UAMILIAJI LUGHA SARUFI
MAJUMUI NA UAMILIAJI LUGHA YA PILI.
Makala haya yataangalia maana ya sarufi
majumui, masuala ya msingi yanayohusu maarifa ya lugha, sifa za sarufi majumui,
sarufi majumui na uamiliaji lugha ya pili na mwisho tathmini. Kwa mujibu wa Chomsky
(1976:29) kama alivyonukuliwa na Ellis (1996:430) sarufi majumui ni mfumo wa
kanuni na sheria ambazo ni msingi wa lugha za binadamu (tafsiri yangu). Muasisi
wa nadharia hii ni Noam Chomsky. Msingi wa nadharia hii ni kwamba binadamu
anapozaliwa anakuwa na maarifa asilia ambayo humsaidia katika ujifunzaji lugha;
mambo ya ndani na nje ambao husaidia katika uamiliaji wa lugha. Maarifa haya
hupatikana pale tu binadamu anapozaliwa kwani huwa na kifaa cha uamiliaji lugha
ambacho kinakuwa na kanuni majumui na kanuni badilifu ambazo hukutana na
tajiriba (uwezo wa jamii katika lugha) na kusababisha uamiliajli lugha kutokea.
Waamiliaji wa lugha ya kwanza huwa na maarifa asilia ambayo huwawezesha
kuiamili lugha yao kwa kutumia maarifa hayo. Hivyo maarifa hayo yanaamshwa na
tajiriba ambayo mjifunzaji anaikuta katika jamii iliyomzunguka na hatimaye
kukutana na maarifa asilia katika kifaa cha uamiliaji lugha hatimaye kuzalisha
sarufi mahsusi ya lugha husika. Waamiliaji wa lugha ya pili wanakuwa na lugha
ya kwanza ambapo sifa za sarufi majumui bado humwezesha kuamili lugha ya pili,
kwani kanuni badilifu na kanuni majumui zilizojengwa kwa misingi ya lugha ya
kwanza hutumika katika kuamilia lugha ya pili. Hivyo kwa mujibu wa nadharia ya
sarufi majumui inamsaidia mjifunzaji katika kuamili lugha ya pili. Wataalam
mbalimbali wameweza kujadili juu ya uwezo wa sarufi majumui wa kuwa kifaa
weazeshi cha kujifunza lugha ya pili, kuna wataalam wanaokubali na wanaokataa
mchango huo. Kama Flyn (1984-1987) anavyoelezea kama alivyonukuliwa na Ellis
(1996:453) kifaa cha uamiliaji lugha ya kwanza kitahusika na mchakato wa ujifunzaji lugha ya pili. Akaendelea
kusema kanuni badilifu za lugha ya kwanza na lugha ya pili zikiwa sawa
ujifunzaji utakuwa rahisi kwa sababu mjifunzaji wa lugha ya pili ana uwezo wa
kuhusisha miundo wakati kanuni hizo zikitofautiana kati ya lugha ya kwanza na
lugha ya pili ni vigumu kujifunza. Flyin yeye anaunga mkono juu ya sarufi
majumui kuwa kifaa wezeshi katika ujifunzaji wa lugha ya pili. Kwani anaamini
bado maarifa ambayo mjifunzaji wa lugha ya kwanza anayoyatumia katika
ujifunzaji wa lugha hiyo, ndiyo yale yale anayoyatumia mjifunzaji wa lugha ya
pili. Hata hivyo Clahsen na Muysken (1986-1991) kama walivyonukuliwa na Ellis
(1996:454) wanasema uamiliaji wa lugha ya pili ni tofauti na uamiliaji lugha ya
kwanza muamiliaji lugha ya kwanza huwa na kifaa wezeshi cha uamiliaji lugha
wakati wa lugha ya pili hutumia mbinu za lugha ya kwanza katika kujifunza lugha
ya pili wanaendelea kusema muamiliaji lugha ya pili huhitaji nadharia ya isimu
wakati wajifunzaji lugha ya pili huhitaji naharia tambuzi. Hata hivyo sarufi
majumui imeangaliwa katika mitazamo tofautitofauti, hivyo kuonesha ubora lakini
pia mapungufu yake katika ufundishaji wa lugha: Kwa kuwa na sarufi majumui tunaona
kuwa sifa za lugha huingiliana, hivyo mwingiliano wa lugha ya kwanza na ya pili
unaweza kumwezesha muamiliaji lugha ya pili pale miundo ya lugha ya kwanza na
lugha ya pili itafanana na hata ikitofautiana mjifunzaji anakuwa na uwezo wa
kujiundia miundo yake itakayomsaidia katika ujifunzaji wake kwa kutumia sifa
majumui za lugha. Flynn (1984;1987) kama alivyonukuliwa na Ellis(1996;453)
anaeleza kuwa “kifaa cha uamiliaji lugha ya kwanza kinaweza kutumika katika
uamiliaji wa lugha ya pili. Kama kanuni badilifu za lugha ya kwanza na ya pili
zinauhusiano hurahisisha ujifunzaji”. Hivyo yeye anakubali kabisa kuwa sarufi
majumui ni kifaa wezeshi katika ujifunzaji wa lugha ya pili, anaamini sifa za
mjifunzaji wa lugha ya kwanza ndizo ambazo anakuwa nazo mjifunzaji wa lugha ya
pili. Aidha Ellis (1994:461) anaeleza ubora wa sarufi majumui kuwa imetoa
msingi wa uibukaji wa nadharia zingine za ujifunzaji lugha baada ya kuegemea
kwenye maarifa asilia anayozaliwa nayo binadamu. Pia imeweza kueleza sifa
majumui za lugha mbalimbali za ulimwengu kwa ufupi, hivyo kusababisha sifa za
lugha kueleweka kwa urahisi kwa wajifunzaji wa lugha ya pili. Kwa mujibu wa
Ellis (1994:458) udhaifu huu unajidhihirisha katika maeneo kadhaa, kiini cha
sarufi majumui yenyewe, pia mbinu zilizotumika kukusanyia data. Hivyo
inaonekana kuwa kuna tatizo katika mbinu za ufundishaji na namna ya ufundishaji
wa lugha ya pili. Nadharia ya sarufi majumui haikuonyesha namna gani mjifunzaji
anapata ujuzi wa kutumia maarifa asilia aliyozaliwa nayo lakini pia mbinu
iliyotumia katika ukusanyaji wa data ni ile mbinu ya kukusanya data isiyo ya
vipindi maalum. Hivyo kupelekea data zake kutoweza aminika. Vilevile clahsen na
Muysken (1986), Meisel(1991) kama walivyonukuliwa na Ellis (1996;454)
muamiliaji wa lugha ya pili atakuwa tofauti na muamiliaji wa lugha ya kwanza
kwa sababu kifaa cha uamiliji lugha kipo tu kwa mtu anayejifunza lugha ya
kwanza na yule anayejifunza lugha ya pili huweza kusaidiwa na maarifa/mbinu
mbalimbali ya ufundishaji na mazingira. Hivyo hawa wanaona kuwa safuri majumui
si kifaa wezeshi katika ujifunzaji wa lugha ya pili. Kuibuka kwa nadharia
zingine kunaonesha udhaifu wa nadharia ya sarufi majumui, mfano Fabisz, N.[1]
Anaelezea nadharia ya uzawa iliyoasisiwa na Andersen ambayo inasisitiza juu ya
urithishaji wa lugha, pia nadharia ya utamadunishi iliyoasisiwa na John
Schumann (1978)inayosisitiza jinsi utamaduni wa jamii ulivyo na mchango mkubwa
katika ujifunzaji lugha kwani lugha huendana na utamaduni mfano ni vigumu
kujifunza lugha ya kiingereza kwa mswahili kwasababu tunatofautiana katika
utamaduni hata kama utajua kiingereza hautafanana na mwingereza mzawa kwa kuwa
yeye atatumia miundo ya lugha hiyo akihusisha na utamaduni wake. Hivyo katika
kujifunza lugha sarufi majumui sio kifaa wezeshi pekee cha uamiliaji lugha
pekee ambacho hutumika bali kuna vitu kama mazingira, motisha na urudiaji wa
mara kwa mara humpelekea muamiliaji lugha ya pili kujifunza lugha ingawa kuna
utofauti wa uamiliaji kuna wengine huchukua muda mrefu na wengine muda mfupi,
si lazima waamiliaji wa lugha ya pili wawe na sarufi majumui inayofanana, hivyo
tofauti zao wakati mwingine haziepukiki. Kama ubora na udhaifu wa sarufi
majumui unavyojidhihirisha, hii inaonesha kuwa sarufi majumui peke yake
haitoshi kumfanya mjifunzaji wa lugha aweze kuamili lugha ya pili vizuri, hivyo
walimu wanashauriwa kutumia nadharia changamani katika ufundishaji wao wa lugha
ya pili ili kumwezesha mjifunzaji wa lugha ya pili kuamili lugha hiyo vizuri.
Kimsingi sarufi majumui inajidhihirisha kuwa ni kifaa wezeshi katika ujifunzaji
wa lugha ya pili licha ya kuwa na udhaifu wake, haipelekei kuiondoa katika hali
ya uwezeshi katika ujifunzaji wa lugha ya pili, kwani sifa majumui
zinazopatikana katika lugha mbali kwa kiasi kikubwa zinawasaidia wajifunzaji kujifunza
lugha ya pili, mfano wajifunzaji wanapogundua miundo ya lugha na uundaji wa
misamiati unaolingana itawawia rahisi katika ujifunzaji wao. Lakini hata
ikitofautiana sarufi majumui imefafanua namna ambavyo mjifunzaji huyu ataweza
kujiundia sarufi yake ambayo itakuwa imejengeka kwa misingi ya lugha ya kwanza.
Kuna umuhimu wa kuwa na mazingira bora ya ujifunzaji ambapo mawasiliano
yanapewa msisitizo mkubwa katika nadharia mbalimbali, hivyo walimu hawana budi
kujenga mazingira hayo kwa wanafunzi wao ili waweze kujifunza lugha ya pili kwa
usahihi. Ikiwa ni pamoja na kubadilisha mazingira ya darasa kuwa mazingira
rafiki kwa mwanafunzi ambapo mawasiliano ndiyo kiini cha ujifunzaji. Nadharia
ya sarufi majumui imeonekana ina mchango mkubwa katika tendo la ujifunzaji,
lakini haitoshi kusema ndiyo nadharia pekee ambayo inapaswa kutumiwa na walimu
katika ufundishaji wao kwani pia imeonekana kuwa na udhaifu, hivyo nadharia
zingine kama za utamadunishi, uzawa na urithishaji ni muhimu kuzipa umuhimu pia
ili tendo zima la kujifunza liweze fanyika, lakini pia cha msingi ni kujua
wajifunzaji hawawezi kuwa na uwelewa wa aina moja hata kama haya yote
yatatimia, hivyo kinachoangaliwa ni kufikia ile hali ya kawaida katika matumizi
ya lugha, ambapo kila mjifunzaji anatarajiwa afikie.
MAREJEO
Ellis, R. (1994),
Second Language Acquisition, USA: Oxford University Press Fabisz, N. ANALYSIS
OF KRASHEN’S THEORY OF SECOND
LANGUAGEACQUISITION,http://webspace.webring.com/people/ap/panandrew/sla.html,
ISTILAHI
Externa approach - mkabala wa nje
Intuition - ujuzi
Internar approach - mkabala wa ndani
Parameter - kanuni badilifu
Principles - kanuni majumui
Prompted - Papo hapo
Universal grammar -
sarufi majumui