Subcribe to our RSS feeds Join Us on Facebook Follow us on Twitter Add to Circles

Alhamisi, 12 Juni 2014

UHAKIKI WA DIWANI ZA KISWAHILI.


UHAKIKI WA DIWANI YA WASAKATONGE


UTANGULIZI

Diwani ya Wasakatonge ni miongoni mwa diwani za hivi karibuni zinazotanabaisha matatizo mbalimbali yanayoikumba jamii katika maisha yake ya kila siku. Matatizo hayo yanaonekana kuwa kama saratani isiyo na tiba. Hata hivyo, msanii ana matumaini kwamba, iwapo wananchi wa kawaida wataungana na kuamua kupambana, ni dhahiri kwamba matatizo hayo yatatoweka kabisa. Miongoni mwa matatizo hayo yataoneshwa kwenye kipengele cha maudhui huku yakishadidiwa na fani.

MAUDHUI: ni jumla ya mambo muhimu yanayoelezwa katika kazi ya kifasihi. Maudhui yanajengwa na vipengele vidogovidogo vifuatavyo; dhamira, ujumbe, mgogoro, mtazamo na falsafa.

DHAMIRA: ni jumla ya maana anayovumbua mwandishi aandikapo kazi yake na jumla ya maana anayoipata msomaji pindi anapoisoma kazi fulani ya kifasihi. Kifasihi kuna aina mbili za dhamira yaani dhamira kuu na dhamira ndogondogo. Dhamira kuu ni lile wazo kuu la mwandishi katika kazi, wakati dhamira ndogondogo ni zile dhamira zinazojitokeza ili kuipa nguvu dhamira kuu. Dhamira zilizojitokeza katika diwani hii ni kama ifuatavyo:

UONGOZI MBAYA: ni aina ya uongozi ambao haujali maslahi ya wananchi na taifa kwa ujumla. Ni uongozi unaotumia mabavu na unaojali maslahi binafsi, yaani haufuati misingi ya utawala wa sharia. Katika diwani hii msanii anaonesha kuwa nchi nyingi duniani hasa zile za kiafrika zinakabiliwa na tatizo la uongozi mbaya. Viongozi walio wengi ni madikteta ambao hawataki kuachia madaraka wala kuwapa watawaliwa uhuru wa kuzungumza.

Hali hii tunaopata katika shairi la “MADIKTETA” (uk.21) ambapo msanii anasema kuwa harakati za kusaka uhuru au demokrasia kwa njia ya mtu haijawahi kuzaa matunda yanayotarajiwa. Harakati hizi zimekuwa zikizalisha viongozi “Miungu watu” au marais walio madikteta, kama ilivyokuwa kwa Mabutu Seseko-huko Zaire (kwa sasa DRC), Bokosa-huko Afrika ya Kati na Idd Amini-huko Uganda. Madikteta hawa wamekuwa na kila aina ya uovu ikiwa ni pamoja na kukumbatia ukabila, udini na uvamizi kwa nchi nyingine. Haya tunayapata katika shairi la “SADDAM HUSSEIN” (uk.26:4) anasema;

4. “Nakuafiki, Saddam, si kwa uvamizi wako,Na ujue kwamba,
Huo si uasi
Kwa wakubwa mila,
Saddam, yamesha tendeka sana!”

Viongozi wa aina hii huwanyima wananchi wao uhuru wa kusema ikiwa ni pamoja na ule wa kujiamulia mambo yao wenyewe kama katika shairi la “MARUFUKU” namba 45 (uk.36)
“Sitakiki uone,
Ingawa una macho,
Sitaki useme,
Ingawa una mdomo,
Sitaki usikie,
Ingawa una masikio,
Sitaki ufikiri,
Ingawa una akili,
Sababu utazinduka,
Utakomboka,
Uwe mtu,
Hilo sitaki,
Marufuku.”

Viongzozi wabovu (madikteta) ni wapenda dhuluma na manyanyaso. Huwadhulumu na kuwanyanyasa raia wao na raia wa nchi nyingine kama inavyojidhihirisha katika mashairi ya “KOSA” (uk.3), na “FAHARI LA DUNIA” (uk.45). Katika shairi la “KOSA”, tunaona kuwa unyanyasaji wa wananchi wa kawaida hutokea pale ambapo wanapokuwa wanadai haki zao. Mshairi anasema:
3. “Kosa letu kubwa,
Kudai haki?
Yetu miliki?
Mna hamaki,
Na huku mnatukashifu!”

Katika shairi la “FAHARI LA DUNIA” (uk.45) tunaambiwa kuwa kuna kiongozi mwenye nguvu (Marekani) ambaye mchana kutwa usiku kuchwa linanyanyasa nchi nyingi bila sababu za msingi. Msanii anasema:
5. “Fahari la Dunia,
Kwa kiburi, linatesa,
Lajigamba,
Linatamba,
Kuwa mwamba,
Linaoneya.”

Viongozi wabovu siku zote ni wanyonyaji na hushirikiana na watu wengi wenye nguvu kubeba mirija ya unyonyaji na kuanza kuwanyonya raia wa kawaida. Hali hii hujitokeza sana katika nchi za Dunia ya tatu. Haya yote tunayapata katika mashairi ya “MVUJA JASHO” (uk.12-13), “MIAMBA” (uk.29-30), “MUMIANI” (uk.34) Katika shairi la “MVUJA JASHO” msanii anaonesha kuwa raia wa kawaida wanafanya kazi kubwa na ngumu sana lakini malipo yao hayalingani na jasho wanalolitoa. Katika shairi la “MIAMBA” tunaambiwa kuwa wanyonge hawana chao, jasho lao na wao wenyewe ni chakula cha wakubwa na watawala wao. Ubeti wa 4 wa shairi hili msanii anahoji juu ya suala hili kwa kutumia taswira ya wanyama:
4. “Wanyonge,
Wamo shidani,
Digidigi na nyani,
Wamo makimbizoni,
Fisi wafurahia,
Ni sharia za mbuga?”

Katika shairi la “MUMIANI” linaonesha waziwazi unyonyaji unaofanywa na viongozi au watu wa tabaka la juu dhidi ya tabaka la chini ambao wanaishi vijijini na mijini, waendao hospitalini na wapelekwao mahakamani. Katika ubeti wa 1 tunaambiwa kuwa:-
1. “Mumiani,
Mijini,
Watembea kwa mato,
Kuzifanya kazi zao,
Kuzinyonya damu zetu,
Hawangoji,
Tulale.”

Diwani hii inaendelea kuonesha kuwa viongozi wabovu ni wasaliti na wanafiki. Viongozi hawa wanakuwa wepesi kuwaomba wananchi ili kufanikisha jambo fulani. Lakini pindi jambo hilo linapofanikishwa tu viongozi hao huwaweka wananchi pembeni (huwasaliti wananchi). Miongoni mwa mashairi yanayoonesha usaliti na unafiki wa viongozi wa dini na wa kisiasa ni “SIKULIWA SIKUZAMA” (uk.22-23), “WASO DHAMBI” (uk.1), “UASI” (uk.8), “PEPO BILA KIFO” (uk.14), vilevile shairi la “NAHODHA” (uk.41) linaonesha kuwa kuna viongozi wengi wanaoshindwa kazi lakini hawataki kuachilia madaraka. Hata hivyo msanii anaonesha kuwa viongozi wa aina hii wanaweza kuondolewa madarakani iwapo tu wananchi wote wataungana na kuwapiga vita.

KUPIGA VITA UKOLONI: Ukoloni ni hali ya kuvuka mipaka ya nchi na kwenda kuitawala nchi nyingine kisiasa, kiuchumi na kiutamaduni. Kutokana na madhara yanayosababishwa na ukoloni, msanii ameona kuwa tusiukumbatie bali tuupige vita ili tuweze kuishi maisha mazuri ambayo huja baada ya kujitawala. Katika shairi la “NURU YA MATUMAINI” (uk.9-10) tunaambiwa kwamba wananchi wa kusini mwa Afrika walipiga vita ukoloni ili kuondokana na ubaguzi, dharau, ubwana na utwana na hatimaye kuishi katika mazingira ya haki na usawa.

Kwa vile ukoloni unamadhara, kama inavyooneshwa katika shairi hilo, wananchi hawanabudi kuacha tabia ya kuukaribisha tena. Katika shairi la “HATUKUBALI” (uk.30) linatuambia kuwa;
4. “Hatukubali tena,
Kutuletea usultani,
Kutuletea na ukoloni,
Kutuletea na uzayuni,
Hatukubali katu,
Ndani ya nchi yetu,
Iliyo huru.”

Mbali na kupiga vita ukoloni mkongwe bali tunajukumu la kuutokomeza ukoloni mamboleo ambao kwa kiasi kikubwa unachangia kutufanya masikini. Ukoloni mamboleo hutufanya tusiwe na kauli juu ya bidhaa tunazozalisha na hatimaye Taifa letu kuishia kwenye lindi la umasikini. Inaonesha kuwa ukoloni mamboleo hutufanya tutekeleze matakwa ya mataifa makubwa kwa lengo la kuwa nufaisha wao huku sisi tukibaki taabani. Haya tunayapata katika shairi la “HATUNA KAULI” (uk.8-9)
6. “Tumepewa yake mitaji,
Tuwe wasimamiaji,
Pia watekelezaji.”

Hali hii pia inajitokeza hata katika shairi la “WAFADHILI” (uk.38-39) ambapo tunaambiwa kuwa wafadhili hutupenda tu pale tunapokubali masharti yao na matakwa yao.


1. “Wafadhili kufurahishwa,
Ni sera zao kupitishwa,
Rais anaamrishwa,
Tekeleza!”

Hali hii hutufanya tuwe watumwa wa ukoloni mamboleo baada ya kuondokana na ukoloni mkongwe. Katika shairi la “BUNDI” (uk.43) tunaambiwa kuwa uhuru wetu tulioupata hatujaufaidi hata kidogo kutokana na kupigwa nyundo ya kichwa na ukoloni mamboleo. Ukoloni huu ambao umefanikishwa na Bundi, tunaambiwa kuwa uko nasi kila kukicha. Ukoloni mamboleo ni mfumo usio na usawa hata kidogo. Ni mfumo ambao unawafanya wanyonge waendelee kuwa masikini, wasiomithilika huku matajiri wakiendelea kuwa watu wenye mali kupindukia. Haya yote tunayapata katika shairi la “KLABU” (uk.50) juu ya ukoloni mamboleo kwa kutuasa tuchapekazi, tujenge viwanda, tuboreshe kilimo na ufugaji, tuinue elimu, kukuza uchumi na tupige vita rushwa.

UMASKINI, UJINGA NA MARADHI: Mwalimu Julius K. Nyerere aliwahi kusema kuwa, jamii yetu inakabiliwa na maadui wakuu watatu; Umasikini, Ujinga na Maradhi. Hali hii inajitokeza katika diwani hii kwani msanii anatuambia kuwa Bara la Afrika ni kama mgonjwa aliyemahututi katika shairi la “TIBA ISOTIBU” (uk.18) Hii ni kutokana na ujinga, umasikini na maradhi. Hali hii imekuwa ikisababisha njaa, vita, chuki na visasi vya kila aina na hivyo kufanya bara la Afrika lisiwe na amani kama ilivyo DRC, Sudani, Rwanda, Burundi, Tunisia nk. Mshairi anakereka sana na hali hii kwa kuhoji haya katika shairi la “AFRIKA” (uk.6-7)
1. “Lini
Afrika utakuwa,
Bustani ya amani,
Ukabila kuuzika,
Udini kuufyeka,
Ni lini?”

Kwa ujumla Bara la Afrika limejaa watu masikini ambapo umasikini wao unatokana na mambo mengi kama vile unyonyaji unaofanywa na viongozi wao kwa kushirikiana na nchi za nje. Lakini pia umasikini hutokana na ujinga yaani elimu ndogo. Hali hii pia tunaikuta katika mashairi ya “WASAKATONGE” (uk.5), “MVUJA JASHO” (uk.12-13), “WALALAHOI” (uk.36-37)

MSUGUANO WA KITABAKA NA KIITIKADI (MATABAKA): Katika diwani hii msanii anaonesha msuguano mkali wa kitabaka uliopo katika jamii na katika nchi masikini na nchi tajiri. Matabaka haya yote ni zao la maisha ya kitajiri na kimasikini katika jamii. Tunaambiwa kuwa katika msuguano huu mkali baina ya matabaka, tabaka masikini linajaribu kujifaragua ili lipate angalau tonge la ugali wakati tabaka tajiri likijaribu kunyang’anya tonge linalopiganiwa na tabaka masikini. Haya tunayapata katika shairi la “TONGE LA UGALI” (uk.20)
4. “Wanapigana
Wanaumizana,
Wanauwana,
Kwa tonge la ugali!”

Katika shairi la “WASAKATONGE” tunaambiwa kuwa wasakatonge na jua kali ni watu wa hali ya chini sana, wanaofanya kazi duni na ngumu na ndio waliowaweka madarakani viongozi wanaowanyonya na kuwanyanyasa. Wananchi hawa wana hali duni sana kutokana na kutothaminiwa na viongozi wao. Shairi la “WASAKATONGE” halinatofauti na mashairi ya “MVUJAJASHO” (uk.12) na “WALALAHOI” (uk.36-37) kwani yote yanazungumzia matatizo ya watu wa tabaka la chini yanayosababishwa na tabaka la juu. Katika shairi la “MIAMBA” (uk.29-30) na “MUMIANI” (uk.34) tunaona jinsi msongamano wa kitabaka unavyofanana na ule wa shairi la “TONGE LA UGALI.” Katika mashairi haya, wenye nguvu ndio hutawala na kuwanyonya wanyonge kama inavyojishihirisha katika shairi la “MIAMBA” ambalo limetumia taswira ya wanyama katika kuonesha matabaka hayo, kama msanii anavyosema:


1. “Miamba,
Chui na Simba,
Mbugani wanatamba,
Vinyama vinayumba,
Chakula cha wakubwa
Ni sharia za mbuga?”

Hali ilivyo katika jamii yetu haina tofauti na ile ya mataifa tajiri na mataifa masikini, tunaendelea kuambiwa kuwa, mataifa masikini hayana chao mbele ya mataifa tajiri. Kazi ya mataifa masikini ni kutengeneza mipango ya mataifa tajiri kama inavyojionesha katika shairi la “HATUNA KAULI” (uk.8-9)
4. “Maagizo tunapewa,
Mipango tunapangiwa,
Na amri tunapangiwa.”

Mashairi mengine yanayoonesha hali hii ni “WAFADHILIWA” (uk.38) na “KLABU” (uk.50-51). Pamoja na masuluhisho yanayotolewa dhidi ya hali hii kama vile tabaka masikini kuungana na kupambana na hali hii, hasa kati ya nchi lakini bado msanii anawasiwasi juu ya kuondoka kwa hali hii katika jamii yetu. Hii inatokana na maswali anayojiuliza katika mashairi ya “TONGE LA UGALI” na “WASAKATONGE” ambapo msanii anaonesha hali ya kutokuwa na jibu rahisi katika kukomesha hali hiyo.

Pia msanii huyu amedokeza kuhusu mgongano au msuguano wa kiitikadi. Katika diwani hii tunaoneshwa kuwa, hatuna itikadi ya kisiasa inayoeleweka. Tupo kama hatupo na hatuelewi kama bado sisi ni wajamaa au mabepari. Hii inajidhihirisha katika shairi la “TWENDE WAPI” (uk.20-21)


3. “Twende wapi?
Mashariki “siko”!
Magharibi “siko”!
Wapi tuendako?
Tunatapatapa!”

Kutapatapa kiitikadi kunatusababishia tufanye mambo kama vipofu na matokeo yake ni kudaka kila kitu iwe kinachotoka magharibi au mashariki na hivyo kuathiri mfumo mzima wa maisha yetu ikiwemo mmomonyoko wa kimaadili.

UNAFIKI: Katika diwani hii tunaambiwa kuwa baadhi yetu hasa wanasiasa, viongozi au wananchi ni wanafiki wakubwa. Kwani kitendo cha baadhi ya watu kujiona kuwa hawana dhambi ni cha kinafiki kwa sababu, hakuna mwanadamu asiye na dhambi kama shairi la “WASODHAMBI” (uk.1) linavyosema;


2. Wavilemba!
Wavilemba, na majoho, tasibihi,
Wajigamba, safi ni roho, ni kebehe,
Wanotenda,
Unafiki.

Pia hata katika la “MAMA NTILIYE” (uk.17) nalo linadhibitisha hilo.


2. “Majungu na makaango, jinsi unavyoyapika,
Na kibwebwe kiachiye, au utaadhirika,
Kazi hiyo isusiye, hasara sijekufika.”

Diwani hii inaendelea kuonesha unafiki wa watu wa dini kupitia shairi la “UASI” (uk.8) Watu hawa hujidai mbele za watu ni waongofu wakati ni wachafu na wadhaifu katika matendo yao. Hawa ni watu wanaokashifu dini za wenzao kwa kudai kuwa zao ndizo safi na sahihi. Shairi linasema:


“Uasi
Masheikh na masharifu,
Mapadri na maaskofu,
Kauli zao nadhifu,
Hujigamba waongofu,
Wengi wao ni wachafu,
Wenye vitendo dhaifu,
Dini wanazikashifu,
Wanafiki.”

Unafiki wa baadhi ya watu unaendelea kuoneshwa kwenye shairi la “PEPO BILA KIFO” (uk.14) ambapo baadhi yatu hupenda vitu fulani fulani bila kufuata kanuni za upatikanaji wa vitu hivyo. Kitendo cha mtu kupenda pepo bila kuonja mauti ni cha kinafiki. Vilevile kitendo cha kupenda starehe za wanawake ni cha kinafiki kwani peponi si mahali pa kufanyia umalaya bali ni mahali patakatifu. Hivyo afikiriaye mambo haya ni mnafiki kwani hajui neno la Mungu linasemaje kuhusu pepo. Katika kuonesha unafiki shairi hili linasema:


5. “Nibembee na hurulaini,
Wanawake wazuri wa shani,
Wawashindao wa duniani,
Nipumbazike.”

Unafiki mwingine unajionesha katika siasa ambapo baadhi ya viongozi hupata uongozi kwa kujipendekeza na kutoa maneno ya hapa na pale kwa wale wanawapatia hivyo vyeo. Haya tunayapata katika shairi la “WARAMBA NYAYO” (uk.46-47)


1. ‘Wajikomba,
Ili kupata vyeo,
Na uluwa.”

USALITI: Mshairi Mohammed Seif Khatibu ameonesha suala la usaliti katika diwani hii ya WASAKATONGE, kwani tunaambiwa kuwa, mara nyingi tunakuwa pamoja katika safari ya kutafuta kitu fulani lakini pindi kinapopatikana tu tunawatenga baadhi ya watafutaji wenzetu. Haya yanadhihirishwa wazi katika shairi la “SIKULIWA SIKUZAMA” (uk.22-23) ambapo msanii anabainisha kwa kusema kuwa;


1. “Nilitoswa baharini,
Ya dharuba na tufani,
Walitaka nizame,
Wao wanitazame,
Nife maji wakiona,
Waangue na vicheko,
Na kushangilia,
Ushindi wao!”

Usaliti wa aina hii unajitokeza tena katika shairi la “ASALI LIPOTOJA” (uk.37-38), Shairi hili linaweza kufananishwa na hekaheka za kupigania uhuru ambapo baada ya kupata uhuru baadhi ya watu walioshiriki katika kuutafuta uhuru huo, walitengwa kabisa. Lakini pia matunda yaliyotegemewa baada ya uhuru hayajapatikana kwa wote bali kwa watu wachache tu wenye mirija mirefu (viongozi) kama lisemavyo shairi hili:


2. “Mili ikatuvimba,
Ila hatukuyumba,
Tukabakia shambani,
Kutumaini kwamba,
Faida itawamba,
Heri itafika.”


3. “Asali lipotoja,
Wengi walikuja,
Na mirefu mirija,
Kwao kawa tafrija,
Wakapata faraja,
Sisi tukatengwa.”

Katika shairi la “VINYONGA” (uk.49) tunabaini pia usaliti wa wanasiasa kwa wananchi. Shairi hili linaonesha kuwa wanasiasa wanatenda mambo kinyume na maadili na hivyo kuwasaliti wananchi waliowaweka madarakani. Viongozi hawa hawatekelezi yale wanayoahidi kwa wananchi wao badala yake wanatumia nafasi walizo nazo katika kujitajirisha wao wenyewe. Shairi linasema;


2. “Jukwaa,
Meingiliwa,
Wanasiasa vinyonga,
Maisha ya ufahari,
Kauli zao nzuri,
Vitendo vyao hatari,
Ni kinyume na maadili,
Ni usaliti.”

Usaliti mwingine umejitokeza katika mapenzi. Mshairi anasema kuwa alikesha kwa ajili ya kumsubiri wake mahaba, ili baadaye wawe wawili. Hata hivyo mkesha wake haukuzaa matunda kwani mwenzie alimsaliti kwa kutofika katika eneo la tukio kama anavyoonesha katika shairi la “NILIKESHA” (uk.23-24)


4. “Nilikesha,
Na kulikucha sikukuona,
Nathibitisha wako uungwana,
Kosa langu kukupenda sana,
Hustahiki heshima hiyo,
Sisahau sikusamehe,
Nilikesha.”

Pia katika shairi la “SIKUJUA” (uk.28) linaonesha usaliti wa baadhi ya watu. Msanii anasema kuwa, aliyemfuga kwa mategemeo ya kumsaidia mambo mbalimbali amegeuka na kufanya kinyume na mategemeo au makubaliano. Msanii anadhihirisha hili kwa kusema;
4 “Kumbe nimefuga punda, mashuzi ndio heshima,
Ni ukaidi wa inda, mateke kurusha nyuma,
Nyama limekuwa nunda, mfugaji humuuma.”

MAPENZI/MAHABA: Miongoni mwa dhamira ambazo zimezungumziwa kwa kina katika diwani hii ni Mapenzi. Mshairi huyu anaonesha kuwa, mapenzi yana raha yake na pindi yanapokwenda mrama huleta karaha kubwa kwa mtu mmoja au wawili waliofarakana. Mshairi anasema kuwa mapenzi ni kitu muhimu sana kwake na yupo tayari kuitwa jina lolote lile kwa sababu ya kuyathamini mapenzi. Haya tunayapata kupitia shairi la “MAHABA” (uk.1-2)


4. Kama mahaba wazimu, sihitaji nitibiwe,
Bora niwe chakaramu, nipigae watu mawe,
Kuwa kwangu mahamumu, wewe isikusumbuwe,
Dawa yangu siyo ngumu, mimi nipendwe na wewe.

Kwa vile mshairi huyu anaona kuwa mapenzi ndicho kitu cha thamani kubwa kwake ayakosapo au amkosapo yule ampendaye hukonda na kudhoofika mwili kama asemavyo katika shairi la “SILI NIKASHIBA” (uk.17)


2. “Sili nikashiba, nikikukumbuka,
Hula haba, na kushikashika,
Ni chozi za huba, kweli nasumbuka.

Hali ya kupenda kwa dhati inajitokeza katika shairi la “NILIKESHA” (uk.23-24) ambapo mtu anaamua kukesha kwa kusubiri ahadi ya huba ingawa apendwaye huenda hayuko tayari kupenda. Shairi hili linasema;


1. “Nilikesha,
Si kwa ibada au shakawa,
Sio kwa ngoma ama takuwa,
Ila kwa hamu na nyingi hawa,
Ikawa hakupambazuki,
Ni mtekwa wa huba zako.”
Nilikesha.

Katika mashairi ya “USIKU WA KIZA” (uk.27-28) na “MACHOZI YA DHIKI” (uk.28) yanaendelea kuzungumzia hali hiyo ya mapenzi. Katika shairi la “USIKU WA KIZA” tunaoneshwa majonzi ya mpenzi mmoja aliyeondokewa na kipenzi chake. Kutoweka kwa mahabuba wake kunamfanya asile na kushiba kama shairi linavyosema;


2. “Meniondokeya, wangu mahabuba,
Nilikuzoweya, kwa yako mahaba,
Nnajikondeya, sili nikashiba.”

Vilevile katika Shairia la “MACHOZI YA DHIKI” (uk.28) mpenda anabubujikwa machozi kwa kuadimikiwa na wake mahabuba, yaani anateseka kutokana na kuadimika kwa mpenzi wake.

Mshairi anaendelea kutetea mapenzi ya dhati katika shairi la “PEPO TAMU” (uk.35) ambapo anasema kuwa penzi tamu ni penzi lililojaa raha na lina ladha kushinda asali. Pendo tamu hufukuza uchoyo uheka.


4 “Pendo lenye tabasamu, za dhati si za uheka,
Na nyoyo za ukarimu, uchoyo ni sumu yake,
Haliishi yake hamu, hupendi imalizike.”

Kwa kuwa mpendwa anaonesha pendo la dhati, apendwaye pia anatakiwa aoneshe pendo lake kwa kutoa kauli kuhusu kupenda au kutopenda kwake kwa yule anayemtaka. Hii ni katika shairi la “ITOE KAULI YAKO” (uk.27)


1. “Itoe yako sauti, kama, kweli wanipenda,
Niweze kujizatiti, moyo uondoke funda,
Nizidi kukudhibiti, sikuache hata nyanda.”

Shairi hilo linataka mpendwa atoe kauli yake kwani mpenda ameshatoa kauli yake ya upendo kama asemavyo katika shairi la “WEWE WAJUA” (uk.25)


1. “Nakupenda, nawe wajua,
Tusitupane,
Tupendane,
Kwa salama.”

Hali hii pia inajitokeza katika shairi la “NAKUSABILIYA” (uk.23) ambapo msanii anatoa pendo lake lote kwa yule ampendaye kama asemavyo katika ubeti wa kwanza;


1. “Nakusabiliya, pendo lote kwako,
Litaseleleya, litabaki kwako,
Sitaliachiya, kwenda kwa mwenzako.”

Kama apendwaye ataonesha pendo la dhati kwa yule ampendaye basi watalindana na kulifanya pendo lao kuwa la wawili tu kama lisemavyo shairi la “NILINDE” (uk.15)


1. Nilinde sichukuliwe, hata kwa moja shubiri,
Tubaki mimi na wewe, pendo letu linawiri,
Tuwazidishe kiwewe, wasotutakia heri.

Pia hali kama hii itasaidia kudumisha penzi lao milele na milele watabaki wawili peke yao huku wakifurahia pendo lao maridhawa. Haya tunayapata katika shairi la “TUTABAKI WAWILI” (uk.26) na “YEYE NA MIMI” (uk.39). Katika shairi la “TUTABAKI WAWILI”, tunaambiwa kuwa;


2. Hakuna wa kulizima, pendo langu kufifiya,
Litabakia daima, na kwako kuseleleya,
Hadi siku ya kiyama, pendo litaendelea,

Shairi la “YEYE NA MIMI” linadai kuwa penzi tamu na dhati huwafanya watu wawili wapendanao wakeshe katika mapenzi bila kuchoka

4. “Yeye na mimi wawili, hatuna tunobakisha,
Humsabilia mwili, hana anapobakisha,
Ana mahaba ya kweli, usiku kucha hukesha.”

Katika diwani hii tunaambiwa kuwa kama unampenda mtu asiyekupenda basi usimchukui isipokuwa muagane kwa wema pale inapobidi kama inavyojionesha katika shairi la “KWA HERI” (uk.29)


3. Ingawa menisusia kujipa kunigomeya,
Mvua hunyesha masika, masika hukesha,
Hakuna ukame,
Kwa heri.

Diwani hii inaonesha kuwa kukataliwa kimapenzi si mwisho wa dunia bali ni njia mojawapo ya kufunguliwa mlango kwa wengine hasa yule akupendaye kwa dhati. Haya yote tunayapata katika shairi la “NILICHELEWA KUPENDA” (uk.41)


1. Katika uhai wangu, nilichelewa kupendwa,
Waliowakija kwangu, wale wa kunizuzuwa,
Mwaka huu mwaka wangu, nami nimejaaliwa.

Kwa upande wa pili msanii anakemea mapenzi ya sio ya dhati (ulaghai) kutokana na kutokuwa na faida yoyote kwa mtu na kwa jamii kwa ujumla. Mapenzi ya namna hii tunayapata katika shairi la “SI WEWE” (uk.21-22) ambapo msanii anahoji na kumsuta mtu aliyempenda kwa chati. Mapenzi haya hayana faida yoyote isipokuwa mateso makali kwa mhusika au wahusika;



4. Umeshapwelewa baharini,
Wako werevu umekwisha,
Sasa unatweta,
U taabani,
Ni wewe ulo mlafi,
Si wewe?

Msanii anaendelea kusema mapenzi ya chati katika shairi la “WEWE JIKO LA SHAMBA” (uk.44) Hapa msanii anakemea tabia ya watu wanaofanya mapenzi kiholela kuwa waachane na tabia hiyo kwani haina faida isipokuwa karaha na kusutwa. Anaendelea kuwaambia kuwa;

4 Takula wako ujuvi, na mwingi uhayawani,
Upikavyo haviivi, ni vibichi sahanini,
Vitachacha hivihivi, kuozea mikononi.

Watu wa aina hii sharti wajitakase ili wakubalike katika jamii yaani “wayapangue mafiga, jiko halitaivisha” wasipofanya hivyo, hawatapata kitu chochote cha maana kwani wapenzi (wawezeshaji) wamekuwa wengi. Shairi la “BUZI LISILOCHUNIKA” (uk.45)

4 Msumeno utafute, na makali kuyaweka,
Ukwereze na uvute, na watu kukusanyika,
Na hutafika popote, buzi halitachunika.

Kwa ujumla msanii anazungumzia mapenzi ya aina mbili, mapenzi ya dhati ambayo kwake ndio ngao na mapenzi ya chati ambayo huleta karaha tupu katika maisha ya mwanadamu.




Swali.


Soma makala ya M.M.Mlokozi katika jarida la mulika (1989) namba 21 kisha jadili vigezo alivyovitumia katika kugawa tanzu na vipera vya Fasihi Simulizi.

DONDOO:

UTANGULIZI:

Maana ya Fasihi Simulizi

Maana ya tanzu

Maana ya vipera

KIINI:

Kuchambua vigezo alivyotumia Mulokozi katika kugawanya tanzu na vipera vya Fasihi Simulizi.

Kwa mujibu wa Mulokozi katika Mulika namba 21, (1989). Pamoja na kwamba Fasihi ni kongwe lakini kitaaluma bado ni changa kwa sababu ilianza kuchungunzwa hivi karibuni. Hivyo imepelekea kutokuwepo kwa nadharia, marejeo, wala istilahi zenye kutosheleza mahitaji ya taaluma hiyo. Tatizo hili linadhihirika pale tunapoangalia kazi za wataalamu mbalimbali kuhusu tanzu za Fasihi Simulizi. Kwa upande wa nadharia kitabu pekee kinachozijadili tanzu za Fasihi Simulizi kwa urefu ni kitabu cha Ruth Fennegan kinachoitwa Oral Literature in Africa (1970). Kwa upande wa Kiswahili hakuna kitabu kinachojadili uwanja wa tanzu za Fasihi Simulizi. Badala yake kunamiongozo michache kwa ajili ya shule za sekondari kama vile Balisidya, N (1975) na Taasisi ya Elimu (1987)

Mulika namba 21 ni jarida la kitaaluma linalotoa fursa kwa wataalamu, waalimu na wanafunzi katika kujadili mada mbalimbali za kiswahili. Jarida hili lililoandikwa mwaka 1989 ndani yake kuna makala ya Fasihi Simulizi inayohusu tanzu za Fasihi Simulizi na vipera vyake iliyoandikwa na M.M.Mulokozi.

Hivyo basi kutokana na kukosekana kwa nadharia zinazoongoza ugawaji wa tanzu za Fasihi Simulizi ya Kiswahili wataalamu wengi wamekuwa wakitumia vigezo mbalimbali ambavyo ni maudhui, fani, matukio, idadi ya waimbaji, vifaa vinavyotumika na namna ya uimbaji.

Fasihisi Simulizi imejadiliwa na wataalamu mbalimbali miongoni mwa waalamu hao ni M.M.Mulokozi (1996) anasema Fasihi Simulizi ni fasihi inayotungwa au kubuniwa kichwani na kuwasilishwa kwa hadhira kwa njia ya mdomo na vitendo bila kutumia maandishi.

TUKI (2004) Fasihi Simulizi ni kazi ya fasihi inayohifadhiwa na kurithishwa kutoka kizazi kimoja hadi kingine kwa njia ya mdomo kama vile; hadithi, ngoma na vitendawili.

Hivyo basi Fasihi Simulizi ni fasihi inayotokana na maneno ambayo huzungumzwa, hutolewa au kuimbwa ambapo mtungaji na mwasilishaji hutumia sanaa.

Tanzu ni istilahi inayotumiwa kuelezea au kurejelea aina ya kazi mbalimbali za kifasihi. Inawezekana utanzu mkuu kuwa na vitanzu vingine mbalimbali kwa mfano, tanzu kuu za kifasihi ni Riwaya, Tamthilia, Shahiri, Novela, Insha na Hadithi (Wamitila (2003).

Vipera ni dhana inayotumiwa kuelezea vijitanzu katika fasihi hasa fasihi simulizi. Mfano: semi methali, mafumbo, vitendawili nakadhalika. (Wamitila 2003)

M.M.Mulokozi katika makala yake ya tanzu za Fasihi Simulizi iliyo katika jarida la Muulika namba 21(1989) amezigawa tanzu na vipera vya Fasihi Simulizi kwa kutumia vigezo viwili ambavyo ni,kigezo cha kwanza ni umbile na tabia ya kazi inayohusika na kigezo cha pili ni muktadha na namna ya uwasilishaji wake kwa hadhira.

Umbile na tabia ya kazi inayohusika: katika kigezo hiki Mulokozi ameangalia vipengele vya ndani vinavyoiumba sanaa hiyo na kuipa muelekeo au mwenendo. Baadhi ya vipengele hivyo vya ndani ni namna lugha inavyotumika (kishahiri, kinathari, kimafumbo, kiwimbo na kighani), muundo wa fani hiyo na wahusika. Kwa upande wa muktadha na namna ya uwasilishaji amezingatia kuwa, Fasihi Simulizi ni tukio hivyo huambatana na muingiliano wa mambo matatu ambayo ni muktadha, watu na mahali. Mwingiliano huu ndio unaotupa muktadha na muktadha ndio unaoamua fani fulani ya Fasihi Simulizi ichukue umbo lipi, iwasilishwe vipi kwa hadhira, kwenye wakati na mahali hapo. Hivyo hadithi inaweza kugeuzwa wimbo, utendi unaweza kuwa hadithi na wimbo unaweza kugeuzwa ghani au usemi kutegemea muktadha unaohusika (Mulokozi 1989).

Kwa hiyo kwa kutumia vigezo hivi, Mulokozi amezigawa tanzu na vipera vya Fasihi Simulizi kama ifuatavyo;

Masimulizi; hii ni tanzu ya Fasihi Simulizi yenye kusimulia habari fulani. Katika kugawa utanzu huu vigezo vilivyotumika ni pamoja na kigezo cha lugha ambapo lugha inayotumika katika masimulizi ni ya kinathari. Pia kigezo kingine ni kigezo cha muundo, mara nyingi masimulizi huwa na muundo unaojitofautisha na tanzu nyingine kama vile ushairi. Katika masimulizi muundo wake mara nyingi huwa wa moja kwa moja yaani mtiririko wa visa na matukio. Vilevile kigezo kingine ni kigezo cha wahusika ambapo katika kigezo hiki huhusisha wahusika wa pande mbili ambao ni mtendaji na watendwaji. Pia kigezo kingine ni kigezo cha namna ya uwasilishaji. Katika uwasilishwaji huwasilishwa na msimuliaji mbele ya hadhira. Kigezo kingine ni kigezo cha mandhari ambayo huwa maaluma kama vile chini ya mti mkubwa na uwanjani. Masimulizi pia hufanyika katika muda maalum. Mfano, baada ya kazi.

Masimulizi yamegawanyika katika tanzu kuu mbili ambazo ni tanzu za kihadithi (za kubuni) na tanzu za kisalua (kihisitoria). Tanzu za kihadithi zina kipera kimoja ambacho ni ngano. Ngano (vigano/hurafa), hizi ni hadithi za kimapokeo zitumiazo wahusika kama wanyama, miti na watu kuelezea na kuonya kuhusu maisha. Vigezo vilivyotumika katika kugawa ngano ni kigezo cha lugha ambayo ni lugha ya kinathari, kigezo cha dhima ambacho huelezea au kuonya kuhusu maisha na kufurahisha. Kigezo kingine kilichotumika ni kigezo cha wahusika ambao ni wanyama, miti na watu. Kipera hiki cha ngano kinajumuisha vijipera vifuatavyo ambavyo ni istiara, mbazi na kisa.

Istiara; hii ni hadithi ambayo maana yake ya wazi inawakilisha maana nyingine iliyofichika. Vigezo vilivyotumika katika kugawa kipera hiki ni kigezo cha lugha ambayo ni lugha ya mafumbo.

Mbazi; hii ni hadithi fupi yenye mafunzo itolewayo kama kielelezo wakati wa maongezi au kumkanya mtu. Kigezo kilichotumika katika kugawa kipera hiki ni kigezo cha dhima.

Kisa; hii ni hadithi fupi ya kufurahisha kuhusu tukio la kweli. Kigezo kilichotumika ni kigezo cha kidhima.

Utanzu mwingine wa masimulizi ni utanzu wa kisalua. Utanzu huu umegawanyika katika vipera vifuatavyo ambavyo ni visakale, mapisi, tarihi, kumbukumbu na visasili.

Visakale; haya ni masimulizi ya mapokeo juu ya wahenga au mashujaa wa kabila au taifa yenye kuchanganya chuku na historia (kama hadithi ya Liyongo). Vigezo vilivyuotumika hapa ni kigezo cha wahusika ambao wapo katika historia yaani mashujaa fulani. Kigezo kingine ni fani ya ubunifu.

Mapisi; haya ni maelezo ya kihistoria bila kutia mambo ya kubuni. Hapa pia kigezo kilichotumika ni kigezo cha dhima ambacho huelezea mambo ya kihistoria yaliyo ya kweli.

Tarihi; haya ni maelezo au jedwali la matukio muhimu na tarehe zake. Kigezo kilichotumika hapa ni kigezo cha kidhima ambacho ni kuelezea matukio muhimu na tarehe zake. Pia kigezo kingine ni namna ya uwasilishaji ambapo huwasilishwa kwa kutumia jedwali na lugha yake huwa katika maandishi.

Kumbukumbu; haya ni maelezo ya matukio muhimu yanayomuhusu mtu binafsi au jamii ya watu. Hapa kimetumika kigezo cha fani, ambayo ni fani za wasifu na tawasifu. Pia kigezo kingine ni kigezo cha wahusika ambao ni watu.

Visasili; hiki ni kipera kinachofungamana na imani za dini na mizungu ya kajamii pia hizi ni hadithi za kale zenye kuwakilisha imani na mtazamo wa jamii inayohusika kuhusu asili ya ulimwengu na maisha yao. Kigezo kilichotumika ni kigezo cha kidhima ambacho huelezea shabaha ya maisha.

Utanzu mwingine wa Fasihi Simulizi ni utanzu wa Semi. Semi ni tungo au kauli fupi fupi za kisanaa zenye kubeba maana au mafunzo. Kigezo kilichotumika katika kugawa utanzu huu ni kigezo cha lugha ambayo ni lugha ya mkato. Kigezo kingine ni kigezo cha kidhima ambacho ni kufunza.

Utanzu huu umegawanyika katika vipera vifuatavyo ambavyo ni methali, vitendawili, misimu, mafumbo na lakabu.

Methali ni semi fupi fupi zenye kueleza kwa mukhtasari fikra au mafunzo mazito yaliyotokana na uzoefu wa kijamii. Vigezo vilivyotumika katika kipera hiki ni kigezo cha lugha ambayo ni lugha ya mafumbo. Vilevile kimetumika kigezo cha muundo ambapo methali huundwa na muundo wa pande mbili ambazo hutegemeana.

Vitendawili; huu ni usemi uliofumbwa ambao hutolewa kwa hadhira ili ufumbuliwe. Vigezo vilivyotumika ni kigezo cha lugha. Hapa lugha inayotumika ni lugha ya kimafumbo.

Misimu; ni semi za muda na mahali maalum ambazo huzuka na kutoweka kutegemea mazingira maalum. Hivyo vigezo vilivyotumika katika kugawa kipera hiki ni kigezo cha muktadha yaani hutokea wakati maalum na mazingira maalum.

Mafumbo; ni semi za maonyo au mawaidha ambazo maana zake za ndani zimefichika. Kigezo kilichotumika ni kigezo cha kidhima ambacho ni kuonya pamoja na kigezo cha lugha ambayo ni lugha ya mafumbo.

Lakabu; haya ni majina ya kupanga ambayo baadhi ya watu hupewa au hujipatia kutokana na sifa zao za kimwili, kinasaba, kitabia au kimatendo. Kigezo kilicho tumika katika kipera hiki ni kigezo cha lugha ambayo lugha iliyotumika ni lugha kificho yaani maana yake hufichwa.

Utanzu mwingine wa Fasihi Simulizi ni ushairi. Huu ni utanzu wa fasihi simulizi unaowasilishwa kwa hadhira kwa njia ya uimbaji au ughani badala ya usemaji wa kawaida. Vigezo vilivyotumika katika kugawa utanzu huu ni kigezo cha lugha ambayo ni lugha ya kishairi. Pia kimetumika kigezo cha fani ambapo fani inayotumika ni wizani, lugha ya mkato, lugha ya mafumbo na uimbaji au ughani.

Katika utanzu huu kuna vipera viwili ambavyo ni nyimbo na maghani;

Nyimbo ni kila kinachoimbwa. Vigezo vilivyotumika katika kipera hiki cha ushairi ni kigezo cha fani ambapo huangalia muziki wa sauti ya muimbaji au waimbaji, muziki wa ala (kama ipo), matini au maneno yanayoimbwa. Pia kuna kigezo cha muktadha ambacho huzingatia hadhira inayoimbiwa na muktadha unaofungamana na wimbo huo, kwa mfano sherehe, ibada, kilio nakadhalika. Kwa vigezo hivi utanzu wa nyimbo umegawanyika katika vijipera vifuatavyo ambavyo ni, tumbuizo, bembea, kongozi, nyimbo za dini, wawe, tenzi, tendi, mbolezi, kimai, nyiso, nyimbo za vita, nyimbo za uwindaji, nyimbo za taifa, nyimbo za watoto na nyimbo za kazi.

Tumbuizo; hizi ni nyimbo za furaha ziimbwazo kuwafurahisha watu kwenye matukio mbalimbali kama vile ngomani au harusini. Vigezo vilivyotumika hapa ni kigezo cha kidhima ambacho hulenga kuwafurahisha watu, pia kigezo kingine ni kigezo cha kimuktadha ambapo huwasilishwa katika matukio yanayoendana na dhima ya kufurahisha.

Bembea; hizi ni nyimbo za kubembeleza watoto. Kigezo kilichotumika hapa ni kigezo cha kidhima ambapo hulenga kubembeleza watoto.

Kongozi; hizi ni nyimbo za kuaga mwaka. Vigezo vilivyotumika hapa ni kigezo cha kidhima ambapo dhima yake ni kuaga mwaka na kigezo cha kimuktadha ambapo muktadha wake ni muktadha maalum yaani huimbwa mwishoni mwa mwaka.

Nyimbo za dini; hizi ni nyimbo zinazoimbwa kwa lengo la kumsifu Mungu au miungu. Vigezo vilivyotumika ni kigezo cha kidhima ambapo dhima yake ni kumsifu Mungu au miungu, pia kimetumika kigezo cha kimuktadha ambapo huimbwa katika muktadha wa kidini.

Wawe; hizi ni nyimbo za kilimo. Vigezo vilivyotumika ni kigezo cha kimuktadha ambapo huuimbwa wakati wa kulima, pia kigezo cha kidhima kimetumika ambapo dhima yake ni kuchapusha kazi.

Tenzi; hizi ni nyimbo ndefu za kimasimulizi au mawaidha. Kigezo kilichotumika ni kigezo cha kifani ambapo fani yake ni masimulizi au mawaidha.

Tendi; hizi ni nyimbo ndefu za masimulizi juu ya matendo ya mashujaa. Vigezo vilivyotumika hapa ni kigezo cha kifani ambapo wahusika wa tendi ni watu wenye historia za matendo ya kishujaa, pia kigezo cha lugha kimetumika ambapo lugha yake ni ya kinathari.

Mbolezi; hizi ni nyimbo za kilio au maombolezo. Vigezo vilivyotumika katika kugawa kipera hiki ni kigezo cha kimuktadha ambapo huwasilishwa katika muktadha wa maombolezo au kilioni/msibani, pia kimetumika kigezo cha kidhima ambapo dhima yake ni kuomboleza.

Kimai; hizi ni nyimbo zihusuzo shughuli za baharini. Vigezo vilivyotumika hapa ni kigezo cha kidhima ambapo dhima yake ni kuchapusha kazi. Vilevile katika kigezo cha kimuktadha kimai huwasilishwa katika mazingira ya baharini.

Nyiso; hizi ni nyimbo za jandoni. Vigezo vilivyotumika ni kigezo cha kidhima ambapo dhima yake ni kutoa mafunzo kwa vijana kuhusu maisha ya utu uzima. Kigezo kingine ni kigezo cha kimuktadha ambapo nyiso huwasilishwa katika mazingira maalumu, kama vile porini nakadhalika.

Nyimbo za vita; hizi ni nyimbo ziimbwazo na askari wakati wa vita. Vigezo vilivyotumika katika kugawa kipera hiki ni kigezo cha kimuktadha ambapo muktadha wake huwa ni wakati wa vita, na kigezo kingine ni kigezo cha wahusika au waimbaji ambapo waimbaji wake huwa ni maaskari.

Nyimbo za watoto, hizi ni nyimbo waimbazo watoto wakati wa michezo yao. Vigezo vilivyotumika ni pamoja na kigezo cha kimuktadha ambapo huwasilishwa wakati wa michezo ya watoto. Kigezo kingine ni kigezo cha wahusika au waimbaji ambapo waimbaji wake huwa ni watoto.

Nyimbo za uwindaji; hizi ni nyimbo ambazo huimbwa na makundi ya wawindaji wakati wa shughuli au sherehe zao. Vigezo vilivyotumika hapa ni kigezo cha wahusika au waimbaji ambapo huimbwa na wawindaji na kigezo kingine ni kigezo cha kimuktadha ambapo huwasilishwa wakati wa shughuli au sherehe za uwindaji.

Nyimbo za Taifa; hizi ni nyimbo za kisifia Taifa au kabila. Kigezo kilichotumika hapa ni kigezo cha kidhima ambapo dhima yake ni kusifia Taifa au kabila.

Nyimbo za kazi; hizi ni nyimbo zinazoimbwa katika shughuli mbalimbali kama vile, kulima, kutwanga, kusuka, uvuvi, uashi, useremala na kadhalika. Vigezo vilivyotumika hapa ni kigezo cha muktadha wa uwasilishaji ambapo huwasilishwa kulingana na shughali maalumu. Pia kigezo kingine ni kigezo cha kidhima ambapo dhima ya nyimbo za kazi ni kuchapusha kazi.

Maghani; hiki ni kipera cha ushairi kinachotolewa kwa kalima badala ya kuimbwa. Kwa mujibu wa Wamitila (2003) maghani ni istilahi inayotumiwa kuelezea aina ya ushairi ambao hutolewa kwa kalima au maneno badala ya kuimbwa. Vigezo vilivyotumika katika kugawa utanzu huu ni lugha ambayo ni lugha ya kishairi. Pia ametumia kigezo cha wahusika ambapo wahusika wakuu ni binadamu. Hivyo vigezo hivi ndivyo vilivyopelekea utanzu huu kuwekwa kwenye utanzu wa ushairi.

Kipera hiki kina vijipera vitatu ambavyo ni maghani ya kawaida, sifo na maghani masimulizi. Maghani ya kawaida ni kundi ambalo tunaweza kuingiza fani mbalimbali za ushahiri simulizi kama vile ushairi wa mapenzi, siasa, maombolezo, kazi, dini ilimradi unaghanwa katika namna ya uwasilishwaji wake.

Sifo; hizi ni tungo za kusifu ambazo husifu watu, wanyama na mimea. Baadhi ya sifo huwa zinakashifu au kukejeli. Vigezo vilivyotumika katika kugawa kipera hiki ni kigezo cha wahusika, wahusika wake wakuu ni binadamu wanyama au mimea. Kigezo kingine ni muktadha ambao huelezea matukio yaliyopita au yaliyopo. Sifo huwa na tanzu muhimu kama vile vivugo (majigambo), pembezi na tondozi.

Kivugo; hili ni ghani la kujisifia, hutungwa na kughanwa na muhusika mwenyewe. Vigezo vilivyotumika katika kugawa kijipera hiki cha sifo ni lugha, katika lugha zimetumika mbinu kama vile sitiari, mkato, vidokezo, ishara, takriri na vina. Kigezo kingine ni kigezo cha wahusika ambapo wahusika wake wakuu ni binadamu pia kimetumika kigezo cha muktadha ambapo muktadha wake hufungamana na tukio maalum katika maisha ya muhusika, mfano vitani. Vilevile katika kigezo cha uwasilishaji huweza kuwa na masimulizi ndani yake. Muundo wake hutegemea shabaha za mtunzi na jadi ya utunzi anayoiwakilisha hakiandikwi na kutungwa papo kwa papo.

Tondozi; hizi ni tungo za kusifu watu, wanyama au vitu. (Pembezi pia ni aina ya tondozi ambayo imekusudiwa watu wa aina fulani tu). Vigezo vilivyotumika katika kugawa kipera hiki ni kigezo cha wahusika ambao ni wanyama na mimea. Mfano wa wanyama ni kama vile Simba. Kigezo kingine ni lugha ambayo ni lugha ya kishairi.

Ghani masimulizi: hizi ni ghani ambazo hutambwa ili kusimulia hadithi, historia au tukio fulani. Vigezo vilivyotumika kugawa kipera hiki ni pamoja na kigezo cha lugha, lugha inayotumika katika kijipera hiki ni lugha ya kishairi na fani iliyotumika ni kusimulia hadithi/tukio kwa kirefu. Vile vile kuna kigezo cha namna ya uwasilishaji huambatana na ala za muziki mfano zeze na marimba.

Ghani masimulizi ina vipera vinne ambavyo ni rara, ngano, sifo na tendi.

Rara ni hadithi fupi nyepesi ya kishairi yenye visa vya kusisimua, vigezo vilivyotumika katika kugawa kipera hiki ni pamoja na lugha inayotumika, lugha inayotumika katika kipera hiki ni lugha ya kishairi, fani iliyotumika ni fani ya kihadithi ambayo ni hadithi fupi, nyepesi na inavisa vya kusisimua na kigezo kingine ni muktadha wa uwasilishaji ambapo huimbwa au kughanwa ikiambatana na ala za muziki.

Ngano; hizi ni hadithi za mapokeo zitumiazo wahusika kama wanyama, miti na watu katika kuelezea au kuonya kuhusu maisha. Katika kipera hiki kigezo kilichotumika ni muktadha wa uwasilishaji, kwamba huwasilishwa pamoja na ala ya muziki. Ngano huwa ghani masimulizi inapowasilishwa pamoja na ala ya muziki.

Sifo; hizi ni tungo za kusifu, kigezo kilichotumika ni muktadha wa uwasilishaji: sifo huwa ghani masimulizi inapoingiza muziki katika utondozi wake, lugha iliyotumika ni lugha ya kishairi.

Tendi; hizi ni ghani ndefu za masimulizi juu ya matendo ya mashujaa yenye uzito kijamii au kitaifa. Vigezo vilivyotumika katika kugawa kipera hiki ni fani ambayo ni huhusu matukio muhimu ya kihisitoria au ya kijamii. Kigezo kingine ni muktadha wa uwasilishaji, hutungwa na kuwasilishwa papo kwa papo.

Utanzu mwingine wa Fasihi Simulizi ni utanzu wa mazungumzo. Mazungumzo ni maongozi au maelezo ya mdomo katika lugha ya kawaida juu ya jambo lolote lile. Si kila mazungumzo ni fasihi ili mazungumzo yaitwe fasihi lazima yawe na usanii wa aina fulani. Vigezo vilivyotumika katika kugawa utanzu huu ni kigezo cha lugha ambapo lugha iliyotumika ni lugha ya kifasihi. Kigezo kingine ni kigezo cha kimuundo ambapo muundo wake huwa wa kidayalojia.

Utanzu huu wa mazungumzo una vipera vifuatavyo ambavyo ni hotuba, malumbano ya watani, soga, mawaidha na ulumbi.

Hotuba; haya ni mazungumzo ambayo huwasilishwa kwenye vikao rasmi vya kimila, kisiasa au kidini. Vigezo vilivyotumika katika kugawa kipera hiki ni kigezo cha lugha ambapo lugha yake huwa rasmi, sanifu na ya kisanaa. Kigezo kingine ni kigezo cha kimuktadha ambapo hotuba huwasilishwa katika mazingira maalumu kwa mfano katika vikao rasmi au mikutano.

Malumbano ya watani; haya ni mazungumzo yanayozingatia masharti yanayotawala uhusiano wao wa kiutani. Huweza kuwa utani wa kikabila, utani wa mababu au mabibi na wajukuu. Vigezo vilivyotumika katika ugawaji wa kipera hiki ni kigezo cha lugha ambapo lugha huwa ni ya kimafumbo. Kigezo kingine ni kigezo cha wahusika ambapo wahusika huwa na uhusiano wa karibu.

Soga; haya ni mazungumzo ya kupitisha wakati ili kusubiri kitu fulani. Vigezo vilivyotumika katika kugawa kipera hiki ni kigezo cha kidhima ambapo dhima yake ni kupitisha wakati. Kigezo kingine ni kigezo cha lugha ambapo lugha inayotumika siyo rasmi. Vilele kuna kigezo cha muktadha ambapo muktadha wake huwa ni mahali popote.

Mawaidha; haya ni maneno ya maonyo au mafunzo aghalabu huwa ya kidini na yenye muongozo. Kigezo kilichotumika katika kugawa kipera hiki ni kigezo cha kidhima ambapo dhima yake ni kuonya au kutoa muongozo.

Ulumbi; huu ni uhodari wa kuzungumza ambao huwa ni wa kiufasaha na madoido. Vigezo vilivyotumika katika kugawa kipera hiki ni kigezo cha kifani ambapo lugha iliyotumika ni lugha ya kimadoido na kifasaha.

Utanzu mwingine katika Fasihi Simulizi ni utanzu wa maigizo. Maigizo ni michezo ambayo hutumia watendaji wa kuiga tabia na matendo ya watu au viumbe wengine ili kuburudisha na kutoa ujumbe fulani kwa hadhira. Vigezo vilivyotumika katika kutenga utanzu huu ni kigezo cha namna ya uwasilishaji ambapo huwasilishwa kwa kuiga matendo ya watu au wanyama. Kigezo cha kidhima ambapo dhima yake ni kuburudisha, kuelimisha au kuonya. Pia kimetumika kigezo cha mandhari ambapo maigizo huambatana na matukio maalumu kama vile kwenye maadhimisho ya sherehe fulani na katika matukio ya kijamii.

Utanzu mwingine wa Fasihi Simulizi ni utanzu wa ngomezi. Ngomezi ni ile hali ya kupeleka ujumbe kwa kutumia mdundo wa ngoma. Vigezo vilivyotumika katika utanzu huu ni kigezo cha kifaa cha uwasilishaji ambacho ni ngoma. Pia kigezo kingine ni kigezo cha kidhima ambapo dhima yake ni kupeleka taarifa fulani kwa jamii. Mfano taarifa hiyo yaweza kuwa ya msiba, mkutano na kadhalika.

Pamoja na ugawaji huu wa tanzu na vipera vya Fasihi Simulizi uliofanywa na Mulokozi kwa kuzingatia vigezo vyake alivyovitumia, bado ugawaji huu unaudhaifu mkubwa tu. Udhaifu au changamoto za vigezo alivyovitumia Mulokozi ni kama ifuatavyo:-

Vigezo vyote hivi vinaweza kuingiliana; mfano kigezo cha kidhima, kama vile kuonya au kuelimisha huweza kuonekana katika tanzu zaidi ya moja au hata katika vipera mbalimbali.

Pia kigezo cha namna ya uwasilishaji huweza kuingiliana kutoka utanzu mmoja hadi mwingine. Mfano, katika utanzu wa masimulizi na mazungumzo.

Vilevile kigezo cha wahusika; kigezo hiki huweza kuingiliana katika utanzu mmoja na mwingine. Mfano, unaweza kuwa na hadithi yenye wanyama, binadamu, mizimu na kadhalika. Hivyo inakuwa si jambo rahisi kuona tofauti zilizopo.

Kwa kuhitimisha, tunaweza kusema kwamba ni vigumu kuainisha tanzu na vipera vya Fasihi Simulizi kutokana na kwamba, Fasihi Simulizi hubadilika badilika kifani, kimaumbo na hata kimaudhui kwa kutegemea muktadha na namna ya uwasilishaji wake. Kwa mfano ngano iliyopo katika masimulizi ni tofauti na ngano iliyopo katika maghani. Hivyo basi tatizo hili linaweza kutatuliwa kwa kutumia istilahi tofauti katika vipera au tanzu zinazoingiliana.

MAREJEO:

Mulokozi, M. M. (1989). Tanzu za Fasihi Simulizi: Katika Mulika 21. TUKI. Dar es Salaam.

Mulokozi, M.M. (1996). Utangulizi wa Fasihi Simulizi ya Kiswahili. TUKI. Dar es Salaam.

Wamitila, K.W. (2003). Kamusi ya Fasihi, Istilahi na Nadharia. Focus Publications Ltd. Nairobi.

TUKI, (2004). Kamusi ya Kiswahili Sanifu. (Toleo la Pili). East Africa: Oxford University Press na Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili (TUKI).




UHAKIKI WA RIWAYA ZA KISWAHILI.

                                       UHAKIKI WA RIWAYA YA KUFIKIRIKA
                                                     MWANDISHI S. ROBERT

Riwaya ya kufikirika ni riwaya iliyotungwa na mwandishi mashughuli Shaabani Robert, katika riwaya hii mwandishi anaeleza juu ya mila na desturi zilizopitwa na wakati kuwa hazina nafasi katika kipindi cha sasa. Mwandishi anaeleza kuwa jamii ya watu wakufikirika ilikuwa inaamini juu ya uganga na mambo ya kijadi. Hivyo kupitia mhusika utu busara ambaye alikuwa anaelimu kubwa ya dunia. Utu Busara alijiingiza katika kundi la utabiri ili aweze kuleta mabadiliko katika nchi ya kufikirika. Kutokana na utabiri wake Mfalme na Malkia wanafanikiwa kupata mtoto na baadae Utu Busara tena anakuwa mwalimu wa mtoto wa mfalme na kuanza kumfundisha elimu ya dunia ambayo ni kinyume na matakwa ya mfalme, baada ya kufukuzwa na mfalme, Utu Busara anaamua kujiingiza katika kilimo ambapo ikapelekea kukamatwa kwa kudhaniwa kuwa ni mjinga. Kutokana na elimu na weledi alionao utu busara anafanikiwa kujiokoa kutoka gerezani na kufanikiwa kumponya mtoto wa mfalme kwa kutoa ushauri kuwa apelekwe hospitali. Mwisho mtoto wa mfalme anapona na kufanya utu busara kufanikiwa katika nia yake ya kuleta mabadiliko katika nchi ya kufikirika.

Katika kuhakiki na kuchambua riwaya hii ya Kufikirika tutazingatia vipengele vya fani na maudhui. Hivyo tutaanza kwa kuchambua vipengele vya maudhui ambavyo hujumuisha dhamira, ujumbe, migogoro, mtazamo, na falsafa na kisha tutatalii kwa kina juu ya fani na vipengele vyake..

Dhamira, Katika riwaya hii ya Kufikirika mwandishi shaaban Robert ameonesha dhamira kuu ni ukombozi wa kiutamaduni. Kiujumla riwaya ya kufikirika inajdili harakati zinazofanywa na Utu Busara za kupambana na tamaduni zilizopitwa na wakati. Kupitia mhusika Utu Busara mwandishi anaonesha kuwa mila na tamaduni zilizopitwa na wakati hazina budi kutupiliwa mbali hasa katika kipindi hiki cha sayansi na teknolojia.

Licha ya dhamira kuu, pia mwandishi amejadili dhamira ndogondogo kupitia wahusika lukuki ambao amewatumia katika riwaya hii, Dhamira hizo ni kama zifuatazo:

Suala la uongozi, Mwandishi Shaban Robert hakupuuzia suala la uongozi katika riwaya hii, anaonesha kuwa viongozi wa nchi ni lazima wawe mstari wa mbele katika kuhakikisha maslahi ya nchi yanalindwa na wananchi wanaishi kwa amani. Mwandishi anabainisha suala hili kwa kumtumia mhusika mfalme (uk 1-2)

“Nimejaliwa kupata ufalme kuliko wafalme wengine walio majirani zangu. Binafsi yangu nimepigana vita nyingi kulinda nchi isitekwe adui. Ushindi wa kila vita umenipa utukufu wa namna ya peke yake. Milki yangu pana imeenea kaskazini, kusini, mashariki na magharibi.”

Suala la ugumba na utasa,mwandishi shaban robert hakusita kulielezea suala la ugumba na utasa katika riwaya hii ambalo ndio lilipelekea kuibua dhamira mbalimbali. Mwandishi anamtumia mhusika mfalme na malkia katika kuonesha tatizo hili. Mwandishi anaonesha kuwa licha ya ujasili, uzalendo na furaha yote aliyokua nayo mfalme na malkia lakini walijiona sio kitu kutokana na kukosa mtoto, ambaye angekuja kurithi madaraka mara baada ya kufa kwa mfalme.(uk 3)

“................jina lake litachorwa kwa majohari, wa watu hawa na pia nashukuru kwa kuwa bwana juu ya vitu vya faraja visivyokwisha, lakini nina sikitiko kubwa kwa kukosa mtoto. Maskini mwenye mtoto namuona kuwa bora kuliko mimi.............”

Kutokana na tatizo hili mfalme akatafuta kila njia ili aweze kupata mtoto. Hapa ndipo mfalme alipoamua kuweka bayana tatizo lake hili aweze kuaidiwa.

Suala la imani potofu, mwandishi anaonesha juu ya dhana potofu zilizojengeka katika vichwa vya watu wa kufikilika juu ya mtu mwerevu na mjinga. Wanaona kuwa mjinga na mwelevu hujulikana kutokana na kazi anayoifanya mtu, utu busara alionekana kama mtu mjinga kutokana na shughuli ya kilimo aliyokuwa anaifanya halikadhalika mfanyabiashara alionekana mwelevu kutokana na kazi yake (uk 39)

”............mtu wa kwanza alikuwa na umbo kuza. Kazi yake ilikuwa ni biashara mjini. Ajali ya kukamatwa ilikua amekaa kitako dukani pake. Yeye alihesabiwa kuwa ni mwerevu. Mtu wa pili alikua na umbo la wastani. Amali yake ilikuwa ni ukulima. Ajali ya kufanywa mahabusi wa kafara ilimkuta shambani pake analima. Huyu alidhaniwa kuwa ni mjinga........”

Kutokana na mtazamo huu, hatimaye mwelevu aliweza kujinasua na kifo hicho, hivyo mwandishi shaban robert anajaribu kutoa mwanga kwa jamii juu ya dhana potofu na kuitaka jamii kubadilika ili kuendana na wakati.

Halikadhalika imani potofu imekisili katika jamii ya watu wa kufikirika kwani wanaamini juu ya mambo ya jadi hasa uganga na kupuuzia huduma za kisasa kama vile hospitali. Hivyo mwandishi shaban robert kupitia mhusika wake Utubusara anaitaka jamii kuachana na mila na tamaduni zilizopitwa na wakati kwani huweza kusababisha hasara kubwa kwa jamii husika kama ilivyowapata watu wa kufikirika ambao walipoteza vitu vingi kwa ajili ya uganga (Uk 8-14)

Nafasi ya mwanamke, mwandishi shaaban robert hakupuuza nafasi ya mwanamke katika riwaya yake. Katika riwaya hii mwandishi amemchora mwanamke kama mtu muhimu katika jamii mwenye kutoa ushauri na ukakubalika. Mfalme analithibitisha hili katika ( uk 1) anasema

“.........alikuwa tayari kupokea msaada uliotolewa kwa hiyari na mwanamke lakini kulazimisha kutendewa msaada hakupenda. Aliona kazi na faraju zitendwazo na wanawake katika maisha zilitosha kuwa mzigo mzito juu yao.....”

Hivyo mwandishi anaonesha jinsi mwanamke anavyofanya mambo makubwa katika jamii, hivyo anapaswa kuheshimiwa na kuthaminiwa.

Pia mwanamke amechorwa kama mtu mvumilivu, mwandishi Shaaban Robert amemuonesha mwanamke kama mtu mwenye kuvumilia matatizo mbalimbali yanayomkabili. Malkia licha ya kukumbwa na tatizo la kukosa mtoto hakuvunjika moyo aliendeleza upendo wake kwa mfalme mpaka pale mungu alipowajalia kupata mtoto.

Dhamira nyingine ni dharau na majivuno, dhamira hii imejitokeza pale ambapo mhusika Mfanyabiashara alipokuwa gerezani alikuwa anamdharau utu busara. Kutokana na kazi aliyokuwanayo mfanyabiashara alijiona kuwa ni bora kuliko mkulima( uk 40)

.............Huwaje, wewe mvaa koja la ushanga shingoni kama mwanamke kupata njia! Una sifa zaidi ya ujinga. Nashangaa kwanini hawakutakiwa wajinga wawili kwa kafara hii! Ujinga ni ila ya kustahili upanga wa chakali.

Umuhimu wa elimu ni dhamira nyingine ambayo mwandishi Shaaban Robert ameijadili katika kazi yake. Mwandishi anaonesha kuwa watu wa Kufikirika walikuwa hawana elimu ya dunia walijiegemeza zaidi katika mambo ya uganga, hivyo utu busara alijaribu kuleta mabadiliko katika nchi ya kufikirika kwa kuwapatia elimu ya dunia ambayo baadae ilisaidia kuikomboa nchi ya kufikirika.

Pia dhamira nyingine ni matumizi mabaya ya mali, kutokana na mfalme kukosa mtoto, waganga walitumia sehemu kubwa ya mali ya nchi ya kufikirika hadi ikapelekea matatizo katika nchi ya kufikirika( uk 14)

Nchi ambayo zamani ilikuwa ya shibe, utajili, nguo, tafrija na neema zote sasa ilikuwa imegeuka nchi ya njaa, umaskini, uchi, uzito na uhitaji wa kila namna ulikuwa mbele ya watu.........

Kipengele kingine ni ujumbe. katika riwaya ya kufikirika kupitia dhamira mbalimbali zimeweza kutuibulia ujumbe ufuatao.

· Umoja ni nguvu na utengano ni udhaifu. Mfano wananchi wa kufikirika walikuwa na umoja katika kufanikisha ustawi wa nchi yao hali kadhalika watu wa kufikirika walikuwa na umoja na ushirikiano katika kufanikisha mfalme wao anapata mtoto.

· Kwenye upendo, umoja na ushirikiano hakuna vurugu na matatizo mbalimbali.ustawi wa nchi ya Kufikirika umetokana na umoja na ushirikiano waliokuwa nao.

· Jamii isijiegemeze katika imani za kimila na kitamaduni tu bali iangalie upande mwingine. Hii inatokana na ukweli kwamba wanakufikirika walikuwa hawaamini masuala ya hospitali badala yake walikuwa wanaamini mambo ya kimila na kitamaduni.

· Ujinga na werevu wa mtu hupimwa kwa matendo na sio kazi anayoifanya. Hii inatokana na watu wa kufikirika ambayo walikuwa wanapima werevu na ujinga wa mtu kutokana na kazi zao.

· Ujumbe mwingine ni kwamba viongozi lazima wadumishe sheria za nchi ili kuleta usawa na amani katika nchi.

Hivyo Shaaban Robert anaitaka jamii ibadilike kwa kuzingatia maonyo na maadili yapatikanayo katika riwaya ya kufikirika.

Kipengele kingine ni migogoro, mgogoro ni mvutano kati ya pande mbili au zaidi.mwandishi Shaaban Robert katika riwaya hii ya kufikirika ameonyesha migogoro mbalimbali kama vile mgogoro wa kiuchumi,kijamii,kisiasa,utamaduni na mgogoro wa nafsi.

Tukianza na mgogoro wa kiuchumi, Mwandishi ameonyesha jinsi nchi ya kufikirika ilvyoyumba kiuchumi kutokana na mali zote za nchi zilivyotumika katika kumtibu mfalme na malkia na mwishowe shughuli za nchi zilisimama.uk (8-12).

Pia kuna mgogoro wa kijamii, mwandishi ameonyesha mgogoro wa mfalme na malkia kwa kukosa mtoto,kwakua walijiona hawana umuhimu katika jamii ingawa walikua na mali nyingi. Uk(1-6).

Pia mgogoro mwingine wa kijamii ni kati ya mfalme na waganga kwamba makundi matano ya waganga waliokusudiwa kumtibu mfalme na malkia walishindwa kuwatibu.uk(8-13).

Mgogoro mwingine wa kijamii ni kati ya mfalme na waliotakiwa kutolewa kafara,kwamba katika nchi ya kufikirika suala la mtu kutolewa kafara ni suala ambalo haliendani na sheria za nchi ya kufikirika.

Vilevile kuna mgogoro wa nafsi uliojitokeza kwa mfalme,jinsi mfalme alivyokua akiumia juu ya kukosa mtoto kwa muda mrefu takribani miaka kumi baada kuoana na malkia.

Pia malkia alikua na mgogoro na nafsi yake juu ya kukosa mtoto kwa muda mrefu tangu kuoana kwao.

Hali kadhalika kuna mgogoro kati ya waziri mkuu na wajumbe juu ya kubadili mfumo wa uongozi.

Pia kuna mgogoro kati ya ukale na usasa,kwamba wananchi wa kufikirika waliamini sana mambo ya kishirikina wakati Utubusara alikua akijaribu kuwaelimisha juu ya mambo ya sayansi na teknolojia na waachane na mambo ya zamani.

Pia kuna mgogoro wa kisiasa, mwandishi ameonyesha jinsi mfalme alivyokua ameegemea kuongoza nchi yake kupitia mila na desturi, lakini tunaona jinsi Utubusara alivyokua akijaribu kuishauri jamii ya kufikirika kuepukana na mila zilizopitwa na wakati na waegemee katika sayansi na teknolojia ili waweze kuleta mabadiliko.

Falsafa, kiujumla falsafa ni mchujo wa welekeo wa mawazo muhimu yajitokezayo kila mara katika kazi mbalimbali za msanii ( Senkoro 2011). Katika kazi hii shabaan Robert anaonekana kutawaliwa na falsafa kuwa mila na tamaduni zilizopitwa na wakati hazina nafasi katika nkipindi hiki cha sayansi na teknolojia.

Msimamo, msimamo ndio uwezao kuwatofautisha wasanii wawili wanaotunga kazi za fasihi zilizo na kiini na chimbuko moja ( senkoro 2011). Katika kazi hii mwandishi shaaban Robert anaonekana kuwa na msimamo wa kiyakinifu. Kwa mujibu wa mwandishi anaona katika kipindi cha sayansi na teknolojia mila na tamaduni za zamani zisipewe nafasi.

Mtazamo, mwandishi shaaban robert anaonekana kuwa na mtazamo wa kimapinduzi, mwandishi anaona kuwa ili jamii isiangalie mila na tamaduni tu bali iangalie mambo ya sayansi na teknolojia.

Baada ya kuchambua vipengele vya maudhui sasa tugeukie vipengele vya kifani.kiujumla fani katika fasihi ni ule ufundi wa kisanaa anaotumia msanii katika kazi yake(Senkoro 2011). Katika kuchambua vipengele vya fani tutajikita katika muundo, mtindo, wahusika, mandhari na matumizi ya lugha.

Wahusika, hawa ni watu, ama viumbe, waliokusudiwa wawakilishe dhana, mawazo au tabia za watu, katika kazi za fasihi. Katika riwaya ya kufikirika mwandishi Shaaban Robert amepambanisha wahusika mbalimbali katika kuibua au kusindikiza dhamira zake. Baadhi ya wahusika aliowatumia ni kama wafuatao

Mfalme, huyu alikuwa ndiye kiongozi au mfalme wa nchi ya kufikirika ambaye aliongoza vema na alikuwa mtu mwenye huruma na upendo na watu wake. Hali kadhalika mfalme alikuwa ni jasiri na mzalendo aliyepigania haki za raia wake na kuzilinda sheria za nchi ya kufikirika. Licha ya mali na furaha yote aliyonayo mfalme lakini kwa kipindi kirefu cha maisha yake mfalme amekuwa akisumbuliwa na tatizo la kukosa mtoto. Kupitia uhusika alioubeba mfalme ameibua dhamira mbalimbali kama vile suala la uongozi, ujasiri na uzalendo, umuhimu wa kuwajali wanawake na imani potofu.

Malkia, huyu alikuwa ni mke wa mfalme ambaye pia alikuwa anasumbuliwa na tatizo la utasa. Ni mwanamke mvumilivu na mwenye subira hivyo anafaa kuigwa na jamii. Mwandishi kwa kumtumia mhusika malkia ameibua dhana ya utasa na uvumilivu.

Utu busara ujinga hasara, ni mhusika aliyeibua dhamira nyingi katika riwaya hii ya kufikirika, alikuwa ni mtu makini na mwenye upeo mkubwa katika kufikiria mambo. Huyu ndiye aliyetabiri kuzaliwa kwa mtoto wa mfalme, baadae akawa mwalimu wa mtoto wa mfalme na baadae akajiingiza katika ukulima( uk 49). Hekima na uelewa aliokuwa nao ulikuwa ngao tosha iliyomsaidia kujikomboa kutoka katika vikwazo vyote alivyokumbana navyo, hakika ni mtu anayefaa kuigwa katika jamii.

Mwerevu, huyu alikuwa ni mfanyabiashara ambaye alionekana ni mwerevu kutokana na kazi yake. Ama hakika ni mtu aliyajaa dharau na majivuno( uk 40) anasema,

.............Huwaje, wewe mvaa koja la ushanga shingoni kama mwanamke kupata njia! Una sifa zaidi ya ujinga. Nashangaa kwanini hawakutakiwa wajinga wawili kwa kafara hii! Ujinga ni ila ya kustahili upanga wa chakali.

Kwa hakika utu busara alileta mwanga katika nchi ya kufikirika juu ya imani na tamaduni zilizopitwa na wakati.

Waziri mkuu, huyu uwakilisha viongozi wanaopindisha sheria kwa manufaa ya watu wachache. Mwandishi anamchora mhusika huyu kama mtu ambaye aliyetumia vitisho na nguvu katika kushawishi wajumbe kukubaliana na ubadilishaji wa sheria. Hakika hafai kuigwa na jamii hasa katika kipindi hiki cha mabadiliko.

Muundo, Katika kazi ya fasihi muundo ni mpango na mtiririko wa kazi hiyo kwa upande wa visa na matukio( Senkoro 2011). Hivyo katika riwaya hii ya Kufikirika mwandishi Shaaban Robert ametumia muundo wa moja kwa moja ambapo amesimulia kitabu mwanzo hadi mwisho. Katika kuipamba kazi yake mwandishi Shaaban Robert ameigawa riwaya yake katika sehemu ndogondogo , Kila sura ina kichwa cha habari. Sura hizo ni kama vile Mfalme, Waganga, Matokeo ya utabiri, Mtoto wa mfalme na Kafara. Pia sura ya tano ameigawa katika sehemu kuu mbili na kuipa jina la Baraza na Gereza.

Mtindo, katika kazi ya fasihi ni ile nama mbayo msanii hutunga kazi hiyo na huipa sura ambayo kifani na kimaudhui huainisha kanuni au kawaida zilizofuatwa kama ni zilizopo( za kimapokeo) au ni za kipekee( senkoro 2011). Mwandishi shaaban Robert katika kazi yake hii ametumia mtindo wa masimulizi yaani amesimulia matukio yote katika mtiririko unaofaa.pia nafsi zote zimetumika, hali kadhalika katika kuipamba kazi yake mwandishi ametumia ushairi ( uk 18-19) anasema.
Jina lipewe wana
Kulikariri kwa moyo
Waelezewe maana
Wakuze wayatendayo
Kama milivyoona
Matendo ya mtu huyo
Katenda bora sana
Kwa tuzo apewayo

Pia katika riwaya hii, mwandishi ametumia mtindo wa kutoa maana ya meneno magumu mwishoni ili kufanya kazi yake ieleweke kwa urahisi.

Mandhari. Mandhari ni mahali au sehemu ambayo kazi ya fasihi inatendeka. Katika riwaya ya kufikirika mwandishi shabani robert ametumia mandhari ya Kufikirika, kwani hata nchi inayozungumziwa ni ya Kufikirika, pia nchi zilizopakana na nchi ya Kufikirika nazo ni za kufikirika. Pia mwandishi ametumia muktadha halisi kama vile Gerezani, Nyumbani kwa Mfalme, Bustanini ( uk 1) na Shambani. Kupitia mandhari hizi mwandishi Shabani Robert ameibua dhamira mbalimbali ambazo tumejadili hapo awali.

Matumizi ya lugha, hujumuisha jinsi mtunzi alivyotumia lugha katika kuwasilisha kazi yake. Matumizi ya lugha hujumuisha misemo, nahau, methali na tamathali za semi.

Methali, methali zilizotumika katika riwaya hii ni kama vile, nyumba ya mgumba haina matanga (uk 5),mwenye haya hazai (uk 6),

Misemo, katika riwaya ya kufikirika misemo iliyotumika ni kama ifuatayo. Dunia haifichi siri (uk 23), maisha ni kama kuwa katika bahari ( uk 24).

Tamathali za semi, haya ni maneno ambayo hutumiwa na wasanii wa fasihi ili kutia nguvu katika maana, mtindo na hata sauti katika maandishi au kusema. Pia tamathali za semi hutumika ili kupamba lugha au mazungumzo. Katika riwaya ya kufikirika mwandishi Shaaban Robert ametumia tamathali mbalimbali kama ifuatavyo:

Tashibiha, katika tamathali hii watu ama vitu viwili au zaidi hulinganishwa na watu ama vitu vingine kwa kutumia maneno kama mithili, kama, n.k, katika riwaya hii tahibiha zilizojitokeza ni kama vile kichwa chake kilishindiliwa kama gunia (uk 29),sauti ya waafrika ni kali kama ile ya radi ( uk 6)waliweza kunusa kama mbwa mwitu( uk 8), akili yake kali kama wembe ( uk 38), maswali aliyamimina kama maji ( uk 29), mtu mdogo kama mbilikimo (uk 41)

Tashihisi, katika aina hii vitu visivyo na sifa walizonazo watu hupewa sifa hizo. Katika riwaya hii mwandishi Shaaban Robert anabainisha tashihisi zifuatazo,sauti ya ndege waliokuwa wakiimba matawini kwa kuagana na mchana ilikuwa na simanzi masikioni (uk 1)

Sitiari, hii ni tamathali ambayo hulinganisha vitu bila kutumia viunganishi, mwandishi wa riwaya hii ametumia sitiari zifuatazo, mjinga ni mnyama ( uk 41), wanawake ni malaika( uk 40).

Mubalagha, ni tamathali ya semi ambayo hutia chumvi au hukuza jambo. Katika riwaya ya Kufikirika mwandishi ametumia mbinu hii katika( uk 11) siku hiyo kuni, mkaa, na mafuta yote yalikwisha kwa kuchoma hirizi hizo, moshi mwingi uliruka juu ukatanda katika hewa kama wingu kubwa la mvua.

Jinala kitabu, Jina lakitabu kufikirika linasadifu yaliyomo .Kwanza nchi yenyewe ya kufikirika ni nchi ambayo haipo,mwandishi anaonyesha kwamba hata mfalme mwenyewe haijui mipaka ya nchi yake.Hata nchi zinazopakana nazo ni nchi za kufikirika tu.Nchi kama Anasa,Majaribu,Bahari ya kufaulu na safu ya milima ya Jitihada vyote ni vya kufikirika tu.

Kwa upande wa maudhui, mambo ya kafara ni ya kufikirika tu,kwani mambo hayo katika jamii zetu hayapo.Matibabu mengi siku hizi hufanywa hospitalini,ambako kuna wataalamu waliosomea taaluma hii ya uganga na sio miti shamba kama wananchi wa kufikirika.

Kwa kuhitimisha tunaweza kusema kuwa mwandishi shaaban robert kwa kiasi kikubwa ameonesha matatizo mbalimbali yanayoikumba jamii na kuyatolewa ufumbuzi.

Marejeo

Robert, S (1991) Kufikirika.Dar es salaam. Mkuki na nyota publishers.

Senkoro, F.E.M.K (2011) Fasihi. Dar es salaam. KAUTTU.

UHAKIKI WA RIWAYA YA KUSADIKIKA

UTANGULIZI

Katika kujadili vipengele mbalimbali vya Fani na maudhui vilivyotumiwa katika riwaya ya kusadikika iliyoandika na Shaaban Robert Washiriki hatukujikita zaidi katika kujadili maana ya riwaya za wataalamu mbalimbali bali tuliweza kujadili kazi hii kwa kuchambua vipengele vya fani na maudhui kutokana na masimulizi ya nchi ya Kusadikika.

Masimulizi ya kitabu kwa kifupi.

Riwaya ya kusadikika ni kitabu kinachoelezea masimulizi ya nchi ya kusadikika ambayo mwandishi ameanza kwa kusimulia tukio la kushitakiwa kwa Karama ambaye ndiye Mhusika mkuu kwa tuhuma za kuihujumu serikali ya Kusadikika. Kwa maelezo ya Waziri Majivuno aliwasilisha mashitaka haya mbele ya Mahakama eti kwa sababu Karama alikuwa akitoa elimu ya sheria ambayo kwa Mtazamo wa Waziri huyu alidai kuwa angewafanya raia wa kusadikika kuelewa haki zao ambako kungepelekea wananchi hao kutotii serikali au kwa namna nyingine kungekomesha unyanyasasaji, uonevu na uongozi mbaya wa watawala wa kusadikika na hivyo waziri Majivuno alijawa hofu kubwa sana.

Riwaya imeendelea kusimulia namna mshitakiwa Karama alivyowasilisha utetezi wake mbele ya Mahakama ya Kusadikika iliyoundwa na Mfalme na Madiwani. Karama aliwasilisha utetezi huo kwa kuthibitisha jinsi serikali ilivyoshindwa kuthamini michango mbalimbali ya wananchi wake kwa kuelezea historia wajumbe mbalimbali waliojitoa kwenda kufanya utafiti wa namna ya kuendeleleza nchi yao. Masimulizi yake yaliwataja hasa wajumbe 6 waliotumwa mipakani au pande zote 6 ambazo nchi ya kusadikika inapakana nayo. Pande hizo ni Kaskazini, Mashariki, Kusini, Magharibi, Mbinguni na Ardhini. Hatima ya wajumbe hawa ambao walikuwa wazalendo waliishia Kifungoni pindi waliporejea kutoka walikotumwa.

Mwisho wa riwaya hii mwandishi anaelezea hukumu ya Karama ambapo Mahakama iliyoongozwa na Mfalme ilivyomtoa hatia mtuhumiwa kwa kauli moja ya kuwa hana hatia na Mfalme kuagiza wajumbe wote waliokuwa wanatumikia kifungo kufunguliwa na kulipwa fidia kwa kunyanyaswa pamoja na jitihada zao.

Baada ya muhtasari wa masimulizi ya nchi ya kusadikika tuliweza kujadili vipengele vinavyounda Fani na Maudhui ya kazi ya riwaya ya kusadikika kama ifuatavyo;-

Fani ni ujuzi au Mbinu mbalimbali azitumiazo msanii kuwasilisha ujumbe au Fikra zake kwa hadhira aliyoikusudia. Fani inaundwa na vipengele vya Mandhari, Wahusika, muundo, Mtindo na Matumizi ya lugha.

Maudhui ni jumla ya mawazo yanayowasilishwa na msanii wa kazi ya kifasihi katika kazi yake. Maudhui huundwa na vipengele vya Dhamira, Ujumbe, Falsafa, Migogoro, Mtazamo na Msimamo.

Uchambuzi wa Vipengele mbalimbali alivyovitumia mwandishi wa riwaya hii ya Kusadikika ni:

Mandhari: ambayo humaanisha mahali au sehemu ambayo tukio linafananyika. Mwandishi ametumia mandhari ya Kufikirika ambayo haiwezi kujidhihirisha kwa macho ya kawaida (haionekani) kwani ni nchi inayoelea angani. Pia ametumia mji wa sadiki na mipaka au pande sita zinazopakana na nchi hii za Kaskazini, Mashariki, Kusini, Magharibi, Ardhini na Mbinguni.

Wahusika ni mtu au watu, wanyama, na mimea anaotumia mwandishi katika kuwasilisha kazi yake kwa hadhira iliyokusudiwa. Kwa kiasi kikubwa Mwandishi ametumia Wahusika ambao aliowapa majina yanayosawiri tabia zao na wahusika ambao hawabadiliki badiliki ;-

Karama, Huyu ni mhusika mkuu ambaye pia alikuwa Jasiri na Shujaa, Mwanasheria, Mzalendo mtetezi wa haki na Mshitakiwa. Vilevile mhusika huyu alichorwa mwema kuanzia mwanzo hadi mwisho.

Majivuno, Waziri wa kusadikika, mwenye uchu wa madaraka, mwenye haiba, asiye na uzalendo, kiongozi anayelindwa na Mfalme na asiye na shukurani.

Mfalme, Kiongozi wa kusadikika, Katili, Mjinga, mwenye tama ya uongozi, mkuu wa baraza la Mahakama.

Madiwani, Wasaliti, wakuu wa mahakama, waonevu, wakatili, wenye dhuluma na sio wazalendo.

Mudir wa sheria, mwanasheria wa serikali, Mjinga, msaliti na asiye mzalendo.

Buruhani, Mjumbe wa kaskazini, Jasiri, Mzalendo mpenda haki, Mwanaharakati, Mfungwa na maskini. Msanii anasema “Hii ilikuwa safari ya ujasiri iliyotaka uthabiti na matumaini, mwenye heshima, hodari na mwaminifu alitakiwa ajitolee mwenyewe kwa safari hii” uk.12.

Fadhili, Mjumbe aliyetumwa mashariki, Jasiri, Mzalendo, mpenda haki, Mfungwa na maskini. “Mtu mwenye sifa njema alitakiwa kujitolea mwenyewe kwa ujumbe wa mashariki na mtu kama huyu alipatikana upesi sana kuliko ilivyokuwa ikitazamiwa” uk.16.

Kabuli, Mjumbe wa kusini, jasiri, Mzalendo, Mpenda haki, Maskini na mfungwa.

Auni, Mjumbe wa Magharibi, Jasiri, Mzalendo, Mpenda haki, Mwananchi wa kawaida na mfungwa.

Sapa na Salihi, walikuwa vipofu, wananchi wa magharibi, Sapa alikuwa mwenye tama na wivu, Sapa alikuwa mpole, Sapa aliomba upofu.

Radhaa, mjumbe wa mbinguni, Jasiri, mzalendo, mpenda haki, Mfungwa na Maskini.

Amini, mjumbe wa ardhini, Jasiri, mpenda haki, mzalendo na mfungwa.

Wahusika wengine ni wananchi, bwana Taadabuni, katibu wa serikali, bwana Komeni, Amiri jeshi, bwana fujo, mlinda hazina, bwana Baromini na wananchi wa pande zingine.

Muundo, ni namna au jinsi mwandishi anavyopangilia visa na matukio katika kazi yake ya kifasihi. Mwandishi ametumia muundo wa moja kwa moja ambapo katika mpangilio wa masimulizi ameanza mwanzo wa kisa kwa kuonesha jinsi mashitaka yalivyowasilishwa, kukafuatiwa na utetezi wa mshitakiwa au kile mwandishi alichokiita maombezi mbele ya Mfalme na Madiwani kwa kusimulia historia ya kusadikika kupitia wajumbe sita waliotumwa pande sita na kuishia kifungoni kama sehemu ya pili ya kisa na hatimaye alimalizia kwa kuelezea hukumu ya kesi ya Karama ambapo Mfalme na Madiwani walionesha kuwa mtuhuma hakuwa na hatia na kufunguliwa kwa wajumbe sita na kuachiwa huru huku Mfalme akiamuru walipwe fidia.

Mtindo. Ni namna mwandishi anavyoiumba kazi yake ya kifasihi. Mwandishi Shaaban Robert ametumia mitindo mbalimbali katika kazi hii ya riwaya ya kusadikika kama vile, ametumia maswali hasa katika sehemu ya mwisho ya kitabu, ametumia dayalojia kati ya Sapa na Salihi uk. 29, ametumia masimulizi kwa kiasi kikubwa katika kazi hii ambayo kwake ndio mbinu kuu pamoja na matumizi ya nafsi ya pili na tatu umoja na nafsi ya tatu wingi sehemu kubwa ya riwaya.

Lugha. Mwandishi ametumia lugha ngumu ambayo si rahisi kueleweka kwa msomaji kutokana na kutumia misamiati isiyoeleweka. Hali hii ya kutumia lugha ngumu ililengwa kukwepa makucha ya wakoloni. Mfano wa misamiati hiyo ni sudusi, takirifu, kafaungo, hutasawari, akapatilizwa, ali, kujikagajuu, Kuyabisika, kujikaga, Kadura n.k. Pia mwandishi ametumia vipengele vya Tamathali za semi ambazo ni ;-

Methali. Kitanda usichokilalia hujui Kunguni wake.

Msiba wa kujitakia hauna kilio. Lila na fila hawatangamani.

Misemo.

Kumtosa mshitakiwa katika bahari ya maangamizi.

Tashibiha.

Umri wake mkubwa ulizofanya nywele zake za kichwani kuwa nyeupe kama fedha.

Uso wa kipofu wa kwanza ulikuwa na furaha kama bwana harusi.

Alikuwa na tabia ya kuficha siri kama kaburi lifunikalo maiti.

Anamaneno kama kitabu

Tashihisi.

Giza limezalo nuru na ufupisho uoni wa macho.

Wakati una mabawa kama ndege uk. 11.

Jina la Kitabu (KUSADIKIKA). Jina la kitabu linasawiri yaliyomo katika riwaya hii kwani limetokana na neno “sadiki” likimaanisha “Amini” hivyo linaweza kusemwa kuwa ni kuaminika. Mwandishi anatuonesha kuwa Wasadikika ni wajinga kwani hawakujihusisha na uchambuzi wa masuala yake waliishia kuamini na kukubali kila jambo mwandishi anasema “Imani ya Kusadikika ni nguzo imara ya majengo ya utawala wa Wasadikika” wakati mataifa mengine yalipojifananisha kwa mambo kama vile enzi, uwezo na fahari nyingine taifa la kusadikika lilijivuna kwa sababu ya kusadiki mambo yaliyotoka vinywani mwa watu wake” uk. 4-5.

Kwa washiriki wa uchambuzi huu wanakiri kuwa kwa kiasi kikubwa tumefanikiwa kuchambua haya katika vipengele vya fani na maudhui alivyotumia msanii Shaabani Robert katika riwaya ya Kusadikika ingawa si vyote vilivyotumika katika vipengele hivi tumeweza kuviainisha. (rejea masimulizi ya kitabu)
KIPENGELE CHA MAUDHUI.

Maudhui ni jumla ya mawazo aliyonayo msanii katika kazi yake ya kifasihi, Kipengele cha maudhui kinaundwa na ujumla, dhamira, migogoro, falsafa, Msimamo/Mtazamo.
Dhamira mbalimbali

Dhamira kuu ni Ukombozi: Dhamira hii ndio kuu katika riwaya ya kusadikika iliojikita kwenye ukombozi wa kifikra na ukombozi wa kisiasa. Mwandishi amemtumia mhusika karama aliyeanzisha elimu ya sheria yenye lengo la kuwezesha wananchi ili wawezekushiriki katika mambo mbalimbali ya nchi.

Ukombozi wa kisiasa unarejelea harakati zilizoongozwa na Karama na wajumbe sita zenye lengo la kuleta mabadiliko katika nchi ya kusadikika kuhusu haki na uongozi (viongozi). Msanii anasema “Kwa nini wanasiasa wa kusadikika hawakuwaacha kama Karama kujishughulisha na mambo yaliyowapita vimo vyao”

Matabaka. Hali ya wahusika kuwa na hadhi au makundi au madaraja tofauti tofauti. Katika riwaya ya kusadikika ameonesha matabaka ya namna mbalimbali kama;-

Tabaka la viongozi na wananchi, matajiri na wasomi na wasio wasomi na wenye haki na wasio na haki. Katika kudhihirisha matabaka haya mwandishi ameeleza kwa mifano baadhi ya maeneo haya anasema “Sheria za wasadikika zilikuwa hazimuamuru mshitakiwa kujitetea juu ya ushahidi wa mshitaki. Aghalabu mashitaka mengi yalikubaliwa bila ya swali wala kiapo kama mashitaka yaliletwa mbele ya baraza na wafalme, watoto wao, matajiri au watu wengine maarufu nguvu ya desturi hii ilifanywa maradufu. Hapana shaka salama ya watu wadogo ilikuwa kidogo sana katika nchi ya kusadikika” uk.7.


Uongozi Mbaya. Mwandishi amedhihirisha hili kwa kuwatumia wahusika waziri Majivuno, Wafalme, Madiwani na matajiri ambao ndio waliochorwa kwa taswira ya kuwa Wanahaki zaidi kuliko wananchi wa kawaida. Tunapozungumzia uongozi mbaya ni hali ya utawala kutowajali kwa kuwasaidia wananchi wa kawaida kisiasa, uchumi, na kijamii.

“Aghalabu Mashitaka mengi yalikubaliwa bila ya swali wala kiapo kama mashitaka yaliletwa mbele ya baraza na wafalme, watoto wao, matajiri au watu wengine maarufu nguvu ya desturi hii ilifanywa maradufu” uk.7.

Uzalendo na ujasiri. Uzalendo ni hali ya mtu kuipenda nchi yake na kujitoa kuipigania katika mambo mbalimbali yanayokwamisha maendeleo. Mwandishi anasema “pigano la kufa na kupona lilikuwa mbele yake” uk.8. “alikuwa hana silaha nyingine za kuokolea maisha ila zana hizi” uk.9. “Msema kweli hukimbiwa na marafiki zake, siwezi kuikana kweli kwa kuchelea upweke wa Kitambo nikajinyima ushirika wa milele unaotazamiwa kutokea baada ya kushindwa kwa uongo”uk.9.

Mwandishi amewatumia wahusika Karama, Buruhani, Fadhili, Kabuli, Auni, Radhaa, Amini kuonesha ujasiri na uzalendo walijitoa na kufanyakazi katika masahibu mengi tena bila ya kukata tama huku baadhi wakiishia kifungoni. Hatimaye waliweza kushinda. Mwandishi anasema “kwa kazi zake bora na uaminifu mwingi hakushukuriwa bali kuvunjiwa kadiri, aliaibishwa kuwa alileta uzushi ulikuwa hauna faida katika nchi zaidi ya hayo alitumbukizwa katika kifungo cha maisha”

Ujinga. Hali ya watu kutoelewa mambo mbalimbali ya msingi kijamii kisiasa, kiutamaduni na kiuchumi. Mfano haki sheria na uongozi nakadhalika. Shaaban Robert amethibitisha uwepo wa ujinga katika nchi ya kusadikika kupitia viongozi na wananchi waliosadiki mambo yao na kuyakana ya nje. Pia mwandishi amewatumia wananchi waliohudhuria mahakamani siku ya kwanza ya mashitaka. Msanii anasema “Baadhi ya watu wachache waliokuja barazani kusikiliza kesi hii walimsikitikia mshitakiwa wengi walikuwa wakinong’onezana kuwa msiba wa kujitakia hauna kilio” uk 7. “ujinga wao haukuyazuia maendeleo tu lakini hasa ulirudisha nchi nyuma vilevile” uk. 14. “Twaona kuwa mshitakiwa hana hatia ila alikuwa akitafuta jinsi ya kuisaidia sheria ya kusadikika kwa njia ngeni” Maelezo haya ni matokeo ya ufumbuzi wa ujinga uliokuwa umekithiri kwa viongozi wa kusadikika na wananchi wake.

Uonevu na Ukandamizaji (kukosekana kwa haki). Hali ya kutothaminiwa, kupewa haki na kuhukumiwa bila ya kufanya kosa lolote, na wakati mwingine kutopewa nafasi ya umuhimu katika tabaka fulani la watu “sheria za kusadikika zilikuwa hazimuamuru mtu yeyote kujitetea juu ya ushahidi wa mshitaki” uk.7. Buruhani, Fadhili, Kabuli, Auni, Radhaa, Amini walifungwa tena kwa kunyanyaswa Mwandishi anasema “Natoa amri watu sita waliotajwa wafunguliwe mara moja, inasikitisha sana kwa dhuluma juu ya watu hawa hazikutengenezwa mpaka leo. Gereza ni makao ya wahalifu na watu hawa si wahalifu” Mhusika mkuu karama pia alishitakiwa na Waziri majivuno kwa hulka tu za ukandamizaji.

Umaskini. Ni hali ya kutomudu kujipatia mahitaji mbalimbali ya kila siku kwa kiwango kinachoridhisha (cha kutosha) Mwandishi anasema “kwa kukosekana kwa Madaraja mito inafanya shida juu ya watu walio ng’ambo moja kukutana na Ng’ambo nyingine, maradhi hayajapata uuguzaji, vifo vya mapema hapa katika mwaka mmoja jumla yake yatisha kuliko ile ya vifo vitokeavyo katika nchi nyingine katika karne moja” Uk. 25. Pia “Aghalabu Mashitaka mengi yalikubaliwa bila ya swali wala kiapo kama mashitaka yaliletwa mbele ya baraza na wafalme, watoto wao, matajiri au watu wengine maarufu nguvu ya desturi hii ilifanywa maradufu. Hapana shaka salama ya watu wadogo ilikuwa kidogo sana katika nchi ya kusadikika” uk. 7. Maelezo haya yanaonesha uwezekano mkubwa wa uwepo wa kundi kubwa la watu masikini ambao ndio walioguswa na sheria za kusadikika.

Dhamira nyingine ndogondogo zilizomo katika riwaya hii ni tamaa iliyooneshwa kupitia Salihi na Majivuno, Unafiki na woga wa wananchi wa kusadikika, utengano na kukosekana kwa umoja.

Migogoro. Hali ya kutoelewa au kuridhishwa na jambo fulani na kupelekea kutoelewana kwa makundi au pande mbili za watu. Katika riwaya hii kuna migogoro ya kijamii, kisiasa na kiuchumi.

Migogoro ya kijamii. Mfano wa migogoro ya kijamii ni mgogoro wa Sapa na Salihi uliotokea baada ya Sapa kuomba upofu kutokana na tama ya Salihi kutamani vitu vya Sapa, Mwandishi anasema “kwa sababu hii tuliafikiana kushirikiana kila kitu atakachoomba tukaandikiana hati mbele ya Kadhi. Palepale mwenzangu aliinua mikono yake juu akaomba upofu” uk.30

Mgogoro nafsia: ni hali ya mtu kuhofia jambo fulani na kupelekea mtu huyo kuwa namsongo wa mawazo, Mwandishi amemtumia waziri Majivuno aliyekuwa na hofu ya kupoteza madaraka na kukomeshwa kwa ukandamizaji endapo wananchi wataelewa sheria mbalimbali za kusadikika waliokuwa wakielimishwa na Karama. Hatimaye aliamua kumshitaki katika baraza msanii anasema “Upelelezi huo ulidhihirisha bila ya shaka yoyote kuwa mshitkiwa akiwafunza watu sio kuomba msamaha na huruma katika baraza tu lakini hata kuzibatilisha hukumu za baraza la kusadikika kwa njia zote hii inaonesha kuwa mgogoro mkubwa utakuwako kati ya sheria za nchi na watu wake” uk 2.

Migogoro ya Kiuchumi. Mgogoro wa walionacho/matajiri ambao ndio waliopewa haki na upendeleo na Maskini walionyimwa haki hata mbele ya sheria na mahakaka.Katika nchi ya kusadikika watu hawa hawakuweza kabisa kushirikiana.Mwandishi anasema “Aghalabu Mashitaka mengi yalikubaliwa bila ya swali wala kiapo kama mashitaka yaliletwa mbele ya baraza na wafalme, watoto wao, matajiri au watu wengine maarufu nguvu ya desturi hii ilifanywa maradufu. Hapana shaka salama ya watu wadogo ilikuwa kidogo sana katika nchi ya kusadikika” uk. 7.

Migogoro wa Kisiasa. Huu ni mgogoro unaowahusisha wanaharakati wazalendo walioongozwa na karama dhibi ya serikali na viongozi wan chi ya kusadikika. Wanaharakati hao walihitaji mabadiliko na walichoshwa na uonevu wa viongozi wao, mgogoro huu ndio uliopelekea wananchi kuishia kifungoni pindi walipojitolea kudai mabadiliko.

Ujumbe. Uongozi mbaya unachangia kwa kiasi kikubwa kukwamisha maendeleo ya wananchi. Kuwepo kwa hali ya uzalendo katika nchi ni chachu ya maendeleo na mafanikio katika jamii. Suala la uelimishaji (elimu) ni muhimu katika utambuzi wa wananchi katika shughuli mbalimbali za kijamii.Tamaa na viongozi kujali maslahi kunapelekea hali duni ya wananchi walio wengi. Viongozi wanapaswa kuthamini haki za wananchi wanaowatumikia.

Msimamo wa Mwandishi. Msimamo wa mwandishi katika riwaya hii ni wa kimapinduzi kwani anaonesha jinsi jamii ilivyopaswa kujituma tena kwa ujasiri, kupigania haki na mabadiliko ya wananchi wote.

Mtazamo wa Mwandishi. Mtazamo wa mwandishi wa riwaya hii ni wa Kiyakinifu kwani kwa kiasi kikubwa umeakisi mambo ambayo yanaweza kufuatwa katika kufanikisha maendeleo ya jamiii yeyote kama vile mgongano wa mawazo uzalendo na ujasiri, uelewa na mambo mengine. Aidha yapo baadhi ya maeneo yanagusia mtazamo wa kidhanifu kama vile kusadiki kila kinachosemwa na watawala.

Falsafa ya mwandishi. Falsafa ya mwandishi ni ya wema hushinda ubaya, amedhihirisha hili kupitia mhusika Karama aliyechorwa kama mtu mwema dhidi ya Majivuno aliyechorwa kama mtu mbaya. Kwa taswira hii Karama amewakilisha wema wote katika jamii ya wasadikika na Majivuno anawakilisha wabaya wote katika jamii hiyohiyo.






UCHAMBUA WA KITABU CHA MAISHA YANGU NA BAADA YA MIAKA HAMSINI-MWANDISHI: SHAABAN ROBERT

UTANGULIZI

Kitabu cha Maisha Yangu na Baada ya Miaka Hamsini ni riwaya iliyoandikwa na Shaaban Robert (1936-1946) yenye insha na mashairi yanayoelezea mambo aliyoyafanya kuanzia umri wa ujana mpaka uzee wake, pamoja na mafanikio mbalimbali aliyoyafikia, changamoto alizokumbana nazo na namna alivyozitatua.

DHAMIRI YA MTUNZI

Kwa mujibu ya kamusi ya Karne ya 21(2011) inafafanua kwamba, dhamiri ni ile azma, kusudio au nia ya kufanya jambo. Katika muktadha wa kifasihi tunaweza kusema dhamiri ni lile lengo au kusudi la mtunzi katika kuitunga kazi yake. Na hii inatuthihirishia kwamba, kila mtunzi husukumwa na jambo fulani (ama zito ama jepesi) katika utunzi wake. Hakuna mtunzi anayetunga kazi yake katika ombwe. Mwandishi yoyote yule hata kama anaandika tungo za kubuni, kwa kawaida huwa amesukumwa na jambo au mambo fulani aliyowahi kusikia, kushuhudia katika fikra zake au katika hali halisi maishani; na fikra hizo hujengwa na mambo fulani ya tajiriba halisi katika maisha halisi.

Hivyo Shaaban Robert katika kitabu chake cha “Maisha Yangu na Baada ya Miaka Hamsini” suala la msingi lililomsukuma mpaka kuandika kitabu hiki ni kutaka kuweka kumbukumbu nzuri juu ya maisha yake kwa yale yote ambayo aliyafanya akiwa kama mwandishi maarufu wa Afrika Mashariki na Kati, hususani kwa vizazi vijavyo ambavyo havikupata bahati ya kumwona mwandishi huyu, kwa hiyo kwa kupitia kazi yake hii waweze kujifunza mengi na kupata mafanikio katika maisha.

NADHARIA YA UHALISIA

Kwa mujibu wa Ntarangwi (2004) anasema nadharia hii katika upana wake, humaanisha uwakilishi wa uhalisi wa mambo katika fasihi. Nadharia hii ilizuka katika karne ya kumi na tisa hususani kwa lengo la kupinga mkondo wa ulimbwende. Mhalisia huamini katika matokeo ya mambo na ukweli anaouzingatia ni ule unaoweza kuonekana na kuthibitishwa kwa tajirba. Vile vile, wanauhalisia huiamini demokrasia kama hali ya maisha, na malighafi ya kuelezea maisha ya kawaida, ya kadiri na ya kila siku. Hivyo basi uhalisia hujikita katika mambo yaliyopo, tukio mahsusi na matokeo yanayoweza kuthibitika.

Imani ya mhalisia ni kwamba kazi ya fasihi yapaswa kuwaweka wanajamii husika katika ulimwengu wao wa kawaida, wa kweli, na halisi. Hivyo basi hata picha za ulimwengu atakazoumba msanii, zapaswa kudhihirisha hali hiyo.

Mhakiki anayezingatia nadharia hii ya uhalisia, hupembua namna mtunzi alivyodhihirisha uhalisi wa mambo kupitia maudhui aliyoyazingatia na wahusika aliowasawiri. Hivyo basi, mhakiki hutizama jinsi ukweli ulivyodhihirishwa katika juhudi za mtunzi za kuchora hali halisi ya mambo katika wakati maalum. Kwa muhtasari basi msanii anatarajiwa kusawiri wahusika, matukio na mandhari yanayokubalika na kuaminika katika jamii ya wakati wake. Ufahamu wa mazingira na maisha anayoyalenga mtunzi ni nguzo muhimu kwa mhakiki wa kihalisia. Shida inayoletwa na nadharia hii ni kuchukulia kwamba uhalisi na maana yake hauna utata wowote katika jamii yoyote, ni kwamba unachukulia kuwa watu wote katika jamii hiyo wanaona uhalisi mmoja na kuwa na fasili sawa kuhusu maisha yao.

Haki na uaminifu; Shaaban Robert anaona kuwa uaminifu na kutenda haki ni nuru ya maisha bora kwa mwanadamu hapo baadaye. Dhamira hii inajidhihirisha katika insha yake ya Umri uk.2 anasema, “Milango ya nyuma ya kuifikia bahati ilikuwa mingi lakini haikunishawishi hata kidogo”. Suala hili linahusisha hata katika jamii zetu za leo, kwani watu wengi hutumia milango ya nyuma katika kufikia mafanikio. Kwa mfano; kwa kutoa rushwa, ufisadi nk.

Dhuluma na uonevu; Shaaban Robert anaeleza kuwa dhuluma na uonevu vimekuwa ni vipingamizi vikubwa katika mafanikio ya mtu ya kila siku, kwa mfano kama vile kunyimwa jambo fulani au kukandamizwa kwa sababu fulani ni ukuta katika maendeleo binafsi na ya jamii kwa ujumla. Jambo hili linajibainisha katika uk.1 “Mara kwa mara niliposimama wima kuiendea niliteleza nikaanguka chini. Nilipotaka kunyoosha mkono kuishika yalitokea mazuio ambayo sikuyatazamia au nilifungiwa milango ya mbele nisionane nayo”.

Vilevile katika insha ya Mwandishi S. Robert ameonesha ni kwa namna gani alivyodhulumiwa katika uchapaji wa kazi zake. Kwa mfano, uk.78 anasema; “Kwa kazi yangu iliyoweza kuleta sh.25000/- kwa vitabu 5000/- katika mwaka 1954 sikupewa hata pesa moja ya shaba kwa muda wa miaka kadhaa…sikupata kitu kwa kazi yangu iliyoleta karibu sh.15000/- kwa vitabu 5000/- katika mwaka 1958”. Pia anaonesha ni kwa namna gani alivyozidi kudhulumiwa na hata wale ambao walichukua madaraka baadaye. Mfano; uk.79 “Nilikuwa mtumishi wa bure na mtu wa chini kuliko pembe nyeusi yoyote iliyopata kuwako katika ulimwengu huu. Kwa nani? Kwa wale waliofadhiliwa na waliotajirishwa na waliotumikiwa na waliofunzwa na kazi zangu”

Katika jamii yetu ya leo hususani Tanzania tunaona mambo haya yamekithiri sana. Hivyo basi, ili jamii iweze kuondokana na hali hii ni lazima iungane pamoja na kupinga dhuluma na uonevu. Pia kwa kuzingatia haki ya mwandishi S. Robert anasema; uk.80 “Mwandishi si mtu wa ajabu awezae kuishi kwa kula hewa na kunywa ukungu. Ni mtu wa desturi ambaye kama watu wengine wa desturi, hafarijiwi na hasara”.

Ugumu wa soko la vitabu; Mwandishi ameonesha ugumu wa suala hili pale alipofungua duka la vitabu lakini watu hawakuhamasika kununua vitabu hivyo, hali hii ilitokana watu wengi kutokujua kusoma na kutokana na utamaduni wa jamii hiyo katika suala zima la usomaji wa vitabu kwani hawakujua thamani yake, kama asemavyo; uk.110 “Walikuwa katika tarehe ya ujinga wa kujua kuwa mazoea ya kusoma yalikamilisha utu wetu katika dunia. Hawakufahamu kwamba katika vitabu ndimo ghala za utamaduni wa elimu zilimopatikana”. Hali hii inahalisika sana katika jamii ya leo kwani watu wengi wanajua kusoma lakini hawana utamaduni wa kusoma hivyo husababisha soko la vitabu kuwa gumu.

Uzalendo; Suala hili limeoneshwa na S. Robert jinsi gani alivyokuwa mzalendo kwa nchi yake (Tanganyika) katika kupinga mifumo yote ya kiutawala wa kikoloni ambaye ilimdharau mwafrika hususani katika kipengele hiki cha kisiasa, kuwa mwafrika hawezi kufanya chochote. Mfano uk.75 “Mwafrika aliweza kufanya nini? Alikuwa mtu gani mbele ya watu?” hali hii ilimfanya Shaaban Robert kujitoa muhanga katika kushiriki misafara mbalimbali ya kisiasa ili kuhamasisha maendeleo ya mwafrika, japokuwa gharama zote za safari hiyo zilikuwa juu yake. Na hii ilitokana na hali ya uzalendo iliyojaa kifuani mwake, kama asemavyo katika uk.74“Sikuwa na kago juu ya ari hii. Alivyokuwa kila mtu ndivyo nilivyokuwa mimi vilevile. Nilitekwa na uzalendo kama alivyotekwa mtu yoyote mwingine. Sikupenda kuwa mgeni katika nchi ya asili na uzazi wangu”.

Hivyo basi suala hili la uzalendo linahalisika katika jamii ya sasa, kwani watu mbalimbali huingia katika siasa na kutetea maslahi ya haki zao ili kujipatia maendeleo hivyo mwandishi anaitaka jamii ya sasa kujitoa muhanga katika kupingana na utawala mbovu uliojaa dharau kwa wale wanaowaongoza.

Kifo na maisha; Haya ni mambo yaliyomo ndani ya jamii, kama binadamu tunapaswa kuyapokea, kuyakubali na pia kuangalia ni kwa namna gani tutakabiliana nayo. Shaaban Robert anaeleza ugumu wa maisha ya upweke na ukiwa na jinsi alivyoyakabili baada ya kufiwa na mkewe Amina. Uk.4 “…mauti yake ya mapema yalikuwa ni msiba na hasara kubwa kwangu.” Lakini Shaaban Robert anatuonesha kwamba pamoja na matatizo hayo jamii inapaswa kuwa na moyo wa uvumilivu kwani upo wakati mwingine mzuri ujao.

Mapenzi ya dhati; Shaaban Robert anaonesha mapenzi ya dhati aliyokuwa nayo kwa mkewe baada ya kifo. Mfano katika uk.3 anasema, “…tokeo hili lilikuwa pigo kubwa sana kwangu na msiba katika nyumba nzima. Marehemu huyu alikuwa johari ya maisha yangu, tegemeo na mshauri mwema”.

Vilevile alionesha mapenzi ya dhati kwa kuwajali wanae ambao nao walikuwa na upweke wa kumkosa mama yao, alionesha upendo mkubwa kwao kwa kutoacha mwanya wa kujisikia wakiwa. Mfano aliwapatia elimu; uk.5 anasema, “…niliwapenda kwa mapenzi sawa kama baba na mama, nikawatunza kama mboni za macho yangu”. Shaaban Robert anaiasa jamii kuwa suala la kulea watoto baada ya kifo cha mzazi mmoja si la mama tu, bali hata baba kama mzazi anapaswa kuwalea watoto walioachwa tena kwa mapenzi yote ya baba na mama, hivyo si budi jamii kubadilika katika hili.

Nafasi ya mwanamke; Mwandishi Shaaban Robert anamuona mwanamke kama kiungo muhimu sana katika safari hii ya maisha, anamchukulia katika nafasi mbalimbali kama ifuatavyo:

· Mwanamke kama tegemeo na mshauri mwema. Mfano; uk.3 “…marehemu huyu alikuwa jahari ya maisha yangu, tegemeo na mshauri mwema”.

· Pia anamuona mwanamke kama mtu mwenye ushirikiano na asiye mvivu. Mfano; uk.3 “…alinisaidia katika mambo mengi wakati wa maisha yetu pamoja ambayo yangalinishinda kuyatenda mimi peke yangu”. Pia hata katika isha ya Idara ya Utawala Shaaban Robert anaeleza uhodari na uchapakazi wa mke wa Mudir. Mfano; uk. 61 “bibi huyu alikuwa hodari na mcheshi sana”

· Vilevile anaona mwanamke kama mlezi muhimu sana. Kwa mfano; uk.5 “…nilisikitishwa mno kwa ukosefu wa malezi ya mama yao lakini nilikuwa sina uwezo wa kumwita arudi duniani tena”.

· Shaaban Robert anamuona mwanamke kama pambo na faraja katika maisha ya ndoa. Anasema katika uk.3 “Sura yake ilikuwa jamali kwa kimo cha kadirio, uso wake ulikuwa mviringo wa yai, nywele nyeusi za kushuka, paji pana, nyusi za upinde, macho mazuri yaliyokuwa na tazamo juu ya kila kitu, kope za kitana, masikio ya kindo yasiyopitwa na sauti ndogo, meno ya mwanya…”

· Mwanamke pia ameoneshwa kama mtu mpole na mwenye heshima. Jambo hili Shaaban Robert ameliweka wazi makusudi ili jamii iweze kuiga na kubadilika kwani wanawake wengi sasa wamepungukiwa na hilo. Mfano; uk.37 “Mke huyu wa pili alikuwa mpole, mwenye madaha na heshima, alikuwa na sura ya haya ambayo ilichuana na utawa kama uso kwa kioo”.

Kufanya kazi kwa bidii; Kwa kiasi kikubwa Shaaban Robert ameonesha mfano hai katika utendaji bora wa kazi akiwa kazini, kwani alikuwa ni mtu wa kujituma na vilevile alikuwa ni kiongozi mzuri na mwenye kupenda kushirikiana na wafanyakazi wenzake. Amelibainisha hili kama nyenzo kuu na muhimu sana katika kazi wakati wote, kwani kupitia nyezo hii kuna manufaa mengi sana kama vile kupendwa na watu, kupandishwa cheo na hata kuaminiwa sana ndani ya jamii. Jambo ambalo jamii ya leo yapaswa kuiga. Mfano; uk.41 “Niliaminiwa sana hata kuliko nilivyotazamia. Mapendeleo niliyotendewa yalikuwa mengi sana”. Pia hata katika uk.40 “Nilitenda yote yaliyokuwa katika uwezo wangu kutimiza wajibu”. Pia hata katika Insha ya Idara ya Utawala makarani walikuwa ni wachapakazi.

Utu wema, urafiki na uhusiano mzuri na watu; Jambo hili Shaaban Robert ameliona kama nguzo muhimu sana kwa maisha ya mwanadamu yoyote. Anasihi kuwa maisha ya uadui ni maisha mabaya yasiyo na furaha, hakutaka uadui, kumkwaza mtu, aliishi kwa wema na kujenga urafiki daima. Na hivi ndivyo inavyopaswa kuwa kwa mwanadamu yoyote yule kuenenda, kwani hayo huleta maendeleo binafsi na ya jamii kwa ujumla. Mfano; uk.39 “…miguu yangu ilikuwa tayari kwenda kutafuta urafiki…maisha ya uadui kila upande ni mazito kwa mtu yeyote”.

Utii na unyenyekevu; Shaaban Robert ameonesha hali ya utii na unyenyekevu kwa wakuu wake wa kazi na hata wafanyakazi wenzake. Mara zote alijidunisha na kujishusha ilihali akiacha watu waseme juu ya uzuri na ubora wake. Mfano; uk.43 alipopandishwa cheo alisema, “Kisha moyo ulinikua kwa kuona kuwa kazi yangu ilikuwa imehesabiwa na kuonekana thamani yake, wakati mimi mwenyewe nilikuwa nimeidunisha”. Uk.45 “Sifa ilikuwa kubwa kuliko niliyotenda, nikainama chini kwa haya; na huzuni ilikuwa kubwa vilevile moyo ukanilemea”. Shaaban Robert anatuonesha kwamba suala hili aliliona tangu hapo mwanzo na ndiyo maana anaifundisha jamii kuwa yapaswa kutenda vivyo hivyo ili iwe taa ya kuangaza na sabuni ya kung’arisha maisha yao.

Suala la mirathi; Mwandishi Shaaban Robert anatuonesha ugumu uliopo katika suala zima la ugawanyaji wa mirathi. Suala hili linahalisika hata katika maisha yetu ya sasa tunaona jinsi ndugu wanavyopingana na hata kuchukiana kwa sababu ya mirathi. Kutokana na hali hii Shabaan Robert hajasita kutuonesha umuhimu wa kuacha wasia juu ya ugawanyaji wa mali. Kwa mfano; uk. 48 “Choyo cha warithi mbalimbali kilifanya magawanyo kuwa magumu ajabu”

Ubaguzi wa rangi na matabaka; Enzi za ukoloni kulikuwa na ubaguzi wa rangi wa watu weupe na weusi katika mambo mbalimbali ya kijamii, mfano; kusalimiana kwa kushikana mikono, vyombo vya usafiri vilikuwa katika madaraja, daraja la kwanza walikuwa watu weupe (wazungu) wakati daraja la tatu walikuwa watu weusi (waafrika).

Vilevile hata sehemu za malazi zilikuwa katika misingi ya kiubaguzi. Shaaban Robert alilionesha hili katika uk.50 “Karibu ningalilala nje Korogwe kwa ukosefu wa malazi ya abiria waafrika”. Pia uk.52 “Huyo alikuwa ni mzungu, hakuwa tayari kushikana mikono na mimi”.

Pia hata katika Insha ya Msuso uk.105 anasema; “Mtu yoyote aliyekuwa si mweupe katika Afrika kusini hakuwa na ustahili, dhamani wala heshima ya uanadamu. Aliweza kutendewa ukatili wowote ambao haukuwezekana kujaribiwa hata kwa wanyama wa porini bila ya lawama katika nchi nyingine za ulimwengini.” ya mambo haya leo hii yapo hata katika jamii yetu japo yanajidhihirisha kwa namna nyingine. Leo ubaguzi kati ya matajiri na masikini, wenye vyeo na wasionavyo ni mkubwa sana.

Wema na ubaya; Mwandishi huyu ameonesha nguvu kubwa ya wema juu ya ubaya, anasema palipo na wema ubaya hushindwa na kutupwa kabisa. Mfano; uk.51 anasema kwamba, “Idadi ya watu wema ni kubwa siku zote kuliko jumla ya watu wabaya”. Katika jamii yetu ya leo wema upo lakini bado unamezwa na ubaya kwa kiasi kikubwa kutokana na woga, uroho wa madaraka, ubabe wa baadhi ya watu, nk. Ila Shaaban Robert anaipa jamii suluhu ya ubaya kuwa yatupasa kuwa wema.

Dharau; Suala la kudharauliwa kwa waafrika lilioneshwa wazi na wazungu pamoja na wahindi. Hii ni pale ambapo hata kama mwaafrika angekuwa na cheo cha juu kuliko mzungu bado mzungu angeheshimiwa sana kuliko mwaafrika huyo. Shaaban Robert katika utumishi wake alilionja hili na lilimpa mfadhaiko mkubwa sana. Mfano; uk.54 anasema, “Nilikuwa ni radhi kuwekwa chini ya wakubwa wangu lakini niliona dharau wadogo kuwekwa juu yangu”. Uhalisia wa jambo hili ndani ya jamii yetu ya leo lipo katika sehemu mbalimbali za kazi, kwani watu wanaangalia undugu, urafiki na mahusiano mengine ambayo hayana hadhi yoyote katika cheo fulani.

Dhamira nyingine zilizojitokeza katika kazi hii zipo katika insha mbalimbali, kwa mfano Insha ya “Naondoka Mpwapwa” kuna dhamira ya umuhimu wa elimu kwa watoto wa kike, ujasiri na tamaa ya mali. Masuala haya ni masuala ambayo yapo katika jamii yetu ya sasa, hivyo ni vyema jamii ichukue mazuri yote na kuacha mabaya kama vile tamaa ya mali.

Pia katika Insha ya “Idara ya Utawala” dhamira ambayo imejitokeza ni suala zima la utawala, ambapo mwandishi anatueleza ni kwa namna gani viongozi wanavyotakiwa kuwajibika katika nafasi zao za kazi. Kwa mfano; uk.61 mwandishi amemuonesha Mudir na masaidizi wake jinsi walivyokuwa wakiwajibika.

vilevile katika Insha ya “Nilikuwa Mshairi” kuna dhamira ya umuhimu wa ushairi. S. Robert anaonesha ni kwa namna gani ushairi ulivyo muhimu, kwani huweza kutunza kumbukumbu na uhai wa mwandishi. Mfano; uk.64 “Mauti huua mwili wa mwandishi ukawa vumbi tupu kaburini lakini mchoro alioandika wakati wa maisha yake hudumisha uhai wa jina lake duniani milele”.

Kipengele kingine cha Maudhui ni Mgogoro;Ni hali ya kutokuelewana baina ya pande mbili yaani mtu na mtu, mtu na kikundi au mtu mwenyewe na nafsi yake.Migogoro mbalimbali imeweza kujitokeza ambapo tunaweza kuigawa katika vipengele vifuatavyo; Mgogoro wa nafsi,Mgogoro wa kiuchumi,Mgogoro wa kijamii na Mgogoro wa kiuchumi.

Katika mgogoro wa nafsi tunamwona Shaaban Robert akionesha hali ya kujiuliza juu ya maisha mazuri yakoje na je afanye nini ili awe na jina zuri duniani. Mfano; uk.2 “Ukosefu wa jina zuri ni ukiwa mkubwa duniani. Jambo hili sikulipenda.” Suluhisho la mgogoro huu; Shaaban Robert aliamua kufanyakazi kwa bidii na kuwa mtu mwema.

Mgogoro mwingine wa nafsi unajitokeza kwa S. Robert kwamba ni kwa vipi angepata mke aliye na sifa kama za Amina! (mke wake wa kwanza ambaye ni marehemu). Anasema uk.37 “Nilikuwa na marafiki na wenye huruma kadha wa kadha lakini, kati yao palikuwa hapana mtu niliyeweza kumwita mke. Nafasi yake ilikuwa haina mtu nyumbani”. Suluhisho la mgogoro huu, alimpata mke wa pili aliyekuwa na sifa alizozihitaji.

Pia kuna mgogoro wa kijamii ambapo umetokea pale Shaaban Robert alipodharauliwa kuhusu cheo chake. Hii ilijitokeza pale ambapo S. Robert hakutendewa haki kazini kwake, kwani badala ya kuwekwa wa kwanza katika orodha ya mshahara kutokana na cheo chake aliwekwa mwishoni kwa kuwa tu yeye alikuwa ni mwaafrika. Suluhisho la mgogoro huu Shaaban Robert aliamua kuandika barua kwa mkuu lakini barua hiyo haikufanyiwa kazi. Basi S. Robert aliamua kuvumilia. Uk.55 “Katika ulimwengu watu wengine walikuwa wamepatwa na madhila kuliko yaliyonipata mimi wakavumilia. Mimi nilikuwa ni nani nisivumilie?”

Mgogoro mwingine wa kijamii ni kati ya S. Robert na ndugu wa mke wake. Chanzo cha mgogoro huu ni uchoyo wa baadhi ya warithi wa mirathi. Suluhisho lake ni pale S. Robert alipowapa uhuru wa kuchagua sehemu waliyotaka na zile zilizoachwa kuwa zake na watoto wake. Uk.48 “Basi nilitoa shauri kuwa isipokuwa mimi na watoto wangu kila mrithi alikuwa na idhini ya kuchagua sehemu yake katika shamba apendalo, na sehemu zisizochaguliwa itakuwa haki ya watoto na mimi. Shauri hili lilisuluhisha mambo kama uchawi”.

Pia mgogoro wa kijamii mwingine ni kati ya S. Robert na msimamizi wa safari, chanzo cha mgogoro huu ni ubaguzi au dharau, hii ilijionesha pale ambapo S. Robert alipoambiwa kushuka katika lori la daraja la pili ili kuwapisha wahindi wanne wakati yeye alistahili kuwa katika hilo gari kutokana na yeye alistahili kuwa mfanyakazi wa serikali. Suluhisho la mgogoro huo S. Robert na watoto wake aliwapisha na kushuka. “Msimamizi wa safari, mhindi vilevile, hakuona mtu mwingine wa kushuka ila mimi”.

Katika mgogoro wa kiuchumi tunamwona Shaabani Robert akilalamika namna alivyodhurumiwa pesa za manunuzi ya vitabu vyake,uk 78 anasema “Kwa kazi yangu iliyoweza kuleta sh 25000/= kwa vitabu 5000 katika mwaka 1954 sikupewa hata pesa moja ya shaba kwa muda wa miaka kadhaa….sikupata kitu kwa kazi yangu iliyoleta karibu sh 15000/= kwa vitabu 5000 katika mwaka 1958.Suluhisho la mgogoro huu ni kwamba Shaabani Robert alizidi kuwa mvumilivu pasipo kuvunjika moyo katika kazi yake ya uandishi uk 79 anasema…..sijavunjika moyo,tena ningali nayo bado furaha katika uandishi kama alivyo bi-arusi kwa mpenzi wake.Katika maisha baadhi husumbuka na wengine hucheka.

Ujumbe; mwandishi S. Robert ametoa ujumbe wa aina tofauti tofauti kwa lengo la kuiasa na kuionya jamii ili iweze kubadilika na kufikia maendeleo yenye kuleta tija kwa mtu binafsi, jamii na taifa kwa ujumla.

· Kufanya kazi kwa bidii ni msingi mzuri katika maisha. Mfano S. Robert alifanya kazi kwa bidii na ndio maana alifanikiwa katika maisha yake yote na hivyo kujijengea jina zuri.

· Jambo la msingi na bora katika maisha ni kutokata tamaa, hata kama tunashindwa kupata mafanikio makubwa ni bora kupata kidogo kuliko kukosa kabisa. S. Robert anasema kuwa; uk 2. “Jaribu dogo la wema ni bora kuliko kubwa la ubaya”.

· Utu wema ni matendo mazuri. Shaaban Robert anatuasa tuwe na matendo mema, matendo mema yaoneshwe nyakati zote. Mfano; mahusiano mema na marafiki, kauli nzuri kwa watu nk.

· Haki na uaminifu katika maisha humfanya mtu aheshimike na kukubalika wakati wote.

· Shaaban Robert anatuasa kuwa na mapenzi ya dhati katika maisha kwani hutufanya kuishi vyema.

· Suala la kumtegemea Mungu katika kila jambo ni muhimu, na kitu kizuri kinatoka kwa Mungu. Mfano; mke mwema au mume mwema.

· Suala la malezi ni la watu wote wawili na sio suala la mmoja. Hivyo hakuna budi baba na mama kushiriki kikamilifu katika malezi hasahasa baba.

· Hakuna haja ya kujilimbikizia madaraka na majukumu kwani maisha ya duniani ni ya mpito.

· Uandishi ni silaha muhimu katika utunzaji wa kumbukumbu za kihistoria.

· Nafasi ya elimu itolewe kwa watu wote.

· Ni vema kuwa wavumilivu katika kufanikisha jambo Fulani.

Falsafa ya mtunzi; Shaaban Robert anaamini kuwa mtu hupendwa na kukubalika kwa watu kutokana na matendo yake mazuri kama vile, kauli njema, ufanyaji kazi kwa bidii, utii na unyenyekevu, msamaha, uvumilivu na kuwa na moyo wa kujitoa. Anasema; “Wema hushinda ubaya na haki ya mtu haipotei”.

Mtazamo; Mtazamo wa S. Robert ni wa kimapinduzi anaona kuwa kufanya kazi kwa bidii huleta maendeleo.

Msimamo; Shaaban Robert ameonesha msimamo wa aina mbili kwanza msimamo wa kidhanifu ambao umetokana na imani yake aliyoishikilia kwamba Mungu ndiye tegemeo. Na anatudhihirishia kwamba mtu akimtegemea Mungu atafanikiwa. Pili ameonesha msimamo wa kiuyakinifu kwani anaeleze kuwa, mtu anayefanya kazi kwa bidii na mwenye ushirikiano na maadili mema ndiye hujitengenezea jina zuri katika jamii. Na hii inajidhihirisha wazi katika Maisha yake ya kabla na baada ya miaka hamsini na ndiyo maana mpaka leo anakumbukwa.

Baada ya kuangalia maudhui katika insha mbalimbali sasa tuangalie umbo la ndani na la nje katika ushairi. Hapa tutachambua mashairi pamoja tenzi. Kwa kuanza na shairi la “Amina” katika umbo la ndani (maudhui) kwa kutumia nadharia ileile ya Uhalisia.

Mwandishi S. Robert ameonesha dhamira mbalimbali kama ifuatavyo:

Mapenzi ya dhati na ndoa; Shaaban Robert anaeleza mapenzi yake ya dhati kwa Amina (marehemu) anaona kwamba Mungu ndiye anayefunga na kufungua mapenzi. Mfano; katika ubeti wa 2 uk.4 anasema; 2.


“Nilitaka unyanyuke, kwa kukuombea dua,


Sikupenda ushindike, maradhi kukuchukua,


Ila kwa rehema yake, Mungu amekuchagua,


Mapenzi tuliyofunga, hapana wa kufungua”

Dini na imani kwa Mungu: Shaaban Robert anaamini uwepo wa Mungu ndio maana katika ubeti wa 2 anamwombea mke wake dua kwa Mungu ili ayashinde maradhi. Anaamini kuwa Mungu hashindwi na kitu lakini kwa mapenzi yake ameamua kumchukua.

Maadili mema na maonyo: hali hii imejidhihirisha pale Shaaban Robert alipokuwa anawaasa watoto wake katika utenzi wa Hati na Adili, juu ya kuwa na maadili mema. Anataja mambo kama adabu na utii, utu wema, umuhimu wa mwanamke kujitunza, kujali wakati, umuhimu wa elimu, kuepuka fitina, kumcha Mungu, kuwaheshimu wazazi, mapenzi ya dhati katika ndoa, kuepuka uvivu, kutii mamlaka, kutunza ahadi nk. mfano katika ubeti wa 34. Anaelezea uvumilivu katika maisha ya ndoa. 34.


“Na mume msishindane,
Wala msinuniane,
Jitahidi mpatane,
Ndiyo maisha ya ndoa”

Pia katika ubeti wa 36 anaelezea usafi na kutunza mazingira;


36. “Nyumba yako inadhifu,
Kwa kufagia uchafu
Kila mdudu dhaifu
Asipate pa kukaa”

Maana ya kifasihi ya ubeti huu ni kwamba, mwanamke anapaswa kutunza mwili, moyo na akili yake ili visije vikaingiliwa na mawazo machafu/fikra potofu ambazo zitadhoofisha mahusiano/mapatano katika ndoa au familia yake.

Umuhimu wa elimu: katika ubeti wa 31, uk 10. Shaaban Robert anaonesha jinsi gani elimu ilivyomuhimu katika maisha. Anasema; .


31. “Elimu kitu kizuri,
Kuwa nayo ni fahari,
Sababu humshauri,
Mtu la kutumia”.

Heshima kwa wazazi: ili kuishi maisha mema na yenye baraka, Shaaban Robert anawaasa Hati na Adili wawaheshimu wazazi na wala wasioneshe dharau ili wapate taadhima. Mfano katika ubeti wa 36.uk.26 anasema;


36. “Tatu baba na mama,
Wataka taadhima,
Na kila lililojema,
Ukiweza watendee”.

Vivyo hivyo hata katika jamii yetu ya leo tunaona jinsi gani watoto na vijana wengi wanavyo wadharau wazazi wao na hata watu waliowazidi umri. Hivyo basi si budi jamii kubadilika kwani heshima ni kitu muhimu sana katika maisha.
Ujane: Shaabani Robert anaonesha athari za kuondokewa na mume au mke na pia umuhimu wa mke na mume. Mfano; ubeti. 13:1 “Dunia mume na mke, kwa watu hata wanyama”


Vilevile anaonesha umuhimu wa kuwa pamoja kati ya mume na mke. Mfano; ubeti 3:3 “Adamu pasipo mke, Mungu hakuona vyema”,

Katika uhalisi suala la ujane lipo na halikwepeki ni kitu ambacho kinaumiza sana iwapo mmoja anaondokewa na mwezi wake.

Umuhimu wa ndoa; katika shairi la Ndoa ni Jambo la Suna Shaabani Robert anasisitiza kwamba katika dini ya kiislamu ndoa ni kitu muhimu sana katika maisha ya duniani, hivyo anawahamasisha vijana waoe kwani ndoa ni jambo la kheri na ni suna kutoka kwa Mtume. Pia anawahamasisha vijana waache zinaa. Ubeti 8:2 “Huko kubibirishana, ni haramu vitabuni”,

Ubaya wa unafiki; hii inajitokeza katika shairi la “Ndumakuwili” mwandishi anaonesha ubaya wa mtu mnafiki na jinsi alivyo kwani si rahisi kumtambua kama anavyosema katika ubeti 2.


2. Hujivika pande zote, mkapa akavikika,
Litengezwalo lolote, hangui huridhika,
La sharia au tete, lisemwalo hutosheka,
Ndumakuwili si mwema, hujidhuru nafsia.

Hata katika jamii yetu ya leo watu kama hao wapo, hivyo mwandishi anaiasa jamii kuachana na tabia ya ndumakuwili kwani hukwamisha maendeleo.

Umuhimu wa shukrani; katika shairi la “Namshukuru” mwandishi anatufundisha kwamba katika maisha tunapaswa kuwa watu wenye shukrani kwa Mungu katika kila jambo. Mfano, ubeti.10 uk 104.


“Namshukuru Manani, mwenye uwezo arifu,
Hafi maji baharini, mzawa kufa kwa sefu,
Mambo yake yanafani, kila akiyasarifu,
Alhamdulillahi, namshukuru Latifu”.

Nafasi ya mwanamke: Shaaban Robert hakuacha kujadili suala la mwanamke katika jamii. Hili linajidhihirisha kwenye utenzi wa “HATI”, anamuasa binti yake kuwa awe mtii, msafi, mpishi bora, mvumilivu katika ndoa nk. mfano katika ubeti wa 33.uk.10 anasema;


33. “Upishi mwema kujua
Na mume kumridhia
Neno analokwambia,
Kwako itakuwa taa”.

Ujumbe; katika mashairi yake mwandishi S.Robert ametoa ujumbe huhimu sana katika kuiasa jamii kama ifuatavyo:

· Maisha ya kumtegemea Mungu ni yenye fanaka.

· Jamii yapaswa kuzingatia elimu kwani ni mwanga wa maisha.

· Ili vijana wafanikiwe katika maisha wanapaswa kuwa na utii na adabu.

· Tuwe makini katika katika maneno tutamkayo yasiwe na athari mbaya kwa jamii, kama matusi, kunena uongo nk.

· Kupekuwa uvivu na kufanya kazi kwa bidii ni silaha ya maendeleo.

Baada ya kuangalia umbo la ndani katika ushairi sasa tuangalie umbo la nje katika ushairi. Kwa kutumia nadharia ya Umuundo-mpya.

Nadhari ya Umuundo-mpya ni zao la nadharia ya Umuundo. Nadharia hii inatumia neno Umuundo-mpya kuonyesha mtizamo wa kimuundo katika fasihi ambao ulitokea baada ya ukinzani wa nadharia ya Umuundo. Japo dhana hii haiwezi kupewa maana moja maalum, imehusishwa na maendeleo kutoka au katika kazi za Derrida (1973, 1976), Lacan (1977), Kristeva (1981, 1984, 1986), Althusser (1971) na Foucault (1978, 1979a na b, 1981, 1986). Kazi hizi nazo zilichangiwa na kazi za Ferdinand de Saussure na Emile Benveniste (kuhusu isimu-jamii ya umuundo). Nadharia hii ya Umuundo-mpya hujikita zaidi katika kusisitiza kuwa maana inaweza kubadilika kulingana na miktadha husika. Kwa mfano. Maana ya neno tajiri hutofautiana katika lugha mbalimbali na hata kati ya miundo tofauti ya lugha moja, na hutegemea matumizi na muktadha wa matumizi hayo. Ndipo sasa hapana maana moja ya neno au fungu la maneno.

Kulingana na nadharia hii basi, neno 'mama' kwa mfano, huwa halina maana ya kindani inayotokana na lugha husika bali huwa na maana za kijamii zilizotokana na lugha hiyo na ambazo zinakinzana na kubadilika kulingana na mazingira na kipindi cha kihistoria.

Kwa kuanza na kipengele cha mtindo:

Mtindo; kwa mujibu wa Senkoro (2011), “Mtindo katika kazi ya fasihi ni ile namna ambavyo msanii hutunga kazi yake na huipa sura ambayo kifani na kimaudhui huainisha kanuni au kawaida za zilizofuatwa kama ni zilizopo (za kimapokeo) au ni za kipekee”.

Kwa ujumla mtindo uliotumiwa na mwandishi ni wa kipekee kabisa kwani ameweza kuchanganya insha,mashairi pamoja na tenzi ambazo kwa ujumla huelezea maisha yake S.Robert hususani katika insha, na katika mashairi na tenzi kuna majonzi, mawaidha, maonyo na maadili.

Katika kipengele cha mashairi mtindo uliotumika ni wa kimapokeo kwa sababu amezingatia urari wa vina na mizani, urari wa mishororo, kibwagizo na utoshelevu katika kila beti. Mfano ubeti wa 2 katika shairi la “Amina” anasema;


2. “Nilitaka unyanyuke, kwa kukuombea dua,
Sikupenda ushindike, maradhi kukuchukua,
Ila kwa rehema yake, Mungu amekuchagua,
Mapenzi tuliyofunga, hapana wa kufungua”

Muundo; kwa mujibu Senkoro (kashatajwa), “muundo hutokana na umbo na mpango wa kazi ya fasihi; kwa hiyo hapa ndipo tutapata katika ushairi wa Kiswahili, mashairi yenye miundo mbalimbali iainishwayo na idadi ya mistari (vipande/mishororo) katika kila ubeti, mathalani mashairi ya uwili, utatu, unne” nk.

Muundo uliotumika katika mashairi yote na tenzi zote ni muundo wa tarbia yaani mistari minne katika kila beti. Mfano, shairi la Amina ubeti.1 uk.4


Anima umejitenga, kufa umetangulia,
Kama ua umefunga, baada ya kuchanua,
Nakuombea mwanga peponi kukubaliwa,
Mapenzi tuliyofunga hapana wa kufungua.

Vilevile hata katika “UTENZI HATI” na “UTENZI WA ADILI” mwandishi ametumia muundo wa tarbia (mistari minne). Mfano; utenzi wa ADILI uk.


Kijana lete kalamu,
Nina habari muhimu,
Napenda uifahamu,
Dadayo kasha zamuye,

Matumizi ya lugha; mwandishi ametumia lugha fasaha na inayoeleweka na wote hasa katika upande wa insha, lakini katika upande wa ushairi kwa kiasi fulani ametumia msamiati wa lugha ya kiarabu. Mfano katika shairi la “Namshukuru” kuna maneno kama vile, Illahi, Alhamdulillahi, Latifu, rakadha, ashrafu, nk. Vilevile ametumia tamathali za semi kama vile:

Tashbiha: shairi la “Amina” ubeti wa 1:2 uk.4 “Kama ua umefunga baada ya kuchanua”. Neno “kama” ni tashbiha inayotumika kulinganisha vitu viwili.

Vilevile hata katika “UTENZI WA HATI” uk.7 ubeti wa 7:4 tunaona tashbiha zikijitokeza. Anasema, “Nakupenda kama Hidaya” na ubeti wa 6:3 anasema, “Tunza kama sahibu” pia uk.7 ubeti wa 5:3 “Itunze kama fedha”

Takriri: urudiaji wa neno, sentensi au kifungu cha maneo ili kusisitiza jambo. ubeti wa 1:3 na 4 “Nakuombea mwanga, peponi kukubaliwa” pia ubeti wa 4:3 “Nawe wangu penzi, peponi utaingia”. Neno “peponi” limerudiwa ili kuonesha msisitizo kwamba baada ya maisha haya kuna maisha mengine peponi (mbinguni). Pia uk.6 ubeti wa 5:2 “Nijaze kadha wa kadha”, vilevile katika “UTENZI WA HATI” neno “hati” limejitokeza mara nyingi mfano, ubeti wa 1, 2, 5, 6, 7, 8, 9, 10, 17, 18, 19… pia neno binti katika ubeti wa 1, 92, 93, 94, 95.

Ritifaa: Ngure (2003:128) ni kitu kisicho na uhai kama vile maiti huwa kinasemeshwa kana kwamba nafsi yake ingali hai. Mfano; katika shairi la Amina S.Robert anaongea na marehemu Amina kana kwamba yu hai. Hii imejidhihirisha katika shairi zima. Mfano; ubeti wa 4 na 5

Tashihisi: kukipa kitu kisicho hai uwezo wa kutenda. Mfano; ubeti wa 6:2;3 uk.5 anasema,

“Vumbi tena likiunga, roho likirudishiwa,

Mauti yakijitenga, mapenzi yatarejea”,

Pia katika UTENZI WA HATI uk.7 ubeti wa 6:1 anasema, “Dunia ina aibu”. Hapa dunia inapewa sifa ya ubinadamu ya kuona aibu. Vilevile uk.8 ubeti wa 17:3 anasema,

“Sauti yendavyo mbio”. Hapa napo sauti inapewa uwezo wa kukimbia kama kitu chenye uhai. Pia uk.27 ubeti wa 43:2 “Viungo vyake husema”. Viungo mbalimbali vya mwili vinapewa uwezo wa kusema kama binadamu.

Sitiari: kitu kupewa jina la kitu kingine. Hii ni katika “UTENZI WA HATI” uk.13 ubeti wa 50:3 anasema, “Mtu mwongo ni msongo”. Mtu mwongo anafananishwa na mtu asiyechezwa unyago/asiyefundwa. Pia hata katika uk.17 ubeti wa 81:1 chungo inafananishwa na kitu kilichooza. Anasema, “Chongo mbaya ni uvundo”, vilevile uk.26 ubeti wa 37:3 baba anafananishwa na mbegu. “Baba yako ni mbegu”, uk.15 ubeti wa 64:1 mama anafananishwa na kitu cheupe, kitu safi. Anasema “Mke ni nguo nyeupe”,

Jazanda (matumizi ya picha na ishara). Ubeti wa 1. Katika shairi la Amina Mwandishi anasema;


“Amina umejitenga, kufa umetangulia,
Kama ua umefunga, baada ya kuchanua”,

Hapa anafanisha kifo cha Amina na jinsi ua linavyonyauka.

Pia hata katika shairi la ndoa, mwandishi ametumia neno kunguru akimaanisha wale watu wasio tulia katika ndoa zao.

Taashira: maana inayotajwa si ile inayomaanishwa. Mfano uk.7 ubeti wa 6:1 katika “UTENZI WA HATI” anasema “Dunia ina aibu” pia uk.16 ubeti wa 73:1 na 74:1 anasema “Tumbo la rutuba”, “Tumbo hili la dhahabu”. Mwandishi anaposema “tumbo la rutuba” ni dhahiri kuwa anamaanisha tumbo la uzazi la mwanamke. Pia anaposema “tumbo hili la dhahabu” anamaanisha tumbo lenye thamani na la pekee wengine hawana.

Misemo: ni kauli fupifupi zenye ujumbe mzito. Kwa mfano: uk.9 ubeti wa 20:1 “Dunia ni Mvurugo” yaani inamaanisha kuwa duniani kuna mabaya na mazuri, hivyo tunapawa kuwa waangalifu. Pia uk.6 ubeti wa 5:1, “Ulimwengu una adha” pia uk.13 ubeti wa 54:1 “Ulimi wa pilipili”

Methali: uk.9 ubeti wa 22:2 “Cheche huzaa moto” yaani kitu kidogo chaweza kuleta madhara makubwa. Pia uk10 ubeti wa 28:1 “Dunia mali ya roho” pia katika shairi la “UJANE” uk. 82 ubeti wa 4:1 “Ujane neno la feli, kugombana watu wema”,

Taswira: katika “UTENZI WA HATI” uk.26 kuna taswira ya “hereni”. Hapa mwandishi anamfananisha hati na pambo la sikioni, anaona kuwa binti yake akizingatia hayo atafanikiwa maishani. Pia kuna taswira ya “pilipili” (kitu kichungu) ubeti wa 54. “UTENZI WA HATI” anamuasa mwanae asiwe na ulimi kama wa pilipili bali awe na kauli ya upole na faraja siku zote.

Jina la kitabu; “Maisha Yangu na Baada ya Miaka Hamsini”. Jina hili linasadifu kabisa yaliyomo katika kitabu, kwani, kazi yake yote mwandishi ameigawa katika sehemu kuu mbili sehemu ya kwanza ni Maisha yangu na sehemu ya pili ni Baada ya Miaka Hamsini. Vilevile katika kuelezea maisha yake ameelezea kwa mtindo wa insha, mashairi na utenzi. Na katika kila kichwa cha insha, shairi na utenzi vimesadifu kabisa yaliyomo ndani yake.

Kufaulu kwa mwandishi; Mwandishi amefanikiwa kwa kiasi kikubwa sana, kwani mambo aliyoyandika yana halisika katika maisha yetu ya kila siku.

Kutokufaulu kwa mwandishi; Mwandishi ameelezea mambo mengi kwa kufuata imani ya dini ya kiislamu na kusahau kwamba anaowaandikia ni mchanganyiko wa imani tofauti tofauti. Pia amejikita zaidi katika mambo dhahania kama vile Mungu. Vilevile hata lugha aliyoitumia kwa kiasi fulani ina msamiati wa kiarabu hasa katika ushairi, hivyo inawawia vigumu kuelewa wale wasiojua lugha ya kiarabu.

Hitimisho; Sisi kama wachambuzi wa kazi hii tunamwona S. Robert kama kivuli kinachoishi, kwani mambo mengi aliyoyaeleza bado yapo katika jamii ya leo na kazi yake bado inamashiko na itaendelea kuwa na mashiko hata kwa vizazi vijavyo.

MAREJEO:

Mdee, J.S. na wenzake (2011). Kamusi ya Karne ya 21. (toleo la pili) Longhorn Publishers (K) Ltd. Nairobi.
Ngure, A. (2003). Fasihi Simulizi kwa Shule za Sekondari. Phoenix Publisher. Nairobi.
Ntarangwi, M. ( 2004). Uhakiki wa Kazi za Fasihi. Augustana College, Rock Island, IL 61201
Robert, S. (1991). Maisha Yangu na Baada ya Miaka Hamsini. Mkuki na Nyota Publishers. Dar es Salaam.
Senkoro, F.E.M.K. (2011) Fasihi. KAUTTU Limited. Dar es Salaam.

TAFSIRI NA FASIHI LINGANISHI YA KISWAHILI.



TAFSIRI NA FASIHI LINGANISHI YA KISWAHILI.


Lengo la makala hii ni kuangalia kwa ufupi fasihi linganishi ya Kiswahili na tafsiri kwa kuzingatia uchambuzi wa utanzu uliofasiriwa zaidi kulingana na data zilizokusanywa huku msisitizo ukiwa katika mchango wa tafsiri katika fasihi linganishi ya Kiswahili pamoja na changamoto zitokanazo na mchakato wa tafsiri katika kufasiri matini za kifasihi.

Ili makala hii iweze kueleweka zaidi kipengele cha fasili ya dhana za msingi kama vile fasihi linganishi pamoja na tafsiri kimezingatiwa kama ifuatavyo:

Maana ya fasihi linganishi; Miongoni mwa wataalam waliofasili dhana ya fasihi linganishi ni Boldor (2003) akimrejelea Compbell (1926) anaeleza kuwa, fasihi linganishi ni taaluma inayochunguza uhusianao uliopo baina ya fasihi mbili au zaidi nje ya mipaka ya kitaifa kwa njia ya kulinganisha mfanano na msigano (tafsiri yangu).

Dhana nyingine ya msingi ni tafsiri; Kwa mujibu wa Mwansoko na wenzake (2006) tafsiri ni uhawilishaji wa mawazo katika maandishi kutoka lugha moja kwenda lugha nyingine. Hivyo, tafsiri ni miongoni mwa nyenzo muhimu katika kukuza na kusambaza fasihi kama ifuatavyo:

Tafsiri imesaidia kuingiza utanzu mpya katika fasihi andishi ya Kiswahili, kwani historia ya fasihi barani Afrika inaonesha kwamba, hapo awali jamii za kiafrika hazikuwa na utanzu huu wa fasihi. Hivyo basi, kupitia tafsiri fasihi ya Kiswahili imeweza kujitanua zaidi.

Pia tafsiri imesaidia kukuza na kusambaza fasihi ya Kiswahili ulimwenguni. Kwa mfano kiswahili kwenda lugha nyingine kama vile, Kijerumani “Kasri ya Mwinyi Fuad” (Dei Sklaverei der Gewiirze). iliyotafsiriwa na Manique Lutgens na Karin Boden (1997). Pia riwaya ya “Uhuru wa Watumwa” (The Freeing of the Slaves). iliyotafsiriwa na E.A.L.B. (1967) “Nagona na Mzingile” imetafsiriwa kwa Kifaransa na Xavier Garnier, “Bwana Myombekere na Bibi Bugonoka” imetafsiriwa kwa Kijerumani na Wilhelm J. G. Mohling nk.

Naye Ruhumbika katika makala yake (2003) anaeleza, kupitia tafsiri wasanii hukomaa kwa kusoma maandishi ya wasanii wengine na kujifunza mbinu mbalimbali ambazo zitasaidia katika kukuza na kueneza fasihi ya Kiswahili.

Vilevile mataifa mbalimbali huweza kujifunza utamaduni na historia za mataifa mengine kupitia kazi za kifasihi zilizotafsiriwa, hivyo fasihi ya taifa husika hukua na kuenea zaidi.

Lifuatalo ni jedwali la mapitio ya vitabu mbalimbali vilivyotafsiriwa kwa lugha ya kiswahili.





JINA LA KZI
UTANZU
JINA LA MFASIRI
MWAKA
LUGHA



“The Well of Gining” Kisima cha Giningi
Tamthilia
Muhamed S. Abdalla
1968
Kiingereza-Kiswahili



Maisha Yangu “Moya Zhizn”
Riwaya
Andrei Zhukov
1968
Kiswahili-Kirusi

3
Historia ya Dunia ya Kale


V. Makarenko
1988
Kirusi-Kiingereza

4
Dada Alyonushka na kaka Ivanushka
Hadithi
M. Mbigili.
2002
Kirusi-Kiswahili

5
Postamasta
Riwaya
Bernard Mapalala
2003
Kirusi-Kiswahili

6
Tufani
Tamthilia
Samuel S. Mushi
1969
Kiingereza-Kiswahili

7
“I will marry when I want” Nitaolewa Nikipenda
Tamthilia
E. A. E. P. Ltd
1982
Kiingereza-Kiswahili

8
(The list) Orodha
Tamthilia
Saifu D. Kiango
2006
Kiingereza-Kiswahili

9
(The Beautiful One are Not yet Born) Wema Hawajazaliwa
Riwaya
Abdilatifa Abdallah
1976


Kiingereza-Kiswahili

10
“The Test of Heaven” Aliyeonja Pepo
Tamthilia
M. Mkombo
1980
Kiingereza-Kiswahili

11
“The Government Inspector” Mkaguzi Mkuu wa Serikali
Tamthilia
Christon Mwakasaka


1979


Kiingereza-Kiswahili

12
Uhuru wa Watumwa “The Freeing of The Slaves in East Africa”
Tamthilia
E. A. L. B.
1967
Kiswahili-Kiingereza

13
“Anthology of Swahili Poetry” Kusanyiko la Mashairi
Ushairi
Ally Ahamed Jahadhmy
1975


Kiingereza-Kiswahili

14
“The Black Hermit” Mtawa Mweusi
Tamthilia
E. A. E. P. Ltd
1970
Kiingereza-Kiswahili

15
“Song of Lawino” Wimbo wa Lawino
Ushairi
Paul Sozigwa
1975
Kiingereza-Kiswahili




Baada ya kuangalia mapitio mbalimbali ya kazi za fasihi ya Kiswahili zilizotafsiriwa ifuatayo ni tathmini fupi ya kazi hizo;

Katika kufanya tathmini imebainika kuwa tamthilia ni utanzu unaonekana kufasiriwa sana kutokana na sababu zifuatazo:

Mwansoko (2006:46) tamthilia ni utanzu uliotafsiriwa sana kutoka na malengo makuu mawili; lengo la kuigizwa na lengo la kusomwa. Pia umefasiriwa sana kutokana na kwamba, ulikuwa ni utanzu mpya katika Afrika, hivyo wageni na wenyeji walitafsiri kwa lengo la kuutambulisha katika mazingira ya kiafrika. Vilevile umeonekana kutafsiriwa sana kutokana na urahisi wa lugha yake, kwani tamthilia hutumia maneno machache na yanayoeleweka tena bila hata ya ufafanuzi wa kina kama ilivyo katika riwaya.

Pia umefasiriwa sana kutokana na umuhimu wa maudhui yake ambayo hujibainisha katika masuala mtambuko duniani kote. Kwa mfano; tamthilia ya “Nitaolewa Nikipenda, Mtawa Mweusi” nk. maudhui yake yanahalisika katika jamii mbalimbali. Vilevile umetafsiriwa sana kwa lengo la kukuza na kueneza lugha adhimu ya Kiswahili, ambayo haikuwa na machapisho mengi yahusuyo fasihi andishi.

Kwa upande wa lugha zilizojitokeza zaidi katika kufanikisha suala la tafsiri ya fasihi ya Kiswahili ni lugha ya kiingereza, na Kiswahili; lugha ya Kiingeza imejitokeza sana katika tafsiri kutokana na kwamba, waingereza ni moja kati ya mataifa yaliyotawala sehemu kubwa ya dunia, na ndio taifa lililokuwa na dola yenye nguvu zaidi. Vilevile waingereza walishapiga hatua kubwa katika maendeleo ya fasihi ukilinganisha na mataifa mengine. Pia hata lugha ya kiingereza ni moja kati ya lugha kubwa duniani na inayofahamika na mataifa mengi.

Lugha ya Kiswahili nayo imeonekana kutafsiriwa sana kutokana na hitaji la kuwa na machapisho mengi ya kifasihi ili kukuza na kueneza fasihi ya Kiswahili. Pia ni lugha inayokua kwa kasi na inayoeleweka sana Afrika Mashariki ukilinganisha na lugha nyingine.

Pamoja na hayo yote, bado inaonekana kuwa, ushairi ni utanzu unaokabiliwa na changamoto nyingi zaidi katika kufasiri kutokana na kwamba, kwa kiasi kikubwa ushairi hutumia lugha ya mkato na ya kisanaa zaidi yenye msamiati mgumu uliosheheni taswira, ishara, lahaja, tamathali za semi pamoja na misemo, mafumbo nk. Hivyo basi, kuna uwezekano mkubwa wa kupotosha maana ya kifasihi pamoja na sanaa iliyomo katika utanzu huu.

Licha ya hayo, vilevile ugumu unasababishwa na kanuni za kiarudhi hasa katika mashairi ya kimapokeo kwani, ni vigumu sana kutafsiri ushairi huku ukizingatia urari wa vina na mizani bila kupotosha maana iliyokusudiwa.

Hivyo basi, ili kuepuka changamoto hizo ingefaa sana mfasiri anayefasiri utanzu huu awe mahiri wa lugha zote mbili, pia awe mtu mwenye upeo mkubwa katika uwanja huu na mwenye juzi mkubwa wa kutunga mashairi au naye awe kiasi fulani msanii. Hivyo haitamwia vigumu sana katika kuteua maneno mwafaka.

Baada ya kuangalia tathmini ya mapitio hayo ufuatayo ni uchambuzi wa tamthilia ya “Mkaguzi Mkuu wa Serikali” kwa muongozwa wa nadharia ya usawe wa aina matini.

Newmark (1982) matini yoyote ile ifasiriwe kwa kuzingatia aina yake. Hii ina maana kwamba, kazi itakayotokea itafanana na matini chanzi. Vilevile mbinu ya “Ulinganishaji Matini” itatumika katika kufanya uchambuzi wa kazi teule, kwani katika mbinu hii matini lengwa hulinganishwa na matini chanzi ili kubaini vipengele vya kifani na kimaudhui vilivyoongezwa, vilivyopunguzwa na vilivyopotoshwa.

Kipengele hiki kitajihusisha na uchambuzi wa tamthilia ya “Mkaguzi Mkuu wa Serikali” iliyoandikwa na Nikolai V. Gogol katika lugha ya Kirusi na kutafsiriwa katika lugha zote kuu duniani ikiwemo Kiswahili. Tafsiri ya Kiswahili imefanywa na Christon Mwakasaka kupitia tafsiri ya Kiingereza iliyofanywa na D. J. Campbell kutoka katika lugha ya Kirusi.

“Mkaguzi Mkuu wa Serikali” ni moja kati ya tafsiri za kifasihi ambazo ni bora kwa kiasi fulani katika upande wa maudhui na ni mbovu kwa kiasi kikubwa katika upande wa fani. Ubovu huu unatokana na mfasiri kutozingatia nadharia ya “Usawe wa Aina Matini”. Hali hii imesababishwa na kufasiri tafsiri, yaani kufanya tafsiri kupitia matini iliyotafsiriwa bila kutumia matini chanzi kama ifutavyo:

Mfasiri amepotosha muundo asilia wa tamthilia na kusababisha kutokea kwa tafsiri tenge/mbovu. Kwa mujibu wa Gromova (2004) tafsiri ya Kiswahili ya Mkaguzi Mkuu wa Serikali iliegemea tafsiri ya Kiingereza, ambayo ilifupisha matini asilia na kuigawa tamthilia ya Gogol katika matendo matatu badala ya matano. Kitendo hiki kinapunguza ubora katika taaluma ya fasihi linganishi ya kiswahili kwa kuifanya fasihi ya kiswahili kuwa na mapungufu.

Vilevile kuna upotoshaji mkubwa katika kufasiri majina ya wahusika. Mchambuzi Gromova katika makala yake anafafanua kwamba, ni vigumu sana kutafsiri katika Kiswahili majina ya Kirusi, kwani yana maana fulani. Katika tamthilia “Mkaguzi Mkuu wa serikali” kuna wahusika wengi ambao majina yao yanasababisha msomaji Mrusi apate taswira ya tabia zao. Kwa mfano, katika tafsiri ya Kiingereza lile jina la Constables ambalo katika Kiswahili ni Askari na katika Kirusi ni “Dyerzhimorda” halina maana ileile iliyokusudiwa kwa msomaji wa Kiswahili au Kiingereza. Kwani kwa Kirusi neno “morda” ni uso wa mnyama, na neno hili linatumika kwa ajili ya mtu ambaye unataka kumdharau. Ama lile jina la jaji “Lyapkin-Tyapkin” linatokana na mwigo “lyap-tyap”, maana yake ni kufanya kazi ovyo, bila nidhamu.

Pia kuna upunguzaji wa matini: Ukilinganisha matini ya Kiingereza na matini ya Kiswahili utaona kuwa katika tafsiri ya Kiswahili mfasiri hakueleza wasifu wa wahusika wakati katika tafsiri ya Kiingereza uk.16 mfasiri ameeleza kwa kirefu wasifu wa baadhi ya wahusika. Mbinu hii kama ingeingizwa katika matini lengwa ingeleta mchango mzuri katika fasihi linganishi ya kiswahili, kwani msomaji wangepata hamasa ya kutaka kujua zaidi kuhusiana na mhusika aliyemvutia. Mbinu hii haipo kwa waandishi wengi wa fasihi ya Kiswahili.

Vilevile kuna upotoshaji mkubwa wa mandhari. Mfasiri Mwakasaka katika tamthilia ya Mkaguzi Mkuu wa Serikali (uk.vi) anakiri kwa kusema kuwa “...nimekata maelezo ya jukwaani kila nilipoona kuwa si ya lazima.” Kitendo hiki hakifai kabisa katika kazi za kifasihi kwani maelezo ya jukwaani ni muhimu sana katika ujengaji wa mandhari, wahusika na dhamira. mfano katika tafsiri ya Kiingereza “ACT” 1 uk.23 kuna maelezo marefu sana yanayofafanua mandhari, wakati katika Kiswahili ONESHO LA KWANZA hakuna maelezo kama hayo.

Upotoshaji wa kipengele cha mtindo: katika matini lengwa neno “ACT” limefasiri mara mbili yaani act kama onesho uk.41 na act kama tendo uk.64, wakati katika matini chanzi “The Government Ispector” limetumika neno “ACT” mwanzo mpaka mwisho. Upotoshaji huu hauna mchango mzuri katika fasihi linganishi ya kiswahili kwani huleta mkanganyiko kwa wasomaji juu ya kipengele cha mtindo.

Upotoshaji wa jalada la kitabu. Katika matini lengwa mfasiri ameweka picha ya mtu anayedhaniwa kuwa ndiye Mkaguzi Mkuu wa Serikali, wakati katika matini chanzi hakuna picha kama hiyo. Hivyo basi, kitendo hiki kinatoa mchango hasi katika taaluma ya fasihi linganishi ya Kiswahili kwani, huifanya hadhira ifikiri kwamba hivi ni vitabu viwili tofauti.

Pamoja na mapungufu hayo mfasiri kwa kiasi kikubwa amefanikiwa sana katika kipengele cha kimaudhui, hasa katika upande wa dhamira na ujumbe. Dhamira zilizojitokeza katika matini chanzi zimejitokeza pia katika matini lengwa. kwa mfano, uongozi mbaya, rushwa, utapeli, uvivu, ukahaba, uaminifu nk. Mfano, (uk.72) Bw. Posta hakuwa mwaminifu katika kazi yake kwani alikuwa akifungua barua za watu. M/WILAYA: “Lakini uliwezaje kufungua barua ya mtu mashuhuri kama yule...” Vivyo hivyo hata katika matini chanzi suala hili linajitokeza. Mfano, (uk.88) Mayor: “But how dared you open the mail of such an important personage?” Kwa ujumla kipengele hiki cha maudhui katika fasihi linganishi ya kiswahili kina mchango mkubwa sana katika fasihi ya kiswahili kwani watunzi wa kazi za kifasihi hujifunza mbinu mbalimbali katika kuelezea masuala ya kijamii. Pia hata wasomaji kupitia kazi za fasihi zilizotafsiriwa huweza kujifunza tamaduni za mataifa mbalimbali.

Hivyo basi, pamoja na yote yaliyojadiliwa katika makala hii bado mchakato wa kufasiri kazi za kifasihi unakabiliwa na changamoto mbalimbali kama ifuatavyo:

Umahiri wa lugha zote mbili au moja kwa wafasiri; yaani lugha chanzi na lunga lengwa. Kwa mfano, Mwakasaka amefasiri kupitia tafsiri ya Kiingereza kutoka na kutomudu lugha ya Kirusi, hivyo anarudia makosa yaliyopo katika tafsiri ya Kiingereza kwenye Kiswahili.

Changamoto nyingine ni tofauti za kiutamaduni. Mambo kama dini, mavazi, mila na desturi. Kwa mfano, majina ya Kirusi huwa na maana yenye ujumbe mahususi, hivyo yanapofasiriwa katika kiswahili hupoteza ile maana halisi na kupotosha ujumbe uliokusudiwa.

Vilevile changamoto ya tofauti za kiisimu baina ya lugha mbili katika muundo wa sentensi na maumbo ya maneno. Kwa mfano muundo wa Kiingereza ni tofauti na muundo wa Kiswahili.

Pia changamoto nyingine ni kutoelewa mbinu mwafaka ya tafsiri husika, hivyo husababisha tafsiri kuwa tenge/mbovu.

Hivyo basi, ni dhahiri kwamba si rahisi kupata tafsiri iliyosahihi kwa asilimia zote, isipokuwa tunaweza kupata tafsiri bora kama tu wafasiri wa kazi za kifasihi watakuwa na sifa stahiki.

Kwa mfano, uwezo wa kumudu lugha, kujua utamaduni wa lugha husika pamoja na mazingira yake, kuwa na ujuzi wa taaluma husika kabla ya kufasiri nk. Kwa misingi hii tunaweza kupata tafsiri za kifasihi zilizobora zaidi


MAREJEO

Boldor, A. (2003). etd.lsu.edu/docs/available/etd-0408103.../Boldor_thesis.pdf “Perspectives on comparative literature”. Babes-Bolyai University, Cluj. May 2003.

Gogol, N. (1836). The Government Inspector. (Translated & adapted by D.J.Campbel 1974). East African Educational Publishers. Nairobi.

Gogol, N. (1836). The Government Inspector. (Mkaguzi Mkuu wa Serikali 1979). Kimetafsiriwa na Christon Mwakasaka. East African Educational Publishers. Nairobi.

Gromova, N.V. (2004). “Tafsiri Mpya za Fasihi ya Kirusi katika Kiswahili”. Swahili forum11 (2004): 121-125.

Newmark, P. (1982). Approaches to Translation. Oxford. Pergamon Press. London.

Ruhumbika, G. (2003). “Tafsiri za Fasihi za Kigeni Katika Ukuzaji wa Fasihi ya Kiswahili.” Makala za Semina ya Kimataifa ya Waandishi wa Kiswahili III (2003). TUKI. Dar es Salaam.

Mwansoko, H.J.M na wenzake. (2006). Kitangulizi cha Tafsiri: Nadharia na Mbinu. TUKI. Dar-es-salaam.