Subcribe to our RSS feeds Join Us on Facebook Follow us on Twitter Add to Circles

Jumapili, 1 Februari 2015

(a) Sarufi ubongo (b) Sarufi kama kaida za kiisimu. (c) Sarufi kama tafiti na uchambuzi wa miundo inavyooneka kwenye lugha.

MJADALA WETU UTAJIKITA KATIKA VIPENGELE VIFUATAVYO
·          Ufafanuzi wa sarufi ubongo
·      Ufafanuzi wa sarufi kama kaida za kiisimu 
·     Ufafanuzi wa sarufi kama tafiti na uchambuzi wa miundo inavyooneka kwenye lugha.

Tofauti zilizopo katika mikabala hii.
Katika mjadala huu, kwanza kabisa tutaanza kwa kuangalia dhana muhimu ambazo zimejitokeza katika mada yetu, ambazo ni sarufi, mkabala wa kimapokeo pamoja na mkabala wa kisasa. Kisha tutangalia kwa kujadili kiini cha mada, ambapo tutaangalia jinsi sarufi ubongo, sarufi kama kaida za kiisimu na sarufi kama tafiti na uchambuzi wa miundo inavyooneka kwenye lugha na inaangukia katika mkabala upi na inatofautiana vipi.
Tukianza na maana ya sarufi kwa mujibu wa wataalamu mbalimbali kama vile:-
Kihore na wenzake (2005) wakimnukuu Gaynor (1968:88), wanaeleza kuwa sarufi ni sayansi ya muundo wa lugha pamoja na sheria, kanuni na matumizi yake ambayo kwa kawaida hukubalika kwa watumiaji wake.
Vile vile Mdee (1999) anafasili sarufi kama mfumo wa kanuni za lugha zinazomwezesha mzungumzaji kutunga sentensi nyingi sahihi na zenye kukubaliwa na wazawa wa lugha.
Pia Massamba na wenzake (1999:31) katika mtazamo wa pili wa kufasili dhana ya sarufi wanaeleza kuwa sarufi ni kanuni sheria au taratibu za uchambuzi zinazotawala lugha.
Hivyo basi wanasarufi hawa wanaonekana kukubaliana kwamba sarufi ni kanuni, sheria na taratibu zinazotawala lugha. Lakini kwa kiasi kikubwa tunakubaliana na fasili iliyotolewa na Mdee kutokana na kwamba ameweza kutufafanulia vizuri kanuni hizo na taratibu za lugha ndizo zinazomwezesha mzungumzaji kutunga sentensi nyingi, sahihi na zenye kukubaliwa na wazawa wa lugha.
Kwa mfano:- sentensi za kiswahili zina muundo wa
                      N + V + T + E
Mtoto mzuri anacheza uwanjani
  N         V          T             E
Baada ya kuangalia dhana ya sarufi kwa mujibu wa wataalamu mbalimbali sasa tunaweza kuangalia mikabala mikuu miwili ya sarufi ambayo ni:-
i.             Mkabala wa kimapokeo
ii.            Mkabala wa kisasa.
Kwa kuanza na mkabala wa kimapokeo kwa mujibu Khamisi na Kiango (2002), wanaeleza kuwa hii ni sarufi ya kale, wataalamu wanaohusishwa na mkabala huu walijitokeza kuanzia karne ya 5 kabla ya kristo na katika karne ya 18 na karne ya 19 baada ya kristo, wataalamu hao ni kama vile Plato, Aristotle, Panin, Protagoras ambao walijihusisha na lugha kwa kutaka kujua asili yake ikiwa ni sehemu ya uchunguzi wa asili ya maumbo hususani walitaka kujua kama lugha ni tukio la maumbile au tukio la unasibu.
Pia Massamba na wenzake (wameshatajwa) wanaeleza kwamba sarufi mapokeo zilikuwa ni sarufi elekezi ambazo zilisisitiza kanuni na nini cha kusema na wajua lugha. Watu wasiojua kanuni za lugha wanapaswa kujifunza kutoka kwa wanaojua sarufi ya lugha. Wanaendelea kusema kuwa, wanaojua lugha hupaswa kutunga kanuni za sarufi.
Vile vile Habwe na Karanja (2004:124), wanadai kuwa mitazamo hii ya wanasarufi hawa wa kimapokeo iliathiri mbinu na njia za kuangalia lugha kwani sarufi mapokeo ilijikita katika lugha za kiulaya kama vile kiyunani na kilatini.
Sifa mbalimbali za lugha hizi ambazo ziliaminiwa kuwa bora, zilichunguza kilatini na kiyunani zilielezwa kuwa ni lugha duni na kutwezwa na kudhalilishwa
Sarufi mapokeo ilielekeza watu jinsi ya kutumia lugha, uelekezi huo hata hivyo ulijikita kwenye sheria za lugha ya kilatini kwa mfano sentensi haikupaswa kuishia na kihusishi wala kuanza na kiunganishi.
Udhaifu mkubwa wa sarufi mapokeo ni kwamba, taratibu za uchanganuzi wa lugha hazikuzingatia lugha ya kuzungumza kama ilivyo leo. Wanasarufi mapokeo walienzi na kuchunguza lugha ya maandishi. Hivyo basi ni dhahiri kwamba mkabala huu unaangukia katika mitazamo ya kifalsafa.
Hivyo basi ni wazi kuwa katika sarufi hii ya mapokeo tunakutana na mikabala miwili inayoangukia katika mkabala huu ambayo ni sarufi ubongo na sarufi kama kaida za kiisimu.
Mkabala wa pili, ni mkabala wa kisasa, unaoongozwa na wanasosiolojia ambao unahusisha sarufi mbalimbali kama vile :-
i.             Sarufi msonge
ii.            Sarufi miundo virai
iii.           Sarufi geuza maumbo zalishi
iv.           Sarufi husiano
Katika mkabala huu ndipo tunapata mkabala wa sarufi kama tafiti na uchambuzi wa miundo inavyooneka kwenye lugha.
Hivyo basi baada ya kujadili mikabala mikuu miwili ambayo ni mkabala wa kimapokeo na mkabala wa kisasa, zifuatazo ni sifa muhimu za sarufi ubongo, sarufi kama kaida za kiisimu na sarufi kama tafiti na uchambuzi wa miundo inavyooneka kwenye lugha ambazo kwazo tutaona jinsi kila moja inavyotofautiana na nyingine.
Kwa kuanza na sarufi ubongo, kwa mujibu wa Nordquist (2012), anaeleza kuwa sarufi ubongo ni sarufi endelevu ambayo inamwezesha binadamu kuzalisha lugha ambayo inaweza kueleweka kwa wengine
Pia Sharpe (2006), anaeleza kuwa sarufi hii hufananishwa na umilisi, anaendelea kueleza kuwa sarufi hii humwezesha mtu kuweza kusikia na kutambua kama sentensi hiyo ni sahihi au si sahihi.
Chomsky (1957), anaeleza kuwa kila binadamu amezaliwa na uwezo wa kuzalisha tungo mbalimbali zisizo na ukomo ambazo humpatia uwezo au uzoefu wa sarufi ya lugha. Pia anafafanua kwamba kila binadamu huzaliwa na kifaa katika ubongo wake ambacho kinamwezesha kuamili lugha ya aina yoyote, amekiita kifaa cha uamiliaji lugha (KIULU). Kwa mfano mtoto mdogo mwenye umri chini ya miaka saba anaweza kuamili lugha yoyote na mahali popote.
Mgullu (1999), anaeleza kuwa sarufi ubongo huchunguza jinsi binadamu anavyojifunza lugha kwa mfano hatua mbalimbali ambazo hupitia wakati anajifunza lugha yake ya kwanza.
Kwa hiyo tunakubaliana na fasili zote zilizotolewa na wataalamu hapo juu kutokana na kwamba sarufi ubongo, hii ni sarufi ambayo inachunguza jinsi binadamu anavyoweza kuamili lugha na kujifunza lugha pia kuweza kuzalisha sentensi mbalimbali ambazo anaweza kuzitumia katika mawasiliano.
Vile vile wataalamu wa mkabala huu hueleza kuwa upo uhusiano mkubwa kati ya akili, kufikiri na lugha bila shaka uhusiano huu ni ule wa taathira ya lugha yaani dhana inayoeleza kuwa kwa kawaida kila lugha huathiri watumiaji wake kwa kiasi kikubwa.
Vile vile wataalamu wa mkabala huu wanaeleza jinsi watu wanavyojifunza lugha ya pili au lugha ya tatu.
Kwa kifupi mkabala huu hujihusisha na mambo kadha kama vile:-
(i)    Kumwezesha binadamu kuweza kuzalisha au kutunga sentensi mbalimbali.
(ii)       Sarufi ubongo huusika na uamiliaji wa lugha na ujifunzaji wa lugha.
(iii)   Sarufi hii huwakilisha maarifa ya mzungumzaji wa lugha (umilisi alionao mzungumzaji).
Mkabala mwingine wa sarufi ambao unaangukia katika mkabala wa sarufi mapokeo ni sarufi kama kaida za kiisimu.
Kwa mujibu wa Encyclopedia (1970), wanaeleza kuwa sarufi kaida ni mpangilio unaoonyesha au kueleza kanuni za kisarufi katika lugha ambazo hushughulika na kanuni za uundaji wa maneno, maumbo ya maneno, miundo ya maneno, miundo ya sentensi, vile vile inahusisha taarifa maalumu kuhusu fonetiki na fonolojia (taaluma inayohusika na utamkaji sahihi unaokubalika)
Pia kwa mujibu wa Babylon Dictionary (1997), wanaeleza kuwa sarufi kaida ni mfumo wa kisarufi ambao unafafanua kipi sahihi na kipi si sahihi katika lugha, pindi mzungumzaji anapozungumza, amezungumza sahihi au si sahihi.
Kwa hiyo tunaweza kueleza kuwa sarufi kaida hujishughulisha sana na:-
i.           Kuelekeza namna ya matumizi sahihi ya lugha.
ii.         Wataalamu wa lugha ndio wanaounda kanuni na miongozo ya lugha ambayo inatakiwa kufuatwa na wale wasiojua lugha.
Kwa mfano:- kanuni mojawapo ya miundo ya sentensi za Kiswahili huwa na muundo wa kiima na kiarifu.
Vile vile sentensi nyingi za Kiswahili huwa na muundo wa kirai nomino na kirai kitenzi.
Hivyo basi katika mkabala huu wa sarufi watu wasiojua lugha wanapaswa kufuata kanuni na taratibu zilizoundwa na wanaojua lugha kwa mfano wanasarufi.
Pia mkabala mwingine wa sarufi ambao unaangukia katika mkabala wa kisasa ni sarufi kama utafiti na uchambuzi wa miundo inayoonekana katika lugha.
Kwa mujibu wa Besha (2007), anaeleza kuwa huu ni mkabala unaohusika hasa na uchambuzi wa muundo wa lugha, sauti za lugha, muundo wa sentensi na hata maana za tungo za lugha.
Pia mgullu (1999), anaeleza kuwa lengo la mkabala huu ni kufafanua vipengele vyote vya lugha fulani kama vilivyo hivi sasa au vilivyokuwa wakati fulani.
Hivyo basi Besha na Mgullu wanakubaliana kuwa huu ni mkabala unaofafanua namna au jinsi watu wanavyozungumza lugha na sio kuwaelekeza waizungumze vipi lugha yao. 
Hivyo basi kwa ujumla mkabala huu unajihusisha na mamba yafuatayo:-
i.             Hautilii mkazo mabadiliko yaliyotokea katika lugha hata kama mabasiliko hayo yapo.
ii.            Mkabala huu hauamuru watu waseme vipi na vipi wasiseme.
Kutokana na sifa mbalimbali zilizojitokeza katika mikabala hii, tumeweza kubaini tofauti zilizopo baina ya mikabala hii mitatu ambazo ni kama zifuatazo:-
Sarufi ubongo, sarufi kama kaida za kiisimu zinajitokeza katika mkabala wa kimapokeo wakati sarufi kama tafiti na uchambuzi wa miundo inavyooneka kwenye lugha inajitokeza katika mkabala wa kisasa.
Vilevile sarufi ubongo humwezesha binadamu kuweza kuzalisha miundo mbalimbali ya tungo wakati sarufi kama kaida za kiisimu haijihusishi kabisa na masuala ya ubongo bali yenyewe hujihusisha na mazoea ya kawaida ya watumiaji wa lugha ambapo kunakuwa na makosa ambayo huwafanya wataalamu kuunda kanuni za lugha ambazo zinatakiwa kufuatwa na wasiojua lugha hii inatofautiana na sarufi kama tafiti na uchambuzi wa miundo inavyoonekana kwenye lugha kwa kuwa haihusiani na masuala ya ubongo wala kaida, bali yenyewe hujihusisha na utafiti na ufafanuzi wa miundo ya lugha kama inavyotumika na wazungumzaji wa lugha na haiwaelekezi jinsi ya kuzungumza.
Kwa kuhitimisha tunaweza kusema kwamba pamoja na tofauti hizo zilizojitokeza katika mikabala hiyo mitatu, mikabala hii inaonekana kufanana kwani yote inajihusisha na lugha ya binadamu, pia mikabala hii imechangia kwa kiasi kikubwa katika maendeleo ya taaluma ya isimu na ndio imekuwa darajia kwa wataalamu mbalimbali katika kufanya tafiti zao kwa mfano baada ya kushindwa kwa sarufi ubongo na sarufi kama kaida za kiisimu ndipo kukazaliwa kwa sarufi kama tafiti na uchambuzi wa miundo inavyooneka kwenye lugha.
MAREJEO
Babylon Dictionary. (1997). Translation and Information Platform. Babylon Ltd.
Besha, R.M. (2007). Utangulizi wa lugha na Isimu. Macmillan Aidan Ltd. Dar es Salaam.
Chomsky, N. (1957). Syntactic Structures. Mouton The Hague.
Khamis, A.M na John G.K (2002). Uchanganuzi wa sarufi ya Kiswahili. TUKI. Dar es salaam.
Habwe, J na Peter K (2007). Msingi ya sarufi ya Kiswahili.Phoenix Publishers. Nairobi.
Kihore, Y.M na wenzake. (2008). Sarufi Maumbo ya Kiswahili Sanifu (SAMAKISA):Sekondari na Vyuo. TUKI. Dar es Salaam.

Massamba, D.P.B. na wenzake. (2009). Sarufi Miundo ya Kiswahili Sanifu (SAMIKISA): Sekondari na Vyuo. TUKI.
Mgullu, R.S. (1999). Mtalaa wa Isimu: Fonetiki, Fonolojia na Mofolojia 

MAHUSIANO YA KIUTAWALA NA KIUSABIKI KUHUSIANA NA VIAMBAJENGO:-



              IMEANDALIWA NA MANYAMA CHARLES;CHUO KIKUU CHA ARUSHA.

                                                         DONDOO ZA SWALI:-

I. UTANGULIZI:-

II. KUJADILI KUHUSIANA NA DHANA ZIFUATAZO:-

A. Viambajengo Sisisi.

B. Viambajengo Viso-tamati.

C. Viambajengo Tamati.

D. Fundo Dada.

E. Fundo Binti.

F. Fundo Mama.

G. Fundo Baba.

III. HITIMISHO:-


Swali 2.

I. UTANGULIZI:-

II. KUJADILI KUHUSU MAHUSIANO YA KIUTAWALA NA KIUSABIKI KUHUSIANA NA VIAMBAJENGO:-

A. MAHUSIANO YA KIUTAWALA:-

B. MAHUSIANO YA KIUSABIKI:-

III. HITIMISHO:-

IV. MAREJEREO:-


Swali 1.

I. UTANGULIZI:-

Viambajengo ni vijenzi katika sentensi ambavyo hushirikiana na vingine ili kujenga vipashio vikubwa zaidi.viambajengo vya lugha kama fonimu, silabi na hata mkazo.

Katika Nadharia ya umilikifu,Nadharia hii ilihakikiwa na Noam Chomsky.Nadharia hii huweka masharti ya uhamishaji wa viambajengo. Kanuni katika nadharia hii ni kanuni masharti (subjacency condition). Kanuni hii inadai kwamba hatuwezi kuhamisha kiambajengo zaidi ya kifundo kimoja katika uhamishaji mmoja. Kifundo ni kikundi cha maneno yanayohusiana. Viambajengo ni maneno yanayopatikana katika sentensi Fulani.

Kwa mfano; sentensi,

a) Msichana mwerevu amepita mtihani.

Ina viambajengo vinne. Viambajengo msichana na mwerevu vinaunda kifundo kimoja ilihali viambajengo amepita na mtihani vinaunda kifundo kingine kimoja. Yaani; Msichana mwerevu amepita mtihani.

Kifundo (i) Kifundo (ii) Tunapotoa kiambajengo lazima pawe jirani na mahali kiambajengo hicho kinaelekea (landing site). Pale ambapo kiambajengo kimetoka lazima pawe wazi. Pia hatuwezi kuhamisha viambajengo viwili kwa wakati mmoja. Kwa mfano, Katika umbo ndani la sentensi; [ ameenda [mama [sokoni kununua mboga] Katika umbo nje itakuwa; Mama ameenda sokoni kununua mboga.Kutokana na mfano huu tunaweza kuhamisha kiambajengo mama kitangulie kitenzi ameenda lakini hatuwezi kuhamisha kiambajengo sokoni kwa sababu kitakuwa kimehamishwa zaidi ya kifundo kimoja katika uhamishaji mmoja.Yaani kiambajengo sokoni hakiko jirani kwa hivyo hakiwezi kuhamishwa.


II. KUJADILI KUHUSIANA NA DHANA ZIFUATAZO:-

1. Viambajengo Sisisi.

Hivi ni vijenzi au vipashio katika mchoroti ambavyo hutawaliwa kwa karibu hushirikiana na vingine ili kujenga vipashio vikubwa zaidi katika sentensi.Vilevile viambajengo hivi sisisi mtawala wake huwa ni mmoja tu na aghalabu viambajengo hivi huwa vimefuatana.


Mfano wake ni kama;


Mpira unachezwa na Juma.


S






KN KT


T KN


Juma anacheza mpira


Hivyo basi viambajengo sisisi katika mchoroti uliopo hapo juu KT ni T +KN.



2. Viambajengo Viso-tamati.


Hivi ni vijenzi au vipashio katika mchoroti ambavyo mfuatano wake unakuwa haujatimia au vinavyokuwa katikati kwenye mchoroti ambavyo uwepo wake hujenga vipashio vikubwa zaidi katika sentensi ambazo ndizo huja kuwa aina za maneno.


Mfano ni;


Mpira unachezwa na Juma.


S



KN KT


T KN


Juma anacheza mpira


Katika mchoroti huu viambajengo visotamati ni KN,KT,T na KN.Kwamantiki ya kuwa ndivyo viambajengo pekee ambavyo vimekatizwa katika mchoroti



3. Viambajengo Tamati.


Hivi ni vijenzi au vipashio katika mchoroti ambavyo mfuatano au mpangilio wake ndiyo unaokuwa chini kabisa kwenye mchoroti ambavyo uwepo wake hujenga vipashio vikubwa zaidi katika sentensi na ufahamika zaidi kama aina za maneno.


Mfano ni;


Mpira unachezwa na Juma.


S


KN KT


T KN


Juma anacheza mpira


Katika mchoroti hapo juu viambajengo tamati vyaweza bainishwa chini kabisa katika aina za maneno.



4. Fundo Dada.


Ni kile ambacho kinahusiana na kingine kwa sababu ya kuzaliwa au kumilikiwa na kifundo sawa.Fundo KN+KT au T+KN ni mafundo dada na S ndiyo huitwa fundo mama na vifundo vya chini kabisa ya mchoroti ndiyo huitwa vifundo viso-tamati.


Kwa mfano; S


KN KT


T KN


N V


5. Fundo Binti.


Ni kile ambacho kinamilikiwa kwa karibu na kifundo mama. Kwa mfano KN na KT ni vifundo binti vya S.Hivyo basi tofauti kubwa iliyopo baina ya fundo dada na fundo binti ni katika umilikifu pekee.Pia huitajika kutajwa kwa mzazi mmoja.,kama T+KN ni vifundo binti vya KT.


S


KN KT


T KN


6. Fundo Mama.


Ni kifundo ambacho kinamiliki vifundo vingine.Fundo hili ndilo mzazi halisi wa vifundo vingine kama vile fundo binti,fundo dada na hata fundo liso-tamati na fundo tamati.Mfano S ndilo fundo mama la KN+KT na T+KN


S


KN KT


T KN


7. Fundo Baba.


Wanaisimu kama Avram Noam Chomsky (1957) na mwenzake bloomfield (1965).wao kama waanzilishi wa Dhana hii ya Uambajengo,wanasdai kuwa ili kuonesha jinsi viambajengo vinavyohusiana.Wanaisimu hawa wametumia dhana au istilahi za kindugu aghalabu. kwa jinsia ya kike kwa mantiki ya kwamba ndiyo pekee yenye uwezo wa kuzaa na siyo jinsia ya kiume.Hivyo basi kifundo Baba hakiwezi kuwepo kwa madai hayo ya uwezo wa kuzaa,ndomana wakatoa mfano wa fundo mama,fundo dada na hata fundo binti.


Swali 2.


I. UTANGULIZI:-

Viambajengo ni vijenzi katika sentensi ambavyo hushirikiana na vingine ili kujenga vipashio vikubwa zaidi.
Utawala wa kiuambajengo ni hali ya kifundo cha kijenzi kimoja kukimiliki kifundo kingine.
Mahusiano ya kutangulia ni hali ya neno au kifundo kimoja kujitokeza kabla ya kingine katika ulalo. Yaani kinachokuwa kushoto kinakitangulia kilicho kulia.



II. KUJADILI KUHUSU MAHUSIANO YA KIUTAWALA NA KIUSABIKI KUHUSIANA NA VIAMBAJENGO:-


A. MAHUSIANO YA KIUTAWALA:-
Mahusiano ya Utawala wa kiuambajengo ni hali ya kifundo cha kijenzi kimoja kukimiliki kifundo kingine.Hivyo fundo lililo juu ndilo linatawala mafundo mengine yote.Mfano mzuri ni fundo mama kwa namna litawalavyo vifundo dada,fundo binti,fundo liso-tamati na fundo tamati.S inatawala KN na KT.



S

KN KT


V N T KN


Vilevile kuna aina kuu mbili za mahusiano ya kiutawala,ambayo ni utawala wa mbali na utawala wa karibu,Mfano S inatawala kwa karibu KN na KT;Pia S inatawala kwa mbali V,N,T na KN. na viambajengo vinavyotawaliwa kwa karibu ndivyo huitwa viambajengo sisisi na pia viambajengo vinavyokuwa vimetawaliwa kwa mbali ndivyo huitwa viambajengo viso-tamati na viambajengo tamati.



B. MAHUSIANO YA KIUSABIKI:-

Kutokana na Radford (1997);Mahusiano ya kutangulia ni hali ya neno au kifundo kimoja kujitokeza kabla ya kingine katika ulalo. Yaani kinachokuwa kushoto kinakitangulia kilicho kulia. aghalabu uhusiano huo wa kiuambajengo mafundo dada ndiyo haswaa hutanguliana na fundo la kushoto ndilo hutangulia fundo la kulia.Mfano


S


KN KT


V N T KN


KN inatangulia KT kwenye mahusiano ;V inatangulia N kwenye mahusiano na T inatangulia KN kwenye mahusiano.
Vilevile hata katika mahusiano ya kiusabiki kunajitokeza aina zipatazo mbili ambazo ni mahusiano ya kiutangulia kwa karibu na mahusiano ya kutangulia kwa mbali.
Mahusiano ya kutangulia kwa karibuhufuata toka katika fundo lililopo kushoto,na kutangulia kwa mbali ni pale kifundo kilichopo kushoto kutangulia vifundo vyote vilivyopo kulia. Mfano kiutoka katika mcho hapo juu ni kuwa V inatangulia kwa karibu N., na KN inatangulia kwa mbali vifundo vya KT.




MAREJEREO:-

Radford (1997) A syntax minimalist introduction..Cambrodge University Press,New York. Radford (1998) A transformational Grammar,Cambridge University Press, New York. Smith, N (199); Chomsky;Ideas and ideals,Cambridge University Press,New Yo

MICHAKATO YA KIFONOLOJIA KWA UJUMLA.

IMEANDALIWA NA MANYAMA CHARLES

A) UTANGULIZI

i) Maana ya fonolojia
ii) Maana ya michakato ya kifonolojia

B) MICHAKATO YA KIFONOLOJIA

i) Kanuni ya kudondoshaji wa fonimu
ii) Kanuni ya uyeyushaji
iii) Kanuni ya tangamano la irabu
iv) Kanuni ya mvutano wa irabu
v) Kanuni ya ukakaishaji wa fonimu
vi) Kanuni ya usigano
vii) Kanuni ya muungano wa sauti
viii) Kanuni ya usilimisho

UTANGULIZI

Kwa mujibu wa Mgullu (1999) akimrejelea Fudge (1973) anasema kwamba fonolojia ni kiwango kimojawapo cha lugha fulani kilicho na vipashio vidogo zaidi kuliko vipashio vingine vyote vya lugha. Vipashio vya kifonolojia ni fonimu na alofoni zake.


Massamba (2010) anasema kuwa fonolojia ni tawi la isimu linalojishughulisha na mfumo wa sauti (asilia) za lugha. Hii inamaana kwamba, kila lugha mahususi ina mfumo wake wa sauti ambamo maneno hujengwa. Kiukweli fonolojia hujihusisha na namna sauti zinavyotumika katika maneno ya lugha mahususi katika kuleta maana.


Massamba na wenzake (2004) wanafafanua kuwa, fonolojia ni tawi la isimu ambalo hujishughusha na uchunguzi, uchambuzi na uainishaji wa sauti pambanuzi ambazo hutumika katika mifumo mbalimbali ya sauti za lugha za binadamu.


Tuki (2004) inaeleza kuwa mchakato ni mfululizo wa shughuli unaosababisha kitu fulani kufikiwa. Hivyo katika uwanja huu wa fonolojia tunaweza kusema kuwa mchakato utakuwa unafanyika pale ambapo mofimu mbili zinapokutanishwa huweza kutokeza mabadiliko fulani katika mofimu mojawapo au kutotokea badiliko lolote.


Hivyo basi tunaweza kusema kuwa fonolojia ni tawi la isimu ambalo hujishughusha na uchunguzi, uchambuzi na uainishaji wa sauti pambanuzi ambazo hutumika katika mifumo mbalimbali ya sauti za lugha za binadamu.


MICHAKATO YA KIFONOLOJIA

Kanuni ya udondoshaji wa fonimu hii inahusu kuachwa kwa sauti Fulani katika neno /matamshi wakati mofimu mbili zinapokabiliana. Katika mazingira hayo sauti ambayo hapo awali ilikuwepo hutoweka, irabu za Kiswahili hudondoshwa wakati kuna neno la ziada la irabu. Mfano:


muchumi - mchumi


muti- mti


mutoto- mtoto


Hivyo basi “U” imedondoshwa


Umbo la nje/ umbo la ndani


Muumba /mu+umb+ a/


Muumini /mu+umini/


Muuguzi /mu+ugu+z+i/


Mtu /mu+tu/


Kanuni ya uyeyushaji, wataalamu wengine huita irabu kuwa nusu irabu Mgullu (1999) Huu ni mchakato ambapo irabu za juu /u/ na /i/ hubadlika na kuwa /w/ au / j/ katika mazingira ya kufuatiwa na irabu zisizofana nazo. Kwa kifupi ni kwamba /u/ inapofuatiwa na irabu yoyote isiyofanana nayo hubadilika kuwa [w] na /i/ ikifuatiwa na irabu yoyote isiyofanana nayo hubadilika na kuwa [j].


Na sauti hizo hubadilika katika mazingira ya /u/ hubadilika kuwa [w] inapofuatana na irabu nyingine isiyofanana nayo na / i/ inabadilika na kuwa [ϳ] pia inapofuatana na irabu isiyofanana nayo. Mfano wa /u/

umbo la ndani/ umbo la nje

/mu+aminifu/

[mwe:mbamba]

/ku+enu/

[kwe:nu]

/mu+ anafunzi/

[mwa:nafunzi]

/mu+eupe/

[mwe:upe]
/mu+embe/

[mwe:mbe]

Hivyo tunaona wazi kabisa kuwa irabu ya juu nyuma /u/ imebadilika na kuwa kiyeyusho [w] katika mazingira ya kuathiriwa na irabu isiyofanana nayo ambayo ni /a/ na /e/ kwa hapo juu lakini hata ikiwa ni /o/ huweza kubadilisha. Kanuni /u/ [w] I = u. Hivyo tunaona kuwa irabu ya mbele /i/ hubadilika na kuwa [j] inapofuatana na irabu nyingine isiyofanana nayo ambayo ni /e,a na o/. Mfano wa irabu /i/


/umbo la ndani/ [umbo la nje]

/mi+embe/

[mje:mbe]

/mi+endo/

[mje:ndo]

/mi+ezi/

[mje:zi]

/mi+anzo/

[mja:nzo]

/mi+eusi/

[mwe:usi]

/mi+oyo/

[mjo:jo]

Kanuni ya ukaakaishaji wa fonimu kwa mujibu wa Mgullu (1999) akimnukuu Les (1984), anadai kuwa ukaakaishaji wa fonimu hutokea ambapo fonimu zisizo za kaakagumu zinapobadilika na kuwa za kaakagumu. Yeye anadai kuwa katika Kiswahili sauti za kaakagumu zipo mbili tu yaani /ɟ/ na /ʧ/ ambazo ni vizuio kwamizo. Hapa tunaona kwamba kipasuo cha kaakaalaini /k/ hubadili mahali pa matamshi na kuwa kizuio kwamizi /ʧ/ cha kaakaagumu katika mazingira ya kufuatiwa na sauti /ϳ/. Kanuni yake /i/ [ ] I = kisha inabadilika kuwa /k/ [ ] /i/ kwa mfano:


umbo la ndani

umbo la nje/ umbo la nje

/ki+enu/

[kjenui]

[ enu]

/ki+eusi/

[kjeusi]

[ eusi]

/ki+ombo/

[kjombo]

[ ombo]

/ki+umba/

[kjumba]

[ umba]

/ambaki+o/

[ambakjo]

[amba o]

Kanuni ya tangamano la irabu huu ni mchakato wa kiusilimisho baina ya irabu na irabu katika kuathiriana kiasi kwamba hulazimika kufuatana. Katika mchakato huu kinachotokea ni kwamba, kama irabu ya mzizi ni /i, u au a/ basi irabu ya kiambishi cha utendea lazima kiwe ni [i ] , wakati irabu ya mzizi ikiwa ni/ e au o/ katika hali ya utendea kiambishi chake kitakuwa ni [e]. Mfano:Iwapo mzizi wa kitenzi una irabu /e/ na /o/ mnyambuliko utakuwa na irabu /e/

(Som) -som+esh+a =somesha

(chok)-chok+esh+a =chokesha

(kop)-kop+esh+a =kopesha

Iwapo mzizi wa kitenzi una irabu /a/, /i/ na /u/ mnyambuliko utakuwa na irabu /i/

(pig)-pig+ish+a= pigisha

(lim)-lim+ish+a= limisha

(andik)-andik+ish+a= andikisha


Umbo ndani/umbo la nje

/imb+a/

[Imb-i-a]

/andik+a/

[andik-i-a]

/dak+a/

[dak-i-a]

/chun+a/

[ un-i-a]

/og+a/

[og-e-a]

/ ez+a/

[ ez-e-a]

/kom+a/

[kom-e-a]

Kanuni ya muungano wa sauti hii inahusu mabadiliko mengi yanayohusu irabu lakini ambayo yanahusu kudondoshwa au kugeuka kuwa kiyeyusho, pia upo uwezekano wa irabu ya mofimu moja kukabiliana na irabu ya mofimu nyingine kisha irabu hizo mbili zikaungana na kuzaa irabu moja tu. Mfano Umbo la nje 

 umbo la ndani

Wengi / wa+ingi/

Mengi / ma+ingi/

Meno / ma+ino/

Wengi / wa+izi/

Kanuni ya usilimisho kwa mujibu wa Habwe na Karanja (2004), wanaeleza kuwa usilimisho ni kule kufanana kwa fonimu kwa kiasi au kikamilifu kutokana na kuathiriana. Hapa sauti jirani katika neno huathiriana kiasi kwamba fonimu hupokea ama kupoteza sifa za kifonetiki kwa fonimu jirani, na matokeo yakiwa kuwa fonimu hizi hukabiliana sana katika kufanana kwa hiyo kuna usilimisho pamwe wa nazali kuathiri konsonanti na konsonanti kuathiri nazali kwa kawaida sauti n humainisha umoja inapatikaribia na herufi b husilimishwa na kuwa sauti nyingine kwa mfano:


Umbo la ndani umbo la nje

Ulimi /u+limi/

Ndani /n+limi/

Urefu /u+refu/

Ndefu /n+refu/

Mbao /n+bao/

Kanuni ya mvutano wa irabu, badiliko hili la mvutano wa irabu hutokea pale ambapo irabu mbili zinapokabiliana katika maneno, hususa ni irabu ya juu na ya chini. Irabu ya juu, huvutana na irabu ya chini matokeo ni kwamba tunapata irabu ambayo si ya juu wala ya chini bali ipo katikati ya irabu hizo. Kwa mfano, irabu /a/ ambayo ni ya chini inapokabiliana na irabu /i/ ambayo ni ya juu mvutano hutokea, hali ambayo hupelekea utokeaji wa irabu. Kwa mfano:

Umbo la ndani umbo la nje

Ma+ino meno

Wa+ingi wengi

Wa+itu watu

Kanuni ya usigano ni kinyume cha usilimisho, katika usilimisho baadhi ya sauti huathiriwa na sauti fulani na kuzifanya zifanane na sauti hizo. Lakini katika usigano sauti moja huchukua sifa fulani ili kutofautiana na sauti iliyo karibu nayo. Badiliko hili mara nyingi hutokea katika lugha za kibantu. Katika lugha ya Kiswahili inapoongezwa kwa maneno yenye sauti tangulizi ambayo si ghuna kwa mfano /k/ hubadilika na kuwa /g/ ambayo ni tofauti kabisa na kifonetiki.


Kuimarika kwa fonimu hili ni badiliko ambalo linahusu fonimu ambazo hutamkwa kwa kutumia nguvu kidogo zinapobadilika zinakuwa fonimu ambazo hutamkwa kwa kutumia nguvu nyingi kwa mfano kitambaza /l/ kinapobadilika na kuwa kipasuo /b/ katika neno /ulimi/. Neno ulimi lipo katika ngeli ya U-N, linatarajiwa katika wingi wa mofu (U) ya umoja libadilike na kuwa (N), lakini badala yake tunapata neno “ndimi”.


Fonimu /l/ huhitaji nguvu kidogo katika utamkaji lakini fonimu /d/ huhitaji nguvu nyingi kwa hivyo fonimu /l/ inapobadilika na kuwa fonimu /d/ katika wingi inasemekana kuwa fonimu /l/ imeimarika. Mfano:

Umbo la nje umbo la ndani fonimu iliyoimarika

Mwana mu+ana /u/ = /w/

Mwokozi mu+okozi /u/ = /w/

Myaka mi+aka /i/ =/j/

Kwao ku+ao /u/ =/w/

Kudhoofika kwa fonimu ni badiliko ambalo hutokea pale fonimu inayotamkwa kwa kutumia nguvu nyingi inapobadilika na kuwa fonimu inayotamkwa kwa kutumia nguvu kidogo kuliko ile ya awali, katika lugha ya Kiswahili badiliko hili hutokea zaidi katika nomino zinazoundwa kutokana na vitenzi. Fonimu /d/, /g/, /k/, /b/ huhitaji nguvu nyingi katika utamkaji ikilinganishwa na fonimu /z/, /s/, na /f/. kwa hivyo kutokana na mifano hiyo hapo juu ni bayana kuwa fonimu /d/, /g/, /k/, /b/ na /p/ zimedhoofika. Kwa mfano katika vitenzi vifuatavyo:

Umbo la ndani umbo la nje fonimu inayodhoofika

Mpendi mpenzi /d/ =/z/

Mnjengi mjenzi /g/ =/z/

Mpiki mpishi /k/ =/ʧ/

Mwibi mwizi /b/ =/z/

Ogopya ogofya /p/ =/f/

Unazalishaji wa irabu kwa mujibu wa Massamba (2011) anadai kuwa unazalishaji wa irabu ni aina ya usilimisho ambao irabu hupata sifa ya unazali kutokana na irabu yenyewe kutangamana na konsonanti ambayo ni nazali. Hivyo irabu nyingi hupewa sifa za unazali kutokana na ama kufuatiwa kwa nazali ama kutanguliwa na nazali. Na alama inayowakilisha unazalishaji ni alama ya kiwimbi [ ̴ ], hivyo sauti zote zilizowekewa alama ya kiwimbi ( ̴ ) zina unazali kwa sababu zimefuatana na nazali na hivyo zimefanywa kuwa unazali. Zaidi tuangalie mifano ifuatayo.Mifano


umbo la ndani umbo la nje

/nondo/

[nondo]

/penya/

[penya]

/mama/

[mama]

/ngambo/

[ ambo]

/nyumba/

[ umba]

/muwa/

[muwa]


HITIMISHO

Kwa hiyo tunaweza kusema kwamba mifanyiko ya kifonolojia huhusu mabadiliko ambayo hutokea pale ambapo fonimu mbili huambatana katika kuunda vipashio vikubwa kuliko fonimu (yaani silabi, mofu na maneno ). Mabadiliko hayo hutokea kwa sababu ya sauti moja kuathiri nyingine au sauti mbili kuathiriana katika mazingira maalum ya utokeaji, Kutokana na kuathiriana kwa fonimu za lugha na mabadiliko yanayojitokeza.


kuna kanuni ambazo zimeundwa na wanaisimu ijapo mabadiliko hayo huathiri mofu na maneno hujikita zaidi katika sifa za kifonolojia ambazo ni kama vile udondoshaji wa fonimu, mvutano wa irabu, tangamano la irabu, ukakaihsaji wa fonimu, uyeyushaji, kuimarika na kudhoofika kwa fonimu, usilimisho pamwe wa nazali na mengine mengi ambayo hatukuyasema katika uchambuzi watu wa michakato ya kifonolojia.


MAREJEO

Habwe, J. na Peter, K (2004) MISINGI YA SARUFI YA KISWAHILI. Phoenix Publisher. Nairobi.

Hyman, L.M. (1975) PHONOLOGY: THEORY AND ANALYSIS. New York HRW Press

Massamba, D.P.B. na wenzake (2004) FONOLOJIA YA KISWAHILI SANIFU (FOKISA): Sekondari na vyuo. Dar es salaam. TUKI

Massamba, D.P.B. (2010) PHONOLOGICAL THEORY: HISTORY AND DEVELOPMENT. Dar es Salaam. TUKI.

Mgullu, R.S. (1999) MTALAA WA ISIMU: FONETIKI, FONOLOJIA NA MOFOLOJIA YA KISWAHILI. Longhorn Publishers Ltd. Nairobi.

Matinde, S.R. (2012) DAFINA YA LUGHA ISIMU NA NADHARIA. Sekondari na vyuo vya kati na vyuo vikuu. Serengeti Educational Publishers Ltd.

TUKI, (2004) KAMUSI YA KISWAHILI SANIFU. Oxford University Press: Nairobi.