Subcribe to our RSS feeds Join Us on Facebook Follow us on Twitter Add to Circles

Alhamisi, 22 Mei 2014

AINA ZA MANENO KATIKA LUGHA YA KISWAHILI.

  1. Nomino.

Nomino ni neno linalosimamia jina la kitu, mtu, mnyama, mahali, hali na kadhalika.

Aina za Nomino
  • Nomino za Kawaida
Haya ni majina ya kawaida yanayoweza kutumiwa kurejelea vitu mbalimbali, watu, wanyama, mahali na kadhalika. Nomino hizi zinaweza kuwa katika umoja au wingi kulingana na ngeli yake.
Kwa mfano nyumba, mbuzi, daktari, soko, kalamu, jua

  • Nomino za Kipekee
Haya ni majina maalum ya watu, mahali, bidhaa, kampuni, na kadhalika. Herufi ya kwanza ya nomino hizi huwa ni herufi kubwa. Nomino za kipekee haziwezi kubadilika, na hivyo basi hazina wingi.
Kwa mfano Tanzania, Nairobi, Anita, Gafkosoft, Athi, Kimbo, 

Tanbihi: Nomino ya kawaida inapotumika kutangulia au kurejelea nomino ya kipekee moja kwa moja, huandikwa kwa kutumia herufi ya kwanza kubwa. 
Kwa mfano Mlima Kilimanjaro, Waziri Mwasimba,  Chifu Mtesi, Mwalimu Makunza, Daktari Maraka

  • Nomino za Jamii
Nomino za jamii hurejelea kundi la vitu au wanyama, kwa ujumla. Aghalabu vitu vinavyorejelewa hutokea kwa makundi ya vitu mbili au zaidi. Nomino hizi hutumia wingi tu tunaporejelea makundi zaidi ya moja.
Kwa mfano  jozi la viatu, umati wa watu, bustani la maua, bunga la wanyama

  • Nomino za Wingi
Nomino hizi hurejelea vitu ambavyo hutokea kwa wingi na haziwezi kuhesabiwa. Vitu kama hivyo hutumia aina nyingine ya vipimo ili kurejelea kiasi chake. Nomino za wingi hazina umoja.
Kwa mfano maji, maziwa, changarawe, pesa, nywele

Tanbihi: Hauwezi kuhesabu pesa lakini unaweza kuhesabu sarafu za pesa kama vile shilingi, dola n.k 

  • Nomino za Vitenzi Jina
Nomino hizi huundwa kutokana na vitenzi kwa kuongeza kiungo KU mwanzoni mwa mzizi wa kitenzi.
Kwa mfano  kulima, kuongoza, kucheza, kulala
  • Kutembea kwake kutamfanya aanguke
  • Kuimba huku kunapendeza mno
  • Nomino za Dhahania

Haya ni majina ya hali au vitu ambavyo havionekani wale haviwezi kushikika. 
Kwa mfano  upendo, furaha, imani, elimu, ndoto, mawazo, maisha, usingizi

 2.Vitenzi

Vitenzi ni maneno yanayosimamia kitendo. Kila kitenzi huwa na shina la kitenzi (sehemu ndogo zaidi ya kitenzi ambayo ndiyo huwakilisha tendo hilo). Shina la kitenzi huambatanishwa na viambishi ili kutoa maana iliyokusudiwa kama vile mtendaji, mtendewa, wakati kitendo kinafanyika na pia kauli ya kitenzi hicho.
Angalia pia Mnyambuliko wa Vitenzi
Aina za Vitenzi
  1. Vitenzi Halisi
  2. Vitenzi Visaidizi + Vitenzi Vikuu
  3. Vitenzi Vishirikishi
  4. Vitenzi Sambamba

Vitenzi Halisi
Hivi ni vitenzi vinavyorejelea kitendo moja kwa moja. Vitenzi hivi haziambatanishwi na vitenzi vingine katika sentensi. Vitenzi halisi vinaweza kuambatanishwa na vitenzi 
Kwa mfano soma, kula, sikiza
  • Waziri Mwasimba aliwasili jana kutoka ng'ambo.
  • Kawia atapikia wageni.
  • Funga mlango wa dirisha.
Vitenzi Visaidizi na Vitenzi Vikuu
Vitenzi visaidizi hutumika kusaidia vitenzi vikuu katika sentensi ili kuleta maana inayokusudiwa kulingana na wakati au hali. 
Kwa mfano -kuwa, -ngali, 
  • Jua lilikuwa limewaka sana.
  • Bi Safina angali analala


Vitenzi Vishirikishi
Vitenzi vishirikishi hutumika kuelezea hali iliyopo au mazingira. Kuna aina mbili za vitenzi vishirikishi:

a) Vitenzi Vishirikishi Vikamilifu - havichukua viambishi vyovyote.
Kwa mfano ni, si, yu
  • Kaka yako ni mjanja sana. 
  • Huyo si mtoto wangu!
  • Paka wake yu hapa.
b) Vitenzi Vishirikishi Vipungufu - huchukua viambishi vya nafsi au ngeli. Vitenzi hivi vinaweza kusimama peke yake au vinaweza kufuatiliwa na vitenzi vikuu.
Kwa mfano ndiye, ndio, ndipo
  • Sanita ndiye mkurugenzi wa kampuni
  • Huku ndiko kulikoibiwa

Vitenzi Sambamba
Vitenzi vikuu viwili au zaidi vinapoandamana katika sentensi huitwa vitenzi sambamba. Aghalabu mojawapo ya vitenzi hivi hutumia viungo vingine kama vile KI, KA, PO, KU n.k
Kwa mfano -  alicheka akioga, alikula akashiba
  • Kidori alilima akachoka.
  • Mama ameenda kumtafuta baba.
  • Mwalimu alikuwa ameanza kufundisha Juma alipoingia darasani.



3.Viwakilishi

Viwakilishi vya Nomino ni maneno yanayotumika badala ya nomino. Kiwakilishi hakiwezi kuambatanishwa na nomino inayorejelewa.
Aina za Viwakilishi

Viwakilishi vya Nafsi
Viwakilishoi hivi hutumika kwa niaba ya nafsi kwa umoja na kwa wingi
Kwa mfano mimi, wewe, yeye, sisi, nyinyi, wao
Nafsi Umoja Wingi
Nafsi ya Kwanzamimisisi
Nafsi ya  Piliwewenyinyi/ninyi
Nafsi ya Tatuyeyewao
  • Sisi tuliwatangulia nyinyi kufika hapa.
  • Mimi si mjinga kama vile yeye anavyofikiria
Viwakilishi Viashiria
Viwakilishi viashiria (vionyeshi) hutumika badala ya nomino kwa kutumia kuonyesha nomino inayorejelewa bila kuitaja.    
Kwa mfano  huyu, yule, hapa, n.k
  • Hiki hakina maandishi yoyote.
  • Hao hawajui tofauti ya viwakilishi na vivumishi
  • Tumekuja hapa ili kuwaburudisha kwa nyimbo tamu tamu.


Viwakilishi Visisitizi
Hutumika kwa niaba ya nomino kwa kutumia kiashiria chake mara mbili mfululizo.
Kwa mfano yuyu huyu, wawa hawa, kiki hiki, papo hapo, mumu humu, 
  • Zizi hizi ndizo zilizovunjika wiki jana
  • Yule yule aliyekamatwa juzi, ameiba tena


Viwakilishi vya Sifa
Husimama badala ya nomino kwa kurejelea sifa yake.
Kwa mfano  -eupe, -zuri, -tamu, -embamba, -rembo
  • Vyekundu vimehamisha
  • Warembo wamewasili.
  • Kitamu kitaliwa kwanza.

Viwakilishi vya Idadi
Hutumika kusimama badala ya nomino kwa kurejelea idadi yake.
a) Idadi Kamili - hutumia nambari kuelezea idadi ya nomino
Kwa mfano saba, mmoja, ishirini
  • Wawili wamepigwa risasi polisi leo jioni.
  • Alimpatia mtoto wake hamsini kununua chakula
b) Idadi Isiyodhihirika - huelezea kiasi cha nomino kwa ujumla, bila kutaja idadi kamili
Kwa mfano chache, nyingi, kadhaa, kidogo, wastani
  • Tutazungumza na wachache kabla ya kuanzisha maonyesho yetu.
  • Kadhaa zimeripotiwa kupotea.


Viwakilishi Viulizi
Viwakilishi viulizi hutumika kwa niaba ya nomino katika kuulizia swali.
Baadhi ya viwakilishi viulizi huchukua viambishi vya ngeli
Kwa mfano -ngapi?, -pi?
  • Vingapi vinahitajika? - kuulizia idadi
  • Zipi zimepotea? 

Kunavyo viwakilishi viulizi vingine ambavyo havichukui viambishi vyovyote.
Kwa mfano wapi?, gani?,  nini?, vipi?
  • Gani imefunga bao hilo?
  • Wapi hapana majimaji?
  • Yule mvulana alikupatia nini?
  • Uliongea naye vipi? - kuulizia namna

Viwakilishi Vimilikishi
Viwakilishi hivi hurejelea nomino kwa kutumia vimilikishi.
Kwa mfano  -angu, -ako, -ake, -etu, -enu, -ao 
  • Kwetu hakuna stima.
  • Lake limekucha.
  • Zao zimeharibika tena
Viwakilishi Virejeshi
Hutumia O-rejeshi kurejelea na kusimamia nomino
Kwa mfano ambaye, ambao, ambalo, ambacho, huyo, yule
  • Ambalo lilipotea limepatikana.
  • Ambaye hana mwana, aeleke jiwe
Viwakilishi Vya A-Unganifu

Huwakilishi nomino kwa kutaja kinachomiliki nomino hiyo. Huundwa kwa kuambatanisha kiambishi cha nafsi/ngeli pamoja na kiambishi -a cha a-unganifu, kisha nomino nyingine
Kwa mfano cha, la, kwa, za, ya
  • Cha mlevi huliwa na mgema
  • Za watoto zitahifadhiwa.


Muundo wa Vitenzi
  1. Vitenzi vya Silabi Moja
  2. Vitenzi vya Kigeni
  3. Vitenzi vya Kawaida
Vitenzi vya Silabi Moja
Hivi ni vitenzi vyenye silabi moja pekee. Ili kuleta maana kamili, vitenzi hivi huambatanishwa na kiungo KU- katika kauli ya kutenda. Kama vitenzi vingine, vitenzi vya silabi moja vinaweza kunyambuliwa.

mfano:
  • -cha - kucha - jua linapochomoza asubuhi k.m kumekucha 
  • -fa kufa - kuacha kupumua, kupoteza uhai  k.m amekufa 
  • -jakuja - fika mahali hapa k.m nimekuja  
  • -lakula - kutia chakula mdomoni k.m anakula
  • -nyakunya - kutoa mabaki ya chakula toka tumboni k.m mtoto amekunya  
  • -nywakunywa - kutia kinywaji kama vile maji au maziwa mdomoni k.m ninakunywa uji
  • -pakupa - kumkabithi/kumpatia mtu kitu k.m amenipa pesa
  • -pwakupwa - kujaa hadi pomoni - k.m kisima kimekupwa maji
  • -takuta -   
  • -twakutwa - jua linapozama magharibi na usiku kuingia  k.m kumekutwa 
  • -wakuwa - kutokea katika hali au mahali fulani  k.m alikuwa 
Angalia mengi zaidi kuhusu vitenzi vya silabi moja katika ukurasa huu wa Mnyambuliko




Vitenzi Vya Kigeni
Hivi ni vitenzi vyenye asili kutoka kwa lugha nyingine badala ya Kibantu. Baadhi ya lugha hizo ni Kiarabu, Kizungu, Kireno, Kihispania n.k. Vitenzi hivi havifuatilii muundo wa kawaida wa vitenzi vya Kiswahili ambavyo huishia kwa sauti -a. Badala yake, vitenzi hivi huishia kwa sauti nyingine kama vile -e, i, -o, na u

mfano:
  • haribu
  • tubu
  • shukuru
  • salimu
  • thamini
  • amini
  • samehe
  • baleghe

Vitenzi Vya Kibantu
Hivi ni vitenzi vyenye asili ya Kibantu na ambavyo huishia kwa sauti -a. Kitengo hiki hujumuisha asilimia kubwa zaidi ya vitenzi vya Kiswahili
mfano:
  • simama
  • shika
  • tembea
  • beba
  • soma
  • lia



























4.Vivumishi


Vivumishi au visifa ni maneno yanayotuelezea zaidi kuhusu nomino. Aghalabu vivumishi hutanguliwa na nomino. 
Aina za Vivumishi

Vivumishi vya Sifa
Hivi ni vivumishi ambavyo hutoa sifa ya kitu, mtu, mahali, n.k
Kwa mfano kizuri, kali, safi, mrembo
  • Yule mama mweusi hupika chakula kitamu.
  • Mvulana mkorofi aliadhibiwa na mwalimu kutokana na tabia zake mbaya.
  • Sauti nzuri humtoa nyoka mkali pangoni
Vivumishi Vimilikishi
Vivumishi hivi hutumika kuonyesha nomino inamiliki nyingine. Mizizi ya vivumishi hivi huundwa kulingana na nafsi mbalimbali.  -angu, -ako, -ake, -etu, -enu, -ao
Kwa mfano changu, lako, yake, kwetu, vyenu, zao
  • Nitatumia talanta zangu kwa manufaa ya taifa letu.
  • Aliweka kitabu chako sebuleni mwako
  • Katosha amepata nguo yake miongoni katika sanduku lao.

Vivumishi vya Idadi
Hutueleza zaidi kuhusu kiasi, au idadi ya nomino. Kuna aina mbili za vivumishi vya idadi.
a) Idadi Kamili - hutumia nambari kuelezea idadi ya nomino
Kwa mfano tatu, mbili, kumi
  • Msichana mmoja amewauwa nyoka wawili
  • Siku kumi zimepita tangu Bi Safina alipojifungua watoto watatu
b) Idadi Isiyodhihirika - huelezea kiasi cha nomino kwa ujumla, bila kutaja idadi kamili
Kwa mfano chache, nyingi, kadhaa, kidogo, wastani
  • Watu wachache waliohudhuria mazishi ya Kajuta walikula chakula kingi sana.
  • Baba yao alikuwa mateka kwa miaka kadhaa



Vivumishi Viulizi
Vivumishi viulizi hutumika kuuliza swali. 
Baadhi ya vivumishi viulizi huchukua viambishi vya ngeli
Kwa mfano -ngapi?, -pi?
  • Ni walimu wangapi wamefukuzwa? - kuulizia idadi
  • Je, ni dawati lipi lenye funguo zangu? 

Kunavyo vivumishi viulizi vingine ambavyo havichukui viambishi vyovyote.
Kwa mfano wapi?, gani?
  • Unazungumza kuhusu kipindi gani?
  • Je, mmefika mahali wapi? - kuulizia mahali



Vivumishi Viashiria / Vionyeshi
Vivumishi viashiria hutumika kuonyesha au kuashiria nomino kulingana na mahali.
Kwa mfano 
Karibu -  hapa, huyu, hiki, hili, huku, haya, ule, wale, pale
Mbali kidogo - hapo, huyo, hiyo, hicho
Mbali zaidi - pale, lile, kile, 
  • Msichana huyu ni mkubwa kuliko yule
  • Jani hili la mwembe limekauka
  • Tupa mpira huo
Vivumishi Visisitizi
Husisitiza nomino fulani kwa kurudia rudia kivumishi kiashiria
Kwa mfano yuyu huyu, wawa hawa, kiki hiki, papo hapo, mumu humu, 
  • Jahazi lili hili
  • Wembe ule ule
  • Ng'ombe wawa hawa
Vivumishi Virejeshi
Hivi ni vivumishi ambavyo hurejelea nomino. Vivumishi hivi vinaweza kuwa vivumishi vya O-rejeshi au vivumishi viashiria vinapotumika kurejelea nomino.
Kwa mfano ambaye, ambao, ambalo, ambacho, huyo, yule
  • Msichana ambaye alikuja ni Sheila
  • Sauti ambayo uliisikia ilikuwa ya Mzee Kasorogani
  • Mti ule mkubwa umeanguka.
Vivumishi vya KI-Mfanano
Vivumishi vya KI- ya Mfanano hutumika kulinganisha sifa ya nomino na hali au tabia nyingine.  Vivumishi hivi hutanguliwa na nomino, kiunganishi cha A-unganifu na huchukua kiungo KI.
Kwa mfano  wa kifalme, za kijeshi, ya kitajiri, n.k
  • Chifu wa Vikwazoni anaishi maisha ya kimasikini
  • Chali anapenda kusikiliza mziki wa kizungu
  • Bi Naliza huvulia mavazi ya kifalme.


Vivumishi Vya A-Unganifu
Vivumishi hivi hutuelezea zaidi kuhusu nomino kwa kuonyesha kitu kinachomiliki nomino hiyo. Huundwa kwa kuambatanisha kiambishi cha nafsi/ngeli pamoja na kiambishi -a cha a-unganifu, kisha nomino
Kwa mfano cha, la, kwa, za, ya
  • Watoto wa mwalimu mkuu wana tabia nzuri
  • Chai ya daktari imemwagika


5.Vielezi.


Vielezi ni maneno yanayotoa habari zaidi kuhusu kitendo kilivyofanyika. Pia vielezi hutoa habari zaidi kuhusu hali, vivumishi na vielezi vingine.
Aina za Vielezi


  1. Vielezi vya Namna
  2. Vielezi vya Mahali
  3. Vielezi vya Idadi
  4. Vielezi vya Wakati

Vielezi vya Mahali

Vielezi vya mahali hutoa habari kuhusu mahali ambapo kitendo kilifanyika. Aghalabu vielezi hivi huundwa kwa kutumia jina la mahali au kwa kuongeza kiungo -NI mwishoni mwa neno linaloashiria mahali.
Kwa mfano nyumbani, kazini, shuleni
  • Mtoto huyo hajatulia nyumbani tangu alipotoka Mombasa.
  • Msipitie sokoni mkienda kanisani.
Vielezi vya Wakati
Huelezea zaidi kuhusu wakati kitendo kipofanyika
Kwa mfano jioni, jana, asubuhi, saa saba, mwaka juzi
  • Mzee Kasorogani amesema kwamba ataoga mwaka ujao
  • Musa alilazimishwa kuchimba mtaro saa sita usiku
  • Kisaka na Musa watakutana kesho


Vielezi vya Idadi/Kiasi
Vielezi vya idadi hutulezea kitendo kilifanyika mara ngapi

a) Idadi Kamili - hutaja idadi kamili ya mara ngapi kitendo kilifanyika
Kwa mfano mara mbili, siku mbili kwa juma, mara kumi
  • Gibi alimzaba kofi mara tatu na kisha akakimbia.
  • Daktari alimwagiza mama huyo achukue dawa mara tatu kwa siku  na arudi hospitalini siku mbili kwa mwezi
b) Idadi Isiyodhihirika - huelezea kiasi cha nomino kwa ujumla, bila kutaja idadi kamili
Kwa mfano mara chache, mara kwa mara, mara nyingi, mara kadhaa
  • Mwizi wa kuku alipigwa mara kadhaa kabla ya kuokolewa na polisi.
  • Yeye hunipigia simu mara kwa mara



6.Viunganishi.

 

Viunganishi ni maneno yanayoutumika kuunganisha, kulinganisha au kuonyesha uhusiano wa dhana mbili au zaidi.

Viunganishi vya A-Unganifu (Vimilikishi)Viunganishi vya ngeli huundwa kwa kufungamanisha viambishi viwakilishi vya ngeli pamoja na kiungo -a
Kwa mfano:
    • wa
    • la
    • za
    • vya
    • mwa
    • pa
    • cha
    • ya
  • Kiungo KWA-  hutumika kuonyesha umiliki wa mahali, sababu, ala/kitumizi, mbinu na kadhalika. Soma ukrasa huu ili ujue matumizi zaidi ya kiungo KWA

Kujumuisha
Kwa mfano:
    • Na
    • Pia
    • Pamoja na
    • Licha ya 
    • Fauka ya
    • Zaidi ya
    • vilevile

Kuonyesha Tofauti - Jambo kufanyika kinyume na matarajio
    • bila - 
    • bali -
    • ila - 
    • lakini - 
    • tofauti na - 
    • kinyume na - 
    • hata hivyo - 
    • ingawa - 
    • ingawaje - 
    • japo
    • ijapokuwa
    • ilhali
    • ijapokuwa
    • minghairi ya
    • dhidi ya


Kuonyesha Sababu

    • ili
    • kwa
    • kwa vile
    • kwa maana
    • kwa kuwa
    • kwani
    • kwa minanjili ya
    • maadam
    • madhali



Kuonyesha Matokeo

    • basi
    • kwa hivyo
    • hivyo basi
    • ndiposa
Kuonyesha Kitu kimoja kama sehemu ya kingine

    • Katika
    • Miongoni mwa
    • Baadhi ya
    • Mojawapo ya

Kuonyesha Kitendo kufanyika baada ya kingine

    • Kisha
    • halafu
    • basi


Kuonyesha Kitu kufanyika badala ya kingine

    • Badala ya
    • kwa niaba ya
    • kwa
Kulinganisha

    • Kama
    • Kuliko
    • Sawa na
    • Vile




Kuonyesha uwezekano

    • Labda
    • Pengine
    • Ama
    • Au
    • huenda










Kuonyesha Masharti

    • Ikiwa
    • Iwapo
    • bora
    • Al muradi

7.Vihusishi.

Vihusishi ni maneno yanayotuarifu zaidi kuhusu uhusiano wa nomino na mazingira yake
Kuna aina mbili za Vihusihi
  1. Vihusishi vya Mahali
  2. Vihusishi vya Wakati

Vihusishi vya Mahali
  • Juu ya
  • Chini ya
  • Kando ya 
  • Karibu na
  • Mbali na
  • Mbele ya
  • Nyuma ya
Vihusishi vya Wakati
  • Kabla ya
  • Baada ya

8.Vihisishi.

Vihisishi (I) ni maneno yanayotumika kuonyesha hisia kama vile hasira, furaha, mshangao n.k


Mifano ya Vihisishi
  • Lo!
  • Salaale!
  • Masalale!
  • Kumbe!
  • Po!
  • Ng'o!
  • Hata!
  • Akh!
  • AkaI
  • Ah!
  • Ala!
  • Haha!
  • Haya!
  • Ehee!
  • Hmmm!
  • Ebo!
  • Kefule!
  • Wee!
  • La!
  • Hoyeee!
  • Huraa!




Vielezi vya Namna

Huelezea jinsi au namna kitendo kinavyofanyika. Kitendo kinaweza kufanyika kwa namna mbalimbali. Hivyo basi kuna aina mbalimbali za vielezi vya namna:

    
a) Vielezi Halisi
Hutufahamisha jinsi kitendo kinavyofanyika kwa kutumia maneno halisi (bila kuambatanishwa na maneno mengine au viambishi vingine). 
Kwa mfano  vizuri, ovyo, haraka,
    • Kioo cha bibi harusi kilianguka na kuharibika vibaya
    • Mama alipika chakula upesi
    • Amepigwa kalamu kwa kufanya kazi kiholela
b) Vielezi Hali
Hutufahamisha hali ambayo kitendo kilifanyika. Vielezi hivi hujihusisha na tabia ya kitu/mtendaji wa kitendo 
Kwa mfano kwa furaha, kwa makini, 
  • Bibi harusi aliingia kanisani kwa madaha
  • Mtoto alilia kwa maumivu mengi
c) Vielezi Vitumizi/ala
Hutoa habari kuhusu kifaa, ala au mbinu iliyotumiwa kufanya kitendo fulani
Kwa mfano kwa kisu, kwa jembe, kwa meno, kwa moto, kwa maji
  • Mkulima aliangusha mti mkubwa kwa shoka
  • Mzee huyo alimpiga mke wake kwa bakora kabla ya kuchoma nguo zake kwa makaa
d) Vielezi Vikariri
Husisitiza kitendo kinavyofanyika kwa kutaja kielezi kinachorejelewa mara mbili mfululizo. 
Kwa mfano  haraka haraka, ovyo ovyo, juu juu
    • Polisi walipoingia, wezi walitawanyika haraka haraka.
    • Wanafunzi wengi hufanya kazi yao ovyo ovyo
e) Vielezi Mfanano
Vielezi mfanano hutumia KI-mfanano kuelezea kitendo kinavyofanyika kwa kulinganisha.
Kwa mfano kitoto, kiungwana,  
  • Babake huongea kiungwana.
  • Harida hutembea kijeshi
f) Vielezi Viigizi
Vielezi hivi huigiza sauti au mlio wa kitu, kitendo kitendo kilipofanyika kwa kutumia tanakali za sauti
Kwa mfano tuli, chubwi, tifu, chururu, 
  • Mwanafunzi alitulia tuli mwalimu alipomzaba kofi pa!
  • Kaswimu aliangusha simu changaraweni tifu na kujitumbukiza majini chubwi
g) Vielezi vya Vielezi
Vielezi hivi hutumika kuelezea kielezi kingine. Hivyo basi, hutanguliwa na kielezi badala ya kitendo. 
Kwa mfano  sana, kabisa, hasa, mno, 
    • Mamake Kajino alitembea polepole sana.
    • Chungu kilivunjika vibaya kabisa
h) Vielezi vya Vivumishi
Hutoa habari zaidi kuhusu kivumishi
Kwa mfano sana, kabisa, hasa, mno 
  • Yeye ni mrefu sana
  • Mtoto wake ana tabia nzuri mno
 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni