Subcribe to our RSS feeds Join Us on Facebook Follow us on Twitter Add to Circles

Jumatano, 7 Januari 2015

KATEGORIA ZA KISARUFI KULINGANA NA MTIZAMO WA WANAMAMBOLEO NA MTAZAMO WA WANAMAPOKEO:- :-

        I.            KATEGORIA ZA KISARUFI KULINGANA NA MTIZAMO WA WANAMAMBOLEO:-
Kategoria ya Sarufi ya kimamboleoInaoongozwa na wanasosiolojia ambao unahusisha sarufi mbalimbali kama vile :- Sarufi msonge , Sarufi miundo virai na Sarufi geuza maumbo zalishi iv. Sarufi husiano Katika kategoria hii huu ndipo tunapata kuona  sarufi kama tafiti na uchambuzi wa miundo inavyooneka kwenye lugha.
a)      Kategoria ya Muundo wa Kirai;
Kirai ni fungu la maneno yanayohusiana kimuundo lisilokuwa na muundo wa kiima kiarifu. Maneno katika kirai humilikiwa na neno moja ambalo ndilo neno kuu. Kirai hubainishwa na kategoria ya neno kuu. Kwa mfano: KN, KT, KV, KE KH n.k.
Virai huundwa na viambajengo. Kiambajengo ni kikundi cha maneno au hata neno moja pia inayofanya kazi kama kitu kimoja. Kirai, kishazi au sentensi ni mkusanyiko wa viambajengo kadha.
Kirai ni mkusanyiko wa viambajengo vilivyojengwa kuzunguka neno kuu. Kwa mfano, KN huundwa na nomino na vivumishi vyake, kwa hivyo muundo wa kirai ni maneno yanayokiunda yakiwakilishwa na alama za kategoria za maneno hayo.
Kwa mfano: a) ‘Mtoto mdogo’.    Hiki ni Kirai Nomino (KN) kilichoundwa na N (nomino) na V (kivumishi).  Kwa hivyo KN  N+V       b) ‘analima shamba’.
Hiki ni kirai kitenzi (KT) chenye kuundwa na kitenzi (T) na kirai nomino (KN). Kwa hivyo KT  T+KN.

b)      Kategoria ya Muundo wa Vishazi na Sentensi
Kishazi ni kikundi cha maneno kilicho ndani ya sentensi chenye muundo wa kiima na kiarifu. Kishazi kina muundo sawa na sentensi.
Sentensi ni kikundi cha maneno chenye maana iliyo kamili. Sentensi ndicho kipashio lugha cha kimuundo ambacho ni kikubwa kuliko vipashio vingine. Vipashio vya lugha ni pamoja na: mofimu, neno, kirai, kishazi na sentensi yenyewe. Sentensi na kishazi huundwa na virai vikuu viwili: KN na KT. KT yaweza kuundwa na kitenzi na nomino, kitenzi na kielezi .
Kwa hivyo S- KN + KT
c)      Kategoria ya Sarufi geuza umbo zalishi;
Kategoria ya  geuza umbo zalishi huonyesha ujuzi alionao mzungumzaji ambao humwezesha kutunga sentensi sahihi na zisizo na kikomo. Uwezo wa mzungumzaji kutunga sentensi zisizo na ukomo unatokana na kufahamu kanuni za kutunga sentensi sahihi ambazo mzawa wa lugha anazijua kutokana na kuwa na umilisi na lugha yake. Kanuni za kutunga sentensi sahihi hubainisha sentensi sahihi na zisizo sahihi.
Kwa mujibu wa kategoria hii, sentensi ina umbo la nje ambalo ndilo linalojitokeza katika usemaji na hata inapoandikwa, na umbo la ndani ambalo huwa limefichika na hujidhihirisha katika umbo jingine wakati wa kuongea (maana).
Kategoria hii imeweza kuonyesha uhusiano wa tungo ambazo japo zilikuwa na umbo la nje tofauti, zina umbo la ndani sawa.
Kwa mfano:
Juma  anacheza  mpira
KN       KT           KN

Mpira  unachezwa na  Juma
               KN    KT           KU   KN
Mfanano wa tungo hizi umekitwa katika maana. Japokuwa sentensi a) inaanza na Juma, na ile b) inaanza na Mpira, mtenda na mtendwa katika sentensi zote ni yule yule.
d)      Kategoria ya Sarufi miundo virai zalishi;
Katika  kategoria ya sarufi miundo virai zalishi muundo wa sentensi huelezwa kwa kuchanganua vijenzi vyake ambavyo ni viambajengo. Viambajengo hivi huchanganuliwa hadi kufikia neno moja ambalo hubainishwa kwa kategoria yake ya kisarufi. Uchanganuzi huu wa sentensi huelezwa kwa kanuni ambazo huwezesha kutunga sentensi nyingi zaidi.
Kanuni za muundo virai.    KN  N --- mtoto
Hii ina maana kuwa KN ina N (yaani Kirai Nomino kina kiambajengo kimoja tu ambacho ni nomino). Hii yaweza pia kuelezwa hivi:
KN  N     Mtoto
Hii ina maana kuwa kirai hiki ni neno moja. ‘mtoto’Kirai chenye viambajengo zaidi kimoja, yaani chenye maneno zaidi ya moja  huelezwa kwa kanuni:
KN N V au KN N V      Mtoto mzuri Hii ina maana kuwa KN kinaundwa na maneno mawili, yaani ‘mtoto mzuri’Vivyo hivyo kwa Kirai kitenzi (KT).


KATEGORIA ZA KISARUFI KULINGANA NA MTAZAMO  WA WANAMAPOKEO:-
Kama ilivyoelezwa hapo mwanzoni kuwa kategoria za kisarufi zinahusu sifa zinazoambatanishwa katika aina za maneno nazo ni kama ifuatavyo:-
Kategoria za nafsi, ni sifa ama ni kipashio kinachodhihirisha muhusika katika usemaji nazo zipo za aina tatu ambazo nafsi ya I, II, na  III ambapo huwakilishwa na ni-tu, u-m na a-wa.viwakilishi katika ngazi hii ni tegemezi kwani haviwezi kusimama peke yake na kuleta maana iliyokusudiwa.kwa mfano
Nafsi ya I ninaimba- tunaimba
Nafsi II  unaimba- mnaimba
Nafsi III anaimba – wanaimba
Kategoria za njeo/wakati, ni viambishi vinavyoambikwa katika mashina ya vitenzi vikionesha au kutoa taarifa ya tendo lililtendeka, linatendeka au litatendeka muda gani.viambishi hivi ni vingi lakini vimewekwa katika katika hali ya uyakinishi na viambishi vya tendo katika hali ya ukanushi, njeo hiyo iliyopo, iliyopita, na ijayo katika hali ya uyakinishi na ukanushi kwa mfano. Njeo iliyopita   Alicheza -   hakucheza
                         Walicheza – hawakucheza
Njeo iliyopo     ninasoma -  sisomi
                          Tunasoma – hatusomi
Njeo ijayo          utalima – hautalima
                         Mtalima- hamtalima
Kategoria za hali,ni viwakilishi ni viwakilishi vinavyopachikwa katika mashina ya vitenzi ambavyo huangalia utendekaji wa lile tendo. Kategoria hizi huwa viko karibu sana na kategoria za njeo.japo zina utofauti kuna aina zaidi ya tatu za hali kwa mfano hali ya mazoea huwakilishwa na (hu-) hali ya kuendelea huwakilishwa na kiambishi (na-), hali ya masharti huwakilshwa na kimbishi (-ki-/-nge-/-ngali-/-ngeli-) na hali timilifu inayowakilishwa na kiambishi (-me-). Katika hali ya kutokea viambishi hivi havitokei katika shina moja la kitenzi ilavinaweza vikatokea katika sentensi moja katika mashina tofauti ya vitenzi.kwa mfano mwalimu alikuwa anafundisha /amefundisha . katika sentensi hii -li- inaonesha njeo na -na- /-me- inaonesha hali
Kategoria za idadi, hivi ni viambishi vinavyoambikwa katika aina mbalimbali za maneno vikionesha umoja na wingi ambapo katika Kiswahili hudhihirika kupitia viambishi ngeli vya upatanisho wa kisarufi . kwa mfano mwalimu analima, walimu wanalima (a-wa) huonesha umoja na wingi hivyo hudokeza idadi.
        

Kategoria za kauli, ambalo ni umbo ni umbo la kitenzi ambalo linadhihirisha uhusiano baina ya kiima na yambwa mfano kauli ya kutenda na kutendwa

MAANA YA VIAMBAJENGO,VIFUNDO MAMA,DADA NA BINTI.






1.Viambajengo ni vijenzi katika sentensi ambavyo hushirikiana na vingine ili kujenga vipashio vikubwa zaidi.

2.Utawala wa kiuambajengo ni hali ya kifundo cha kijenzi kimoja kukimiliki kifundo kingine.

3.Kutawala kwa karibu ni hali ya kifundo kikubwa kukimiliki vifundo vingine pasi ukingo kati yake.

4Mahusiano ya kutangulia ni hali ya neno au kifundo kimoja kujitokeza kabla ya kingine katika ulalo. Yaani kinachokuwa kushoto kinakitangulia kilicho kulia.

5.Kifundo mama ni kifundo ambacho kinamiliki vifundo vingine. Mfano S ni kifundo mama cha KN na KT.

6.Kifundo binti ni kile ambacho kinamilikiwa kwa karibu na kifundo mama. Kwa mfano KN na KT ni vifundo binti vya S.

7Kifundo dada ni kile ambacho kinahusiana na kingine kwa sababu ya kuzaliwa au kumilikiwa na kifundo sawa. Kwa mfano kifundo KN ni dada kwa KT.


SEMANTIKI NA PRAGMATIKI

MAARIFA YA LUGHA NA MAARIFA YA ULIMWENGU

IMEANDALIWA NA MANYAMA CHARLES


Maarifa ya lugha ni elimu ya kupambanua vijengo mbalimbali vya lugha na kanuni zake kulingana na taratibu za lugha hio. Ulimwengu halisi ni mukatadha ambao maarifa ya lugha huweza kutumika ili kuleta taathira kama ilivyokusudiwa na msemaji au mwandishi.

Richmond Thomason (2012) anafafanua maana ya semantiki kwamba ni tawi la isimu ya lugha linalohusu maana za viyambo vya lugha. Hivyo basi ni kusema kuwa, semantiki ni utanzu wa isimu unaojishughulisha na maana ya maneno au viyambo vya maneno katika lugha. Swali kuu katika wanasemantiki ni kuhusu ninini maana ya maana.

Hata hivyo wanasemantiki hujikita katika kuchunguza maana katika viwango mbalimbali kama vile; ngazi ya sauti (fonimu), neno, virai, vishazi na hata sentensi. Tawi hili la isimu limekuwa ni muhimu sana hasa kutokana na umuhimu wa mazungumzo, kwani ili mazungumzo yaeleweke na ujumbe ufahamike panahitajika maana. Aidha nivyema ifahamike kuwa semantiki inajihusisha na maana za maneno kiisimu, kwani maana yake hupatikana kutokana na muundo wa maneno hayo au maarifa ya lugha husika.

Kwa upande wa pragmatiki Richmond Thomason (2012), anasema kwamba ni tawi la lugha linalojihusisha na matumizi ya lugha kwa kuzingatia muktadha wa wazungumzaji walugha husika. Hivyo Thomson anadai kuwa pragmatiki inahusu zaidi mambo mawili; matumizi na muktadha.

Geoffrey Finch (2000) anasema kuwa, dhana ya pragmatiki ilivumbuliwa katika miaka ya 1930 na mwanafalsafa C.W. Morris, na imeanza kujulikana kama tawi tegemezi la isimu lugha miaka ya 1970 ambapo kabla ya hapo pragmatiki ilihusishwa kama tawi la kifalsafa, na kufafanuliwa kwa kuzingatia misingi mikuu miwili; matumizi na muktadha.

Kuanazia miaka ya 80 wataaklamu walianza kuiangalia pragmatiki kama maana ya msemaji na tafsiri kilichosemwa, yaani maana ya msikilizaji. Kwa upande wake Yule (1996) anafafanua dhana ya pragmatiki kwa kusema kuwa ni taaluma inayohusu mahusiano yaliyopo kati ya maana ya lugha na watumiaji wa mambo hayo.

Betty J. Birner (2012) anasema kuwa dhana hizi ni dhana zinazoshabihiana. Tofauti kubwa iliyopo kati ya dhana hizi bado ni mjadala mpana kwa baadhi ya wanaisimu wa lugha, hii ni kwa sababu, pragmatiki na semantiki zinajishughulisha na maana, kwa hio zipo hisia za ukaribu mno katika taaluma hizi mbili, licha kwamba pia zipo hisia za karibu za kuonesha utofauti wao.

Niukweli usiopingika kwamba kuna maarifa ya lugha na wakati huohuo kuna maarifa ya ulimwengu halisi, hii inamaana kuwa kufahamu lugha peke yake haitoshi lazima lugha hiyo itumike kulingana na muktadha au ulimwengu halisi ambapo lugha hio imetumika. Hali hii inaweza kuthibitishwa kutokana na kuwepo kwa matumizi ya maana tofauti kwa kadri ya watumiaji husika kama ifuatavyo.

Matumizi ya maana ya msingi katika kufafanua maana. Hii ndiyo njia kuu ya kulipa neno maana, ambayo kwa kawaida haibadiliki kutegemeana na athari za kimazingira. Hii inamaana kuwa maana ya neno au tungo itabaki ile ile hata kama mazingira yatabadilika. Maaaana hii ndiyo inayojulikana kama maana ya kileksika. Kwa mfano; kichwa- kikimaanisha sehemu muhimu katika mwili wa binaadamu kinachokusanya viungo kama vile; macho, masikio, pua na mdomo. Hii ndiyo maana pekeyake inayohitaji ulimwengu wa lugha kwa kiwango kidogo sana, hata hivyo bado ulimwengu halisi utahitajika kutokana na matumizi ya maneno kama vile homophoni na homonimia. Mfano neno kama kaa licha ya kuwepo kwa maarifa ya lugha lakini bado maarifa yaulimwengu halisi yanahitajika kuelewa kusudio la mzungumzaji, kwani yapo mazingira ambayo neno hilo litaendelea kutumika kama kitendo cha kuketi, na mazingira mengine litumike kama cheche la moto, na yote hayo ni maana ya msingi ya neno kulingana na miktadha tofauti tofauti.

Maana ya ziada au kisarufi. Ni maana abayo huibuka kutokana na maana ya msingi. Maana hii inatudhihirishia kuwepo kwa maarifa ya lugha na wakati huohuo kuna maarifa ya ulimwengu halisi. Hii ni kutokana na ukweli kwamba, maana hizi hutegemeana na kuhusiana na mazingira halisi ya matumizi. Kuelewa maana ya ziada sio tu kuelewa maarifa ya lugha, bali pia ulimwengu halisi au muktadha ambapo maneno au fahiwa hizo zimetumika. Mfano pale mzungumzajia atakapo sema “Samahani kaka! Hivi utaendelea kuwa kupe hadi lini? haya ni maisha tu!” utagundua kuwa, hapa kufahamu maana ya tungo hii si kutokana tu na kufahamu maarifa ya lugha, lakini pia inahitajika ufahamu wa ulimwengu halisi ambao tungo hio imetumika, kwa kusema kupe kumaaanisha mtu mnyonyaji au mtegemezi.

Maana ya kimtindo. Hii ni maana inayohusiana moja kwa moja na matumizi ya lugha kulingana na muktadha husika. Katika aina hii ya maana, neno au kiyambo hupata maana kulingana na mtindo ambao neno au kiyambo hicho kimetumika. Mfano mtindo wa kilahaja, mtindo wa wakati, mtindo wa kieneo, au hata mtindo wa taaluma ua fani fulani. Ni lazima tukiri kwamba kuna marifa ya lugha lakini wakati huo huo kuna ulimwengu halisi. Hii ni kwa maana kwamba katika maana hii, lazima mtumiaji wa lugha licha ya kufahamu maarifa ya lugha hio, lakini lazima azingatie ulimwengu halisi ambao lugha hio imetumika. Mfano matumizi ya mtindo wa kilahaja, kuna baadhi ya maneno kiuhalisia huibua hisia zingine na wakati mwingine kushindwa kufahamika kutokana na tofauti za kilahaja. Mfano maneno kama vile, shule, ugali na bomba, maneno haya yanaweza kutumika katika hali tofauti kwa wakaazi wa Tanzania bara na visiwa vya Zanzibar. Kwa upande wa Zanzibar wangeweza kutumia skuli, sembe na mfereji kwa mfuatano. Hivyo basi, kwa mzungumzaji inampasa kujua ni akina nani anazungumza nao na nani wangeweza kumuelewa ingawa wate wana maarifa ya lugha moja.


Aidha, kuwepo kwa maana hisia ni ithibati tosha ya kuthibitisha kuwepo kwa maarifa ya lugha na wakati huohuo ulimwengu halisi katika dhana ya semantiki na pragmatiki zinazohusu maana. Tunapozungumzia maana ya hisia ni aina ya maana ambayo huibuka kutokana na hisia au mtazamo wa msemaji au mwandishi. Na maana hii huweza kuwasilishwa kwa njia mbalimabali zikiwemo, njia ya maana kama dokezi au njia isiyo ya moja kwa moja. Kwa mfano “kweli wewe ni kidume wa mbegu kwelikweli!” katika tungo hii ni vigumu kufahamu mzungumzaji amemaanisha nini ikiwa msikilizaji hatohusisha maana au kauli hii na ulimwengu halisi au muktadha ambao msemaji au mwandishi amezungumza au kukusudia, kwani maana ya msemaji itakua tofauti na maana ya msikilizaji atakayojengwa kwa kuzingatia tu maarifa ya lugha. Mathalani hapa tunaweza kusema kuwa, msemaji amekusudia huyu kijana ni mchapakazi kwelikweli. Au kwa waswahili wanakawaida ya kumsifia mtu kwa kusema kwa mfamo, huyu mchezaji yaani hafai, mshenzi kwelikweli! Kiuhalisia neno hafai linamaanisha hali hasi ya mtu, vile vile mshenzi ni neno linalotaswira mbaya ya ufedheheshaji, lakini waswahili husema hivyo kuonesha sifa njema za mtu, tofauti n auhalisia. Hivyo kwa mtu kufasiri maana kulingana na maarifa ya lugha inapelekea kupotosha maana iliyokusudiwa.

Maana tangamani. Hii ni maana inayopatikana kutokana na matumizi ya lugha kulingana na muktadha husika wa matumizi kwa kuzingatia maana ya maneno mbalimbali na jinsi yanavyotumiwa kwa pamoja ili kuleta maana iliyokusudiwa. Maana hii pia inatuthibitishia kuwepo kwa maariufa ya lugha na wakati huohuo ulimwengu halisi. Hii inamana kuwa si kujua tu maariufa ya lugha ndio kuweza kuitumia lugha hio, lakini ni kwa vipi lugha hio ingeweza kutumika. Kwa mfano kauli kama vile “Mabibi na mabwana”, mvulan amtanashati, dada mrembo. Ukichunguza tungo hizi utagundua kuwa si kufahamu tu maarifa ya lugha, bali lazima mtumiaji afahamu ulimwengu halkisi wa matumizi ya maneno hayo. Mfano msemaji angeweza kusema, ‘mabibi na mababu” au “dada mtanashati” na ‘mvulana mrembo” jambo ambalo lisengekubalika kajika jamii za waswahili.

Maana mangwi au akise. Ni aina ya maana ambayo huibuka katika hali ambayo maana moja hukonyeza maana nyingine na hivyo humfanya mtu afikirie maana nyingine pia. Mfano kauli “naenda kujisaidia” Katik tungo hii inahitaji mtumiaji wa lugha au msikilizaji kufahamu ulimwengu halisi, yaani wanajamii fulani wanavyosema kujisaidia wanamaanisha nini? Kwa mfano mara nyingio katika jamii za kiafrika kujisaidia humaanisha ima kuenda haja ndogo au kubwa. Jambo hili katu lisengefahamika kwa sababu tu ya kufahamu maariga ya lugha hio.

Mwisho ni maana ya dhamira au muhimu. Hii ni aina ya maana ambayo hutegemea kile ambacho mtoa ujumbe ana kipa umuhimu zaidi. Mara nyingi kile kinachopewa umuhimu zaidi hutokeza mwanzoni mwa senmtensi. Msingi wa kupata maana katika aina hii inathibitisha kuwa pamoja na kuwa na marifa ya lugha pia panakuwepo n aulimwengui halisi wa lugha. Kupitia aina hii ni vigumu mtu kutambua umuhimu wa msemaji au mzungumzaji kwa msingi tu wa maarifa ya lugha bila kuhusisha hali gani lugha hio imetimika. Mfano kauli ya kusema “Kikwete atashinda uchaguzi wa mwaka 2015” Katika mfano huu umuhimu zaidi upo kwa Kikwete ndiye ambaye ana tarajiwa kushindsa uchaguzi na sio uchaguzi wala mwaka 2015. Haya yote yatabainika ikiwa tu msikilizaji atakuwa anamaarifa ya lugha na wakati huohuo anaujua ulimwegu halisi.

Kwa kuhitimisha tunaweza kusema kuwa, semantiki na pragmatiki zote kwa pamoja zinahusiana, kwa mana kwamba zinajihusisha na maana ya maana katika lugha. Wala haitokuwa sahihi kudhani kwamba kufahamu tu maana ya viambajengo katika tungo, iwe neno, kirai, kishazi au hata sentensi kuwa ndio kufahamu kwa kile kilichokusudiwa bila kujali muktadha ambao neno hilo imetumika.

Hat hivyo, taaluma hizi bado zitaendelea kuwa tofauti kwa kuwa semantiki hujihusisha na maana za maneno au viyambo vya maneno kama vilivyo kupitia kwa masemaji na msikilizaji. Wakati huohuo pragmatiki hujishughulisha na jinsi gani muktadha unapelekea kupata maana ya kile kilichokusudiwa kulingana na muda mahsusi.

Aidha ifahamike kuwa Semantiki na Pragmatiki zote kwa pamoja zimelenga kutoa ufafanuzi kuhusu mchakato wa lugha na matumizi yake kulingana na muktadha wa uzungumzaji au utumikaji wake. Kama sehemu ya mfumo wa mazungumzo , sambamba na kufasiri na kufafanua mfumo fungamanifu wa mazungumzo katika lugha, na hili litafikiwa tu kwa kuzingatia maarifa ya lugha sambamba na ulimwengu halisi wa mazungumzo.




MAREJEO.

Geoffrey Finch, (2000). Linguistic Terms and Concepts. Palgrave Macmillan.

Jacob L. Mey, (2001). Pragmatics: An Introduction, 2nd ed. Wiley-Blackwell.

Richmond H Thomason (2012). What is semantics? Second version.

Wwww.wisegeek.com Publishing & Printing International Journal. (USA), downloaded on Friday, 30th May 2014, at 12:30 pm.

Yule, G. (1996). Pragmatics. Oxford: Oxford University Press.