Subcribe to our RSS feeds Join Us on Facebook Follow us on Twitter Add to Circles

Jumatatu, 19 Mei 2014

FANI NA MAUDHUI KATIKA FASIHI


FANI NA MAUDHUI KATIKA FASIHI
FANI: huu ni ufundi wa kisanaa autumiao msanii katika kutoa ujumbe wake kwa hadhira iliyokusudiwa. Katika fani kumegawanyika vipengele mbalimbali kama vile wahusika, mitindo, muundo, mandhari, matumizi ya lugha, kufaulu na kutokufaulu kifani. Vipengele muhimu vinavyoangaliwa ni hivi vifuatavyo:
Mtindo; hii ni mbinu ya kipekee kifani na kimaudhui, zinazotofautisha msanii mmoja na mwingine.
Muundo; huu ni mpangilio wa kiufundi anaoutumia mwandishi katika kupangilia kazi yake.
Wahusika; hawa ni watu au viumbe ambavyo mwandishi wa fasihi huwatumia ili kufanikisha ujumbe kwa jamii husika. Katika kazi ya fasihi mwandishi huwagawa wahusika katika makundi mawili yaani wahusika wakuu na wahusika wadogo.
Wahusika wakuu ni wale ambao wanajitokeza kuanzia mwanzo mpaka mwisho wa kazi ya fasihi. Wahusika wadogo ni wale wote ambao wanajitokeza sehemu mbalimbali katika kazi ya fasihi kwa mfano, mwanzoni mwa kitabu hadi mwishoni mwa kitabu.
Mandhari; hii ni sehemu ambayo matukio ya hadithi au masimulizi hutokea. Mandhari huweza kuwa halisi au ya kufikirika.
Maudhui; Maudhui katika kazi ya fasihi ni jumla ya mawazo yote yanayozungumzwa pamoja na mtazamo wa mwandishi juu ya mawazo hayo. Maudhui hujumuisha mawazo pamoja na mafunzo mbalimbali yaliyomsukuma msanii hadi akatunga na kusanii kazi fulani ya kifasihi. Vipengele vya maudhui ni pamoja na dhamira, migogoro, falsafa ujumbe na msimamo.
Dhamira; hili ni wazo kuu au mawazo mbalimbali yanayojitokeza katika kazi ya fasihi. Senkoro anataadharisha maana hii isichanganywe na maudhui kwani dhamira ni sehemu tu ya maudhui na aghalabu dhamira kuu ndio hujenga kiini cha kazi ya fasihi. Dhamira zimegawanyika katika makundi mawili, kuna dhamira kuu na dhamira ndogondogo.
Migogoro; ni mivutano na misuguano mbalimbali katika kazi za fasihi. Migogoro inaweza kuwa kati ya wahusika, familia zao, matabaka yao, au hata katika nyadhifa mbalimbali.
Vilevile migogoro yaweza kuwa ya kiuchumi, kijamii, mogogoro ya nafsi, na migogoro ya kisiasa ambayo hujitokeza katika mitazamo tofauti kulingana na mtiririko wa visa na matukio yanavyopangwa na mwandishi.
Kwa ujumla suluhisho la migogoro yote ni jamii kuwa na haki na usawa kuondoa chuki, kuondokana na uvivu, kushirikiana katika kuwafichua wale wanaotumia mali ya umma kwa kujinufaisha wenyewe.
Ujumbe; mwandishi anapoandika kazi yake huwa na ujumbe ambao hutaka uifikie jamii aliyoikusudia. Ujumbe katika kazi fasihi ni mafunzo mbalimbali ambayo hupatikana baada ya kusoma kazi ya fasihi. Katika kazi ya fasihi dhamira kuu hubeba ujumbe wa msingi na dhamira ndogondogo hubeba ujumbe ambao husaidia kuujenga au kuupa uzito zaidi ujumbe wa msingi.
Msimamo; katika kazi ya fasihi, mawazo, mafunzo na falsafa ya msanii hubainisha msimamo wake kuhusu masuala mbalimbali ya kijamii. Msimamo ni ile hali ya mwandishi kuamua kufuata na kushikilia jambo fulani. Jambo hili huweza kukataliwa na wengi lakini akalishikilia tu. Msimamo ndio huweza kuwatofautisha wasanii wawili au zaidi wanaoandika kuhusu mazingira yanayofanana.
UHUSIANO WA FANI NA MAUDHUI KATIKA FASIHI
Fani na maudhui ni dhana mbili ambazo hazitenganiki. Kuna mitazamo miwili ambayo inajaribu kutazama uhusiano wa fani na maudhui katika kazi za fasihi andishi. Mitazamo hiyo ni ya kidhanifu na kiyakinifu.
Katika mtazamo wa kidhanifu wapo wataalam mbalimbali ambao wametoa maelezo yao kuhusu uhusiano wa fani na maudhui katika kazi za fasihi andishi.
Tukianza na Bi. Materu, yeye anasema fani na maudhui ni kama mwili na nguo hivyo anatoa maoni kuwa fani na maudhui ni dhana ambazo zinaweza kutenganishwa kama vile mwili unavyoweza kutenganishwa na nguo. Bi. Materu anasema maudhui ni mwili ambao ndilo umbo la ndani la kazi ya fasihi, wakati nguo ndio fani ambayo ni umbo la nje la kazi ya fasihi.
Fauka ya hayo Mtaalam mwingine ni Penina Muhando (Mlama), anasema kuwa fani na maudhui ni kama sahani na chakula. Sahani yaweza kutengwa na chakula pale ambapo chakula hicho kitaondolewa. Penina Muhando anasema, chakula ndio maudhui yaani umbo la ndani la kazi ya fasihi na sahani ndio fani ambayo ni umbo la nje la kazi ya fasihi. Hivyo yeye anaona kuwa fani na maudhui ni dhana mbili ambazo zinaweza kutenganishwa na bila athari yoyote.
Naye T. Sengho anasema kuwa fani na maudhui ni kama chungwa na ganda, akiwa na maana kuwa chungwa ndio maudhui na ganda ndio fani. Hapa T. Sengho anatoa msimamo kuwa fani na maudhui vinaweza kutenganishwa bila ya athari, kwani chungwa linaweza kutengwa na ganda lake.
Mtaalam mwingine anayeegemea mtazamo wa kidhanifu anasema kuwa fani na maudhui ni kama kikombe na chai. Huyu ni Mtaalam F. Nkwera ambaye anasema kuwa chai ndio maudhui na fani ndio kikombe. Hapa F. Nkwera anataadharisha kuwa chai inaweza kunywewa kwenye kikombe na kikombe kubakia kitupu, hivyo fani yaweza kutengwa na maudhui kama vile chai inavyoweza kutengwa na kikombe.
Katika mtazamo wa kiyakinifu, Senkoro anasema kuwa fani na maudhui ni sawa na sarafu. Hapa anamaanisha kuwa fani na maudhui ni dhana mbili zisizoweza kutenganishwa kama vile pande mbili za sarafu moja.
Senkoro F. E. M. K. anasisitiza kuwa fani na maudhui havitenganishiki bali hutegemeana ili kazi ya fasihi iweze kuwa bora zaidi. Kazi ya fasihi ambayo maudhui yamezidi fani huwa chapwa au fani ikizidi maudhui, kazi hiyo ya fasihi huwa chapwa, hivyo maudhui na fani ni dhana ambazo hutemeana. Fani na maudhui lazima vilingane na kushabihiana ili kazi yenyewe iweze kuwa bora na yenye mvuto zaidi.
Mtazamo mwingine unadai kuwa fani na maudhui hulinganishwa na roho na mwili ambapo haiwezi kutenganishwa na mwili kwani kwa kufanya hivyo athari itakayotokea ni kwamba mwili hautaweza kufanyakazi ipasavyo pasipo roho.
Vilevile tunaweza kufananisha fani na maudhui kama gari na injini. Hii ni dhana ambayo inajidhihirisha kuwa gari haliwezi kutenda bila injini, hivyo ni kuweza kuthibitisha kuwa fani na maudhui ni dhana mbili zisizotenganishwa kwani huleta athari zinapotenganishwa na vilevile fani na maudhui hutenda kazi pamoja.

UKUMUSHAJI


SWALI” Jadili dhana ya ukumushaji na sifa zake kwa kutumia mifano sahihi.

UKUMUSHAJI
Ni dhana ambayo hutoa maelezo zaidi au
Ya ziada kuhusu nomino, kivumishi, kitenzi, kielezi au kikundi cha maneno
KIKUMISHI
Ni neno , kirai au kishazi ambacho hutoa maelezo ya ziada kuhusu nomino, kivumishi, kitenzi, kielezi au kikundi cha maneno. Aidha, kikumushi huweza kuwa sentensi itoayo maelezo zaidi kuhusu sentensi nyingine.
Mfano.
Mtoto aliyekuja juzi ameondoka.
Katika sentensi hii kishazi tegemezi “ aliye kuja juzi” ni kikumushi ambacho kinatoa maelezo ya ziada kuhusu nomino “ mtoto:.
Mwanafunzi mrefu sana ameanguka.;
Neno “sana” ni kikumushi kinachotoa maelezo ya ziada kuhusu kivumishi “ mrefu”
Mifano zaidi
Gari lilikimbia kwa kasi sana
Maduhu anaimba vizuri mno
Ninapenda unavyosema.
Mwalimu aliye kwenda dukani jana amerudi.
Kimsing ukumushaji ni dhana pana zaidi ya uvumishi, kwani ukumushaji hutoa maelelezo zaidi kuliko uvumishaji. Pia kivumishi kipo katika kategoria ya kileksika lakini kikumushi kipo katika kategoria amilifu ya isimu miundo


MAZINGIRA YA UTOKEAJI WA UKUMUSHAJI
Ukumushaji unaweza kutokea baada ya nomino
Kwa mfano:
Kitabu kizuri kimepotea

Wanafunzi wapole wamefaulu mitihani yao vizuri

Askari katili ameuwa

Kijana mtiifu amezadiwa kitabu
Baada ya kiwakilsishi pia kikumishi kinaweza kutokea
Kwa mfano
Wale watundu wamefukuzwa shule

Yule msafi ameondoka chuoni
Kikumishi huweza kutokea baada ya kivumishi
Kwa mfano
Mwanafunzi mrefu kuliko wote ameanguka

Mwimbaji mashuhuri sana amekodiwa Uganda

Mwalimu mlevi kupindukia ameachishwa kazi.
Vivyo hivyo kikumishi huweza kutokea baada ya kielezi
Kwa mfano
Juma anaimba vizuri

Mbwa mkali amejeruhiwa sana

Ninapenda anavyocheza

Mwanariadha anakimbia kwa kasi
Ukumushaji vilevile huweza kutokea baada ya kielezi
Kwa mfano
Juma anaimba polepole mno

Mharifu amejitetea vizuri sana

Mwanafunzi amewasilisha kazi kwa ujasili mwingi
Ukumushaji pia huweza kutokea baada ya kihusishi
Kwa mfano
Janeth anakula wali kwa mkono

Juma amekaa juu ya meza

Maria analia kwa uchungu

SIFA ZA UKUMUSHAJI
Hutoa maelezo ya ziada kuhusu nomino, kivumishi, kitenzi au kikundi cha maneno
Mfano:
Mvulana mwembamba amepotea
Neno “ Mwembamaba” ni kikumushi kinachotoa maelezo ya ziada kuhusu nomino “ mvulana”
Kijana mnene sana anacheka.
Neno “sana” ni kikumushi kinachotoa maelezo ya ziada kuhusu “kivumishi” mnene
Ninapenda unavyocheza
Neno “ unavyocheza “ ni kikumishi kinachotoa malelezo ya ziada kuhusu “ kitenzi” “Ninapenda”.
Mwalimu aliyekuja jana asubuhi ameondoka.
Neno “aliyekuja jana asubuhi” ni kikumushi kinachotoa maelezo ya ziada kuhusu nomino “ mwalimu”
Mchungaji anahubiri vizuri sana
Neno “ sana” ni kikumushi kinachotoa maelezo ya ziada kuhusu kielezi “ vizuri”
Kikumushi kinaweza kuondolewa kwenye tungo bila kupoteza maana ya msingi ya tungo hiyo.
Mfano
Mtoto mzuri amerudi
mtoto amerudi
Ninapenda unavyokula
Ninapenda
kikumushi huweza kuundwa na neno moja au kikundi cha maneno.
Mfano
mtoto anacheza vizuri sana (neno moja)

Msichana aliyekaa mbele yangu ni msafi (kikundi cha maneno)

Kikumushi kipo katika kategoria amilifu ya isimu miundo ( mpangilio wa maneno katika tungo).
Mfano.
Msichana mrembo sana anacheka

Msichana mrembo anacheka
Kikumushi kinaweza kutokea mara moja au zaidi katika tungo
Mfano:
Ng’ombe aliyepotea jana asubuhi amepatikana leo asubuhi

Msichana anacheza vizuri sana na Baba analima vizuri sana.
Ukumushaji huweza kutokea kwenye kiima au kiarifu au pande zote kwa wakati mmoja
Mfano
Mvulana aliyetumwa kwenda kumletea mgonjwa dawa amerudi mapema mno.

Kijana aliyepotea jana ameonekana

Juma anatembea kwa madaha sana
Ukumushaji huweza kutokea katika sentensi changamano ambapo kishazi tegemezi huchukua nafasi ya kikumushi
Kwa mfano
Kijana aliyekuja jana ameondoka leo asubuhi

Mbuzi aliyezalia porini ameletwa nyumbani

Kitabu kilichoibiwa kimerudishwa

Nyimbo zilizoimbwa zinafurahisha
Kwa ujumla dhana ya ukumushaji na uvumishaji kwa jinsi tulivyojadili ni dhana ambazo zinafanana katika utendaji kazi wake lakini upekee wa ukumushaji ni kwamba huweza kutokea katika kikundi nomino pekee.
Hivyo basi ukumushaji ni mpana zaidi kuliko uvumishaji.



MAREJELEO
Matinde, S.R (2012) Dafina ya lugha, Isimu na Nadharia, Mwanza: Serengeti Educational Publishers (T) Ltd
Habwe, J na Karanja, P, (2004). Misingi ya sarufi ya Kiswahili; Nairobi- Kenya: phoenix publishers Ltd

Jumapili, 18 Mei 2014

MIKABALA YA TAALUMA YA SARUFI.


MIKABALA YA TAALUMA YA SARUFI.


(a) Sarufi ubongo
(b) Sarufi kama kaida za kiisimu.
(c) Sarufi kama tafiti na uchambuzi wa miundo inavyooneka kwenye lugha.

UTANGULIZI WETU UTAZINGATIA MAMBO YAFUATAYO.

· Maana ya sarufi.
· Mkabala wa kimapokeo.
· Mkabala wa kisasa.

MJADALA WETU UTAJIKITA KATIKA VIPENGELE VIFUATAVYO


Ufafanuzi wa sarufi ubongo
Ufafanuzi wa sarufi kama kaida za kiisimu
Ufafanuzi wa sarufi kama tafiti na uchambuzi wa miundo inavyooneka kwenye lugha.
Tofauti zilizopo katika mikabala hii.

Katika mjadala huu, kwanza kabisa tutaanza kwa kuangalia dhana muhimu ambazo zimejitokeza katika mada yetu, ambazo ni sarufi, mkabala wa kimapokeo pamoja na mkabala wa kisasa. Kisha tutangalia kwa kujadili kiini cha mada, ambapo tutaangalia jinsi sarufi ubongo, sarufi kama kaida za kiisimu na sarufi kama tafiti na uchambuzi wa miundo inavyooneka kwenye lugha na inaangukia katika mkabala upi na inatofautiana vipi.
Tukianza na maana ya sarufi kwa mujibu wa wataalamu mbalimbali kama vile:-
Kihore na wenzake (2005) wakimnukuu Gaynor (1968:88), wanaeleza kuwa sarufi ni sayansi ya muundo wa lugha pamoja na sheria, kanuni na matumizi yake ambayo kwa kawaida hukubalika kwa watumiaji wake.
Vile vile Mdee (1999) anafasili sarufi kama mfumo wa kanuni za lugha zinazomwezesha mzungumzaji kutunga sentensi nyingi sahihi na zenye kukubaliwa na wazawa wa lugha.
Pia Massamba na wenzake (1999:31) katika mtazamo wa pili wa kufasili dhana ya sarufi wanaeleza kuwa sarufi ni kanuni sheria au taratibu za uchambuzi zinazotawala lugha.
Hivyo basi wanasarufi hawa wanaonekana kukubaliana kwamba sarufi ni kanuni, sheria na taratibu zinazotawala lugha. Lakini kwa kiasi kikubwa tunakubaliana na fasili iliyotolewa na Mdee kutokana na kwamba ameweza kutufafanulia vizuri kanuni hizo na taratibu za lugha ndizo zinazomwezesha mzungumzaji kutunga sentensi nyingi, sahihi na zenye kukubaliwa na wazawa wa lugha.

Kwa mfano:- sentensi za kiswahili zina muundo wa
N + V + T + E
Mtoto mzuri anacheza uwanjani.
N V T E
Baada ya kuangalia dhana ya sarufi kwa mujibu wa wataalamu mbalimbali sasa tunaweza kuangalia mikabala mikuu miwili ya sarufi ambayo ni:-
i. Mkabala wa kimapokeo
ii. Mkabala wa kisasa.
Kwa kuanza na mkabala wa kimapokeo kwa mujibu Khamisi na Kiango (2002), wanaeleza kuwa hii ni sarufi ya kale, wataalamu wanaohusishwa na mkabala huu walijitokeza kuanzia karne ya 5 kabla ya kristo na katika karne ya 18 na karne ya 19 baada ya kristo, wataalamu hao ni kama vile Plato, Aristotle, Panin, Protagoras ambao walijihusisha na lugha kwa kutaka kujua asili yake ikiwa ni sehemu ya uchunguzi wa asili ya maumbo hususani walitaka kujua kama lugha ni tukio la maumbile au tukio la unasibu.
Pia Massamba na wenzake (wameshatajwa) wanaeleza kwamba sarufi mapokeo zilikuwa ni sarufi elekezi ambazo zilisisitiza kanuni na nini cha kusema na wajua lugha. Watu wasiojua kanuni za lugha wanapaswa kujifunza kutoka kwa wanaojua sarufi ya lugha. Wanaendelea kusema kuwa, wanaojua lugha hupaswa kutunga kanuni za sarufi.

Vile vile Habwe na Karanja (2004:124), wanadai kuwa mitazamo hii ya wanasarufi hawa wa kimapokeo iliathiri mbinu na njia za kuangalia lugha kwani sarufi mapokeo ilijikita katika lugha za kiulaya kama vile kiyunani na kilatini.

Sifa mbalimbali za lugha hizi ambazo ziliaminiwa kuwa bora, zilichunguza kilatini na kiyunani zilielezwa kuwa ni lugha duni na kutwezwa na kudhalilishwa
Sarufi mapokeo ilielekeza watu jinsi ya kutumia lugha, uelekezi huo hata hivyo ulijikita kwenye sheria za lugha ya kilatini kwa mfano sentensi haikupaswa kuishia na kihusishi wala kuanza na kiunganishi.
Udhaifu mkubwa wa sarufi mapokeo ni kwamba, taratibu za uchanganuzi wa lugha hazikuzingatia lugha ya kuzungumza kama ilivyo leo. Wanasarufi mapokeo walienzi na kuchunguza lugha ya maandishi. Hivyo basi ni dhahiri kwamba mkabala huu unaangukia katika mitazamo ya kifalsafa.
Hivyo basi ni wazi kuwa katika sarufi hii ya mapokeo tunakutana na mikabala miwili inayoangukia katika mkabala huu ambayo ni sarufi ubongo na sarufi kama kaida za kiisimu.
Mkabala wa pili, ni mkabala wa kisasa, unaoongozwa na wanasosiolojia ambao unahusisha sarufi mbalimbali kama vile :-

i. Sarufi msonge
ii. Sarufi miundo virai
iii. Sarufi geuza maumbo zalishi
iv. Sarufi husiano

Katika mkabala huu ndipo tunapata mkabala wa sarufi kama tafiti na uchambuzi wa miundo inavyooneka kwenye lugha.
Hivyo basi baada ya kujadili mikabala mikuu miwili ambayo ni mkabala wa kimapokeo na mkabala wa kisasa, zifuatazo ni sifa muhimu za sarufi ubongo, sarufi kama kaida za kiisimu na sarufi kama tafiti na uchambuzi wa miundo inavyooneka kwenye lugha ambazo kwazo tutaona jinsi kila moja inavyotofautiana na nyingine.
Kwa kuanza na sarufi ubongo, kwa mujibu wa Nordquist (2012), anaeleza kuwa sarufi ubongo ni sarufi endelevu ambayo inamwezesha binadamu kuzalisha lugha ambayo inaweza kueleweka kwa wengine

Pia Sharpe (2006), anaeleza kuwa sarufi hii hufananishwa na umilisi, anaendelea kueleza kuwa sarufi hii humwezesha mtu kuweza kusikia na kutambua kama sentensi hiyo ni sahihi au si sahihi.
Chomsky (1957), anaeleza kuwa kila binadamu amezaliwa na uwezo wa kuzalisha tungo mbalimbali zisizo na ukomo ambazo humpatia uwezo au uzoefu wa sarufi ya lugha. Pia anafafanua kwamba kila binadamu huzaliwa na kifaa katika ubongo wake ambacho kinamwezesha kuamili lugha ya aina yoyote, amekiita kifaa cha uamiliaji lugha (KIULU). Kwa mfano mtoto mdogo mwenye umri chini ya miaka saba anaweza kuamili lugha yoyote na mahali popote.

Mgullu (1999), anaeleza kuwa sarufi ubongo huchunguza jinsi binadamu anavyojifunza lugha kwa mfano hatua mbalimbali ambazo hupitia wakati anajifunza lugha yake ya kwanza.
Kwa hiyo tunakubaliana na fasili zote zilizotolewa na wataalamu hapo juu kutokana na kwamba sarufi ubongo, hii ni sarufi ambayo inachunguza jinsi binadamu anavyoweza kuamili lugha na kujifunza lugha pia kuweza kuzalisha sentensi mbalimbali ambazo anaweza kuzitumia katika mawasiliano.
Vile vile wataalamu wa mkabala huu hueleza kuwa upo uhusiano mkubwa kati ya akili, kufikiri na lugha bila shaka uhusiano huu ni ule wa taathira ya lugha yaani dhana inayoeleza kuwa kwa kawaida kila lugha huathiri watumiaji wake kwa kiasi kikubwa.
Vile vile wataalamu wa mkabala huu wanaeleza jinsi watu wanavyojifunza lugha ya pili au lugha ya tatu.
Kwa kifupi mkabala huu hujihusisha na mambo kadha kama vile:-
(i) Kumwezesha binadamu kuweza kuzalisha au kutunga sentensi mbalimbali.
(ii) Sarufi ubongo huusika na uamiliaji wa lugha na ujifunzaji wa lugha.
(iii) Sarufi hii huwakilisha maarifa ya mzungumzaji wa lugha (umilisi alionao mzungumzaji).
Mkabala mwingine wa sarufi ambao unaangukia katika mkabala wa sarufi mapokeo ni sarufi kama kaida za kiisimu.
Kwa mujibu wa Encyclopedia (1970), wanaeleza kuwa sarufi kaida ni mpangilio unaoonyesha au kueleza kanuni za kisarufi katika lugha ambazo hushughulika na kanuni za uundaji wa maneno, maumbo ya maneno, miundo ya maneno, miundo ya sentensi, vile vile inahusisha taarifa maalumu kuhusu fonetiki na fonolojia (taaluma inayohusika na utamkaji sahihi unaokubalika)
Pia kwa mujibu wa Babylon Dictionary (1997), wanaeleza kuwa sarufi kaida ni mfumo wa kisarufi ambao unafafanua kipi sahihi na kipi si sahihi katika lugha, pindi mzungumzaji anapozungumza, amezungumza sahihi au si sahihi.
Kwa hiyo tunaweza kueleza kuwa sarufi kaida hujishughulisha sana na:-
i. Kuelekeza namna ya matumizi sahihi ya lugha.
ii. Wataalamu wa lugha ndio wanaounda kanuni na miongozo ya lugha ambayo inatakiwa kufuatwa na wale wasiojua lugha.
Kwa mfano:- kanuni mojawapo ya miundo ya sentensi za Kiswahili huwa na muundo wa kiima na kiarifu.
Vile vile sentensi nyingi za Kiswahili huwa na muundo wa kirai nomino na kirai kitenzi.
Hivyo basi katika mkabala huu wa sarufi watu wasiojua lugha wanapaswa kufuata kanuni na taratibu zilizoundwa na wanaojua lugha kwa mfano wanasarufi.
Pia mkabala mwingine wa sarufi ambao unaangukia katika mkabala wa kisasa ni sarufi kama utafiti na uchambuzi wa miundo inayoonekana katika lugha.
Kwa mujibu wa Besha (2007), anaeleza kuwa huu ni mkabala unaohusika hasa na uchambuzi wa muundo wa lugha, sauti za lugha, muundo wa sentensi na hata maana za tungo za lugha.
Pia mgullu (1999), anaeleza kuwa lengo la mkabala huu ni kufafanua vipengele vyote vya lugha fulani kama vilivyo hivi sasa au vilivyokuwa wakati fulani.
Hivyo basi Besha na Mgullu wanakubaliana kuwa huu ni mkabala unaofafanua namna au jinsi watu wanavyozungumza lugha na sio kuwaelekeza waizungumze vipi lugha yao.
Hivyo basi kwa ujumla mkabala huu unajihusisha na mamba yafuatayo:-
i. Hautilii mkazo mabadiliko yaliyotokea katika lugha hata kama mabasiliko hayo yapo.
ii. Mkabala huu hauamuru watu waseme vipi na vipi wasiseme.
Kutokana na sifa mbalimbali zilizojitokeza katika mikabala hii, tumeweza kubaini tofauti zilizopo baina ya mikabala hii mitatu ambazo ni kama zifuatazo:-
Sarufi ubongo, sarufi kama kaida za kiisimu zinajitokeza katika mkabala wa kimapokeo wakati sarufi kama tafiti na uchambuzi wa miundo inavyooneka kwenye lugha inajitokeza katika mkabala wa kisasa.
Vilevile sarufi ubongo humwezesha binadamu kuweza kuzalisha miundo mbalimbali ya tungo wakati sarufi kama kaida za kiisimu haijihusishi kabisa na masuala ya ubongo bali yenyewe hujihusisha na mazoea ya kawaida ya watumiaji wa lugha ambapo kunakuwa na makosa ambayo huwafanya wataalamu kuunda kanuni za lugha ambazo zinatakiwa kufuatwa na wasiojua lugha hii inatofautiana na sarufi kama tafiti na uchambuzi wa miundo inavyoonekana kwenye lugha kwa kuwa haihusiani na masuala ya ubongo wala kaida, bali yenyewe hujihusisha na utafiti na ufafanuzi wa miundo ya lugha kama inavyotumika na wazungumzaji wa lugha na haiwaelekezi jinsi ya kuzungumza.
Kwa kuhitimisha tunaweza kusema kwamba pamoja na tofauti hizo zilizojitokeza katika mikabala hiyo mitatu, mikabala hii inaonekana kufanana kwani yote inajihusisha na lugha ya binadamu, pia mikabala hii imechangia kwa kiasi kikubwa katika maendeleo ya taaluma ya isimu na ndio imekuwa darajia kwa wataalamu mbalimbali katika kufanya tafiti zao kwa mfano baada ya kushindwa kwa sarufi ubongo na sarufi kama kaida za kiisimu ndipo kukazaliwa kwa sarufi kama tafiti na uchambuzi wa miundo inavyooneka kwenye lugha.

MAREJELEO
Babylon Dictionary. (1997). Translation and Information Platform. Babylon Ltd.
Besha, R.M. (2007). Utangulizi wa lugha na Isimu. Macmillan Aidan Ltd. Dar es Salaam.
Chomsky, N. (1957). Syntactic Structures. Mouton The Hague.
Khamis, A.M na John G.K (2002). Uchanganuzi wa sarufi ya Kiswahili. TUKI. Dar es salaam.
Habwe, J na Peter K (2007). Msingi ya sarufi ya Kiswahili.Phoenix Publishers. Nairobi.
Kihore, Y.M na wenzake. (2008). Sarufi Maumbo ya Kiswahili Sanifu (SAMAKISA):Sekondari na Vyuo. TUKI. Dar es Salaam.

Massamba, D.P.B. na wenzake. (2009). Sarufi Miundo ya Kiswahili Sanifu (SAMIKISA): Sekondari na Vyuo. TUKI.

SENTENSI ZA KISWAHILI.


Sentensi za Kiswahili


Sentensi ni kundi la neno moja au maneno zaidi yenye kiima na kiarifa na inayofuata kanuni za sarufi.


Angalia:


Muundo wa Sentensi => Kikundi Nomino(KN)/Kiima, Kikundi Tenzi(KT)/Kiarifa, Shamirisho na Chagizo


Virai na Vishazi


Uchanganuzi wa Sentensi Sahili



Aina za Sentensi


1. Sentensi Sahili



Hizi ni sentensi zenye kishazi kimoja na huwakilisha wazo moja tu.


Sentensi sahili kutokana na kikundi tenzi pekee:


Ninasoma => KT(T)


Hajakuandikia barua => KT(T + N)


Tulimwona nyoka mkubwa = >KT(T + N + V)


Alikimbia haraka sana => KT(T + E + E)


Kikundi Nomino + Kikundi Tenzi


Sakina anaimba. => KN(N) + KT(T)


Latifa na Kanita wamejipamba vizuri. => KN(N + U + N) + KT(T + E)


Jua kali liliwaka mchana kutwa. => KN(N + V) + KT(T + E + E)


Runinga ya Bwana Kazito imeharibika tena. => KN (N + V + N + N) + KT (T + E)



2. Sentensi Ambatano.


          Sentensi ambatano ni sentensi zenye zaidi ya kishazi huru kimoja na huwakilisha mawazo mawili au zaidi. Aghalabu sentensi hizi hutumia viunganishi(U) au alama za uakifishaji kama vile kituo(,) na nukta-nusu (;) ili kubainisha wazo moja toka nyingine.


Kuunganisha Sentensi Mbili:


Chesi alisoma kwa bidii. Chesi alianguka mtihani.


=>Ingawa alisoma kwa bidii, Chesi alianguka mtihani.


Dadangu amerudi nyumbani. Dadangu amelala.


=>Dadangu amefika nyumbani na kulala.


Mifano mingine:


Tulifika, tukaona, tukapiga na tukatawala.


Leo inaonekana Karimi amejipamba akapambika.


Angalia: Uchanganuzi wa Sentensi Ambatano


3. Sentensi Changamano.


Hizi ni sentensi zinazoundwa kwa kuunganisha kishazi huru pamoja na kishazi tegemezi au sentensi mbili kwa kutumia o-rejeshi ili kuleta zaidi ya wazo moja.


Kuunganisha Sentensi:


Juma amenilitelea kitabu. Nilikuwa nimetafuta kitabu hicho kwa muda mrefu.


=> Juma ameniletea kitabu ambacho nilikuwa nimekitafuta kwa muda mrefu.


Yeye ni mwizi. Alipigwa jana jioni.


=> Yeye ndiye mwizi aliyepigwa jana jioni.


Mifano Zaidi:


Nimemuona yule ninayemtafuta na neema zake.


Ndoto zinazotisha ni za kishetani.


Angalia: Uchanganuzi wa Sentensi Changamano


Tanbihi: Ili kutofautisha sentensi ambatano na changamano kwa urahisi, sentensi changamano hutumia o-rejeshi (k.m ambacho, ambaye, niliye- , nililo- n.k)

MOFOLOJIA YA KISWAHILI.



Mofolojia ya Kiswahili


Mofolojia ya kiswahili


· Malengo ya somo hili • Kueleza na kufafanua maana ya mofolojia • Kutambua na kufafanua zaidi mofolojia na vipashio vyake.


· Kunihusu mimi • STEPHEN MANYAMA CHARLES • MWANAFUNZI WA CHUO KIKUU CHA ARUSHA,NI MWALIMU-MWANAFUNZI WA SOMO LA KISWAHILI KWA VYUO NA SEKONDARI,Karibuni kwa Mchango na Mawazo na hata kwa kujifunza pia.

· Utangulizi • Maana ya mofolojia


· Maana ya mofolojia • Mofolojia ni tafsiri ya neon la kiingereza “Morphology”. Neno hili nalo linatokana na neon la kiyunani “Morphe” lenye maana ya muundo au umbo ( Aurbach et al 1971; 106). • Mofolojia ni neno linalotumiwa kumaanisha utanzu wa isimu unaoshughulikia muundo wa maneno ( Habwe na Karanja 2004).


· Maana.......... • Hartman (1972). Mofolojia ni tawi la sarufi ambalo hushughulika na uchunguzi na uchambuzi wa maumbo, fani na aina za maneno yalivyo sasa pamoja na historia zake


· Maana......... • Kwa ujumla mofolojia ni taaluma inayoshughulikia lugha pamoja na mpangilio wake katika uundaji wa maneno. Vipashio hivyo vya lugha huitwa mofimu


· Uhusiano uliopo kati ya mofolojia na matawi mengine ya sarufi • Mofolojia na fonolojia • Kuna uhusiano wa moja kwa moja kati ya mofolojia na fonolojia:i. Vipashio vya kifonolojia ndivyo hutumika katika kuunda vipashio vya kimofolojia mfano


· Mofolojia na fonolojia • Vipashio vya mofolojia ni fonimu, mfuatano wa fonimu ndio huuna vipashio vya kimofolojia ambavyo ni mofimu Mfano • Fonimu: i, p, t, a, huunda • mofimu: Pit-a • Hivyo basi neno pita limeundwa na mofimu mbili na fonimu nne


· Mofolojia na fonolojia ii) Uhusiano mwingine kati ya fonolojia na mofolojia ni kwamba, kanuni za kifonolojia hutumika kueleza maumbo ya kimofolojia ambayo yanaathiriana. Mfano Katika neno mu-ana mwu-alimu


· Mofolojia na fonolojia • Kipashio [mu] katika mifano hapo juu kinajitokeza kama [mw-] inapofuatwa na irabu ambayo. Mu mw-/-I


· Neno hutumika kuundia sentensiØMofolojia na sintaksia i. Vipashio vya msingi vya kimofolojia ndivyo hutumika katika kuundia daraja hili la sintaksia.·


Mwisho kwa asante usomaji Mawasiliano: charlesmanyama@rocketmail.com,0768326604 ©2014

· Maswali na majibu • Kwa maswali au mchango wowote kuhusuiana na kiswahili nifuate kwenye email yangu ya charlesmanyama@rocketmail.com