CHUO KIKUU CHA ARUSHA
KITIVO CHA FANI NA SAYANSI ZA JAMII
MUHTASARI WA SOMO LA SARUFI YA KISWAHILI NA SINTAKSIA
Msimbo wa somo:KISE 330
Jina la somo: SARUFI YA KISWAHILI NA SINTAKSIA.
IMEANDALIWA NA STEPHEN MANYAMA CHARLES UOA.2012-2015.
Uzito wa somo: Credit 3
Hadhi ya somo: Lazima
Ufafanuzi wa kozi.
Kozi hii itachunguza nadharia kadha za sintaksia. Awali tutaanza na ubainishaji wa kategoria za maneno tukizingatia umuhimu wake katika sintaksia na muundo wa virai au sentensi. Kozi hii itazingatia zaidi nadharia za msingi za sintaksia kama vile sarufi miundo virai, sarufi zalishi, Nadharia ya ungoekaji na uambatishaji (government and binding). Katika kozi hii virai na sentensi vitachanganuliwa ili kubaini miundo yake.
Malengo ya kozi
Katika kozi hii wanafunzi wanatarajiwa kufanya yafuatayo:
a) Kuelewa maana ya sintaksia
b) Kutambua kategoria kuu na kategoria ndogo za sintaksia
c) Kueleza umuhimu wa kategoria za sintasia katika kujifunza sintaksia
d) kufahamu nadharia mbalimbali za sarufi miundo:Sarufi miundo virai, sarufi patanishi na uteuzi na nadharia X-bar
e) kuchanganua sentensi kwa mujibu wa nadharia za sarufi miundo
Maudhui ya kozi
1.0 Maana ya lugha na sarufi
Lugha ni nini?
Lugha ni mfumo wa sauti za nasibu zinazotumiwa na watu ili kupashana habari
Sarufi ni nini?
Sarufi ni mfumo wa kanuni za lugha zilizo katika ubongo wa mzawa wa lugha
ambazo humwezesha kutunga sentensi zisizo na kikomo ambazo hukubalika na wazawa wa lugha wanaoifahamu lugha hiyo barabara
2.0 Umilisi na utendi wa lugha
a) Umilisi ni uwezo wa kuzungumza lugha kwa ufasaha alio nao mtu unaotokana na yeye kuzifahamu vilivyo kanuni za kisarufi hata kumwezesha kuzalisha tungo nyingi zisizo na kikomo.
b) Utendi ni utumiaji wa lugha katika mazingira halisi ambao huweza kuathiri maana za maneno kulingana na matumizi yake au na mambo yanayomhusu mzungumzaji mwenyewe k.v. kutokuwa makini au kukosa kumbukumbu, kuongea akiwa amekasirika, kasoro za ala za sauti k.v. mapengo, kigugumizi n.k.
3.0 Tungo za Kiswahili na Vipengele vyake
Lugha ya Kiswahili ina tungo na vipengele mbalimbali kama zilivyo lugha nyingine. Tofauti yake na lugha nyingine zisizohusiana k.v. Kiingereza au Kimasai ni kwamba huhitilafiana katika uundaji wa maneno na mpangilio wa maneno katika tungo. Mathalani, wingi katika Kiingereza hudhihirika mwishoni mwa nomino ilihali katika Kiswahili na lugha dada za Kibantu huonekana mwanzoni mwa nomino. Isitoshe, kivumishi katika Kiswahili hufuata nomino, lakini katika Kiingereza hutangulia nomino. Kwa hivyo japokwa lugha zote zina maneno, virai,vishazi na sentensi, kila moja ina miundo na vipengele vya kisarufi tofauti na lugha nyingine.
4.0 Kauli za vitenzi na aina zake
Kauli ni uhusiano ulipo baina ya kiima na kitenzi (mtenda) au kiima kitenzi
na yambwa (mtenda)
Aina za kauli
Kauli ya kutenda, kutendwa, kujirejea, kutendana, kutendeka,
5.0 Sentensi na aina zake
Sentensi ni kifungu cha maneno chenye maana kamili chenye muundo wa kiima na kiarifu
a) Sentensi sahili
Sentensi sahili ni tungo yenye mana kamili inayoundwa na KN + KT, na ambayo KT ndicho muhimu katika tungo kwani chaweza kusimama peke yake.
Miundo ya Sentensi sahili:
i) Muundo wa kirai kitenzi (KT)
ii) Muundo kirai nomino na kirai kitenzi (KN+KT)
iii) Uchanganuzi wa sentensi sahili
b) Sentensi ambatani
Hii ni sentensi ambayo hundwa na vishazi huru viwili au zaidi kwa kuunganishwa na viunganishi na, lakini n.k.
Miundo ya sentensi ambatani
i) Miundo yenye vishazi sahili
ii) Miundo yenye vishazi sahili + changamani
iii) Miundo yenye vishazi changamani pekee
iv) Miundo yenye vishazi visivyokuwa na viunganishi
v) Uchanganuzi wa sentensi ambatani
c) Sentensi changamani
Hii ni sentensi yenye kuundwa na kishazi huru na kishazi tegemezi
Miundo ya sentensi changamani
i) Miundo yenye vishazi rejeshi
ii) Miundo yenye vishazi – vielezi
iii) Uchanganuzi wa sentensi changamani
6.0 Kategoria za kisarufi
Kategoria ya kisarufi ni kundi la maneno lenye sifa za kisarufi zinazofanana.
Kwa mfano, mtoto, embe, kiti, mti n.k. ni maneno ya kategoria
nomino kwa sababu yana sifa shirika. Maneno ya kategoria moja ya kisarufi yana sifa za kisemantiki, kimofolojia au kisintaksia zinazofananana ambazo ziwapo katika tungo hujaza nafasi karibu ileile.
Nomino – hutaja jina la kitu, huwa mtenda au mtendwa katika sentensi,
huweza kuwa katika umoja au wingi. Kwa mfano: mtoto – watoto, kitu – vitu, embe –maembe.
Kitenzi – huonyesha tendo au hali ya kufanyika kwa kitu. Kwa mfano: cheza, imba, kimbia.
Kivumishi – hueleza sifa ya kitajwa ambacho ni nomino. Kwa mfano: dogo, zuri
Aina nyingine za maneno ni pamoja na kielezi, kiunganishi, kihusishi n.k.
Aina za maneno hutumika kubainisha aina za virai kwani jina la kirai hutokana na kategoria ya kisarufi ya neno kuu.
7.0 Maana ya sintaksia
Sintaksia ni tawi la isimu ambalo linahusu namna maneno yanavyoungana na kuhusiana katika kirai au sentensi. Sintaksia inachunguza namna maneno yanavyojipanga katika sentensi kwa kuzingatia kanuni za sarufi ya lugha husika.
8.0 Mikabala tofauti ya Sintaksia
Uchambuzi wa muundo wa lugha umefanywa na wanasarufi wa nyakati tofauti na kuzua mikabala tofauti kuhusu muundo wa lugha kama walivyouona kwa wakati wao. Mkabala wa awali uliokuwa umejikita katika lugha kongwe kama Kilatini ulikuja kujulikana baadaye kama wa kimapokeo kwani ndio uliorithishwa kutoka kizazi hadi kizazi na kutumika kuchambua
lugha nyingine za dunia. Mkabala mwingine ni ule ulioichambua lugha kwa kuzingatia vijenzi vinavyounda sentensi na ulioasisiwa na Chomsky. Mkabala huu ulijulikana kama mkabala wa kimuundo ambao hata hivyo baadaye ulifanyiwa marekebisho zaidi na mwenyewe Chomsky na waliomfuata.
8.1 Mkabala wa Kimapokeo
Wanamapokeo walichambua sintaksia ya lugha kwa kuainisha miundo ya sintaksia iliyo katika lugha. Kwa mujibu wa wanamapokeo, virai na sentensi zimeundwa na kategoria za kisarufi yaani maneno ambayo kila moja liliainishwa na uamilifu wake kutajwa. Kwa hivyo mwanaisimu alichambua sentensi kwa:
a) kutaja kategoria za kisarufi za maneno yanayounda sentensi
b) kueleza kazi au uamilifu wa kila neno lililounda sentensi.
Kwa mfano: ‘Mama anapika chakula’.
Sentensi hii ilichambuliwa kwa kueleza:
Muundo: Sentensi hii inaundwa na maneno matatu: ‘mama’, ‘anapika’ na ‘chakula’ na kwamba kila neno lina kategoria yake
Kategoria za maneno yanayounda sentensi: ‘mama’ na chakula’ ni nomino za umoja, na ‘anapika’ ni kitenzi kilicho katika wakati uliopo.
Uamilifu wa kila neno: ‘Mama’ ni kiima, ‘anapika chakula’ ni kiarifu.
Aina ya sentensi: Sentensi hii ni kishazi. Hii ni sentensi arifu.
Aidha wanamapokeo walichambua sentensi kwa kubainisha kategoria za maneno yaani aina za maneno kwa mujibu wa maana zake, vipengele vya kimofolojia na au tendo.
Nomino ilifafanuliwa kuwa ni jina la kitu, mtu, mnyama, hali. Nomino huweza kuhesabika au kutohesabika na kwamba huwa na umoja na wingi au umoja tu au wingi tu.
Kitenzi kilifasiliwa kuwa ni neno lenye kudokeza tendo ambalo huchukua viambishi vya wakati uliopo, uliopita au ujao, mtenda ambaye huwakilisha kiima katika kitenzi , mtendwa n.k. Katika sentensi kitenzi hufuata kiima ambacho ni nomino mtenda au kufuatwa na nomino mtendwa au yambwa. Kwa hivyo sentensi ‘ Mama amelala’ ingechambuliwa hivi:
Sentensi hii ina nomino ‘mama’ ambayo ina uamilifu wa kiima cha sentensi yaani mtenda na kitenzi ‘amelala’ chenye uamilifu wa kiarifu cha sentensi. Kitenzi hiki ni sielekezi.
8.2 Mkabala wa wanamiundo kama ulivyoasisiwa na Noam Chomsky
Nadharia ya Sintaksia ambayo mwasisi wake ni Noam Chomsky imejaribu kueleza vipengele vya kisintaksia vya lugha mbalimbali ili kuonyesha jinsi lugha mahsusi zinavyopanga maneno yao ili kupata sentensi.
Lengo la Chomsky katika uchanganuzi wake wa lugha ni kuunda nadharia ya sintaksia ya jumla itakayonyesha vipengele vya kisintaksia vinavyopatikana katika kila lugha na jinsi vinavyotofautiana. Hii inafahamika kama nadharia ya sarufi ya jumla.
Lengo lingine la Chomsky ni kupinga mtazamo wa wanaisimu wa miaka 1950 (wanamapokeo) waliodai kuwa tofauti za lugha hazina ukomo, mtazamo ambao hakuuafiki kwani ulimaanisha kuwa ingebidi kila lugha iwe na nadharia yake. Alidai kuwa tofauti baina ya lugha ni ndogo na kwamba nadharia ya sarufi ya lugha ingeweza kujumuisha lugha zote isipokuwa kwa tofauti ndogondogo tu. Alibainisha kategoria za virai kuwa ni: KN, KT, KV, KE, KH, KU.
9.0 Sarufi miundo virai
Muundo ni mpangilio wa vitu vidogo vilivyowekwa pamoja na kujenga kitu
kikubwa zaidi.
Sarufi miundo virai ni mkabala wa kuchambua lugha kwa kuigawa sentensi katika virai vinayoiunda na kisha kuvichanganua zaidi hadi kufikia neno moja moja lililokiunda kirai.
Tungo huundwa na viambajengo kwa utaratibu maalumu.Tungo za lugha ni neno, kirai, kishazi na sentensi. Virai, vishazi na sentensi huundwa na maneno.
10.0. Muundo wa kirai na sentensi
Kirai, kishazi na sentensi ni vipashio vya lugha vinavyoundwa na viambajengo ambavyo ni vidogo kuliko vyenyewe. Kirai hujengwa na maneno, na kishazi na sentensi hujengwa na virai. Viambajengo vya tungo ndivyo vinavyofanya muundo wa tungo husika.
10.1 Muundo wa Kirai
Kirai ni fungu la maneno yanayohusiana kimuundo lisilokuwa na muundo wa kiima kiarifu. Maneno katika kirai humilikiwa na neno moja ambalo ndilo neno kuu. Kirai hubainishwa na kategoria ya neno kuu. Kwa mfano: KN, KT, KV, KE KH n.k.
Virai huundwa na viambajengo. Kiambajengo ni kikundi cha maneno au hata neno moja pia inayofanya kazi kama kitu kimoja. Kirai, kishazi au sentensi ni mkusanyiko wa viambajengo kadha.
Kirai ni mkusanyiko wa viambajengo vilivyojengwa kuzunguka neno kuu. Kwa mfano, KN huundwa na nomino na vivumishi vyake, kwa hivyo muundo wa kirai ni maneno yanayokiunda yakiwakilishwa na alama za kategoria za maneno hayo.
Kwa mfano: a) ‘Mtoto mdogo’.
Hiki ni Kirai Nomino (KN) kilichoundwa na N (nomino) na V (kivumishi).
Kwa hivyo KN N+V
b) ‘analima shamba’.
Hiki ni kirai kitenzi (KT) chenye kuundwa na kitenzi (T) na kirai nomino (KN). Kwa hivyoKT T+KN
10.2 Aina za Virai na sifa ya kila moja
a) Kirai Nomino
b) Kirai Tenzi
c) Kirai Vumishi
d) Kirai Elezi
e) Kirai Husishi
f) Kirai Unganishi
11.0 Muundo wa Vishazi na Sentensi
Kishazi ni kikundi cha maneno kilicho ndani ya sentensi chenye muundo wa
kiima na kiarifu. Kishazi kina muundo sawa na sentensi.
11.1 Aina za vishazi na miundo yake
a) Vishazi ambatani
b) Vishazi tegemezi
11.2 Sentensi na Miundo yake
Sentensi ni kikundi cha maneno chenye maana iliyo kamili. Sentensi ndicho kipashio lugha cha kimuundo ambacho ni kikubwa kuliko vipashio vingine. Vipashio vya lugha ni pamoja na: mofimu, neno, kirai, kishazi na sentensi yenyewe. Sentensi na kishazi huundwa na virai vikuu viwili: KN na KT. KT yaweza kuundwa na kitenzi na nomino, kitenzi na kielezi n.k.
Kwa hivyo S- KN + KT
Sentensi na upatanishi wa kisarufi
12.0 Sarufi geuza umbo zalishi
Nadharia geuza umbo zalishi huonyesha ujuzi alionao mzungumzaji ambao humwezesha kutunga sentensi sahihi na zisizo na kikomo. Uwezo wa mzungumzaji kutunga sentensi zisizo na ukomo unatokana na kufahamu kanuni za kutunga sentensi sahihi ambazo mzawa wa lugha anazijua kutokana na kuwa na umilisi na lugha yake. Kanuni za kutunga sentensi sahihi hubainisha sentensi sahihi na zisizo sahihi.
Kwa mujibu wa nadharia hii, sentensi ina umbo la nje ambalo ndilo linalojitokeza katika usemaji na hata inapoandikwa, na umbo la ndani ambalo huwa limefichika na hujidhihirisha katika umbo jingine wakati wa kuongea (maana).
Nadharia hii imeweza kuonyesha uhusiano wa tungo ambazo japo zilikuwa na umbo la nje tofauti, zina umbo la ndani sawa.
Kwa mfano:
a) Juma anacheza mpira
b) Mpira unachezwa na Juma
S
KN KT
T KN
Juma anacheza mpira
S
KN KT
T KU
N U KN
Mpira unachezwa na Juma
Mfanano wa tungo hizi umekitwa katika maana. Japokuwa sentensi a) inaanza na Juma, na ile b) inaanza na Mpira, mtenda na mtendwa katika sentensi zote ni yule yule.
Mchakato wa kubadili umbo la nje la sentensi a) na kuwa b) umesababisha uchopekaji wa kiunganishi ‘na’ na kiambishi tendwa ‘w’ katika kitenzi ‘cheza’.Kanuni geuzi tendwa ndiyo iliyotumika kuingiza mabadiliko haya.
Sentensi yaweza kubadilishwa kutoka umbo moja hadi jingine
Kwa mfano:
c) John anafanya mtihani na Maria anafanya mtihani
d) John na Maria wanafanya mtihani
Umbo la nje la tungo hizi ni tofauti lakini umbo la ndani ni sawa. Tungo d) imedondosha baadhi ya maneno yaliyo katika c).
Kanuni ya udondoshaji imetumika kudondosha ‘anafanya mtihani’ ambayo imerudiwa katika sentensi c).
Kanuni ya kubadilishana viambishi idadi imetumika kubadili idadi ya mtenda kutoka umoja ‘a- ya ‘anafanya’ iliyotumika kwa John na Maria kila mmoja peke yake, na kuingiza kiambishi cha wingi: ‘wa- ya ‘wanafanya’
13.0. Sarufi miundo virai zalishi
Katika sarufi miundo virai zalishi muundo wa sentensi huelezwa kwa kuchanganua vijenzi vyake ambavyo ni viambajengo. Viambajengo hivi huchanganuliwa hadi kufikia neno moja ambalo hubainishwa kwa kategoria yake ya kisarufi. Uchanganuzi huu wa sentensi huelezwa kwa kanuni ambazo huwezesha kutunga sentensi nyingi zaidi.
13.1 Kanuni za muundo virai.
a) KN N --- mtoto
Hii ina maana kuwa KN ina N (yaani Kirai Nomino kina kiambajengo kimoja tu ambacho ni nomino). Hii yaweza pia kuelezwa hivi:
KN
N
Mtoto
Hii ina maana kuwa kirai hiki ni neno moja. ‘mtoto’
Kirai chenye viambajengo zaidi kimoja, yaani chenye maneno zaidi ya moja
huelezwa kwa kanuni:
KN N V au
KN
N V
Mtoto mzuri
Hii ina maana kuwa KN kinaundwa na maneno mawili, yaani ‘mtoto mzuri’
Vivyo hivyo kwa Kirai kitenzi (KT)
b) KT T anakula
Hapa tunaona kuwa KT ina T yaani ina kiambajengo kimoja tu ‘anakula’. Hii inaweza kuelezwa kwa njia ya matawi pia.
KT
T
Anakula
Iwapo KT ina viambajengo viwili, muundo wake huelezwa hivi:
KT T KN. Muundo huu unaelezeka pia kwa njia ya matawi hivi:
KT
T KN
N
anakula chakula
Vivyo hivyo kwa:
c) KV V au KV V E,
KV
V E
mdogo sana
d) KE E au KE E E
KE
E E
polepole mno
e) KH H au KH H KN
KH
H KN
kwa haraka
13.2 Kanuni za msingi za miundo virai
Kanuni za miundo virai hujidhihirisha katika sentensi. Sentensi ifuatayo
huchanganuliwa kwa kuzingatia kanuni za miundo virai.
‘Mama amepika chakula kingi sana
S----- KN KT
S
KN KT
KN KE
N T N V E
Dada amepika chakula kingi sana
1. S ----------- KN KT
2. KN --------- N V
3. KT --------- T KN KE
4. KE --------- E
5. T ----------- pika
6. N ----------- dada, chakula
7. V ----------- kingi
8. E ----------- sana
9. H ----------- kwa
Katika kategoria zilizokuwa ndani ya Kiswahili ni neno la kategoria gani huchagua kategoria ipi? Makala haya yatajadili maana ya kategoria, yataainisha kategoria mbalimbali za maneno kwa mujibu wa wataalamu, yatajadili kategoria gani huchagua kategoria ipi katika tungo za Kiswahili, yatabainisha sababu zinazopelekea kategoria kuchaguana na kujaribu kuunda kanuni mbalimbali na hatimaye kuhitimisha. Kategoria za maneno ni aina za maneno kadri ya uainisho wake kutegemeana na sifa za maneno husika kuwekwa katika kundi moja. Mfano Kategoria ya Nomino, Kategoria ya vitenzi, kategoria ya vivumishi. Kwa mujibu wa Kamusi ya Kiswahili Sanifu (2004) maneno yameainishwa katika makundi nane. Makundi hayo ni Nomino, Kitenzi, Kivumishi, Kiwakilishi, Kielezi, Kihusishi, Kihisishi na Kiunganishi. Ambapo kategoria hizi zimepangwa kulingana na sifa za maneno yanayoingia ndani yake. Kihore na wenzake (2003) wanaainisha kategoria saba za maneno nazo ni nomino, vitenzi, vivumishi, viwakilishi, viunganishi, vielezi na viingizi. Kwa pamoja wataalam hawa wanakubaliana kuwepo kwa kategoria za maneno ingawa wanatofutiana katika idadi ya aina za kategoria.Tofauti hizi zinatokana na baadhi ya maneno yanaonekana kutoingia katika kategoria zilizoainishwa. Kwa mfano kategoria ya maneno kama kwa, la, cha, vya na wa kwa mujibu wa Kihore na Wenzake (2003) yanaonekana kuwa viunganishi lakini tukiangalia dhima yake katika lugha ni kuhusisha aina za maneno mengine ambayo ni ya kategoria tofauti au kategoria finyu tofauti. Vile vile tatizo linajitokeza pale ambapo maneno haya yanapofanya kazi tofauti tofauti katika lugha katika kigezo cha semantiki. Maneno ya lugha mfano neno na linafanya kazi kama kiunganishi na pia kama kihusishi. Hebu tuangalie mifano ifuatayo; Mifano: i) baba na mama ii) Amepigwa na Johari Katika tungo ya kwanza neno “na” limefanya kazi kama kiunganishi na katika tungo ya pili limefanya kazi ya kuhusisha kitenzi amepigwa na nomino Johari. Kwa kuliona tatizo hilo Kamusi ya Kiswahili Sanifu ikaamua kuongeza aina ya nane ya maneno yaani Kihusishi. Tatizo lingine linajitokeza katika baadhi ya maneno hususani kihisishi mara nyingine hutokea katika umbo la Kirai hususani kirai nomino, Mfano Mungu wangu! Mtume! Yesu! Maneno hayo huweza kubainishwa kama vihisishi ingawa ni nomino. Mwingiliano huu ndiyo unaoleta matatizo katika taaluma ya sintaksia, na ipo haja ya kufanya uanishaji wa aina za maneno tena au tukubaliane kuwa baadhi ya maneno ya tabia ya kughairi kanuni za lugha. Sanjari na hilo neno aina ya kitenzi kimekuwa na tabia ya kubadili maana za tungo kadri kinavyonyambulishwa. Kitenzi kinabeba dhima ya mufidi, ufanyizi, unyume, uambatani, mwao kwa uchache kwa mujibu wa Khamis (2008). Kutokana na kitenzi nomino huzalishwa kwa sababu hiyo twaweza kusema bado tunahitaji mchakato utakaotuwezesha kutafuta ufumbuzi wa mwingiliano wa aina hizi. Ingawa kuna mwingiliano huo lakini ni jambo la msingi kuangalia uhusiano wa maneno katika taaluma ya sintaksia . Katika kubaini uhusiano huo tunaangalia neno la kategoria gani huchagua kategoria nyingine, hatua ya kwanza tunaweka vikundi mbalimbali vya maneno ambavyo huashiria kuwepo kwa uhusiano wa karibu wa baadhi ya maneno. Wataalam mbalimbali wamebainisha vikundi vya maneno hayo. Habwe na Karanja (2007:154) wanaainisha maneno katika makundi matatu ambavyo ni kundi Nomino (KN), kundi tenzi (KT) na kundi husishi (KH). Chomsky na Halle (1968:08) wao wanachanganua tungo sentensi kwa kuainisha fungu Nomino (KN) na fungu Tenzi (KT). Hii ina maana kwamba wanatambua kuwepo kwa kundi na hivyo kuona kuwa maneno yanachaguana. Katika mjadala huu maneno yanawekwa katika makundi yafuatayo; Kikundi Nomino (KN), Kikundi kitenzi (KT), Kikundi husishi (KH), Kikundi vumishi (KV) na Kikundi elezi (KE). Katika ugawaji wa makundi haya neno linalotawala maneno mengine hukipatia jina kikundi hicho, mfano katika kundi nomino lifuatalo; Baba mdogo katika kikundi nomino hiki neno Baba linatawala neno mdogo, nomino baba inatawala kivumishi mdogo. Kwa kuchunguza vikundi hivyo vya maneno, tunaweza kugundua kuwa kategoria zina tabia ya kuchaguana. Jambo la kujiuliza ni kwa nini kategoria huchaguana? Kategoria huchaguana kwa sababu zifuatazo: Sababu ya mofo-sintaksia, Katika sababu hii tunazingatia mahusiano ya maumbo ya maneno yanavyopelekea kuchaguana. Msisitizo unawekwa katika upatanisho wa kisarufi unavyoruhusu kategoria anuai kuchaguana. Wazo hili pia limeelezewa na Khamisi kupitia kazi ya Steere (1870) anaeleza kuwa alijishughulisha na kupata maana tu iletwayo na umbo au sauti, hivyo ikafaa kuitwa Maelezo ya Sauti – maana. Pia Khamisi anaeleza “Mchango wa Steere tunaweza kusema kuwa wa kimofolojia na elezi bila kuwa na ufafanuzi” Mfano: Mtoto mzuri N V Kitoto kizuri N V Vitoto vizuri N V Kwa hivyo katika data hiyo hapo juu, maumbo ya maneno yamesababisha kuchaguana kwa maneno hayo. Pia katika data ifuatayo utagundua kuwa maumbo ya maneno pia yanaweza sababisha kutochaguana kwa maneno; Mtoto kizuri Kitoto mzuri Vitoto kizuri Ukichunguza data hiyo unagundua kuwa maneno hayo hayawezi kuchaguana, kwani maumbo ya maneno hayo hayaruhusu viambishi awali katika maneno yanayofuata. Khamis (2008:4), anaeleza juu ya unyambulishaji usio na mipaka na unyambulishaji wenye mipaka. Hii inaonesha kuwa ni sababu nyingine ya kategoria ya maneno kuchaguana. Pia Guthrie (1962:203) kama anavyonukuliwa na Khamis (2008:5) unyambulishaji wenye mipaka huathiri tabia ya kitenzi kisintaksia kwa kuongeza yambwa, kupunguza yambwa au kutofanya chochote kile kwenye kitenzi, anaendelea kuzungumzia aina za minyambuliko kama fanyizi, mufidi, ambatani, nafsi, tendwa, uwezo, tuamo na nyume ambayo hupelekea kitenzi kuteua kategoria za maneno. Mfano wa mnyambuliko mufidi, Neno shika kabla ya kunyumbulishwa linaweza kuchukua nomino mbili mfano baba ameshika kikombe. Lakini kitenzi shika kinaponyumbulishwa kwa kuongeza –i- tunapata shikia hivyo tunaweza kusema baba amemshikia mwalimu kikombe. Hivyo kitenzi hicho kimechukua nomino tatu. Lakini hatuwezi kusema baba ameshika mwalimu kikombe. Kwa sababu kitenzi shika hakidhibiti nomino tatu. Pia katika mnyambuliko fanyizi husababisha kitenzi kibebe Nomino. Mfano; Imb –ish-a watu, kiambishi –ish- kinafanya kitenzi imba kuchagua nomino watu. Ikifanya dhima ya kutendesha. Lakini hatuwezi kusema imbisha ng’ombe, tungo hii haina mantiki, kwani ng’ombe hawezi kuimba. Mnyambuliko wa utendwa pia unasababisha kitenzi kuteua kategoria ya maneno; Mfano, chez-w-a, fund-w-a vitenzi hivyo vinalazimisha kuteua kategoria ya nomino au kielezi. Mfano Mtoto amechezwa unyago Hapa kitenzi chezwa kinaruhusu nomino unyago, kwa sababu unyago unachezwa, lakini hatuwezi kusema mtoto amechezwa nguo, ingawa nguo ni nomino kama ilivyo unyago, lakini nomino hiyo haiwezi kuchezwa kwasababu kimaana tungo hii inakataa. Dhana ya kitenzi si elekezi hujitokeza katika kitenzi ambacho hakiruhusu kuchukua nomino nyingine. Hapa kitenzi kinawekewa hali ya utendeka inayojidhihirisha katika umbo la –k na –ik. Mfano: kikombe kimevunjika Maji yamechemka Pia sababu ya Kisemantiki, ambapo maneno huchaguana kwa kufuata mantiki ya maana inayokusudiwa. Mfano: anakunywa ugali T N Pamoja na ukweli kuwa kitenzi kunywa ni elekezi (kinaweza kubeba nomino, sababu za kisemantiki zinakataa, huwezi kunywa ugali. Kwa kuzingatia kanuni ifuatayo ya kitenzi kunywa: Kunywa (T – ele) - ------ + [___kiminika] +maji, soda, shalubati, bia Sanjari na hilo kitenzi cha lugha ya Kiswahili kina tabia ya kubeba dhana mbalimbali na kusababisha maana kutofautiana. Kwa mfano kitenzi chenye mnyambuliko mufidi kina dhima za kisemantiki zifuatazo kutokana na kuteua nomino zenye kubeba nduni tofauti tofauti kama ifuatavyo: Mfano: pik – i –a + N T + N +sababu +mahali +faida Mfano: a) pikia wali (faida) b) pikia nje (mahali) c) pikia nini? (sababu) Hivyo maneno huweza kuchaguana kutokana na sababu za mofosintaksia, kisemantiki na sababu zinazotokana na tabia mbalimbali za vitenzi. Matumizi ya maneno katika tungo yoyote ile hutegemea sana mahusiano kati ya neno na neno ili tungo hiyo ilete maana, hivyo sio tu kusema Nomino inaweza kukaa na Kitenzi, inabidi kujiuliza maswali zaidi, je kila nomino itakaa karibu na kitenzi fulani? ni muhimu kuzingatia sababu zote zinazosababisha maneno kuchaguana ili kujenga maana katika lugha.
MAREJEREO:-
1. Akmajian, A. et al (2006) Linguistics: An Introduction to Language and Communication, Prentice-Hall of India. Chapter 5 pp 149 – 215
2. Carnie, A. (2007) Syntax, A Generative Introduction. Blackwell publishing. Chapter 1-6 pp 1 -194.
3. Graustein, G. et al (1980) English Grammar, A University Handbook.VEB Verlag Enzykloaedie. Leipzig. Chapter 3 -5.pp 52-205
4. Habwe J na Peter K. (2004) Misingi ya Sarufi ya Kiswahili Phenix Publishers Nairobi
5. Langacker R.W. (1968) Language and Its Structure. Harcourt Bruce. New York.
6. Masamba, D.P.B. 2001 Sarufi Miundo ya Kiswahili Sanifu IKR UDSM, Dar es Salaam pp 84 - 180
7. Radford, A. (1997) Syntax, A minimalist introduction. Chapter 1 – 3 pp 1-81. Cambridge University Press. Cambridge.
8. Syal, P. And D.V. Jindal (2002) An Introduction to Linguistics, Language Grammar and Semantics. Prentice-Hall of India.
9. Yule, G. (1997) The Study of Language. 2nd edition. Cambridge University Press
Cambridge.
2. Carnie, A. (2007) Syntax, A Generative Introduction. Blackwell publishing. Chapter 1-6 pp 1 -194.
3. Graustein, G. et al (1980) English Grammar, A University Handbook.VEB Verlag Enzykloaedie. Leipzig. Chapter 3 -5.pp 52-205
4. Habwe J na Peter K. (2004) Misingi ya Sarufi ya Kiswahili Phenix Publishers Nairobi
5. Langacker R.W. (1968) Language and Its Structure. Harcourt Bruce. New York.
6. Masamba, D.P.B. 2001 Sarufi Miundo ya Kiswahili Sanifu IKR UDSM, Dar es Salaam pp 84 - 180
7. Radford, A. (1997) Syntax, A minimalist introduction. Chapter 1 – 3 pp 1-81. Cambridge University Press. Cambridge.
8. Syal, P. And D.V. Jindal (2002) An Introduction to Linguistics, Language Grammar and Semantics. Prentice-Hall of India.
9. Yule, G. (1997) The Study of Language. 2nd edition. Cambridge University Press
Cambridge.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni