FANI NA MAUDHUI KATIKA FASIHI
FANI: huu ni ufundi wa kisanaa autumiao
msanii katika kutoa ujumbe wake kwa hadhira iliyokusudiwa. Katika fani
kumegawanyika vipengele mbalimbali kama vile wahusika, mitindo, muundo,
mandhari, matumizi ya lugha, kufaulu na kutokufaulu kifani. Vipengele muhimu
vinavyoangaliwa ni hivi vifuatavyo:
Mtindo;
hii ni mbinu ya kipekee kifani na kimaudhui, zinazotofautisha msanii mmoja na
mwingine.
Muundo;
huu ni mpangilio wa kiufundi anaoutumia mwandishi katika kupangilia kazi yake.
Wahusika;
hawa ni watu au viumbe ambavyo mwandishi wa fasihi huwatumia ili kufanikisha
ujumbe kwa jamii husika. Katika kazi ya fasihi mwandishi huwagawa wahusika
katika makundi mawili yaani wahusika wakuu na wahusika wadogo.
Wahusika
wakuu ni wale ambao wanajitokeza kuanzia
mwanzo mpaka mwisho wa kazi ya fasihi. Wahusika wadogo ni wale wote ambao
wanajitokeza sehemu mbalimbali katika kazi ya fasihi kwa mfano, mwanzoni mwa
kitabu hadi mwishoni mwa kitabu.
Mandhari;
hii ni sehemu ambayo matukio ya hadithi au masimulizi hutokea. Mandhari huweza
kuwa halisi au ya kufikirika.
Maudhui;
Maudhui katika kazi ya fasihi ni jumla ya mawazo yote yanayozungumzwa pamoja na
mtazamo wa mwandishi juu ya mawazo hayo. Maudhui hujumuisha mawazo pamoja na
mafunzo mbalimbali yaliyomsukuma msanii hadi akatunga na kusanii kazi fulani ya
kifasihi. Vipengele vya maudhui ni pamoja na dhamira, migogoro, falsafa ujumbe
na msimamo.
Dhamira;
hili ni wazo kuu au mawazo mbalimbali yanayojitokeza katika kazi ya fasihi.
Senkoro anataadharisha maana hii isichanganywe na maudhui kwani dhamira ni
sehemu tu ya maudhui na aghalabu dhamira kuu ndio hujenga kiini cha kazi ya
fasihi. Dhamira zimegawanyika katika makundi mawili, kuna dhamira kuu na
dhamira ndogondogo.
Migogoro;
ni mivutano na misuguano mbalimbali katika kazi za fasihi. Migogoro inaweza
kuwa kati ya wahusika, familia zao, matabaka yao, au hata katika nyadhifa
mbalimbali.
Vilevile migogoro yaweza kuwa ya kiuchumi,
kijamii, mogogoro ya nafsi, na migogoro ya kisiasa ambayo hujitokeza katika
mitazamo tofauti kulingana na mtiririko wa visa na matukio yanavyopangwa na
mwandishi.
Kwa ujumla suluhisho la migogoro yote ni
jamii kuwa na haki na usawa kuondoa chuki, kuondokana na uvivu, kushirikiana
katika kuwafichua wale wanaotumia mali ya umma kwa kujinufaisha wenyewe.
Ujumbe;
mwandishi anapoandika kazi yake huwa na ujumbe ambao hutaka uifikie jamii
aliyoikusudia. Ujumbe katika kazi fasihi ni mafunzo mbalimbali ambayo
hupatikana baada ya kusoma kazi ya fasihi. Katika kazi ya fasihi dhamira kuu
hubeba ujumbe wa msingi na dhamira ndogondogo hubeba ujumbe ambao husaidia
kuujenga au kuupa uzito zaidi ujumbe wa msingi.
Msimamo;
katika kazi ya fasihi, mawazo, mafunzo na falsafa ya msanii hubainisha msimamo
wake kuhusu masuala mbalimbali ya kijamii. Msimamo ni ile hali ya mwandishi
kuamua kufuata na kushikilia jambo fulani. Jambo hili huweza kukataliwa na
wengi lakini akalishikilia tu. Msimamo ndio huweza kuwatofautisha wasanii
wawili au zaidi wanaoandika kuhusu mazingira yanayofanana.
UHUSIANO
WA FANI NA MAUDHUI KATIKA FASIHI
Fani na maudhui ni dhana mbili ambazo
hazitenganiki. Kuna mitazamo miwili ambayo inajaribu kutazama uhusiano wa fani
na maudhui katika kazi za fasihi andishi. Mitazamo hiyo ni ya kidhanifu na
kiyakinifu.
Katika mtazamo wa kidhanifu wapo
wataalam mbalimbali ambao wametoa maelezo yao kuhusu uhusiano wa fani na
maudhui katika kazi za fasihi andishi.
Tukianza na Bi. Materu, yeye anasema
fani na maudhui ni kama mwili na nguo hivyo anatoa maoni kuwa fani na maudhui
ni dhana ambazo zinaweza kutenganishwa kama vile mwili unavyoweza kutenganishwa
na nguo. Bi. Materu anasema maudhui ni mwili ambao ndilo umbo la ndani la kazi
ya fasihi, wakati nguo ndio fani ambayo ni umbo la nje la kazi ya fasihi.
Fauka ya hayo Mtaalam mwingine ni Penina
Muhando (Mlama), anasema kuwa fani na maudhui ni kama sahani na chakula. Sahani
yaweza kutengwa na chakula pale ambapo chakula hicho kitaondolewa. Penina
Muhando anasema, chakula ndio maudhui yaani umbo la ndani la kazi ya fasihi na
sahani ndio fani ambayo ni umbo la nje la kazi ya fasihi. Hivyo yeye anaona
kuwa fani na maudhui ni dhana mbili ambazo zinaweza kutenganishwa na bila
athari yoyote.
Naye T. Sengho anasema kuwa fani na
maudhui ni kama chungwa na ganda, akiwa na maana kuwa chungwa ndio maudhui na
ganda ndio fani. Hapa T. Sengho anatoa msimamo kuwa fani na maudhui vinaweza
kutenganishwa bila ya athari, kwani chungwa linaweza kutengwa na ganda lake.
Mtaalam mwingine anayeegemea mtazamo wa
kidhanifu anasema kuwa fani na maudhui ni kama kikombe na chai. Huyu ni Mtaalam
F. Nkwera ambaye anasema kuwa chai ndio maudhui na fani ndio kikombe. Hapa F.
Nkwera anataadharisha kuwa chai inaweza kunywewa kwenye kikombe na kikombe
kubakia kitupu, hivyo fani yaweza kutengwa na maudhui kama vile chai inavyoweza
kutengwa na kikombe.
Katika mtazamo wa kiyakinifu, Senkoro
anasema kuwa fani na maudhui ni sawa na sarafu. Hapa anamaanisha kuwa fani na
maudhui ni dhana mbili zisizoweza kutenganishwa kama vile pande mbili za sarafu
moja.
Senkoro F. E. M. K. anasisitiza kuwa
fani na maudhui havitenganishiki bali hutegemeana ili kazi ya fasihi iweze kuwa
bora zaidi. Kazi ya fasihi ambayo maudhui yamezidi fani huwa chapwa au fani
ikizidi maudhui, kazi hiyo ya fasihi huwa chapwa, hivyo maudhui na fani ni
dhana ambazo hutemeana. Fani na maudhui lazima vilingane na kushabihiana ili
kazi yenyewe iweze kuwa bora na yenye mvuto zaidi.
Mtazamo mwingine unadai kuwa fani na
maudhui hulinganishwa na roho na mwili ambapo haiwezi kutenganishwa na mwili
kwani kwa kufanya hivyo athari itakayotokea ni kwamba mwili hautaweza kufanyakazi
ipasavyo pasipo roho.
Vilevile tunaweza kufananisha fani na
maudhui kama gari na injini. Hii ni dhana ambayo inajidhihirisha kuwa gari
haliwezi kutenda bila injini, hivyo ni kuweza kuthibitisha kuwa fani na maudhui
ni dhana mbili zisizotenganishwa kwani huleta athari zinapotenganishwa na
vilevile fani na maudhui hutenda kazi pamoja.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni