Subcribe to our RSS feeds Join Us on Facebook Follow us on Twitter Add to Circles

Jumanne, 4 Novemba 2014

MOFOFONEMIKI YA KISWAHILI


Katika mada hii tumeangalia fasili ya mofofonemiki kwa mujibu wa wataalam mbalimbali, kisha tukaangalia kwa ufupi historia ya nadharia ya mofofonemiki na katika kiini cha mada tumejadili sababu zilizopelekea kuibuka kwa nadharia ya mofofonemiki. Kwa kuanza na fasili ya mofofonemiki  kwa mujibu wa mtandao wa Wikipedia wanafafanua mofofonemiki kuwa ni tawi la isimu linalojishughulisha na mwingiliano wa michakato ya kimofolojia na kifonolojia au kifonetiki. Pia hujishughulisha na mabadiliko ya sauti yanayotokea katika mofimu wakati zinapoungana kuunda maneno. (Tafsiri yetu). fasili hii ina mapungufu fulani kwani, mofofonemiki haijishughulishi na michakato yote ya kifonolojia na kimofolojia bali ni baadhi tu ya michakato hiyo ambayo ilishindwa kufafanuliwa kwa kutumia data za kifonolojia au kifonetiki peke yake. The New Oxford American Dictionary inafafanua kwamba, mofofonolojia/mofofonemiki ni tawi la isimu linalojishughulisha na uwakilishi wa kifonolojia wa mofimu. Hivyo basi tunaweza kusema kuwa, mofofonemiki ni tawi la isimu linaloshughulikia matumizi ya kimofolojia katika kueleza baadhi ya tofauti za kifonolojia ambazo isingewezekana kuzielezea kwa kutumia data za kifonetiki au kifonolojia peke yake. Baada ya kuangalia fasili ya neno mofofonemiki ifuatayo ni historia fupi ya nadharia ya mofofonemiki. Kwa mujibu wa Massamba (2010:82) akimrejelea Martnet (1965) anafafanua kwamba, istilahi hii mofofonemiki/mofofonolojia ilipendekezwa kwa mara ya kwanza na N.S. Trubetzkoy (1929). Trubetzkoy alitumia istilahi hii kwa maana ya tawi la isimu ilinaloshughulikia matumizi ya mafolojia katika kuelezea baadhi ya tofauti za kifonolojia ambazo isingewezekana kuzielezea kwa kutumia data za kifonolojia au kifonetiki peke yake. Baada ya kuangalia historia fupi ya mofofonemiki yafuatayo ni mambo yaliyosababisha kuibuka kwa nadharia ya mofofonemiki. Kuchunguza ubadilikaji wa sauti ambao usingeweza kuelezwa kwa kutumia data za kifonolojia peke yake. Baadhi yao wakapendekeza kuwapo kwa kiwango cha kimofofonemiki pamoja na kipashio umbo kiini kama kiwakilishi cha mofimu, kwa hiyo walipendekeza hivyo baada ya kushindwa kujua ipi ni alofoni ya fonimu ipi kwa kutumia kigezo cha kifonetiki pekee  Kwa mfano;  walishindwa kujua /k/ ni alofoni ya /c/ au /c/ ni alofoni ya /k/ Kwa mfano hata katika lugha ya kurusi –                                             ruka = “mkono”                                             ručnoj = “a mkono”                                              Mzizi ni – ruk na ruč Wanamofofonemiki walichunguza wakagundua kuwa katika mazingira fulani /k/ hubadilika kuwa /č/ baada ya kufuatiwa na “noj”. Hivyo wakapendekeza umbo kiini la maneno haya ni ruKa au ruČnoj umbo kiini lake lilitambulika kama {K} au {Č} Katika lugha ya Kiswahili kuna mabadiliko ya sauti yanayotokea katika baadhi ya maneno baada ya sauti fulani kufuatiwa na kiambishi cha unominishaji (i) kwa mfano katika maneno yafuatayo;                    Fuata – fuasi                    Penda – Penzi                    Cheka – Cheshi                    Pika – Pishi Pia wanamofofonemiki walichunguza ubadilishanaji huu wa sauti kwani walishindwa kujua ipi ni alofoni ya fonimu ipi. Ndipo wakagundua kuwa katika mazingira fulani /t/ hubadilika kuwa /s/ baada ya kufuatwa na mofimu ya unominishaji “i” pia sauti /d/ hubadilika na kuwa /z/ baada ya kufuatwa na mofimu ya unominishaji “i” Baada ya kupendekeza umbo kiini maneno haya yakaandikwa kama ifuatavyo: kwa mfano neno {fuaTa} umbo {T} likawa umbo kiini ambalo linawakilisha sauti zote mbili yaani /t/ na /s/, pia neno {piKa} umbo kiini lake ni {K} ambalo linawakilisha sauti /k/ na /ʃ/ Kuchunguza mabadiliko ya sauti yanayotokea mofimu zinapoungana. Kwa mfano; katika lugha ya Kiswahili,             U + ima         –       wima             I + etu            –       yetu             Mu + alimu    –      Mwalimu             U + imbo      –       wimbo             Vi + ake        –      vyake Wanamofofonemiki wakagundua kuwa sauti fulani huweza kuungana na kuunda sauti moja na kubadili umbo la neno. Chunguza muundo wa kifonolojia wa mofimu katika lugha. Kwa mfano katika lugha ya Kiswahili;             Mu + huni – Mhuni             Mu + gonjwa – Mgonjwa             Mu + guu – Mguu             Mu + uguzi – Muuguzi             Mu + tu – Mtu Wanamofofonemiki wakagundua kwamba mofimu fulani huweza kuungana na mofimu nyingine na kuunda umbo la neno. Kuchunguza ubadilishanaji wa sauti ambao una una uamilifu wa kimofolojia lakini husababisha mabadiliko fulani ya kifonetiki. Kwa mfano katika lugha ya kiingereza;             Play + s – [pleiz]             Dog + s – [dogz]             Since – [sins]             Else – [els]             Place – [pleis] Wanamofofonemiki wakachunguza kinachosababisha kuwepo na maumbo tofauti tofauti ya mofimu ya wingi. Kwa mfano; /s/, /iz/, /z/ Wakagundua kuwa kuna mchakato zaidi ya ule wa kifonolojia ambao ni wa kimofolojia unaosababisha umbo ‘s’ kutamkwa /z/ au /iz/ au /s/

                                        MAREJEO:
 The New Oxford American Dictionary. (2005), (2ndEdit), Oxford University Press. New York.


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni