa kuwa wafadhili hutupenda tu pale tunapokubali masharti yao na matakwa yao.


1. “Wafadhili kufurahishwa,
Ni sera zao kupitishwa,
Rais anaamrishwa,
Tekeleza!”

Hali hii hutufanya tuwe watumwa wa ukoloni mamboleo baada ya kuondokana na ukoloni mkongwe. Katika shairi la “BUNDI” (uk.43) tunaambiwa kuwa uhuru wetu tulioupata hatujaufaidi hata kidogo kutokana na kupigwa nyundo ya kichwa na ukoloni mamboleo. Ukoloni huu ambao umefanikishwa na Bundi, tunaambiwa kuwa uko nasi kila kukicha. Ukoloni mamboleo ni mfumo usio na usawa hata kidogo. Ni mfumo ambao unawafanya wanyonge waendelee kuwa masikini, wasiomithilika huku matajiri wakiendelea kuwa watu wenye mali kupindukia. Haya yote tunayapata katika shairi la “KLABU” (uk.50) juu ya ukoloni mamboleo kwa kutuasa tuchapekazi, tujenge viwanda, tuboreshe kilimo na ufugaji, tuinue elimu, kukuza uchumi na tupige vita rushwa.

UMASKINI, UJINGA NA MARADHI: Mwalimu Julius K. Nyerere aliwahi kusema kuwa, jamii yetu inakabiliwa na maadui wakuu watatu; Umasikini, Ujinga na Maradhi. Hali hii inajitokeza katika diwani hii kwani msanii anatuambia kuwa Bara la Afrika ni kama mgonjwa aliyemahututi katika shairi la “TIBA ISOTIBU” (uk.18) Hii ni kutokana na ujinga, umasikini na maradhi. Hali hii imekuwa ikisababisha njaa, vita, chuki na visasi vya kila aina na hivyo kufanya bara la Afrika lisiwe na amani kama ilivyo DRC, Sudani, Rwanda, Burundi, Tunisia nk. Mshairi anakereka sana na hali hii kwa kuhoji haya katika shairi la “AFRIKA” (uk.6-7)
1. “Lini
Afrika utakuwa,
Bustani ya amani,
Ukabila kuuzika,
Udini kuufyeka,
Ni lini?”

Kwa ujumla Bara la Afrika limejaa watu masikini ambapo umasikini wao unatokana na mambo mengi kama vile unyonyaji unaofanywa na viongozi wao kwa kushirikiana na nchi za nje. Lakini pia umasikini hutokana na ujinga yaani elimu ndogo. Hali hii pia tunaikuta katika mashairi ya “WASAKATONGE” (uk.5), “MVUJA JASHO” (uk.12-13), “WALALAHOI” (uk.36-37)

MSUGUANO WA KITABAKA NA KIITIKADI (MATABAKA): Katika diwani hii msanii anaonesha msuguano mkali wa kitabaka uliopo katika jamii na katika nchi masikini na nchi tajiri. Matabaka haya yote ni zao la maisha ya kitajiri na kimasikini katika jamii. Tunaambiwa kuwa katika msuguano huu mkali baina ya matabaka, tabaka masikini linajaribu kujifaragua ili lipate angalau tonge la ugali wakati tabaka tajiri likijaribu kunyang’anya tonge linalopiganiwa na tabaka masikini. Haya tunayapata katika shairi la “TONGE LA UGALI” (uk.20)
4. “Wanapigana
Wanaumizana,
Wanauwana,
Kwa tonge la ugali!”

Katika shairi la “WASAKATONGE” tunaambiwa kuwa wasakatonge na jua kali ni watu wa hali ya chini sana, wanaofanya kazi duni na ngumu na ndio waliowaweka madarakani viongozi wanaowanyonya na kuwanyanyasa. Wananchi hawa wana hali duni sana kutokana na kutothaminiwa na viongozi wao. Shairi la “WASAKATONGE” halinatofauti na mashairi ya “MVUJAJASHO” (uk.12) na “WALALAHOI” (uk.36-37) kwani yote yanazungumzia matatizo ya watu wa tabaka la chini yanayosababishwa na tabaka la juu. Katika shairi la “MIAMBA” (uk.29-30) na “MUMIANI” (uk.34) tunaona jinsi msongamano wa kitabaka unavyofanana na ule wa shairi la “TONGE LA UGALI.” Katika mashairi haya, wenye nguvu ndio hutawala na kuwanyonya wanyonge kama inavyojishihirisha katika shairi la “MIAMBA” ambalo limetumia taswira ya wanyama katika kuonesha matabaka hayo, kama msanii anavyosema:


1. “Miamba,
Chui na Simba,
Mbugani wanatamba,
Vinyama vinayumba,
Chakula cha wakubwa
Ni sharia za mbuga?”

Hali ilivyo katika jamii yetu haina tofauti na ile ya mataifa tajiri na mataifa masikini, tunaendelea kuambiwa kuwa, mataifa masikini hayana chao mbele ya mataifa tajiri. Kazi ya mataifa masikini ni kutengeneza mipango ya mataifa tajiri kama inavyojionesha katika shairi la “HATUNA KAULI” (uk.8-9)
4. “Maagizo tunapewa,
Mipango tunapangiwa,
Na amri tunapangiwa.”

Mashairi mengine yanayoonesha hali hii ni “WAFADHILIWA” (uk.38) na “KLABU” (uk.50-51). Pamoja na masuluhisho yanayotolewa dhidi ya hali hii kama vile tabaka masikini kuungana na kupambana na hali hii, hasa kati ya nchi lakini bado msanii anawasiwasi juu ya kuondoka kwa hali hii katika jamii yetu. Hii inatokana na maswali anayojiuliza katika mashairi ya “TONGE LA UGALI” na “WASAKATONGE” ambapo msanii anaonesha hali ya kutokuwa na jibu rahisi katika kukomesha hali hiyo.

Pia msanii huyu amedokeza kuhusu mgongano au msuguano wa kiitikadi. Katika diwani hii tunaoneshwa kuwa, hatuna itikadi ya kisiasa inayoeleweka. Tupo kama hatupo na hatuelewi kama bado sisi ni wajamaa au mabepari. Hii inajidhihirisha katika shairi la “TWENDE WAPI” (uk.20-21)


3. “Twende wapi?
Mashariki “siko”!
Magharibi “siko”!
Wapi tuendako?
Tunatapatapa!”

Kutapatapa kiitikadi kunatusababishia tufanye mambo kama vipofu na matokeo yake ni kudaka kila kitu iwe kinachotoka magharibi au mashariki na hivyo kuathiri mfumo mzima wa maisha yetu ikiwemo mmomonyoko wa kimaadili.

UNAFIKI: Katika diwani hii tunaambiwa kuwa baadhi yetu hasa wanasiasa, viongozi au wananchi ni wanafiki wakubwa. Kwani kitendo cha baadhi ya watu kujiona kuwa hawana dhambi ni cha kinafiki kwa sababu, hakuna mwanadamu asiye na dhambi kama shairi la “WASODHAMBI” (uk.1) linavyosema;


2. Wavilemba!
Wavilemba, na majoho, tasibihi,
Wajigamba, safi ni roho, ni kebehe,
Wanotenda,
Unafiki.

Pia hata katika la “MAMA NTILIYE” (uk.17) nalo linadhibitisha hilo.


2. “Majungu na makaango, jinsi unavyoyapika,
Na kibwebwe kiachiye, au utaadhirika,
Kazi hiyo isusiye, hasara sijekufika.”

Diwani hii inaendelea kuonesha unafiki wa watu wa dini kupitia shairi la “UASI” (uk.8) Watu hawa hujidai mbele za watu ni waongofu wakati ni wachafu na wadhaifu katika matendo yao. Hawa ni watu wanaokashifu dini za wenzao kwa kudai kuwa zao ndizo safi na sahihi. Shairi linasema:


“Uasi
Masheikh na masharifu,
Mapadri na maaskofu,
Kauli zao nadhifu,
Hujigamba waongofu,
Wengi wao ni wachafu,
Wenye vitendo dhaifu,
Dini wanazikashifu,
Wanafiki.”

Unafiki wa baadhi ya watu unaendelea kuoneshwa kwenye shairi la “PEPO BILA KIFO” (uk.14) ambapo baadhi yatu hupenda vitu fulani fulani bila kufuata kanuni za upatikanaji wa vitu hivyo. Kitendo cha mtu kupenda pepo bila kuonja mauti ni cha kinafiki. Vilevile kitendo cha kupenda starehe za wanawake ni cha kinafiki kwani peponi si mahali pa kufanyia umalaya bali ni mahali patakatifu. Hivyo afikiriaye mambo haya ni mnafiki kwani hajui neno la Mungu linasemaje kuhusu pepo. Katika kuonesha unafiki shairi hili linasema:


5. “Nibembee na hurulaini,
Wanawake wazuri wa shani,
Wawashindao wa duniani,
Nipumbazike.”

Unafiki mwingine unajionesha katika siasa ambapo baadhi ya viongozi hupata uongozi kwa kujipendekeza na kutoa maneno ya hapa na pale kwa wale wanawapatia hivyo vyeo. Haya tunayapata katika shairi la “WARAMBA NYAYO” (uk.46-47)


1. ‘Wajikomba,
Ili kupata vyeo,
Na uluwa.”

USALITI: Mshairi Mohammed Seif Khatibu ameonesha suala la usaliti katika diwani hii ya WASAKATONGE, kwani tunaambiwa kuwa, mara nyingi tunakuwa pamoja katika safari ya kutafuta kitu fulani lakini pindi kinapopatikana tu tunawatenga baadhi ya watafutaji wenzetu. Haya yanadhihirishwa wazi katika shairi la “SIKULIWA SIKUZAMA” (uk.22-23) ambapo msanii anabainisha kwa kusema kuwa;


1. “Nilitoswa baharini,
Ya dharuba na tufani,
Walitaka nizame,
Wao wanitazame,
Nife maji wakiona,
Waangue na vicheko,
Na kushangilia,
Ushindi wao!”

Usaliti wa aina hii unajitokeza tena katika shairi la “ASALI LIPOTOJA” (uk.37-38), Shairi hili linaweza kufananishwa na hekaheka za kupigania uhuru ambapo baada ya kupata uhuru baadhi ya watu walioshiriki katika kuutafuta uhuru huo, walitengwa kabisa. Lakini pia matunda yaliyotegemewa baada ya uhuru hayajapatikana kwa wote bali kwa watu wachache tu wenye mirija mirefu (viongozi) kama lisemavyo shairi hili:


2. “Mili ikatuvimba,
Ila hatukuyumba,
Tukabakia shambani,
Kutumaini kwamba,
Faida itawamba,
Heri itafika.”


3. “Asali lipotoja,
Wengi walikuja,
Na mirefu mirija,
Kwao kawa tafrija,
Wakapata faraja,
Sisi tukatengwa.”

Katika shairi la “VINYONGA” (uk.49) tunabaini pia usaliti wa wanasiasa kwa wananchi. Shairi hili linaonesha kuwa wanasiasa wanatenda mambo kinyume na maadili na hivyo kuwasaliti wananchi waliowaweka madarakani. Viongozi hawa hawatekelezi yale wanayoahidi kwa wananchi wao badala yake wanatumia nafasi walizo nazo katika kujitajirisha wao wenyewe. Shairi linasema;


2. “Jukwaa,
Meingiliwa,
Wanasiasa vinyonga,
Maisha ya ufahari,
Kauli zao nzuri,
Vitendo vyao hatari,
Ni kinyume na maadili,
Ni usaliti.”

Usaliti mwingine umejitokeza katika mapenzi. Mshairi anasema kuwa alikesha kwa ajili ya kumsubiri wake mahaba, ili baadaye wawe wawili. Hata hivyo mkesha wake haukuzaa matunda kwani mwenzie alimsaliti kwa kutofika katika eneo la tukio kama anavyoonesha katika shairi la “NILIKESHA” (uk.23-24)


4. “Nilikesha,
Na kulikucha sikukuona,
Nathibitisha wako uungwana,
Kosa langu kukupenda sana,
Hustahiki heshima hiyo,
Sisahau sikusamehe,
Nilikesha.”

Pia katika shairi la “SIKUJUA” (uk.28) linaonesha usaliti wa baadhi ya watu. Msanii anasema kuwa, aliyemfuga kwa mategemeo ya kumsaidia mambo mbalimbali amegeuka na kufanya kinyume na mategemeo au makubaliano. Msanii anadhihirisha hili kwa kusema;
4 “Kumbe nimefuga punda, mashuzi ndio heshima,
Ni ukaidi wa inda, mateke kurusha nyuma,
Nyama limekuwa nunda, mfugaji humuuma.”

MAPENZI/MAHABA: Miongoni mwa dhamira ambazo zimezungumziwa kwa kina katika diwani hii ni Mapenzi. Mshairi huyu anaonesha kuwa, mapenzi yana raha yake na pindi yanapokwenda mrama huleta karaha kubwa kwa mtu mmoja au wawili waliofarakana. Mshairi anasema kuwa mapenzi ni kitu muhimu sana kwake na yupo tayari kuitwa jina lolote lile kwa sababu ya kuyathamini mapenzi. Haya tunayapata kupitia shairi la “MAHABA” (uk.1-2)


4. Kama mahaba wazimu, sihitaji nitibiwe,
Bora niwe chakaramu, nipigae watu mawe,
Kuwa kwangu mahamumu, wewe isikusumbuwe,
Dawa yangu siyo ngumu, mimi nipendwe na wewe.

Kwa vile mshairi huyu anaona kuwa mapenzi ndicho kitu cha thamani kubwa kwake ayakosapo au amkosapo yule ampendaye hukonda na kudhoofika mwili kama asemavyo katika shairi la “SILI NIKASHIBA” (uk.17)


2. “Sili nikashiba, nikikukumbuka,
Hula haba, na kushikashika,
Ni chozi za huba, kweli nasumbuka.

Hali ya kupenda kwa dhati inajitokeza katika shairi la “NILIKESHA” (uk.23-24) ambapo mtu anaamua kukesha kwa kusubiri ahadi ya huba ingawa apendwaye huenda hayuko tayari kupenda. Shairi hili linasema;


1. “Nilikesha,
Si kwa ibada au shakawa,
Sio kwa ngoma ama takuwa,
Ila kwa hamu na nyingi hawa,
Ikawa hakupambazuki,
Ni mtekwa wa huba zako.”
Nilikesha.

Katika mashairi ya “USIKU WA KIZA” (uk.27-28) na “MACHOZI YA DHIKI” (uk.28) yanaendelea kuzungumzia hali hiyo ya mapenzi. Katika shairi la “USIKU WA KIZA” tunaoneshwa majonzi ya mpenzi mmoja aliyeondokewa na kipenzi chake. Kutoweka kwa mahabuba wake kunamfanya asile na kushiba kama shairi linavyosema;


2. “Meniondokeya, wangu mahabuba,
Nilikuzoweya, kwa yako mahaba,
Nnajikondeya, sili nikashiba.”

Vilevile katika Shairia la “MACHOZI YA DHIKI” (uk.28) mpenda anabubujikwa machozi kwa kuadimikiwa na wake mahabuba, yaani anateseka kutokana na kuadimika kwa mpenzi wake.

Mshairi anaendelea kutetea mapenzi ya dhati katika shairi la “PEPO TAMU” (uk.35) ambapo anasema kuwa penzi tamu ni penzi lililojaa raha na lina ladha kushinda asali. Pendo tamu hufukuza uchoyo uheka.


4 “Pendo lenye tabasamu, za dhati si za uheka,
Na nyoyo za ukarimu, uchoyo ni sumu yake,
Haliishi yake hamu, hupendi imalizike.”

Kwa kuwa mpendwa anaonesha pendo la dhati, apendwaye pia anatakiwa aoneshe pendo lake kwa kutoa kauli kuhusu kupenda au kutopenda kwake kwa yule anayemtaka. Hii ni katika shairi la “ITOE KAULI YAKO” (uk.27)


1. “Itoe yako sauti, kama, kweli wanipenda,
Niweze kujizatiti, moyo uondoke funda,
Nizidi kukudhibiti, sikuache hata nyanda.”

Shairi hilo linataka mpendwa atoe kauli yake kwani mpenda ameshatoa kauli yake ya upendo kama asemavyo katika shairi la “WEWE WAJUA” (uk.25)


1. “Nakupenda, nawe wajua,
Tusitupane,
Tupendane,
Kwa salama.”

Hali hii pia inajitokeza katika shairi la “NAKUSABILIYA” (uk.23) ambapo msanii anatoa pendo lake lote kwa yule ampendaye kama asemavyo katika ubeti wa kwanza;


1. “Nakusabiliya, pendo lote kwako,
Litaseleleya, litabaki kwako,
Sitaliachiya, kwenda kwa mwenzako.”

Kama apendwaye ataonesha pendo la dhati kwa yule ampendaye basi watalindana na kulifanya pendo lao kuwa la wawili tu kama lisemavyo shairi la “NILINDE” (uk.15)


1. Nilinde sichukuliwe, hata kwa moja shubiri,
Tubaki mimi na wewe, pendo letu linawiri,
Tuwazidishe kiwewe, wasotutakia heri.

Pia hali kama hii itasaidia kudumisha penzi lao milele na milele watabaki wawili peke yao huku wakifurahia pendo lao maridhawa. Haya tunayapata katika shairi la “TUTABAKI WAWILI” (uk.26) na “YEYE NA MIMI” (uk.39). Katika shairi la “TUTABAKI WAWILI”, tunaambiwa kuwa;


2. Hakuna wa kulizima, pendo langu kufifiya,
Litabakia daima, na kwako kuseleleya,
Hadi siku ya kiyama, pendo litaendelea,

Shairi la “YEYE NA MIMI” linadai kuwa penzi tamu na dhati huwafanya watu wawili wapendanao wakeshe katika mapenzi bila kuchoka

4. “Yeye na mimi wawili, hatuna tunobakisha,
Humsabilia mwili, hana anapobakisha,
Ana mahaba ya kweli, usiku kucha hukesha.”

Katika diwani hii tunaambiwa kuwa kama unampenda mtu asiyekupenda basi usimchukui isipokuwa muagane kwa wema pale inapobidi kama inavyojionesha katika shairi la “KWA HERI” (uk.29)


3. Ingawa menisusia kujipa kunigomeya,
Mvua hunyesha masika, masika hukesha,
Hakuna ukame,
Kwa heri.

Diwani hii inaonesha kuwa kukataliwa kimapenzi si mwisho wa dunia bali ni njia mojawapo ya kufunguliwa mlango kwa wengine hasa yule akupendaye kwa dhati. Haya yote tunayapata katika shairi la “NILICHELEWA KUPENDA” (uk.41)


1. Katika uhai wangu, nilichelewa kupendwa,
Waliowakija kwangu, wale wa kunizuzuwa,
Mwaka huu mwaka wangu, nami nimejaaliwa.

Kwa upande wa pili msanii anakemea mapenzi ya sio ya dhati (ulaghai) kutokana na kutokuwa na faida yoyote kwa mtu na kwa jamii kwa ujumla. Mapenzi ya namna hii tunayapata katika shairi la “SI WEWE” (uk.21-22) ambapo msanii anahoji na kumsuta mtu aliyempenda kwa chati. Mapenzi haya hayana faida yoyote isipokuwa mateso makali kwa mhusika au wahusika;



4. Umeshapwelewa baharini,
Wako werevu umekwisha,
Sasa unatweta,
U taabani,
Ni wewe ulo mlafi,
Si wewe?

Msanii anaendelea kusema mapenzi ya chati katika shairi la “WEWE JIKO LA SHAMBA” (uk.44) Hapa msanii anakemea tabia ya watu wanaofanya mapenzi kiholela kuwa waachane na tabia hiyo kwani haina faida isipokuwa karaha na kusutwa. Anaendelea kuwaambia kuwa;

4 Takula wako ujuvi, na mwingi uhayawani,
Upikavyo haviivi, ni vibichi sahanini,
Vitachacha hivihivi, kuozea mikononi.

Watu wa aina hii sharti wajitakase ili wakubalike katika jamii yaani “wayapangue mafiga, jiko halitaivisha” wasipofanya hivyo, hawatapata kitu chochote cha maana kwani wapenzi (wawezeshaji) wamekuwa wengi. Shairi la “BUZI LISILOCHUNIKA” (uk.45)

4 Msumeno utafute, na makali kuyaweka,
Ukwereze na uvute, na watu kukusanyika,
Na hutafika popote, buzi halitachunika.

Kwa ujumla msanii anazungumzia mapenzi ya aina mbili, mapenzi ya dhati ambayo kwake ndio ngao na mapenzi ya chati ambayo huleta karaha tupu katika maisha ya mwanadamu.




Swali.


Soma makala ya M.M.Mlokozi katika jarida la mulika (1989) namba 21 kisha jadili vigezo alivyovitumia katika kugawa tanzu na vipera vya Fasihi Simulizi.

DONDOO:

UTANGULIZI:

Maana ya Fasihi Simulizi

Maana ya tanzu

Maana ya vipera

KIINI:

Kuchambua vigezo alivyotumia Mulokozi katika kugawanya tanzu na vipera vya Fasihi Simulizi.

Kwa mujibu wa Mulokozi katika Mulika namba 21, (1989). Pamoja na kwamba Fasihi ni kongwe lakini kitaaluma bado ni changa kwa sababu ilianza kuchungunzwa hivi karibuni. Hivyo imepelekea kutokuwepo kwa nadharia, marejeo, wala istilahi zenye kutosheleza mahitaji ya taaluma hiyo. Tatizo hili linadhihirika pale tunapoangalia kazi za wataalamu mbalimbali kuhusu tanzu za Fasihi Simulizi. Kwa upande wa nadharia kitabu pekee kinachozijadili tanzu za Fasihi Simulizi kwa urefu ni kitabu cha Ruth Fennegan kinachoitwa Oral Literature in Africa (1970). Kwa upande wa Kiswahili hakuna kitabu kinachojadili uwanja wa tanzu za Fasihi Simulizi. Badala yake kunamiongozo michache kwa ajili ya shule za sekondari kama vile Balisidya, N (1975) na Taasisi ya Elimu (1987)

Mulika namba 21 ni jarida la kitaaluma linalotoa fursa kwa wataalamu, waalimu na wanafunzi katika kujadili mada mbalimbali za kiswahili. Jarida hili lililoandikwa mwaka 1989 ndani yake kuna makala ya Fasihi Simulizi inayohusu tanzu za Fasihi Simulizi na vipera vyake iliyoandikwa na M.M.Mulokozi.

Hivyo basi kutokana na kukosekana kwa nadharia zinazoongoza ugawaji wa tanzu za Fasihi Simulizi ya Kiswahili wataalamu wengi wamekuwa wakitumia vigezo mbalimbali ambavyo ni maudhui, fani, matukio, idadi ya waimbaji, vifaa vinavyotumika na namna ya uimbaji.

Fasihisi Simulizi imejadiliwa na wataalamu mbalimbali miongoni mwa waalamu hao ni M.M.Mulokozi (1996) anasema Fasihi Simulizi ni fasihi inayotungwa au kubuniwa kichwani na kuwasilishwa kwa hadhira kwa njia ya mdomo na vitendo bila kutumia maandishi.

TUKI (2004) Fasihi Simulizi ni kazi ya fasihi inayohifadhiwa na kurithishwa kutoka kizazi kimoja hadi kingine kwa njia ya mdomo kama vile; hadithi, ngoma na vitendawili.

Hivyo basi Fasihi Simulizi ni fasihi inayotokana na maneno ambayo huzungumzwa, hutolewa au kuimbwa ambapo mtungaji na mwasilishaji hutumia sanaa.

Tanzu ni istilahi inayotumiwa kuelezea au kurejelea aina ya kazi mbalimbali za kifasihi. Inawezekana utanzu mkuu kuwa na vitanzu vingine mbalimbali kwa mfano, tanzu kuu za kifasihi ni Riwaya, Tamthilia, Shahiri, Novela, Insha na Hadithi (Wamitila (2003).

Vipera ni dhana inayotumiwa kuelezea vijitanzu katika fasihi hasa fasihi simulizi. Mfano: semi methali, mafumbo, vitendawili nakadhalika. (Wamitila 2003)

M.M.Mulokozi katika makala yake ya tanzu za Fasihi Simulizi iliyo katika jarida la Muulika namba 21(1989) amezigawa tanzu na vipera vya Fasihi Simulizi kwa kutumia vigezo viwili ambavyo ni,kigezo cha kwanza ni umbile na tabia ya kazi inayohusika na kigezo cha pili ni muktadha na namna ya uwasilishaji wake kwa hadhira.

Umbile na tabia ya kazi inayohusika: katika kigezo hiki Mulokozi ameangalia vipengele vya ndani vinavyoiumba sanaa hiyo na kuipa muelekeo au mwenendo. Baadhi ya vipengele hivyo vya ndani ni namna lugha inavyotumika (kishahiri, kinathari, kimafumbo, kiwimbo na kighani), muundo wa fani hiyo na wahusika. Kwa upande wa muktadha na namna ya uwasilishaji amezingatia kuwa, Fasihi Simulizi ni tukio hivyo huambatana na muingiliano wa mambo matatu ambayo ni muktadha, watu na mahali. Mwingiliano huu ndio unaotupa muktadha na muktadha ndio unaoamua fani fulani ya Fasihi Simulizi ichukue umbo lipi, iwasilishwe vipi kwa hadhira, kwenye wakati na mahali hapo. Hivyo hadithi inaweza kugeuzwa wimbo, utendi unaweza kuwa hadithi na wimbo unaweza kugeuzwa ghani au usemi kutegemea muktadha unaohusika (Mulokozi 1989).

Kwa hiyo kwa kutumia vigezo hivi, Mulokozi amezigawa tanzu na vipera vya Fasihi Simulizi kama ifuatavyo;

Masimulizi; hii ni tanzu ya Fasihi Simulizi yenye kusimulia habari fulani. Katika kugawa utanzu huu vigezo vilivyotumika ni pamoja na kigezo cha lugha ambapo lugha inayotumika katika masimulizi ni ya kinathari. Pia kigezo kingine ni kigezo cha muundo, mara nyingi masimulizi huwa na muundo unaojitofautisha na tanzu nyingine kama vile ushairi. Katika masimulizi muundo wake mara nyingi huwa wa moja kwa moja yaani mtiririko wa visa na matukio. Vilevile kigezo kingine ni kigezo cha wahusika ambapo katika kigezo hiki huhusisha wahusika wa pande mbili ambao ni mtendaji na watendwaji. Pia kigezo kingine ni kigezo cha namna ya uwasilishaji. Katika uwasilishwaji huwasilishwa na msimuliaji mbele ya hadhira. Kigezo kingine ni kigezo cha mandhari ambayo huwa maaluma kama vile chini ya mti mkubwa na uwanjani. Masimulizi pia hufanyika katika muda maalum. Mfano, baada ya kazi.

Masimulizi yamegawanyika katika tanzu kuu mbili ambazo ni tanzu za kihadithi (za kubuni) na tanzu za kisalua (kihisitoria). Tanzu za kihadithi zina kipera kimoja ambacho ni ngano. Ngano (vigano/hurafa), hizi ni hadithi za kimapokeo zitumiazo wahusika kama wanyama, miti na watu kuelezea na kuonya kuhusu maisha. Vigezo vilivyotumika katika kugawa ngano ni kigezo cha lugha ambayo ni lugha ya kinathari, kigezo cha dhima ambacho huelezea au kuonya kuhusu maisha na kufurahisha. Kigezo kingine kilichotumika ni kigezo cha wahusika ambao ni wanyama, miti na watu. Kipera hiki cha ngano kinajumuisha vijipera vifuatavyo ambavyo ni istiara, mbazi na kisa.

Istiara; hii ni hadithi ambayo maana yake ya wazi inawakilisha maana nyingine iliyofichika. Vigezo vilivyotumika katika kugawa kipera hiki ni kigezo cha lugha ambayo ni lugha ya mafumbo.

Mbazi; hii ni hadithi fupi yenye mafunzo itolewayo kama kielelezo wakati wa maongezi au kumkanya mtu. Kigezo kilichotumika katika kugawa kipera hiki ni kigezo cha dhima.

Kisa; hii ni hadithi fupi ya kufurahisha kuhusu tukio la kweli. Kigezo kilichotumika ni kigezo cha kidhima.

Utanzu mwingine wa masimulizi ni utanzu wa kisalua. Utanzu huu umegawanyika katika vipera vifuatavyo ambavyo ni visakale, mapisi, tarihi, kumbukumbu na visasili.

Visakale; haya ni masimulizi ya mapokeo juu ya wahenga au mashujaa wa kabila au taifa yenye kuchanganya chuku na historia (kama hadithi ya Liyongo). Vigezo vilivyuotumika hapa ni kigezo cha wahusika ambao wapo katika historia yaani mashujaa fulani. Kigezo kingine ni fani ya ubunifu.

Mapisi; haya ni maelezo ya kihistoria bila kutia mambo ya kubuni. Hapa pia kigezo kilichotumika ni kigezo cha dhima ambacho huelezea mambo ya kihistoria yaliyo ya kweli.

Tarihi; haya ni maelezo au jedwali la matukio muhimu na tarehe zake. Kigezo kilichotumika hapa ni kigezo cha kidhima ambacho ni kuelezea matukio muhimu na tarehe zake. Pia kigezo kingine ni namna ya uwasilishaji ambapo huwasilishwa kwa kutumia jedwali na lugha yake huwa katika maandishi.

Kumbukumbu; haya ni maelezo ya matukio muhimu yanayomuhusu mtu binafsi au jamii ya watu. Hapa kimetumika kigezo cha fani, ambayo ni fani za wasifu na tawasifu. Pia kigezo kingine ni kigezo cha wahusika ambao ni watu.

Visasili; hiki ni kipera kinachofungamana na imani za dini na mizungu ya kajamii pia hizi ni hadithi za kale zenye kuwakilisha imani na mtazamo wa jamii inayohusika kuhusu asili ya ulimwengu na maisha yao. Kigezo kilichotumika ni kigezo cha kidhima ambacho huelezea shabaha ya maisha.

Utanzu mwingine wa Fasihi Simulizi ni utanzu wa Semi. Semi ni tungo au kauli fupi fupi za kisanaa zenye kubeba maana au mafunzo. Kigezo kilichotumika katika kugawa utanzu huu ni kigezo cha lugha ambayo ni lugha ya mkato. Kigezo kingine ni kigezo cha kidhima ambacho ni kufunza.

Utanzu huu umegawanyika katika vipera vifuatavyo ambavyo ni methali, vitendawili, misimu, mafumbo na lakabu.

Methali ni semi fupi fupi zenye kueleza kwa mukhtasari fikra au mafunzo mazito yaliyotokana na uzoefu wa kijamii. Vigezo vilivyotumika katika kipera hiki ni kigezo cha lugha ambayo ni lugha ya mafumbo. Vilevile kimetumika kigezo cha muundo ambapo methali huundwa na muundo wa pande mbili ambazo hutegemeana.

Vitendawili; huu ni usemi uliofumbwa ambao hutolewa kwa hadhira ili ufumbuliwe. Vigezo vilivyotumika ni kigezo cha lugha. Hapa lugha inayotumika ni lugha ya kimafumbo.

Misimu; ni semi za muda na mahali maalum ambazo huzuka na kutoweka kutegemea mazingira maalum. Hivyo vigezo vilivyotumika katika kugawa kipera hiki ni kigezo cha muktadha yaani hutokea wakati maalum na mazingira maalum.

Mafumbo; ni semi za maonyo au mawaidha ambazo maana zake za ndani zimefichika. Kigezo kilichotumika ni kigezo cha kidhima ambacho ni kuonya pamoja na kigezo cha lugha ambayo ni lugha ya mafumbo.

Lakabu; haya ni majina ya kupanga ambayo baadhi ya watu hupewa au hujipatia kutokana na sifa zao za kimwili, kinasaba, kitabia au kimatendo. Kigezo kilicho tumika katika kipera hiki ni kigezo cha lugha ambayo lugha iliyotumika ni lugha kificho yaani maana yake hufichwa.

Utanzu mwingine wa Fasihi Simulizi ni ushairi. Huu ni utanzu wa fasihi simulizi unaowasilishwa kwa hadhira kwa njia ya uimbaji au ughani badala ya usemaji wa kawaida. Vigezo vilivyotumika katika kugawa utanzu huu ni kigezo cha lugha ambayo ni lugha ya kishairi. Pia kimetumika kigezo cha fani ambapo fani inayotumika ni wizani, lugha ya mkato, lugha ya mafumbo na uimbaji au ughani.

Katika utanzu huu kuna vipera viwili ambavyo ni nyimbo na maghani;

Nyimbo ni kila kinachoimbwa. Vigezo vilivyotumika katika kipera hiki cha ushairi ni kigezo cha fani ambapo huangalia muziki wa sauti ya muimbaji au waimbaji, muziki wa ala (kama ipo), matini au maneno yanayoimbwa. Pia kuna kigezo cha muktadha ambacho huzingatia hadhira inayoimbiwa na muktadha unaofungamana na wimbo huo, kwa mfano sherehe, ibada, kilio nakadhalika. Kwa vigezo hivi utanzu wa nyimbo umegawanyika katika vijipera vifuatavyo ambavyo ni, tumbuizo, bembea, kongozi, nyimbo za dini, wawe, tenzi, tendi, mbolezi, kimai, nyiso, nyimbo za vita, nyimbo za uwindaji, nyimbo za taifa, nyimbo za watoto na nyimbo za kazi.

Tumbuizo; hizi ni nyimbo za furaha ziimbwazo kuwafurahisha watu kwenye matukio mbalimbali kama vile ngomani au harusini. Vigezo vilivyotumika hapa ni kigezo cha kidhima ambacho hulenga kuwafurahisha watu, pia kigezo kingine ni kigezo cha kimuktadha ambapo huwasilishwa katika matukio yanayoendana na dhima ya kufurahisha.

Bembea; hizi ni nyimbo za kubembeleza watoto. Kigezo kilichotumika hapa ni kigezo cha kidhima ambapo hulenga kubembeleza watoto.

Kongozi; hizi ni nyimbo za kuaga mwaka. Vigezo vilivyotumika hapa ni kigezo cha kidhima ambapo dhima yake ni kuaga mwaka na kigezo cha kimuktadha ambapo muktadha wake ni muktadha maalum yaani huimbwa mwishoni mwa mwaka.

Nyimbo za dini; hizi ni nyimbo zinazoimbwa kwa lengo la kumsifu Mungu au miungu. Vigezo vilivyotumika ni kigezo cha kidhima ambapo dhima yake ni kumsifu Mungu au miungu, pia kimetumika kigezo cha kimuktadha ambapo huimbwa katika muktadha wa kidini.

Wawe; hizi ni nyimbo za kilimo. Vigezo vilivyotumika ni kigezo cha kimuktadha ambapo huuimbwa wakati wa kulima, pia kigezo cha kidhima kimetumika ambapo dhima yake ni kuchapusha kazi.

Tenzi; hizi ni nyimbo ndefu za kimasimulizi au mawaidha. Kigezo kilichotumika ni kigezo cha kifani ambapo fani yake ni masimulizi au mawaidha.

Tendi; hizi ni nyimbo ndefu za masimulizi juu ya matendo ya mashujaa. Vigezo vilivyotumika hapa ni kigezo cha kifani ambapo wahusika wa tendi ni watu wenye historia za matendo ya kishujaa, pia kigezo cha lugha kimetumika ambapo lugha yake ni ya kinathari.

Mbolezi; hizi ni nyimbo za kilio au maombolezo. Vigezo vilivyotumika katika kugawa kipera hiki ni kigezo cha kimuktadha ambapo huwasilishwa katika muktadha wa maombolezo au kilioni/msibani, pia kimetumika kigezo cha kidhima ambapo dhima yake ni kuomboleza.

Kimai; hizi ni nyimbo zihusuzo shughuli za baharini. Vigezo vilivyotumika hapa ni kigezo cha kidhima ambapo dhima yake ni kuchapusha kazi. Vilevile katika kigezo cha kimuktadha kimai huwasilishwa katika mazingira ya baharini.

Nyiso; hizi ni nyimbo za jandoni. Vigezo vilivyotumika ni kigezo cha kidhima ambapo dhima yake ni kutoa mafunzo kwa vijana kuhusu maisha ya utu uzima. Kigezo kingine ni kigezo cha kimuktadha ambapo nyiso huwasilishwa katika mazingira maalumu, kama vile porini nakadhalika.

Nyimbo za vita; hizi ni nyimbo ziimbwazo na askari wakati wa vita. Vigezo vilivyotumika katika kugawa kipera hiki ni kigezo cha kimuktadha ambapo muktadha wake huwa ni wakati wa vita, na kigezo kingine ni kigezo cha wahusika au waimbaji ambapo waimbaji wake huwa ni maaskari.

Nyimbo za watoto, hizi ni nyimbo waimbazo watoto wakati wa michezo yao. Vigezo vilivyotumika ni pamoja na kigezo cha kimuktadha ambapo huwasilishwa wakati wa michezo ya watoto. Kigezo kingine ni kigezo cha wahusika au waimbaji ambapo waimbaji wake huwa ni watoto.

Nyimbo za uwindaji; hizi ni nyimbo ambazo huimbwa na makundi ya wawindaji wakati wa shughuli au sherehe zao. Vigezo vilivyotumika hapa ni kigezo cha wahusika au waimbaji ambapo huimbwa na wawindaji na kigezo kingine ni kigezo cha kimuktadha ambapo huwasilishwa wakati wa shughuli au sherehe za uwindaji.

Nyimbo za Taifa; hizi ni nyimbo za kisifia Taifa au kabila. Kigezo kilichotumika hapa ni kigezo cha kidhima ambapo dhima yake ni kusifia Taifa au kabila.

Nyimbo za kazi; hizi ni nyimbo zinazoimbwa katika shughuli mbalimbali kama vile, kulima, kutwanga, kusuka, uvuvi, uashi, useremala na kadhalika. Vigezo vilivyotumika hapa ni kigezo cha muktadha wa uwasilishaji ambapo huwasilishwa kulingana na shughali maalumu. Pia kigezo kingine ni kigezo cha kidhima ambapo dhima ya nyimbo za kazi ni kuchapusha kazi.

Maghani; hiki ni kipera cha ushairi kinachotolewa kwa kalima badala ya kuimbwa. Kwa mujibu wa Wamitila (2003) maghani ni istilahi inayotumiwa kuelezea aina ya ushairi ambao hutolewa kwa kalima au maneno badala ya kuimbwa. Vigezo vilivyotumika katika kugawa utanzu huu ni lugha ambayo ni lugha ya kishairi. Pia ametumia kigezo cha wahusika ambapo wahusika wakuu ni binadamu. Hivyo vigezo hivi ndivyo vilivyopelekea utanzu huu kuwekwa kwenye utanzu wa ushairi.

Kipera hiki kina vijipera vitatu ambavyo ni maghani ya kawaida, sifo na maghani masimulizi. Maghani ya kawaida ni kundi ambalo tunaweza kuingiza fani mbalimbali za ushahiri simulizi kama vile ushairi wa mapenzi, siasa, maombolezo, kazi, dini ilimradi unaghanwa katika namna ya uwasilishwaji wake.

Sifo; hizi ni tungo za kusifu ambazo husifu watu, wanyama na mimea. Baadhi ya sifo huwa zinakashifu au kukejeli. Vigezo vilivyotumika katika kugawa kipera hiki ni kigezo cha wahusika, wahusika wake wakuu ni binadamu wanyama au mimea. Kigezo kingine ni muktadha ambao huelezea matukio yaliyopita au yaliyopo. Sifo huwa na tanzu muhimu kama vile vivugo (majigambo), pembezi na tondozi.

Kivugo; hili ni ghani la kujisifia, hutungwa na kughanwa na muhusika mwenyewe. Vigezo vilivyotumika katika kugawa kijipera hiki cha sifo ni lugha, katika lugha zimetumika mbinu kama vile sitiari, mkato, vidokezo, ishara, takriri na vina. Kigezo kingine ni kigezo cha wahusika ambapo wahusika wake wakuu ni binadamu pia kimetumika kigezo cha muktadha ambapo muktadha wake hufungamana na tukio maalum katika maisha ya muhusika, mfano vitani. Vilevile katika kigezo cha uwasilishaji huweza kuwa na masimulizi ndani yake. Muundo wake hutegemea shabaha za mtunzi na jadi ya utunzi anayoiwakilisha hakiandikwi na kutungwa papo kwa papo.

Tondozi; hizi ni tungo za kusifu watu, wanyama au vitu. (Pembezi pia ni aina ya tondozi ambayo imekusudiwa watu wa aina fulani tu). Vigezo vilivyotumika katika kugawa kipera hiki ni kigezo cha wahusika ambao ni wanyama na mimea. Mfano wa wanyama ni kama vile Simba. Kigezo kingine ni lugha ambayo ni lugha ya kishairi.

Ghani masimulizi: hizi ni ghani ambazo hutambwa ili kusimulia hadithi, historia au tukio fulani. Vigezo vilivyotumika kugawa kipera hiki ni pamoja na kigezo cha lugha, lugha inayotumika katika kijipera hiki ni lugha ya kishairi na fani iliyotumika ni kusimulia hadithi/tukio kwa kirefu. Vile vile kuna kigezo cha namna ya uwasilishaji huambatana na ala za muziki mfano zeze na marimba.

Ghani masimulizi ina vipera vinne ambavyo ni rara, ngano, sifo na tendi.

Rara ni hadithi fupi nyepesi ya kishairi yenye visa vya kusisimua, vigezo vilivyotumika katika kugawa kipera hiki ni pamoja na lugha inayotumika, lugha inayotumika katika kipera hiki ni lugha ya kishairi, fani iliyotumika ni fani ya kihadithi ambayo ni hadithi fupi, nyepesi na inavisa vya kusisimua na kigezo kingine ni muktadha wa uwasilishaji ambapo huimbwa au kughanwa ikiambatana na ala za muziki.

Ngano; hizi ni hadithi za mapokeo zitumiazo wahusika kama wanyama, miti na watu katika kuelezea au kuonya kuhusu maisha. Katika kipera hiki kigezo kilichotumika ni muktadha wa uwasilishaji, kwamba huwasilishwa pamoja na ala ya muziki. Ngano huwa ghani masimulizi inapowasilishwa pamoja na ala ya muziki.

Sifo; hizi ni tungo za kusifu, kigezo kilichotumika ni muktadha wa uwasilishaji: sifo huwa ghani masimulizi inapoingiza muziki katika utondozi wake, lugha iliyotumika ni lugha ya kishairi.

Tendi; hizi ni ghani ndefu za masimulizi juu ya matendo ya mashujaa yenye uzito kijamii au kitaifa. Vigezo vilivyotumika katika kugawa kipera hiki ni fani ambayo ni huhusu matukio muhimu ya kihisitoria au ya kijamii. Kigezo kingine ni muktadha wa uwasilishaji, hutungwa na kuwasilishwa papo kwa papo.

Utanzu mwingine wa Fasihi Simulizi ni utanzu wa mazungumzo. Mazungumzo ni maongozi au maelezo ya mdomo katika lugha ya kawaida juu ya jambo lolote lile. Si kila mazungumzo ni fasihi ili mazungumzo yaitwe fasihi lazima yawe na usanii wa aina fulani. Vigezo vilivyotumika katika kugawa utanzu huu ni kigezo cha lugha ambapo lugha iliyotumika ni lugha ya kifasihi. Kigezo kingine ni kigezo cha kimuundo ambapo muundo wake huwa wa kidayalojia.

Utanzu huu wa mazungumzo una vipera vifuatavyo ambavyo ni hotuba, malumbano ya watani, soga, mawaidha na ulumbi.

Hotuba; haya ni mazungumzo ambayo huwasilishwa kwenye vikao rasmi vya kimila, kisiasa au kidini. Vigezo vilivyotumika katika kugawa kipera hiki ni kigezo cha lugha ambapo lugha yake huwa rasmi, sanifu na ya kisanaa. Kigezo kingine ni kigezo cha kimuktadha ambapo hotuba huwasilishwa katika mazingira maalumu kwa mfano katika vikao rasmi au mikutano.

Malumbano ya watani; haya ni mazungumzo yanayozingatia masharti yanayotawala uhusiano wao wa kiutani. Huweza kuwa utani wa kikabila, utani wa mababu au mabibi na wajukuu. Vigezo vilivyotumika katika ugawaji wa kipera hiki ni kigezo cha lugha ambapo lugha huwa ni ya kimafumbo. Kigezo kingine ni kigezo cha wahusika ambapo wahusika huwa na uhusiano wa karibu.

Soga; haya ni mazungumzo ya kupitisha wakati ili kusubiri kitu fulani. Vigezo vilivyotumika katika kugawa kipera hiki ni kigezo cha kidhima ambapo dhima yake ni kupitisha wakati. Kigezo kingine ni kigezo cha lugha ambapo lugha inayotumika siyo rasmi. Vilele kuna kigezo cha muktadha ambapo muktadha wake huwa ni mahali popote.

Mawaidha; haya ni maneno ya maonyo au mafunzo aghalabu huwa ya kidini na yenye muongozo. Kigezo kilichotumika katika kugawa kipera hiki ni kigezo cha kidhima ambapo dhima yake ni kuonya au kutoa muongozo.

Ulumbi; huu ni uhodari wa kuzungumza ambao huwa ni wa kiufasaha na madoido. Vigezo vilivyotumika katika kugawa kipera hiki ni kigezo cha kifani ambapo lugha iliyotumika ni lugha ya kimadoido na kifasaha.

Utanzu mwingine katika Fasihi Simulizi ni utanzu wa maigizo. Maigizo ni michezo ambayo hutumia watendaji wa kuiga tabia na matendo ya watu au viumbe wengine ili kuburudisha na kutoa ujumbe fulani kwa hadhira. Vigezo vilivyotumika katika kutenga utanzu huu ni kigezo cha namna ya uwasilishaji ambapo huwasilishwa kwa kuiga matendo ya watu au wanyama. Kigezo cha kidhima ambapo dhima yake ni kuburudisha, kuelimisha au kuonya. Pia kimetumika kigezo cha mandhari ambapo maigizo huambatana na matukio maalumu kama vile kwenye maadhimisho ya sherehe fulani na katika matukio ya kijamii.

Utanzu mwingine wa Fasihi Simulizi ni utanzu wa ngomezi. Ngomezi ni ile hali ya kupeleka ujumbe kwa kutumia mdundo wa ngoma. Vigezo vilivyotumika katika utanzu huu ni kigezo cha kifaa cha uwasilishaji ambacho ni ngoma. Pia kigezo kingine ni kigezo cha kidhima ambapo dhima yake ni kupeleka taarifa fulani kwa jamii. Mfano taarifa hiyo yaweza kuwa ya msiba, mkutano na kadhalika.

Pamoja na ugawaji huu wa tanzu na vipera vya Fasihi Simulizi uliofanywa na Mulokozi kwa kuzingatia vigezo vyake alivyovitumia, bado ugawaji huu unaudhaifu mkubwa tu. Udhaifu au changamoto za vigezo alivyovitumia Mulokozi ni kama ifuatavyo:-

Vigezo vyote hivi vinaweza kuingiliana; mfano kigezo cha kidhima, kama vile kuonya au kuelimisha huweza kuonekana katika tanzu zaidi ya moja au hata katika vipera mbalimbali.

Pia kigezo cha namna ya uwasilishaji huweza kuingiliana kutoka utanzu mmoja hadi mwingine. Mfano, katika utanzu wa masimulizi na mazungumzo.

Vilevile kigezo cha wahusika; kigezo hiki huweza kuingiliana katika utanzu mmoja na mwingine. Mfano, unaweza kuwa na hadithi yenye wanyama, binadamu, mizimu na kadhalika. Hivyo inakuwa si jambo rahisi kuona tofauti zilizopo.

Kwa kuhitimisha, tunaweza kusema kwamba ni vigumu kuainisha tanzu na vipera vya Fasihi Simulizi kutokana na kwamba, Fasihi Simulizi hubadilika badilika kifani, kimaumbo na hata kimaudhui kwa kutegemea muktadha na namna ya uwasilishaji wake. Kwa mfano ngano iliyopo katika masimulizi ni tofauti na ngano iliyopo katika maghani. Hivyo basi tatizo hili linaweza kutatuliwa kwa kutumia istilahi tofauti katika vipera au tanzu zinazoingiliana.

MAREJEO:

Mulokozi, M. M. (1989). Tanzu za Fasihi Simulizi: Katika Mulika 21. TUKI. Dar es Salaam.

Mulokozi, M.M. (1996). Utangulizi wa Fasihi Simulizi ya Kiswahili. TUKI. Dar es Salaam.

Wamitila, K.W. (2003). Kamusi ya Fasihi, Istilahi na Nadharia. Focus Publications Ltd. Nairobi.

TUKI, (2004). Kamusi ya Kiswahili Sanifu. (Toleo la Pili). East Africa: Oxford University Press na Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili (TUKI).




Hakuna maoni:

Chapisha Maoni