Subcribe to our RSS feeds Join Us on Facebook Follow us on Twitter Add to Circles

Alhamisi, 12 Juni 2014

AINA YA LUGHA YA MAZUNGUMZO KWA KUZINGATIA MUKTADHA MBALIMBALI.



MAANA YA LUGHA.


Lugha ya mazugumzo ni maongezi ya watu wawili au zaidi bila kutumia maandishi. Lugha ya mazungumzo ambayo ndiyo lugha kongwe zaidi ya lugha ya maandishi ina dhima kubwa ya kufanikisha mawasiliano miongoni mwa watu au kikundi fulani. Lugha hii ya mazungumzo ilianza punde tu binadamu alipoanza kukabiliana na mazingira yake, hivyo kimsingi lugha ya mazungumzo ndiyo nguzo kuu ya kufanikisha shughuli zote za kibinadamu kutokana na nafasi yake kimatumizi.


Aina ya lugha ya mazungumzo kwa kuzingatia mazingira rasmi na yasiyo rasmi:

Mazingira rasmi: kwa mujibu Kihore (2004) haya ni yale mazingira yanayoendana na kaida za kijamii, kisheria na kiutamaduni ambazo huhusisha matumizi ya lugha iliyosanifu. Huu ni muktadha unaohusisha ushirika wa upande mmoja, kama vile msamiati wa kiufundi na adabu maalum. Mfano wa mazingira rasmi ni kama vile ofisini, mahakamani, bungeni, kanisani, msikitini na katika elimu. Katika mazingira rasmi tunapata aina mbili za lugha ya mazungumzo ambazo ni jagoni na rejesta.

Jagoni: ni aina mojawapo ya lugha inayotumika katika taaluma fulani mahususi kama vile fasihi, isimu, sheria, sayansi, uhandisi, biashara nakadhalika. Hii ina maana kwamba, lugha hii itafahamika na wale tu walioko katika taaluma husika au wenye maarifa ya taaluma hiyo. Kwa mfano wanaisimu hutumia maneno kama vimadende, vitambaza, vipasuo kwamizi nk. wakirejelea jinsi ya utamkaji wa aina fulani za sauti katika lugha.

Rejesta: Halliday (1989), anafasili rejesta kama mtindo wa lugha kutegemeana na kazi au shughuli. Vilevile fasili hii inaendana na fasili ya Habwe na Karanja (2007).

Kwa ujumla tunaweza kufasili rejesta kama mtindo wa lugha kutegemeana na kazi fulani, muktadha wa matumizi, lengo na uhusiano wa wanaowasiliana. Katika muktadha rasmi rejesta hurejelea upande mmoja kama vile, msamiati wa kiufundi, adabu maalum na matumizi ya lugha fasaha, mfano katika elimu, mahakamani nakadhalika.

Mazingira yasiyo rasmi: haya ni mazingira ambayo hayafungwi na kaida, sheria na tamaduni za kijamii. Mazingira haya hutumia msamiati ambao si rasmi yaani lugha isiyokuwa sanifu. Katika mazingira haya tunapata aina zifuatazo za lugha ya mazungumzo: misimu, agoti, rejesta na lahaja.

Misimu: Msanjila na wenzake (2009:19) wanafasili dhana ya misimu kuwa ni aina ya misemo katika lugha ambayo huzuka na kutoweka. Sifa kuu ya misimu ni kwamba haidumu muda mrefu na sio lugha sanifu, na watumiaji wa misimu huwa ni kikundi cha wazungumzaji wa lugha katika jamii ambao kimsingi huishi katika eneo moja.

Ngure (2003:147) anaonekana kukubaliana na Msanjila kwa kiasi kikubwa isipokuwa yeye anaweka mkazo zaidi hasa pale anapodai kwamba, uzukaji wa misimu ni wa ghafla na wakati fulani hufuatana na mambo au matukio maalum ya wakati au msimu huo. Anaendelea kufafanua kuwa misimu huzuka/huibuka na kutokeweka kufuatana na hali mbalimbali za kimazingira. Hata hivyo baadhi ya misimu hudumu na kuwa sehemu ya lugha. Kwa mfano neno matatu (Kenya) au daladala (Tanzania) ni neno lililotumika kurejelea nauli iliyolipwa miaka ya sitini. Hivi leo limekuwa neno linalomaanisha aina fulani ya magari ya usafiri. Katika muktadha wa mazungumzo misimu inachukuliwa kama ni aina mojawapo ya lugha ya mazungumzo itumiayo maneno yanayozuka kutokana na matukio mbalimbali ya kijamii, ambayo hiibuliwa na makundi mbalimbali katika jamii, hivyo misimu hutofautiana baina ya kundi moja na jinguine. Kwa mfano, misimu wanayotumia vijana ni tofauti na wanayotumia wazee au yanayotumia wanaume ni tofauti na wanayotumia wanawake.

Vilevile hata mazingira inamotumika misimu si mazingira rasmi kutokana na maneno yake kuzuka na kutoweka na hayatumiwi katika mazingira rasmi.

Agoti: ni lugha itumiwayo na kundi fulani la wahalifu au watu ambao wanaficha uovu wao usifahamike katika jamii wanamoishi. Mara nyingi lugha hii hutumiwa katika mazingira yasorasmi na kikundi kidogo cha watu kama vile, madereva wa magari, watumiaji wa madawa ya kulevya (mateja), majambazi, vibaka na wahuni wa mtaani. Mfano wa agoti inayotumiwa na watumiaji wa madawa ya kulevya ni kama vile, ndumu – bangi, sherehe ilikuwa na waalikwa wengi – soko la madawa ya kulevya lilikuwa na wateja wengi. Rejesta: Katika mazingira yasiyo rasmi, rejesta hutumia msamiati usio rasmi, matumizi ya misimu na ukatizaji wa maneno pamoja na udondoshaji wa baadhi ya vipashio katika maneno. Mfano, rejesta inayotumika katika mazingira yasiyorasmi kama vile mgahawani au hotelini ni kama vile nani wali ng’ombe? Ikiwa na maana kwamba nani aliyeagiza wali na nyama ya ng’ombe.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni