UTANGULIZI USULI WA TAALUMA YA FONOLOJIA
Neno fonolojia linatokana na
maneno mawili ya Kigiriki phone-sauti za kusemwa na logos- taaluma/mtalaa.
Masimulizi yanadai kuwa taaluma hii ilianza zamani sana kati ya mwaka 460 kabla
ya Masihia huko India ya kale, ambapo mtu aliyeitwa Panini, na ambaye huaminika
kuwa ni baba wa isimu aliandika kuhusu fonolojia ya Kisansikriti katika matini
aliyoiita Shiva Sutras. Ni katika andiko hili ndipo alipobainisha kuwepo kwa
dhana ambazo leo hii hujulikana kama fonimu, mofimu na mzizi. Baada ya andiko
hilo, habari za taaluma ya fonolojia ni kama zilipotea kabisa katika uwanja wa
isimu hadi ilipofika karne ya 19 ambapo wanaisimu wengine waliibuka na
kuzungumzia upya masuala ya fonolojia. Miongoni mwa wanaisimu wa mwanzo
wanaotajwa kujihusisha na fonolojia ni Mpolandi "Jan Baudouin de
Courtenay" , (pamoja na mwanafunzi wake wa zamani "Mikołaj
Kruszewski" alipobuni neno fonimu mnamo mwaka 1876, na kazi yake,
ijapokuwa hairejelewi sana, inachukuliwa kuwa ni mwanzo wa fonolojia mamboleo.
Mwanaisimu huyu si tu alishughulikia nadharia ya fonimu, bali pia vighairi vya kifonetiki
(ambavyo leo huitwa alofoni na mofofonolojia). Maandishi ya Panini (Sarufi ya
Kisanskriti) pamoja na Jan Baudouin de Courtenay yalikuja kuwa na athari kubwa
kwa anayeaminika kuwa baba wa nadharia ya Umuundo Mamboleo, Ferdinand de
Saussure, ambaye pia alikuwa ni profesa wa Sansikriti. Wanaisimu wote hawa
walikuwa wanajaribu kulinganisha sauti za lugha za Asia Mashariki na za Ulaya,
lengo lao likiwa ni kujua mizizi ya lugha zilizoitwa India-Ulaya. Kutokana na
mkabala huo, katika kipindi hicho isimu ilikuwa Isimu-linganishi tu. Kutokana
na tafiti zao hizo waliweza kupata maneno yenye sauti na maana zilizolingana,
kufanana au kukaribiana. Utafiti huo uliweza kugundua jamii mbili za lugha
ambazo ni jamii ya lugha za Kirumi na jamii ya lugha za Kijerumani. Baadhi ya
wanaisimu mahususi kabisa wanaokumbukwa kuchangia katika maendeleo ya fonolojia
ni pamoja na: (i) Jan Baudouin de Courtenay (1845-1929) Kama ilivyoelezwa hapo
awali, huyu ni mwanaisimu aliyebuni dhana za foni na fonimu. Katika nadharia
yake, alidai kuwa sauti za mwanadamu ni za aina mbili—foni na fonimu. Alisema kuwa foni ni sauti za kutamkwa tu
lakini fonimu ni sauti za lugha. Hata hivyo, de Courtenay hakutumia istilahi za
foni na fonimu (kama zinavyotajwa sasa) bali alitumia istilahi za anthrophonics—foni
na psychophonics—fonimu. Yeye alidai kuwa foni zipo karibu sana na taaluma ya
kumuelewa binadamu pamoja na alasauti zake ambazo kwa hakika hutofautiana sana
na za wanyama wengine. Na kuhusu fonimu, alidai kuwa zinahusu kumwelewa
binadamu pamoja na akili zake na namna anavyofikiri katika akili yake. Alidai
kuwa, mara nyingi, binadamu hupokea kinachotamkwa na kufasiliwa. (ii) Ferdinand
de Saussure (1887-1913) Ni mwanaisimu wa Kiswisi anayejulikana kama baba wa
isimu kutokana na mchango wake alioutoa katika taaluma hii. Yeye anakumbukwa
zaidi kutokana na uwezo wake wa kutofautisha dhana alizoziita langue—mfumo wa
lugha mahsusi na parole—matamshi ya mzungumzaji wa lugha husika. Langage
hufafanuliwa kuwa ni uwezo alionao mzungumzaji wa lugha mahususi wa kuzungumza
na kuelewa matamshi ya mzungumzaji mwingine wa lugha hiyohiyo. Ni sehemu ya
lugha inayowakilisha maarifa kati ya sauti na alama. Ni mfumo wa alama kwa
maana ya kiufundi tu. Dai lake la msingi ni kuwa alama inategemea vitu
viwili—kitaja na kitajwa—hivyo ili mawasiliano yafanyike, mfumo wa ishara
lazima ufahamike na ukubaliwe na wanajamii wote. Kwa upande wa parole, anadai
kuwa ni matendo uneni. Ni namna lugha inavyotamkwa katika hali halisi na mtu
mmoja mmoja. Dhana ya parole inalingana na dhana ya performance (utendi) ya
Noam Chomsky. Katika lugha, parole ni matamshi tofauti ya sauti moja—alofoni.
Wanaisimu wanaonekana kukubaliana na madai ya Saussure kwakuwa inaelekea
kuthibitika kuwa hakuna uhusiano wa moja kwa moja kati ya kitaja na kitajwa
[alama (lugha) na kinachowakilishwa (masilugha)], bali makubaliano baina ya
wazungumzaji wa lugha moja husika ndiyo hutawala. (iii) Nikolai Trubetzkoy
(1890-1939) Ni miongoni mwa waanzilishi wa taaluma ya fonolojia akichota mizizi
ya taaluma ya isimu kutoka katika Skuli ya Prague. Mwanaisimu huyu aliandika
misingi ya fonolojia kwa kutumia maarifa yaliyoibuliwa na Ferdinand de
Saussure. Ni mtaalamu wa kwanza kufasili dhana ya fonimu. Aliandika vitabu
vingi kwa lugha ya Kijerumani, miongoni mwake ni Grundzüge der Phonologie
(Principles of Phonology, 1939), ambapo ni katika kitabu hicho ndimo alimotoa
fasili ya fonimu pamoja na kubainisha tofauti baina ya fonetiki na fonolojia.
(iv) Noam Chomsky (1928-) Huyu ni mwanaisimu wa Kimarekani anayevuma sana kwa mchango
wake katika taaluma ya isimu kwa ujumla. Dhana za competence (umilisi) na
perfomance (utendi) zimemfanya awe maarufu ulimwenguni. Dhana hizi zinaelezea
tofauti baina ya maarifa na udhihirishaji wa maarifa hayo ya mtumiaji wa lugha.
Katika fonolojia, Chomsky anakumbukwa kwa ufafanuzi wake wa dhana ya fonimu kwa
mtazamo wa kisaikolojia. Anapochunguza dhana hii, hudai kuwa fonimu ni tukio la
kisaikolojia, hivyo fonimu zimo kichwani mwa mzungumzaji wa lugha. (v) Daniel
Jones (1881-1967) Ni mwanafonetiki kinara na maarufu kabisa katika nusu ya
kwanza ya karne ya ishirini. Ni Mwingereza msomi ambaye alikuwa na shahada ya
kwanza ya hisabati na shahada ya mahiri ya sheria, shahada ambazo hata hivyo,
hakuwahi kuzitumia. Baadae, alisomea lugha na kuhitimu shahada ya uzamivu.
Daniel Jones alifunzwa fonetiki na maprofesa mbalimbali, japokuwa aliathiriwa
zaidi na Paul Passy na Henry Sweet. Hamu yake kuu ilikua kwenye nadharia ya
fonetiki. Anafahamika zaidi kwa ufafanuzi wa dhana ya fonimu kwa mtazamo wa
kifonetiki (ufafanuzi wake tutauchunguza katika sehemu ya mitazamo ya dhana ya
fonimu). FONETIKI NA FONOLOJIA
Fasili ya taaluma ya fonolojia haiwezi kukamilika, na pengine kueleweka, iwapo
hakuna linalosemwa kuhusiana na taaluma ya fonetiki. Hali hii inatokana na
ukweli kuwa kuna uhusiano wa kinasaba kati ya fonolojia na fonetiki. Massamba
na wenzake (2004:5) wananeneleza ukweli huu kwamba: …fonetiki na fonolojia ni
matawi mawili tofauti ya isimu lakini yenye kuhusiana sana. Uhusiano wa matawi
haya unatokana na ukweli kwamba yote mawili yanajihusisha na uchunguzi na
uchambuzi unaohusu sauti za lugha za binadamu. Kutokana na ukweli huu, jitihada
za kufasili dhana ya fonolojia inaelekea kuwa nyepesi, dhana hizi mbili
zinapofasiliwa kwa mlinganyo. Tuanze na fonetiki: FONETIKI NI NINI? Fonetiki ni
tawi la isimu linalochunguza sauti za kutamkwa na binadamu ambazo huweza
kutumika katika lugha asilia. Massamba na wenzake (kama hapo juu) wanafasili
fonetiki kuwa ni tawi la isimu linalohusika na uchunguzi na uchambuzi wa taratibu
za utoaji, utamkaji, usafirishaji, usikiaji, na ufasili wa sauti za lugha za
binadamu kwa ujumla. Wanasisitiza kwamba, kinachochunguzwa katika fonetiki ni
[maumbo] mbalimbali ya sauti zinazoweza kutolewa na alasuti za binadamu (yaani
sauti za binadamu zinazotamkwa tu). Kipashio cha msingi cha uchambuzi wa
kifonetiki ni foni. Foni ni sauti yoyote inayotamkwa na binadamu na inayoweza
kutumika katika lugha fulani. Hivyo basi, foni ni nyingi sana na hazina maana
yoyote. Wanafonetiki hudai kuwa foni zimo katika bohari la sauti (dhana
dhahania) ambalo kila lugha huchota sauti chache tu ambazo hutumika katika
lugha mahususi. Sauti chache zinazoteuliwa na lugha mahususi kutoka katika
bohari la sauti huitwa fonimu. Matawi ya Fonetiki: Kuna mitazamo miwili tofauti
kuhusiana na matawi ya fonetiki. Mtazamo wa kwanza ni unaodai kuwepo matawi
matatu; na mtazamo wa pili ni unaodai kuwepo matawi manne. Mtazamo wa kuwepo
matawi matatu unataja fonetiki matamshi, fonetiki akustika, na fonetiki
masikizi. Mtazamo wa kuwepo matawi manne (kama Massamba na wenzake (kama hapo
juu), pamoja na matawi tuliyokwisha yataja, wanongezea tawi fonetiki
tibamatamshi. Fonetiki matamshi huchunguza jinsi sauti za lugha zinavyotamkwa
kwa kutumia alasauti. Hususani, huchunguza namna na mahali pa kutamkia sauti
husika. Fonetiki akustika huchunguza jinsi mawimbi ya sauti yanavyosafiri
kutoka katika kinywa cha mtamkaji hadi kufika katika sikio la msikilizaji.
Fonetiki masikizi hujihusisha na mchakato wa ufasili wa sauti za lugha,
hususani uhusiano uliopo baina ya neva za sikio na za ubongo. Na fonetiki
tibamatamshi ni tawi jipya lililozuka mwanzoni mwa karne hii, ambalo huchunguza
matatizo ya utamkaji ambayo binadamu huweza kuzaliwa nayo au kuyapata baada ya
kuzaliwa. Ni tawi linalojaribu kutumia mbinu za kitabibu kuchunguza matatizo na
kutafuta namna ya kuyatatua. FONOLOJIA NI NINI? Fonolojia ni taaluma ya isimu
inayochunguza mifumo ya sauti za kutamkwa zinazotumika katika lugha asilia
mahususi za binadamu. Inapolinganishwa na fonetiki, inasisitizwa kuwa fonolojia
ni tawi la isimu linalochunguza mifumo ya sauti za lugha mahususi tu, kama vile
sauti za Kiswahili, Kiingereza, Kigogo, n.k. Hata hivyo, wapo wanaisimu
wanaoelekea kukubaliana kuwa kuna fonetiki ya lugha mahususi pia, na kuna
fonolojia ya jumla, na fonetiki ya lugha mahususi. Mathalani, Massamba (1996)
licha ya kufasili fonolojia kuwa ni taaluma ya isimu inayochunguza mfumo wa
sauti za lugha mahususi, anaenda mbele zaidi na kudai kuwa fonolojia inaweza
kuchunguza sauti kwa ujumla wake bila kuzihusisha na lugha mahususi. Akmajian
na wenzake (2001), nao wanadokeza msimamo kama wa Massamba wanapodai kwamba
fonolojia inaweza kuchunguzwa kwa mitazamo miwili tofauti. Kwanza, fonolojia
kama tawi dogo la isimu linalochunguza mfumo na ruwaza za sauti za lugha
mahususi ya binadamu; na pili, fonolojia kama sehemu ya nadharia ya jumla ya
lugha ya binadamu inayohusika na tabia za jumla za mfumo wa sauti za lugha
asilia za binadamu. Katika mhadhara huu, hata hivyo, tutakuwa wafuasi wa
mtazamo unaoona kuwa fonolojia ni tawi la isimu linaloshughulikia mfumo wa
sauti za lugha mahususi, hivyo tuna, kwa mfano, fonolojia ya Kiswahili,
fonolojia ya Kiingereza, fonolojia ya Kiha, fonolojia ya Kihehe, na fonolojia
ya Kibena. Kipashio cha msingi cha fonolojia ni fonimu. FONIMU Ni kipashio
kidogo kabisa cha kifonolojia kinachoweza kubadili maana ya neno. Hivyo basi,
fonimu ina maana, kwakuwa inaweza kubadili maana ya neno inapobadilishwa nafasi
katika neno husika. Foni chache zilizoteuliwa kutoka katika bohari la sauti ili
zitumike kwenye mfumo wa sauti za lugha mahususi ndiyo fonimu. Hivyo, fonimu ni
chache ikilinganishwa na foni. Idadi ya fonimu za lugha hutofautiana kati ya
lugha moja na nyingine. Mathalani, Kiarabu kina fonimu ishirini na nane (28),
Kiswahili kina fonimu thelathini (30), Kifaransa kina fonimu thelathini na tatu
(33), na Kiingereza kina fonimu arobaini na nne (44). Sauti ambayo huweza
kubadilishwa nafasi yake katika neno lakini maana ikabaki ileile huitwa
alofoni. Alofoni ni kipashio cha kifonolojia kinachotaja hali ambapo fonimu
moja hutamkwa na kuandikwa tofautitofauti bila kubadili maana ya neno. Mfano:
Fedha na feza Sasa na thatha Heri na kheri Kwa kifupi, alofoni ni matamshi
tofautitofauti ya fonimu (sauti) moja. MITAZAMO YA DHANA YA FONIMU Juhudi za
kufasili dhana ya fonimu zilizofanywa na wanaisimu mbalimbali zimezua mitazamo
mbalimbali ya namna ya kuchambua dhana hii. Hadi sasa, mitazamo mitatu ifuatayo
ndiyo hujulikana zaidi. Fonimu ni Tukio la Kisaikolojia Huu ni mtazamo
uliokuzwa na kutetewa na wanasarufi geuzi-zalishi, mwanzilishi wake akiwa ni
Noam Chomksy. Kwa mujibu wa mtazamo huu, fonimu ni dhana iliyo katika akili ya
mzungumzaji wa lugha. Mtazamo huu unadai kuwa kila mzungumzaji wa lugha ana
maarifa bubu ya idadi na jinsi ya kutamka fonimu za lugha yake. Chomsky
anayaita maarifa haya kuwa ni umilisi (competence). Anadai kuwa maarifa haya ya
fonimu hufanana kwa kiasi kikubwa miongoni mwa wazungumzaji wa lugha moja
husika. Kinachotofautiana ni jinsi ya kudhihirisha (kutamka) fonimu hizo, yaani utendi (perfomance).
Chomsky anabainisha kuwa kuna uwezekano mkubwa wa kuhitilafiana baina ya
umilisi na utendi kutokana na matatizo mbalimbali ambayo mzungumzaji
hukabiliana nayo. Matatizo hayo ni kama vile uchovu, ulemavu wa viungo vya
matamshi (alasauti za lugha), athari za mazingira, ulevi, na maradhi. Hivyo,
kutokana na hali hii, fonimu hubaki kuwa tukio la kiakili, yaani kisaikolojia
tu. Fonimu ni Tukio la Kifonetiki Wafuasi wa mtazamo huu wanaongozwa na Daniel
Jones. Daniel Jones anaiona fonimu kuwa ni [umbo] halisi.
..........................Inaendelea