Subcribe to our RSS feeds Join Us on Facebook Follow us on Twitter Add to Circles

Jumatano, 7 Januari 2015

MAANA YA VIAMBAJENGO,VIFUNDO MAMA,DADA NA BINTI.






1.Viambajengo ni vijenzi katika sentensi ambavyo hushirikiana na vingine ili kujenga vipashio vikubwa zaidi.

2.Utawala wa kiuambajengo ni hali ya kifundo cha kijenzi kimoja kukimiliki kifundo kingine.

3.Kutawala kwa karibu ni hali ya kifundo kikubwa kukimiliki vifundo vingine pasi ukingo kati yake.

4Mahusiano ya kutangulia ni hali ya neno au kifundo kimoja kujitokeza kabla ya kingine katika ulalo. Yaani kinachokuwa kushoto kinakitangulia kilicho kulia.

5.Kifundo mama ni kifundo ambacho kinamiliki vifundo vingine. Mfano S ni kifundo mama cha KN na KT.

6.Kifundo binti ni kile ambacho kinamilikiwa kwa karibu na kifundo mama. Kwa mfano KN na KT ni vifundo binti vya S.

7Kifundo dada ni kile ambacho kinahusiana na kingine kwa sababu ya kuzaliwa au kumilikiwa na kifundo sawa. Kwa mfano kifundo KN ni dada kwa KT.


SEMANTIKI NA PRAGMATIKI

MAARIFA YA LUGHA NA MAARIFA YA ULIMWENGU

IMEANDALIWA NA MANYAMA CHARLES


Maarifa ya lugha ni elimu ya kupambanua vijengo mbalimbali vya lugha na kanuni zake kulingana na taratibu za lugha hio. Ulimwengu halisi ni mukatadha ambao maarifa ya lugha huweza kutumika ili kuleta taathira kama ilivyokusudiwa na msemaji au mwandishi.

Richmond Thomason (2012) anafafanua maana ya semantiki kwamba ni tawi la isimu ya lugha linalohusu maana za viyambo vya lugha. Hivyo basi ni kusema kuwa, semantiki ni utanzu wa isimu unaojishughulisha na maana ya maneno au viyambo vya maneno katika lugha. Swali kuu katika wanasemantiki ni kuhusu ninini maana ya maana.

Hata hivyo wanasemantiki hujikita katika kuchunguza maana katika viwango mbalimbali kama vile; ngazi ya sauti (fonimu), neno, virai, vishazi na hata sentensi. Tawi hili la isimu limekuwa ni muhimu sana hasa kutokana na umuhimu wa mazungumzo, kwani ili mazungumzo yaeleweke na ujumbe ufahamike panahitajika maana. Aidha nivyema ifahamike kuwa semantiki inajihusisha na maana za maneno kiisimu, kwani maana yake hupatikana kutokana na muundo wa maneno hayo au maarifa ya lugha husika.

Kwa upande wa pragmatiki Richmond Thomason (2012), anasema kwamba ni tawi la lugha linalojihusisha na matumizi ya lugha kwa kuzingatia muktadha wa wazungumzaji walugha husika. Hivyo Thomson anadai kuwa pragmatiki inahusu zaidi mambo mawili; matumizi na muktadha.

Geoffrey Finch (2000) anasema kuwa, dhana ya pragmatiki ilivumbuliwa katika miaka ya 1930 na mwanafalsafa C.W. Morris, na imeanza kujulikana kama tawi tegemezi la isimu lugha miaka ya 1970 ambapo kabla ya hapo pragmatiki ilihusishwa kama tawi la kifalsafa, na kufafanuliwa kwa kuzingatia misingi mikuu miwili; matumizi na muktadha.

Kuanazia miaka ya 80 wataaklamu walianza kuiangalia pragmatiki kama maana ya msemaji na tafsiri kilichosemwa, yaani maana ya msikilizaji. Kwa upande wake Yule (1996) anafafanua dhana ya pragmatiki kwa kusema kuwa ni taaluma inayohusu mahusiano yaliyopo kati ya maana ya lugha na watumiaji wa mambo hayo.

Betty J. Birner (2012) anasema kuwa dhana hizi ni dhana zinazoshabihiana. Tofauti kubwa iliyopo kati ya dhana hizi bado ni mjadala mpana kwa baadhi ya wanaisimu wa lugha, hii ni kwa sababu, pragmatiki na semantiki zinajishughulisha na maana, kwa hio zipo hisia za ukaribu mno katika taaluma hizi mbili, licha kwamba pia zipo hisia za karibu za kuonesha utofauti wao.

Niukweli usiopingika kwamba kuna maarifa ya lugha na wakati huohuo kuna maarifa ya ulimwengu halisi, hii inamaana kuwa kufahamu lugha peke yake haitoshi lazima lugha hiyo itumike kulingana na muktadha au ulimwengu halisi ambapo lugha hio imetumika. Hali hii inaweza kuthibitishwa kutokana na kuwepo kwa matumizi ya maana tofauti kwa kadri ya watumiaji husika kama ifuatavyo.

Matumizi ya maana ya msingi katika kufafanua maana. Hii ndiyo njia kuu ya kulipa neno maana, ambayo kwa kawaida haibadiliki kutegemeana na athari za kimazingira. Hii inamaana kuwa maana ya neno au tungo itabaki ile ile hata kama mazingira yatabadilika. Maaaana hii ndiyo inayojulikana kama maana ya kileksika. Kwa mfano; kichwa- kikimaanisha sehemu muhimu katika mwili wa binaadamu kinachokusanya viungo kama vile; macho, masikio, pua na mdomo. Hii ndiyo maana pekeyake inayohitaji ulimwengu wa lugha kwa kiwango kidogo sana, hata hivyo bado ulimwengu halisi utahitajika kutokana na matumizi ya maneno kama vile homophoni na homonimia. Mfano neno kama kaa licha ya kuwepo kwa maarifa ya lugha lakini bado maarifa yaulimwengu halisi yanahitajika kuelewa kusudio la mzungumzaji, kwani yapo mazingira ambayo neno hilo litaendelea kutumika kama kitendo cha kuketi, na mazingira mengine litumike kama cheche la moto, na yote hayo ni maana ya msingi ya neno kulingana na miktadha tofauti tofauti.

Maana ya ziada au kisarufi. Ni maana abayo huibuka kutokana na maana ya msingi. Maana hii inatudhihirishia kuwepo kwa maarifa ya lugha na wakati huohuo kuna maarifa ya ulimwengu halisi. Hii ni kutokana na ukweli kwamba, maana hizi hutegemeana na kuhusiana na mazingira halisi ya matumizi. Kuelewa maana ya ziada sio tu kuelewa maarifa ya lugha, bali pia ulimwengu halisi au muktadha ambapo maneno au fahiwa hizo zimetumika. Mfano pale mzungumzajia atakapo sema “Samahani kaka! Hivi utaendelea kuwa kupe hadi lini? haya ni maisha tu!” utagundua kuwa, hapa kufahamu maana ya tungo hii si kutokana tu na kufahamu maarifa ya lugha, lakini pia inahitajika ufahamu wa ulimwengu halisi ambao tungo hio imetumika, kwa kusema kupe kumaaanisha mtu mnyonyaji au mtegemezi.

Maana ya kimtindo. Hii ni maana inayohusiana moja kwa moja na matumizi ya lugha kulingana na muktadha husika. Katika aina hii ya maana, neno au kiyambo hupata maana kulingana na mtindo ambao neno au kiyambo hicho kimetumika. Mfano mtindo wa kilahaja, mtindo wa wakati, mtindo wa kieneo, au hata mtindo wa taaluma ua fani fulani. Ni lazima tukiri kwamba kuna marifa ya lugha lakini wakati huo huo kuna ulimwengu halisi. Hii ni kwa maana kwamba katika maana hii, lazima mtumiaji wa lugha licha ya kufahamu maarifa ya lugha hio, lakini lazima azingatie ulimwengu halisi ambao lugha hio imetumika. Mfano matumizi ya mtindo wa kilahaja, kuna baadhi ya maneno kiuhalisia huibua hisia zingine na wakati mwingine kushindwa kufahamika kutokana na tofauti za kilahaja. Mfano maneno kama vile, shule, ugali na bomba, maneno haya yanaweza kutumika katika hali tofauti kwa wakaazi wa Tanzania bara na visiwa vya Zanzibar. Kwa upande wa Zanzibar wangeweza kutumia skuli, sembe na mfereji kwa mfuatano. Hivyo basi, kwa mzungumzaji inampasa kujua ni akina nani anazungumza nao na nani wangeweza kumuelewa ingawa wate wana maarifa ya lugha moja.


Aidha, kuwepo kwa maana hisia ni ithibati tosha ya kuthibitisha kuwepo kwa maarifa ya lugha na wakati huohuo ulimwengu halisi katika dhana ya semantiki na pragmatiki zinazohusu maana. Tunapozungumzia maana ya hisia ni aina ya maana ambayo huibuka kutokana na hisia au mtazamo wa msemaji au mwandishi. Na maana hii huweza kuwasilishwa kwa njia mbalimabali zikiwemo, njia ya maana kama dokezi au njia isiyo ya moja kwa moja. Kwa mfano “kweli wewe ni kidume wa mbegu kwelikweli!” katika tungo hii ni vigumu kufahamu mzungumzaji amemaanisha nini ikiwa msikilizaji hatohusisha maana au kauli hii na ulimwengu halisi au muktadha ambao msemaji au mwandishi amezungumza au kukusudia, kwani maana ya msemaji itakua tofauti na maana ya msikilizaji atakayojengwa kwa kuzingatia tu maarifa ya lugha. Mathalani hapa tunaweza kusema kuwa, msemaji amekusudia huyu kijana ni mchapakazi kwelikweli. Au kwa waswahili wanakawaida ya kumsifia mtu kwa kusema kwa mfamo, huyu mchezaji yaani hafai, mshenzi kwelikweli! Kiuhalisia neno hafai linamaanisha hali hasi ya mtu, vile vile mshenzi ni neno linalotaswira mbaya ya ufedheheshaji, lakini waswahili husema hivyo kuonesha sifa njema za mtu, tofauti n auhalisia. Hivyo kwa mtu kufasiri maana kulingana na maarifa ya lugha inapelekea kupotosha maana iliyokusudiwa.

Maana tangamani. Hii ni maana inayopatikana kutokana na matumizi ya lugha kulingana na muktadha husika wa matumizi kwa kuzingatia maana ya maneno mbalimbali na jinsi yanavyotumiwa kwa pamoja ili kuleta maana iliyokusudiwa. Maana hii pia inatuthibitishia kuwepo kwa maariufa ya lugha na wakati huohuo ulimwengu halisi. Hii inamana kuwa si kujua tu maariufa ya lugha ndio kuweza kuitumia lugha hio, lakini ni kwa vipi lugha hio ingeweza kutumika. Kwa mfano kauli kama vile “Mabibi na mabwana”, mvulan amtanashati, dada mrembo. Ukichunguza tungo hizi utagundua kuwa si kufahamu tu maarifa ya lugha, bali lazima mtumiaji afahamu ulimwengu halkisi wa matumizi ya maneno hayo. Mfano msemaji angeweza kusema, ‘mabibi na mababu” au “dada mtanashati” na ‘mvulana mrembo” jambo ambalo lisengekubalika kajika jamii za waswahili.

Maana mangwi au akise. Ni aina ya maana ambayo huibuka katika hali ambayo maana moja hukonyeza maana nyingine na hivyo humfanya mtu afikirie maana nyingine pia. Mfano kauli “naenda kujisaidia” Katik tungo hii inahitaji mtumiaji wa lugha au msikilizaji kufahamu ulimwengu halisi, yaani wanajamii fulani wanavyosema kujisaidia wanamaanisha nini? Kwa mfano mara nyingio katika jamii za kiafrika kujisaidia humaanisha ima kuenda haja ndogo au kubwa. Jambo hili katu lisengefahamika kwa sababu tu ya kufahamu maariga ya lugha hio.

Mwisho ni maana ya dhamira au muhimu. Hii ni aina ya maana ambayo hutegemea kile ambacho mtoa ujumbe ana kipa umuhimu zaidi. Mara nyingi kile kinachopewa umuhimu zaidi hutokeza mwanzoni mwa senmtensi. Msingi wa kupata maana katika aina hii inathibitisha kuwa pamoja na kuwa na marifa ya lugha pia panakuwepo n aulimwengui halisi wa lugha. Kupitia aina hii ni vigumu mtu kutambua umuhimu wa msemaji au mzungumzaji kwa msingi tu wa maarifa ya lugha bila kuhusisha hali gani lugha hio imetimika. Mfano kauli ya kusema “Kikwete atashinda uchaguzi wa mwaka 2015” Katika mfano huu umuhimu zaidi upo kwa Kikwete ndiye ambaye ana tarajiwa kushindsa uchaguzi na sio uchaguzi wala mwaka 2015. Haya yote yatabainika ikiwa tu msikilizaji atakuwa anamaarifa ya lugha na wakati huohuo anaujua ulimwegu halisi.

Kwa kuhitimisha tunaweza kusema kuwa, semantiki na pragmatiki zote kwa pamoja zinahusiana, kwa mana kwamba zinajihusisha na maana ya maana katika lugha. Wala haitokuwa sahihi kudhani kwamba kufahamu tu maana ya viambajengo katika tungo, iwe neno, kirai, kishazi au hata sentensi kuwa ndio kufahamu kwa kile kilichokusudiwa bila kujali muktadha ambao neno hilo imetumika.

Hat hivyo, taaluma hizi bado zitaendelea kuwa tofauti kwa kuwa semantiki hujihusisha na maana za maneno au viyambo vya maneno kama vilivyo kupitia kwa masemaji na msikilizaji. Wakati huohuo pragmatiki hujishughulisha na jinsi gani muktadha unapelekea kupata maana ya kile kilichokusudiwa kulingana na muda mahsusi.

Aidha ifahamike kuwa Semantiki na Pragmatiki zote kwa pamoja zimelenga kutoa ufafanuzi kuhusu mchakato wa lugha na matumizi yake kulingana na muktadha wa uzungumzaji au utumikaji wake. Kama sehemu ya mfumo wa mazungumzo , sambamba na kufasiri na kufafanua mfumo fungamanifu wa mazungumzo katika lugha, na hili litafikiwa tu kwa kuzingatia maarifa ya lugha sambamba na ulimwengu halisi wa mazungumzo.




MAREJEO.

Geoffrey Finch, (2000). Linguistic Terms and Concepts. Palgrave Macmillan.

Jacob L. Mey, (2001). Pragmatics: An Introduction, 2nd ed. Wiley-Blackwell.

Richmond H Thomason (2012). What is semantics? Second version.

Wwww.wisegeek.com Publishing & Printing International Journal. (USA), downloaded on Friday, 30th May 2014, at 12:30 pm.

Yule, G. (1996). Pragmatics. Oxford: Oxford University Press.

Jumanne, 4 Novemba 2014

UAMILIAJI LUGHA

UAMILIAJI LUGHA SARUFI MAJUMUI NA UAMILIAJI LUGHA YA PILI.
 Makala haya yataangalia maana ya sarufi majumui, masuala ya msingi yanayohusu maarifa ya lugha, sifa za sarufi majumui, sarufi majumui na uamiliaji lugha ya pili na mwisho tathmini. Kwa mujibu wa Chomsky (1976:29) kama alivyonukuliwa na Ellis (1996:430) sarufi majumui ni mfumo wa kanuni na sheria ambazo ni msingi wa lugha za binadamu (tafsiri yangu). Muasisi wa nadharia hii ni Noam Chomsky. Msingi wa nadharia hii ni kwamba binadamu anapozaliwa anakuwa na maarifa asilia ambayo humsaidia katika ujifunzaji lugha; mambo ya ndani na nje ambao husaidia katika uamiliaji wa lugha. Maarifa haya hupatikana pale tu binadamu anapozaliwa kwani huwa na kifaa cha uamiliaji lugha ambacho kinakuwa na kanuni majumui na kanuni badilifu ambazo hukutana na tajiriba (uwezo wa jamii katika lugha) na kusababisha uamiliajli lugha kutokea. Waamiliaji wa lugha ya kwanza huwa na maarifa asilia ambayo huwawezesha kuiamili lugha yao kwa kutumia maarifa hayo. Hivyo maarifa hayo yanaamshwa na tajiriba ambayo mjifunzaji anaikuta katika jamii iliyomzunguka na hatimaye kukutana na maarifa asilia katika kifaa cha uamiliaji lugha hatimaye kuzalisha sarufi mahsusi ya lugha husika. Waamiliaji wa lugha ya pili wanakuwa na lugha ya kwanza ambapo sifa za sarufi majumui bado humwezesha kuamili lugha ya pili, kwani kanuni badilifu na kanuni majumui zilizojengwa kwa misingi ya lugha ya kwanza hutumika katika kuamilia lugha ya pili. Hivyo kwa mujibu wa nadharia ya sarufi majumui inamsaidia mjifunzaji katika kuamili lugha ya pili. Wataalam mbalimbali wameweza kujadili juu ya uwezo wa sarufi majumui wa kuwa kifaa weazeshi cha kujifunza lugha ya pili, kuna wataalam wanaokubali na wanaokataa mchango huo. Kama Flyn (1984-1987) anavyoelezea kama alivyonukuliwa na Ellis (1996:453) kifaa cha uamiliaji lugha ya kwanza kitahusika na mchakato  wa ujifunzaji lugha ya pili. Akaendelea kusema kanuni badilifu za lugha ya kwanza na lugha ya pili zikiwa sawa ujifunzaji utakuwa rahisi kwa sababu mjifunzaji wa lugha ya pili ana uwezo wa kuhusisha miundo wakati kanuni hizo zikitofautiana kati ya lugha ya kwanza na lugha ya pili ni vigumu kujifunza. Flyin yeye anaunga mkono juu ya sarufi majumui kuwa kifaa wezeshi katika ujifunzaji wa lugha ya pili. Kwani anaamini bado maarifa ambayo mjifunzaji wa lugha ya kwanza anayoyatumia katika ujifunzaji wa lugha hiyo, ndiyo yale yale anayoyatumia mjifunzaji wa lugha ya pili. Hata hivyo Clahsen na Muysken (1986-1991) kama walivyonukuliwa na Ellis (1996:454) wanasema uamiliaji wa lugha ya pili ni tofauti na uamiliaji lugha ya kwanza muamiliaji lugha ya kwanza huwa na kifaa wezeshi cha uamiliaji lugha wakati wa lugha ya pili hutumia mbinu za lugha ya kwanza katika kujifunza lugha ya pili wanaendelea kusema muamiliaji lugha ya pili huhitaji nadharia ya isimu wakati wajifunzaji lugha ya pili huhitaji naharia tambuzi. Hata hivyo sarufi majumui imeangaliwa katika mitazamo tofautitofauti, hivyo kuonesha ubora lakini pia mapungufu yake katika ufundishaji wa lugha: Kwa kuwa na sarufi majumui tunaona kuwa sifa za lugha huingiliana, hivyo mwingiliano wa lugha ya kwanza na ya pili unaweza kumwezesha muamiliaji lugha ya pili pale miundo ya lugha ya kwanza na lugha ya pili itafanana na hata ikitofautiana mjifunzaji anakuwa na uwezo wa kujiundia miundo yake itakayomsaidia katika ujifunzaji wake kwa kutumia sifa majumui za lugha. Flynn (1984;1987) kama alivyonukuliwa na Ellis(1996;453) anaeleza kuwa “kifaa cha uamiliaji lugha ya kwanza kinaweza kutumika katika uamiliaji wa lugha ya pili. Kama kanuni badilifu za lugha ya kwanza na ya pili zinauhusiano hurahisisha ujifunzaji”. Hivyo yeye anakubali kabisa kuwa sarufi majumui ni kifaa wezeshi katika ujifunzaji wa lugha ya pili, anaamini sifa za mjifunzaji wa lugha ya kwanza ndizo ambazo anakuwa nazo mjifunzaji wa lugha ya pili. Aidha Ellis (1994:461) anaeleza ubora wa sarufi majumui kuwa imetoa msingi wa uibukaji wa nadharia zingine za ujifunzaji lugha baada ya kuegemea kwenye maarifa asilia anayozaliwa nayo binadamu. Pia imeweza kueleza sifa majumui za lugha mbalimbali za ulimwengu kwa ufupi, hivyo kusababisha sifa za lugha kueleweka kwa urahisi kwa wajifunzaji wa lugha ya pili. Kwa mujibu wa Ellis (1994:458) udhaifu huu unajidhihirisha katika maeneo kadhaa, kiini cha sarufi majumui yenyewe, pia mbinu zilizotumika kukusanyia data. Hivyo inaonekana kuwa kuna tatizo katika mbinu za ufundishaji na namna ya ufundishaji wa lugha ya pili. Nadharia ya sarufi majumui haikuonyesha namna gani mjifunzaji anapata ujuzi wa kutumia maarifa asilia aliyozaliwa nayo lakini pia mbinu iliyotumia katika ukusanyaji wa data ni ile mbinu ya kukusanya data isiyo ya vipindi maalum. Hivyo kupelekea data zake kutoweza aminika. Vilevile clahsen na Muysken (1986), Meisel(1991) kama walivyonukuliwa na Ellis (1996;454) muamiliaji wa lugha ya pili atakuwa tofauti na muamiliaji wa lugha ya kwanza kwa sababu kifaa cha uamiliji lugha kipo tu kwa mtu anayejifunza lugha ya kwanza na yule anayejifunza lugha ya pili huweza kusaidiwa na maarifa/mbinu mbalimbali ya ufundishaji na mazingira. Hivyo hawa wanaona kuwa safuri majumui si kifaa wezeshi katika ujifunzaji wa lugha ya pili. Kuibuka kwa nadharia zingine kunaonesha udhaifu wa nadharia ya sarufi majumui, mfano Fabisz, N.[1] Anaelezea nadharia ya uzawa iliyoasisiwa na Andersen ambayo inasisitiza juu ya urithishaji wa lugha, pia nadharia ya utamadunishi iliyoasisiwa na John Schumann (1978)inayosisitiza jinsi utamaduni wa jamii ulivyo na mchango mkubwa katika ujifunzaji lugha kwani lugha huendana na utamaduni mfano ni vigumu kujifunza lugha ya kiingereza kwa mswahili kwasababu tunatofautiana katika utamaduni hata kama utajua kiingereza hautafanana na mwingereza mzawa kwa kuwa yeye atatumia miundo ya lugha hiyo akihusisha na utamaduni wake. Hivyo katika kujifunza lugha sarufi majumui sio kifaa wezeshi pekee cha uamiliaji lugha pekee ambacho hutumika bali kuna vitu kama mazingira, motisha na urudiaji wa mara kwa mara humpelekea muamiliaji lugha ya pili kujifunza lugha ingawa kuna utofauti wa uamiliaji kuna wengine huchukua muda mrefu na wengine muda mfupi, si lazima waamiliaji wa lugha ya pili wawe na sarufi majumui inayofanana, hivyo tofauti zao wakati mwingine haziepukiki. Kama ubora na udhaifu wa sarufi majumui unavyojidhihirisha, hii inaonesha kuwa sarufi majumui peke yake haitoshi kumfanya mjifunzaji wa lugha aweze kuamili lugha ya pili vizuri, hivyo walimu wanashauriwa kutumia nadharia changamani katika ufundishaji wao wa lugha ya pili ili kumwezesha mjifunzaji wa lugha ya pili kuamili lugha hiyo vizuri. Kimsingi sarufi majumui inajidhihirisha kuwa ni kifaa wezeshi katika ujifunzaji wa lugha ya pili licha ya kuwa na udhaifu wake, haipelekei kuiondoa katika hali ya uwezeshi katika ujifunzaji wa lugha ya pili, kwani sifa majumui zinazopatikana katika lugha mbali kwa kiasi kikubwa zinawasaidia wajifunzaji kujifunza lugha ya pili, mfano wajifunzaji wanapogundua miundo ya lugha na uundaji wa misamiati unaolingana itawawia rahisi katika ujifunzaji wao. Lakini hata ikitofautiana sarufi majumui imefafanua namna ambavyo mjifunzaji huyu ataweza kujiundia sarufi yake ambayo itakuwa imejengeka kwa misingi ya lugha ya kwanza. Kuna umuhimu wa kuwa na mazingira bora ya ujifunzaji ambapo mawasiliano yanapewa msisitizo mkubwa katika nadharia mbalimbali, hivyo walimu hawana budi kujenga mazingira hayo kwa wanafunzi wao ili waweze kujifunza lugha ya pili kwa usahihi. Ikiwa ni pamoja na kubadilisha mazingira ya darasa kuwa mazingira rafiki kwa mwanafunzi ambapo mawasiliano ndiyo kiini cha ujifunzaji. Nadharia ya sarufi majumui imeonekana ina mchango mkubwa katika tendo la ujifunzaji, lakini haitoshi kusema ndiyo nadharia pekee ambayo inapaswa kutumiwa na walimu katika ufundishaji wao kwani pia imeonekana kuwa na udhaifu, hivyo nadharia zingine kama za utamadunishi, uzawa na urithishaji ni muhimu kuzipa umuhimu pia ili tendo zima la kujifunza liweze fanyika, lakini pia cha msingi ni kujua wajifunzaji hawawezi kuwa na uwelewa wa aina moja hata kama haya yote yatatimia, hivyo kinachoangaliwa ni kufikia ile hali ya kawaida katika matumizi ya lugha, ambapo kila mjifunzaji anatarajiwa afikie.

MAREJEO
Ellis, R. (1994), Second Language Acquisition, USA: Oxford University Press Fabisz, N. ANALYSIS OF KRASHEN’S THEORY OF SECOND LANGUAGEACQUISITION,http://webspace.webring.com/people/ap/panandrew/sla.html,

ISTILAHI

 Externa approach  - mkabala wa nje
Intuition              - ujuzi
 Internar approach  - mkabala wa ndani
Parameter             - kanuni badilifu
Principles             - kanuni majumui
 Prompted              - Papo hapo

Universal grammar - sarufi majumui 

FONOLOJIA YA KISWAHILI





UTANGULIZI USULI WA TAALUMA YA FONOLOJIA 
Neno fonolojia linatokana na maneno mawili ya Kigiriki phone-sauti za kusemwa na logos- taaluma/mtalaa. Masimulizi yanadai kuwa taaluma hii ilianza zamani sana kati ya mwaka 460 kabla ya Masihia huko India ya kale, ambapo mtu aliyeitwa Panini, na ambaye huaminika kuwa ni baba wa isimu aliandika kuhusu fonolojia ya Kisansikriti katika matini aliyoiita Shiva Sutras. Ni katika andiko hili ndipo alipobainisha kuwepo kwa dhana ambazo leo hii hujulikana kama fonimu, mofimu na mzizi. Baada ya andiko hilo, habari za taaluma ya fonolojia ni kama zilipotea kabisa katika uwanja wa isimu hadi ilipofika karne ya 19 ambapo wanaisimu wengine waliibuka na kuzungumzia upya masuala ya fonolojia. Miongoni mwa wanaisimu wa mwanzo wanaotajwa kujihusisha na fonolojia ni Mpolandi "Jan Baudouin de Courtenay" , (pamoja na mwanafunzi wake wa zamani "Mikołaj Kruszewski" alipobuni neno fonimu mnamo mwaka 1876, na kazi yake, ijapokuwa hairejelewi sana, inachukuliwa kuwa ni mwanzo wa fonolojia mamboleo. Mwanaisimu huyu si tu alishughulikia nadharia ya fonimu, bali pia vighairi vya kifonetiki (ambavyo leo huitwa alofoni na mofofonolojia). Maandishi ya Panini (Sarufi ya Kisanskriti) pamoja na Jan Baudouin de Courtenay yalikuja kuwa na athari kubwa kwa anayeaminika kuwa baba wa nadharia ya Umuundo Mamboleo, Ferdinand de Saussure, ambaye pia alikuwa ni profesa wa Sansikriti. Wanaisimu wote hawa walikuwa wanajaribu kulinganisha sauti za lugha za Asia Mashariki na za Ulaya, lengo lao likiwa ni kujua mizizi ya lugha zilizoitwa India-Ulaya. Kutokana na mkabala huo, katika kipindi hicho isimu ilikuwa Isimu-linganishi tu. Kutokana na tafiti zao hizo waliweza kupata maneno yenye sauti na maana zilizolingana, kufanana au kukaribiana. Utafiti huo uliweza kugundua jamii mbili za lugha ambazo ni jamii ya lugha za Kirumi na jamii ya lugha za Kijerumani. Baadhi ya wanaisimu mahususi kabisa wanaokumbukwa kuchangia katika maendeleo ya fonolojia ni pamoja na: (i) Jan Baudouin de Courtenay (1845-1929) Kama ilivyoelezwa hapo awali, huyu ni mwanaisimu aliyebuni dhana za foni na fonimu. Katika nadharia yake, alidai kuwa sauti za mwanadamu ni za aina mbili—foni na fonimu.  Alisema kuwa foni ni sauti za kutamkwa tu lakini fonimu ni sauti za lugha. Hata hivyo, de Courtenay hakutumia istilahi za foni na fonimu (kama zinavyotajwa sasa) bali alitumia istilahi za anthrophonics—foni na psychophonics—fonimu. Yeye alidai kuwa foni zipo karibu sana na taaluma ya kumuelewa binadamu pamoja na alasauti zake ambazo kwa hakika hutofautiana sana na za wanyama wengine. Na kuhusu fonimu, alidai kuwa zinahusu kumwelewa binadamu pamoja na akili zake na namna anavyofikiri katika akili yake. Alidai kuwa, mara nyingi, binadamu hupokea kinachotamkwa na kufasiliwa. (ii) Ferdinand de Saussure (1887-1913) Ni mwanaisimu wa Kiswisi anayejulikana kama baba wa isimu kutokana na mchango wake alioutoa katika taaluma hii. Yeye anakumbukwa zaidi kutokana na uwezo wake wa kutofautisha dhana alizoziita langue—mfumo wa lugha mahsusi na parole—matamshi ya mzungumzaji wa lugha husika. Langage hufafanuliwa kuwa ni uwezo alionao mzungumzaji wa lugha mahususi wa kuzungumza na kuelewa matamshi ya mzungumzaji mwingine wa lugha hiyohiyo. Ni sehemu ya lugha inayowakilisha maarifa kati ya sauti na alama. Ni mfumo wa alama kwa maana ya kiufundi tu. Dai lake la msingi ni kuwa alama inategemea vitu viwili—kitaja na kitajwa—hivyo ili mawasiliano yafanyike, mfumo wa ishara lazima ufahamike na ukubaliwe na wanajamii wote. Kwa upande wa parole, anadai kuwa ni matendo uneni. Ni namna lugha inavyotamkwa katika hali halisi na mtu mmoja mmoja. Dhana ya parole inalingana na dhana ya performance (utendi) ya Noam Chomsky. Katika lugha, parole ni matamshi tofauti ya sauti moja—alofoni. Wanaisimu wanaonekana kukubaliana na madai ya Saussure kwakuwa inaelekea kuthibitika kuwa hakuna uhusiano wa moja kwa moja kati ya kitaja na kitajwa [alama (lugha) na kinachowakilishwa (masilugha)], bali makubaliano baina ya wazungumzaji wa lugha moja husika ndiyo hutawala. (iii) Nikolai Trubetzkoy (1890-1939) Ni miongoni mwa waanzilishi wa taaluma ya fonolojia akichota mizizi ya taaluma ya isimu kutoka katika Skuli ya Prague. Mwanaisimu huyu aliandika misingi ya fonolojia kwa kutumia maarifa yaliyoibuliwa na Ferdinand de Saussure. Ni mtaalamu wa kwanza kufasili dhana ya fonimu. Aliandika vitabu vingi kwa lugha ya Kijerumani, miongoni mwake ni Grundzüge der Phonologie (Principles of Phonology, 1939), ambapo ni katika kitabu hicho ndimo alimotoa fasili ya fonimu pamoja na kubainisha tofauti baina ya fonetiki na fonolojia. (iv) Noam Chomsky (1928-) Huyu ni mwanaisimu wa Kimarekani anayevuma sana kwa mchango wake katika taaluma ya isimu kwa ujumla. Dhana za competence (umilisi) na perfomance (utendi) zimemfanya awe maarufu ulimwenguni. Dhana hizi zinaelezea tofauti baina ya maarifa na udhihirishaji wa maarifa hayo ya mtumiaji wa lugha. Katika fonolojia, Chomsky anakumbukwa kwa ufafanuzi wake wa dhana ya fonimu kwa mtazamo wa kisaikolojia. Anapochunguza dhana hii, hudai kuwa fonimu ni tukio la kisaikolojia, hivyo fonimu zimo kichwani mwa mzungumzaji wa lugha. (v) Daniel Jones (1881-1967) Ni mwanafonetiki kinara na maarufu kabisa katika nusu ya kwanza ya karne ya ishirini. Ni Mwingereza msomi ambaye alikuwa na shahada ya kwanza ya hisabati na shahada ya mahiri ya sheria, shahada ambazo hata hivyo, hakuwahi kuzitumia. Baadae, alisomea lugha na kuhitimu shahada ya uzamivu. Daniel Jones alifunzwa fonetiki na maprofesa mbalimbali, japokuwa aliathiriwa zaidi na Paul Passy na Henry Sweet. Hamu yake kuu ilikua kwenye nadharia ya fonetiki. Anafahamika zaidi kwa ufafanuzi wa dhana ya fonimu kwa mtazamo wa kifonetiki (ufafanuzi wake tutauchunguza katika sehemu ya mitazamo ya dhana ya fonimu).       FONETIKI NA FONOLOJIA Fasili ya taaluma ya fonolojia haiwezi kukamilika, na pengine kueleweka, iwapo hakuna linalosemwa kuhusiana na taaluma ya fonetiki. Hali hii inatokana na ukweli kuwa kuna uhusiano wa kinasaba kati ya fonolojia na fonetiki. Massamba na wenzake (2004:5) wananeneleza ukweli huu kwamba: …fonetiki na fonolojia ni matawi mawili tofauti ya isimu lakini yenye kuhusiana sana. Uhusiano wa matawi haya unatokana na ukweli kwamba yote mawili yanajihusisha na uchunguzi na uchambuzi unaohusu sauti za lugha za binadamu. Kutokana na ukweli huu, jitihada za kufasili dhana ya fonolojia inaelekea kuwa nyepesi, dhana hizi mbili zinapofasiliwa kwa mlinganyo. Tuanze na fonetiki: FONETIKI NI NINI? Fonetiki ni tawi la isimu linalochunguza sauti za kutamkwa na binadamu ambazo huweza kutumika katika lugha asilia. Massamba na wenzake (kama hapo juu) wanafasili fonetiki kuwa ni tawi la isimu linalohusika na uchunguzi na uchambuzi wa taratibu za utoaji, utamkaji, usafirishaji, usikiaji, na ufasili wa sauti za lugha za binadamu kwa ujumla. Wanasisitiza kwamba, kinachochunguzwa katika fonetiki ni [maumbo] mbalimbali ya sauti zinazoweza kutolewa na alasuti za binadamu (yaani sauti za binadamu zinazotamkwa tu). Kipashio cha msingi cha uchambuzi wa kifonetiki ni foni. Foni ni sauti yoyote inayotamkwa na binadamu na inayoweza kutumika katika lugha fulani. Hivyo basi, foni ni nyingi sana na hazina maana yoyote. Wanafonetiki hudai kuwa foni zimo katika bohari la sauti (dhana dhahania) ambalo kila lugha huchota sauti chache tu ambazo hutumika katika lugha mahususi. Sauti chache zinazoteuliwa na lugha mahususi kutoka katika bohari la sauti huitwa fonimu. Matawi ya Fonetiki: Kuna mitazamo miwili tofauti kuhusiana na matawi ya fonetiki. Mtazamo wa kwanza ni unaodai kuwepo matawi matatu; na mtazamo wa pili ni unaodai kuwepo matawi manne. Mtazamo wa kuwepo matawi matatu unataja fonetiki matamshi, fonetiki akustika, na fonetiki masikizi. Mtazamo wa kuwepo matawi manne (kama Massamba na wenzake (kama hapo juu), pamoja na matawi tuliyokwisha yataja, wanongezea tawi fonetiki tibamatamshi. Fonetiki matamshi huchunguza jinsi sauti za lugha zinavyotamkwa kwa kutumia alasauti. Hususani, huchunguza namna na mahali pa kutamkia sauti husika. Fonetiki akustika huchunguza jinsi mawimbi ya sauti yanavyosafiri kutoka katika kinywa cha mtamkaji hadi kufika katika sikio la msikilizaji. Fonetiki masikizi hujihusisha na mchakato wa ufasili wa sauti za lugha, hususani uhusiano uliopo baina ya neva za sikio na za ubongo. Na fonetiki tibamatamshi ni tawi jipya lililozuka mwanzoni mwa karne hii, ambalo huchunguza matatizo ya utamkaji ambayo binadamu huweza kuzaliwa nayo au kuyapata baada ya kuzaliwa. Ni tawi linalojaribu kutumia mbinu za kitabibu kuchunguza matatizo na kutafuta namna ya kuyatatua. FONOLOJIA NI NINI? Fonolojia ni taaluma ya isimu inayochunguza mifumo ya sauti za kutamkwa zinazotumika katika lugha asilia mahususi za binadamu. Inapolinganishwa na fonetiki, inasisitizwa kuwa fonolojia ni tawi la isimu linalochunguza mifumo ya sauti za lugha mahususi tu, kama vile sauti za Kiswahili, Kiingereza, Kigogo, n.k. Hata hivyo, wapo wanaisimu wanaoelekea kukubaliana kuwa kuna fonetiki ya lugha mahususi pia, na kuna fonolojia ya jumla, na fonetiki ya lugha mahususi. Mathalani, Massamba (1996) licha ya kufasili fonolojia kuwa ni taaluma ya isimu inayochunguza mfumo wa sauti za lugha mahususi, anaenda mbele zaidi na kudai kuwa fonolojia inaweza kuchunguza sauti kwa ujumla wake bila kuzihusisha na lugha mahususi. Akmajian na wenzake (2001), nao wanadokeza msimamo kama wa Massamba wanapodai kwamba fonolojia inaweza kuchunguzwa kwa mitazamo miwili tofauti. Kwanza, fonolojia kama tawi dogo la isimu linalochunguza mfumo na ruwaza za sauti za lugha mahususi ya binadamu; na pili, fonolojia kama sehemu ya nadharia ya jumla ya lugha ya binadamu inayohusika na tabia za jumla za mfumo wa sauti za lugha asilia za binadamu. Katika mhadhara huu, hata hivyo, tutakuwa wafuasi wa mtazamo unaoona kuwa fonolojia ni tawi la isimu linaloshughulikia mfumo wa sauti za lugha mahususi, hivyo tuna, kwa mfano, fonolojia ya Kiswahili, fonolojia ya Kiingereza, fonolojia ya Kiha, fonolojia ya Kihehe, na fonolojia ya Kibena. Kipashio cha msingi cha fonolojia ni fonimu. FONIMU Ni kipashio kidogo kabisa cha kifonolojia kinachoweza kubadili maana ya neno. Hivyo basi, fonimu ina maana, kwakuwa inaweza kubadili maana ya neno inapobadilishwa nafasi katika neno husika. Foni chache zilizoteuliwa kutoka katika bohari la sauti ili zitumike kwenye mfumo wa sauti za lugha mahususi ndiyo fonimu. Hivyo, fonimu ni chache ikilinganishwa na foni. Idadi ya fonimu za lugha hutofautiana kati ya lugha moja na nyingine. Mathalani, Kiarabu kina fonimu ishirini na nane (28), Kiswahili kina fonimu thelathini (30), Kifaransa kina fonimu thelathini na tatu (33), na Kiingereza kina fonimu arobaini na nne (44). Sauti ambayo huweza kubadilishwa nafasi yake katika neno lakini maana ikabaki ileile huitwa alofoni. Alofoni ni kipashio cha kifonolojia kinachotaja hali ambapo fonimu moja hutamkwa na kuandikwa tofautitofauti bila kubadili maana ya neno. Mfano: Fedha na feza Sasa na thatha Heri na kheri Kwa kifupi, alofoni ni matamshi tofautitofauti ya fonimu (sauti) moja. MITAZAMO YA DHANA YA FONIMU Juhudi za kufasili dhana ya fonimu zilizofanywa na wanaisimu mbalimbali zimezua mitazamo mbalimbali ya namna ya kuchambua dhana hii. Hadi sasa, mitazamo mitatu ifuatayo ndiyo hujulikana zaidi. Fonimu ni Tukio la Kisaikolojia Huu ni mtazamo uliokuzwa na kutetewa na wanasarufi geuzi-zalishi, mwanzilishi wake akiwa ni Noam Chomksy. Kwa mujibu wa mtazamo huu, fonimu ni dhana iliyo katika akili ya mzungumzaji wa lugha. Mtazamo huu unadai kuwa kila mzungumzaji wa lugha ana maarifa bubu ya idadi na jinsi ya kutamka fonimu za lugha yake. Chomsky anayaita maarifa haya kuwa ni umilisi (competence). Anadai kuwa maarifa haya ya fonimu hufanana kwa kiasi kikubwa miongoni mwa wazungumzaji wa lugha moja husika. Kinachotofautiana ni jinsi ya kudhihirisha (kutamka)  fonimu hizo, yaani utendi (perfomance). Chomsky anabainisha kuwa kuna uwezekano mkubwa wa kuhitilafiana baina ya umilisi na utendi kutokana na matatizo mbalimbali ambayo mzungumzaji hukabiliana nayo. Matatizo hayo ni kama vile uchovu, ulemavu wa viungo vya matamshi (alasauti za lugha), athari za mazingira, ulevi, na maradhi. Hivyo, kutokana na hali hii, fonimu hubaki kuwa tukio la kiakili, yaani kisaikolojia tu. Fonimu ni Tukio la Kifonetiki Wafuasi wa mtazamo huu wanaongozwa na Daniel Jones. Daniel Jones anaiona fonimu kuwa ni [umbo] halisi. ..........................Inaendelea

MOFOFONEMIKI YA KISWAHILI


Katika mada hii tumeangalia fasili ya mofofonemiki kwa mujibu wa wataalam mbalimbali, kisha tukaangalia kwa ufupi historia ya nadharia ya mofofonemiki na katika kiini cha mada tumejadili sababu zilizopelekea kuibuka kwa nadharia ya mofofonemiki. Kwa kuanza na fasili ya mofofonemiki  kwa mujibu wa mtandao wa Wikipedia wanafafanua mofofonemiki kuwa ni tawi la isimu linalojishughulisha na mwingiliano wa michakato ya kimofolojia na kifonolojia au kifonetiki. Pia hujishughulisha na mabadiliko ya sauti yanayotokea katika mofimu wakati zinapoungana kuunda maneno. (Tafsiri yetu). fasili hii ina mapungufu fulani kwani, mofofonemiki haijishughulishi na michakato yote ya kifonolojia na kimofolojia bali ni baadhi tu ya michakato hiyo ambayo ilishindwa kufafanuliwa kwa kutumia data za kifonolojia au kifonetiki peke yake. The New Oxford American Dictionary inafafanua kwamba, mofofonolojia/mofofonemiki ni tawi la isimu linalojishughulisha na uwakilishi wa kifonolojia wa mofimu. Hivyo basi tunaweza kusema kuwa, mofofonemiki ni tawi la isimu linaloshughulikia matumizi ya kimofolojia katika kueleza baadhi ya tofauti za kifonolojia ambazo isingewezekana kuzielezea kwa kutumia data za kifonetiki au kifonolojia peke yake. Baada ya kuangalia fasili ya neno mofofonemiki ifuatayo ni historia fupi ya nadharia ya mofofonemiki. Kwa mujibu wa Massamba (2010:82) akimrejelea Martnet (1965) anafafanua kwamba, istilahi hii mofofonemiki/mofofonolojia ilipendekezwa kwa mara ya kwanza na N.S. Trubetzkoy (1929). Trubetzkoy alitumia istilahi hii kwa maana ya tawi la isimu ilinaloshughulikia matumizi ya mafolojia katika kuelezea baadhi ya tofauti za kifonolojia ambazo isingewezekana kuzielezea kwa kutumia data za kifonolojia au kifonetiki peke yake. Baada ya kuangalia historia fupi ya mofofonemiki yafuatayo ni mambo yaliyosababisha kuibuka kwa nadharia ya mofofonemiki. Kuchunguza ubadilikaji wa sauti ambao usingeweza kuelezwa kwa kutumia data za kifonolojia peke yake. Baadhi yao wakapendekeza kuwapo kwa kiwango cha kimofofonemiki pamoja na kipashio umbo kiini kama kiwakilishi cha mofimu, kwa hiyo walipendekeza hivyo baada ya kushindwa kujua ipi ni alofoni ya fonimu ipi kwa kutumia kigezo cha kifonetiki pekee  Kwa mfano;  walishindwa kujua /k/ ni alofoni ya /c/ au /c/ ni alofoni ya /k/ Kwa mfano hata katika lugha ya kurusi –                                             ruka = “mkono”                                             ručnoj = “a mkono”                                              Mzizi ni – ruk na ruč Wanamofofonemiki walichunguza wakagundua kuwa katika mazingira fulani /k/ hubadilika kuwa /č/ baada ya kufuatiwa na “noj”. Hivyo wakapendekeza umbo kiini la maneno haya ni ruKa au ruČnoj umbo kiini lake lilitambulika kama {K} au {Č} Katika lugha ya Kiswahili kuna mabadiliko ya sauti yanayotokea katika baadhi ya maneno baada ya sauti fulani kufuatiwa na kiambishi cha unominishaji (i) kwa mfano katika maneno yafuatayo;                    Fuata – fuasi                    Penda – Penzi                    Cheka – Cheshi                    Pika – Pishi Pia wanamofofonemiki walichunguza ubadilishanaji huu wa sauti kwani walishindwa kujua ipi ni alofoni ya fonimu ipi. Ndipo wakagundua kuwa katika mazingira fulani /t/ hubadilika kuwa /s/ baada ya kufuatwa na mofimu ya unominishaji “i” pia sauti /d/ hubadilika na kuwa /z/ baada ya kufuatwa na mofimu ya unominishaji “i” Baada ya kupendekeza umbo kiini maneno haya yakaandikwa kama ifuatavyo: kwa mfano neno {fuaTa} umbo {T} likawa umbo kiini ambalo linawakilisha sauti zote mbili yaani /t/ na /s/, pia neno {piKa} umbo kiini lake ni {K} ambalo linawakilisha sauti /k/ na /ʃ/ Kuchunguza mabadiliko ya sauti yanayotokea mofimu zinapoungana. Kwa mfano; katika lugha ya Kiswahili,             U + ima         –       wima             I + etu            –       yetu             Mu + alimu    –      Mwalimu             U + imbo      –       wimbo             Vi + ake        –      vyake Wanamofofonemiki wakagundua kuwa sauti fulani huweza kuungana na kuunda sauti moja na kubadili umbo la neno. Chunguza muundo wa kifonolojia wa mofimu katika lugha. Kwa mfano katika lugha ya Kiswahili;             Mu + huni – Mhuni             Mu + gonjwa – Mgonjwa             Mu + guu – Mguu             Mu + uguzi – Muuguzi             Mu + tu – Mtu Wanamofofonemiki wakagundua kwamba mofimu fulani huweza kuungana na mofimu nyingine na kuunda umbo la neno. Kuchunguza ubadilishanaji wa sauti ambao una una uamilifu wa kimofolojia lakini husababisha mabadiliko fulani ya kifonetiki. Kwa mfano katika lugha ya kiingereza;             Play + s – [pleiz]             Dog + s – [dogz]             Since – [sins]             Else – [els]             Place – [pleis] Wanamofofonemiki wakachunguza kinachosababisha kuwepo na maumbo tofauti tofauti ya mofimu ya wingi. Kwa mfano; /s/, /iz/, /z/ Wakagundua kuwa kuna mchakato zaidi ya ule wa kifonolojia ambao ni wa kimofolojia unaosababisha umbo ‘s’ kutamkwa /z/ au /iz/ au /s/

                                        MAREJEO:
 The New Oxford American Dictionary. (2005), (2ndEdit), Oxford University Press. New York.


KANUNI ZA UUNDAJI WA HOJAJI




Makala haya yanahusu kanuni za uandaaji wa hojaji. Katika kujadili mada hii tumegawa kazi hii katika sehemu tatu muhimu, sehemu ya kwanza fasili ya hojaji kulingana na wataalam mbalimbali, sehemu ya pili ni kiini cha swali ambapo inaelezea kanuni muhimu za uundaji wa hojaji, hatimaye hitimisho. Kwa mujibu wa Kothari C.R, (2004), uk 100, anafasili neno hojaji kuwa ni maswali yanayoandikwa katika karatasi ili yaulizwe kwa mtafitiwa kwa lengo la kupata taarifa za tatizo la utafiti. Nayo Kamusi ya Kiswahili sanifu (2004) TUKI uk 116, inasema kwamba hojaji ni karatasi yenye maswali ya uchunguzi. Ni seti ya maswali mengi apewayo mtu/watu kwa lengo la kupata taarifa juu ya jambo fulani (Macmillan Dictionary) [1] Kutokana na fasili hizo hapo juu tunaweza kusema kuwa, hojaji ni maswali yanayoandaliwa na mtafiti kwa lengo la kukusanya data kutoka kwa watafitiwa. Hojaji hizo mtafiti anaweza kupeleka mwenyewe kwa mtafitiwa kwa njia ya mkono au kwa njia ya posta ikiwa na kimbatanisho cha kumwomba mtafitiwa asome na kuelewa maswali kisha ajibu maswali katika nafasi zilizoachwa wazi kwa matumizi tu ya hojaji kisha kuyarudisha kwa mtafiti. Hojaji zinazopelekwa kwa njia ya mkono husambazwa kwa haraka zaidi, na huwafikia watu wengi hususani wale wanaomzunguka mtafiti. Faida yake ni rahisi kukusanya, pia zinachukua muda mfupi, vilevile gharama zake ni ndogo, Faida ya kutumia njia ya posta ni pamoja na kutumia gharama ndogo na husambazwa katika eneo kubwa kwa muda mfupi. Pia mtafitiwa ana muda wa kutosha wa kuweza kutoa majibu kadri maswali yalivyoulizwa. Pia mtafitiwa ambaye hawezi kuingiliwa kwa urahisi hii inaweza kuwa njia nzuri ya kutumia. Licha ya njia hizo kuwa na faida pia zina hasara kama zifuatazo; kwanza mara nyingi hojaji zinazorudi zikiwa zimejazwa ni chache. Hii ni kutokana na mtafitiwa kutokuona umuhimu wa hojaji au kusongwa na majukumu au maswali kutokueleweka. Pili inabagua maana inahitaji watu wanaojua kusoma na kuandika, hojaji zinaweza kupotea zinapokuwa zinatumwa au kurudishwa. Ni vigumu kuelewa kama majibu yatolewayo ni ya kwa kweli au ya uongo. Hata hivyo njia hii ni ya taratibu mno kuliko njia zingine katika ukusanyaji wa data. Hojaji zimegawanyika katika makundi makubwa mawili; kwanza hojaji funge na hojaji za wazi (zisizo funge). Hojaji funge maswali yake yako wazi na yanaeleweka kwa watafitiwa. Maswali yanayoulizwa yanakuwa sawa kwa watafitiwa wote, yanalenga kutoa jibu moja tu. Mfano ndiyo au hapana, au ya kuchagua a,b,c,d…. hayaruhusu mtafitiwa kuweka hisia zake. Muundo wa maswali waweza kuwa funge. Kwa mfano; ANDIKA “N” KAMA JIBU NI NDIYO NA “H” KAMA JIBU NI HAPANA. AU CHAGUA HERUFI YA JIBU SAHII TU. Hojaji isiyo funge ni hojaji ambayo inamruhusu mtafitiwa kutoa maelezo/kujieleza/au kutoa maoni ya ziada (kutoa ufanuzi zaidi kadri ya uelewa wake kulingana na jinsi alivyoulizwa) Hojaji kama njia ya ukusanyaji data ina kanuni muhimu za kuzingatiwa wakati wa kuiandaaa. Mtafiti hana budi kuzingatia mambo yafuatayo; kwanza; ajue TATIZO LA UTAFITI. Mtafiti akishajua tatizo la utafiti itamsaidia kuandaa hojaji yake katika muundo unaotakiwa. Kwa mfano; atajua ni eneo gani ataenda kufanyia utafiti wake, umri wa watafitiwa, jinsia na kiwango chao cha elimu. Tatu izingatie usuli wa watafitiwa kama vile jina, umri jinsia, kabila na kiwango cha elimu. Hii inasaidia mtatifi katika uchambuzi wa data kujua amehoji watu wa umri gani na amehoji watu wa kiwango gani cha elimu. Pili ni mtiririko mzuri wa maswali; ili kutengeneza/kuandaa hojaji nzuri na kupata majiu sahihi mtafiti lazima azingatie mtiririko mzuri wa uaandaaji wa maswali. Mtiririko mzuri unaondoa uvulivuli/ukakasi kwa mtafitiwa, hivyo basi maswali lazima yawe katika mtiririko ufuatao; Kuanzia maswali mepesi kwenda maswali magumu, hii itampa moyo mtafitiwa au kumvutia na kuonesha ushirikiano lakini pia yatamvutia na kumpa moyo hivyo ataonesha ushirikiano au kupata hamasa ya kutaka kutoa majibu zaidi. Maswali hayo yawe na uhusiano/ muwala. Maswali yafuatayo hayana budi kuekwa; maswali yanayomtaka mtafitiwa kufikiri sana maswali yanayomhusu mtafitiwa, mfano una watoto wangapi, mkewe yuko wapi, kwa nini huna mtoto? Maswali yanayohusiana na mali za mtafitiwa, mfano je una magari mangapi? Au unalipwa kiasi gani kwa siku? Maswali yanayofuata baada ya maswali ambayo hayana budi kuepukwa ni maswali yanayohusiana na mada ya utafiti. Ambayo yanamtaka mtafitiwa kufikiri kiundani ili kuweza kutoa majibu sahihi. Mfano, nafasi ya uchaguzi wa lugha ya Kiswahili kama lugha ya kufundishia elimu ya juu. Maswali yalenge nini kinapelekea Kiswahili kuteuliwa kuwa lugha ya kufundishia elimu ya juu. Au tatizo la utafiti ni watoto wa mtaani. Kwa hiyo maswali yalenge sababu za kuwepo watoto wa mitaani. Maswali magumu yaulizwe mwishoni. Hii ina faida kwa sababu, hata kama mtafitiwa atashindwa kujibu kutokana na sababu mbalimbali maswali yale ya awali yatakuwa yanatosha kutoa taarifa muhimu zinazohusu tatizo la utafiti. Pia mtiririko wa maswali lazima uanze na maswali ya jumla kwenda maswali mahususi. Mtafitiwa hana budi kuelewa kuwa majibu yaliyotolewa ni kwa ajili ya utafiti huo. jinsi/namna ya utungaji wa maswali hayo; kutunga maswali katika mtiririko mzuri kwa kuanza na maswali rahisi kwenda magumu lakini pia kwa kuzingatia maswali ya jumla kwenda maswali mahususi. Maswali magumu yanaulizwa mwishoni. Maswali yanayotungwa yawe wazi, yasiwe na upendeleo wa kijinsia au kisiasa au kidini. Maswali yazingatie vigezo vifuatavyo; Maswali, yawe mafupi, yenye wazo moja, pia yawepo maswali ya majibu mafupi ya ndiyo au hapana, ya kuchagua na yawepo maswali ya kutoa maelezo. maswali yaeleweke/yawe sanifu maswali yaendane na uwezo wa kufikiri wa mtafitiwa, mfano unasuka kwa mwaka mara ngapi? Swali hilo ni gumu kwa maana hiyo lingeweza kuulizwa kuwa, kwa wiki unasuka mara ngapi? Hii itasaidia kufikiria kwa haraka. Kanuni ya pili hojaji isiwe ndefu sana, na kila hojaji iwe na lengo moja tu. Matokeo ya hojaji kuwa ndefu itamchosha mtafitiwa. Muhimu maswali yasidokeze majiu. Kwa mfano Hivi wewe ndo Honest? Hapa hospitali nasikia hakuna huduma nzuri ni kweli? Tatu izingatie usuli wa watafitiwa kama vile jina, umri jinsia, kabila na kiwango cha elimu. Hii inasaidia mtatifi katika uchambuzi wa data kujua amehoji watu wa umri gani na amehoji watu wa kiwango gani cha elimu. ***namna/jinsi ya kutunga maswali, mtafiti lazima atambue kwamba kila swali lazima liwe wazi vinginevyo mtafitiwa hataelewa swali linataka nini. Vilevile maswali yasiwe na upendeleo wa kijinsia kwa mfano*** 4. Maswali yazingatie vigezo vifuatavyo; yawe rahisi, na yenye wazo moja la msingi. Maswali yaeleweke kirahisi. Maswali yaendane na uwezo wa kufikiri wa mtafitiwa mfano unasuka kwa mwaka mara ngapi? Swali hilo ni gumu kwa maana hiyo lingeweza kuulizwa kuwa kwa wiki unasuka mara ngapi? Hii itasaidia kufikiria kwa haraka. Pamoja na hayo kuna miundo ya aina mbili ya utungaji wa maswali; maswali yenye majibu ya kuchagua (funge) maswali yanayomruhusu mtafitiwa kujieleza (si funge) FAIDA YA MASWALI FUNGE Kwanza ni rahisi kujibu, yanaeleweka kwa urahisi, mtafitiwa ana uwezo wa kutofautisha swali moja na jingine HASARA Kwanza maswali hayo yanatoa majibu kwa mtafitiwa. Mfano Wahehe wanakula mbwa? Andika ndiyo au hapana, pia huzuia nafasi ya mtafitiwa kujieleza zaidi kwa jambo analolijua, pia hayako sahihi hasa pale ambapo yanakuwa magumu na hasa mtafiti anahitaji majibu sahihi. Kutokana na udhaifu wa maswali funde, ndipo maswali ya wazi yanapohitajika. Maswali ya wazi yanatungwa kwatika mazingira ambayo yanatoa nafasi kwa mtafitiwa kutoa maelezo zaidi kwa kutumia maneno/maelezo yake binafsi. FAIDA YA MASWALI HURU Huruhusu mtafitiwa kutoa maelezo mengi tena kwa maneno yake binafsi, mtafitiwa huwa huru katika kujieleza,. HASARA Ni vigumu kukabiliana nayo, kwa maana kwamba inaibua ugumu wa kubaini majibu sahihi ya swali lililoulizwa hii ni kwa sababu maelezo yanakuwa mengi. Pia mtafitiwa anaweza akawa na mtizamo hasi kwa hiyo akajibu ndivyo sivyo. Kwa hakika hojaji nzuri haina budi kutumia njia zote mbili yaani njia ya maswali funge na njia ya maswali ya wazi. Kwani kwa kufanya hivyo unaweza kupata majibu ya ndiyo au hapana kadri ya maswali yaliyoulizwa, lakini pia utapata maoni mbalimbali na picha halisi kulingana na mtizamo wa mtafitiwa. Mtafiti lazima awe makini katika maneno anayotumia katika kuaandaa maswali, maneno yawe na maana. Pia mtafiti lazima atumie sentensi rahisi. Maneno ambayo ni magumu ambayo hayaeleweke, istilahi za kitaalumaau na yenye maana zaidi ya moja lazima yaepukwe. Pia maneno ambayo hayaendani na utamaduni wa jamii husika lazima yaepukwe Kimsingi utunzi wa maswali na utumiaji wa maneno ni sanaa ambayo inahitaji mtu kujifunza.

MJENGO WA FASIHI SIMULIZI NA FASIHI ANDISHI MJENGO WA FASIHI SIMULIZI YA KISWAHILI. MJENGO WA FASIHI ANDISHI YA KISWAHILI

MJENGO WA FASIHI SIMULIZI NA FASIHI ANDISHI MJENGO WA FASIHI SIMULIZI YA KISWAHILI. MJENGO WA FASIHI ANDISHI YA KISWAHILI